Thursday, June 9, 2016

WAWEKEZAJI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUDUMISHA AMANI YA NCHI

Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wawekezaji kwenye Visiwa vilivyopo Wilayani Mafia kushirikiana na serikali ili kudhibiti usalama wa nchi kukabiliana na wageni wasio waaminifu ambao wanaoweza kuvitumia visiwa hivyo kuhatarisha amani ya nchi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ilipotembelea Kisiwa cha Shungimbili kwenye Hoteli ya Thanda ambayo inamilikiwa na raia wa kigeni na kusema kuwa kuna haja ya kuwa na kituo cha kufuatilia wageni wanaoingia na kutoka.
Ndikilo alisema kuwa kutokana na hali ya sasa kuwa mbaya kiusalama kutokana na matukio ya mauaji ya kutisha ambayo yanatokea hapa nchini ni vema ulinzi ukaimarishwa.
“Kuna haja ya kuwa na ushirikiano na baina ya wawekezaji na serfikali ili kukabiliana na wahalifu ambao wanaweza kutumia visiwa kujiingiza hapa nchini na kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa dunia ya sasa imebadilika na baadhi ya watu wamekuwa wakitumia njia ya Bahari kupitisha wahamiaji haramu, dawa za kulevya pamoja na uingizwaji wa silaha.
“Serikali haina nia mbaya ya kutaka kujua mambo yanayofanywa na wawekezaji kwa kujua wageni wanaoingia na kutoka na wameleta nini wanatoka na nini na hapa kutakuwa na kituo cha ukaguzi ambacho kitakuwa na polisi kwa ajili ya kulinda eneo la Kisiwa kwani wageni watakuwa wanafika kwa wingi,” alisema Ndikilo
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Thanda Island Tanzania Ltd Oscar Pucci alisema kuwa hana tatizo na ushirikiano na serikali kwani anashirikiana vizuri na Halmashauri.
Pucci alisema kuwa wamekuwa wakisaidia shughuli za maendeleo kama kuchangia kwenye Hospitali ya wilaya na hata wavuvi wanaovua jirani na hoteli yao.

Mwisho.

TCRA YATOA MAFUNZO KUHUSU KUFUTWA SIMU FEKI

Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA Kuwa mawasiliano endapo yatatumika vizuri yana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji hapa nchini na kusababisha wananchi kutambua fursa za maendeleo zilizopo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakatia akifungua mafunzo ya siku moja ya wadau wa maweasiliano yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) juu ya zoezi la uzimaji simu bandia linalotarajiwa kufanyika katikati ya mwezi huu.
Ndikilo alisema kuwa makampuni na mashirika kuanzia yale ya nje na ndani ya nchi yameweza kuongeza uwekezaji kwenye sekta mbalimbali kupitia mawasiliano yakiwemo ya  Mitandao ya Kijamii ,Simu, Redio, Televisheni na Magazeti.
“Mawasiliano ni chombo cha maendeleo endapo kinatumika vizuri na tumeona faida ya mawasiliano hasa yale ya intaneti ambapo wananchi wameweza kujua fursa mbalimbali za kufanya biashara za ndani na nje nchi nah ii yote imetokana na kuboreshwa suala la mawasiliano,” alisema Ndikilo.
Alisema kupitia mitandao kasi ya maendeleo imekuwa kubwa kup[itia mitandao kwa wale waliotumia vizuri ila kwa wale wanaotumia vibaya imekuwa ni kero kwani baadhi wameitumia kwa kutoa lugha chafu, wizi, utapeli na wizi kwa njia ya mtandao.
“Faida ni nyingi ikilinganishwa na hasara na katika uboreshaji wa kuondoa simu bandia itasaidia kukabiliana na wizi, matumizi mabaya kama vile kashfa na vitendo vibaya vilivyokuwa vinatumika kupitia mitandao kwani hata wale wezi wa kukwapua simu mwisho wao umefika,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa TCRA Isaac Mruma alisema kuwa wameamua kutoa elimu hiyo kwa wananchi kabla ya kufikia hatua ya kuzima simu bandia ili wawe wanajua na namna ya kugundua simu hizo ambazo zitasitishwa matumizi yake ifikapo Juni 16 mwaka huu.
Mruma alisema kuwa wametoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya mafundi simu, wauzaji wa simu, maofisa wa kamati za ulinzi na usalama, waandishi na wananchi wa kawaida kwenye kanda ambapo kanda ya Mashariki ni ya mwisho ikiwa na mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara, Dar es Salaam na Morogoro.
Naye meneja mradi Injinia Imelda Salum alisema kuwa mbali ya kuondolewa bidhaa bandia za mawasiliano pia zoezi hilo litaambatana na rejesta ya utambulisho wa watumiaji wa wa vifaa vya simu ili kuboresha huduma za mawasiliano.
Salum alisema kuwa kwa mafundi wa simu wanapaswa kutozirekebisha simu hizo ili kuwaaminisha kuwa simu fulani ni aina fulani kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai ambapo mhusika anaweza kuchukuliwa hatua ya kisheria.
Mwisho.   
  
Sunday, June 5, 2016

JUMUIYA YA WAZAZI YASISITIZA UBORA WA ELIMU CHUO CHA KILIMO NA MIFUGO

Na John Gagarini, Chalinze
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kimesema kuwa kitashirikiana na uongozi wa Chuo Cha Kilimo na Mifugo cha Kaole ili kuhakikisha elimu inayotolewa ina kuwa na manufaa kwa nchi.
Hayo yalisemwa Lugoba wilayani humo na mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Abdul Sharifu wakati wa baraza la Wazazi na kusema kusema kuwa chuo hicho ambacho kinamilikiwa na jumuiya kitaboreshwa masomo yanayotolewa chuoni hapo ili wahitimu wake wabadilishe sekta hiyo na kuleta faida kwa wafugaji na wakulima nchini.
Sharifu alisema kuwa chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo watahakikisha wanaziondoa kwa kushirikiana na makao makuu ya Jumiya hiyo ili kiweze kutoa elimu bora ambayo itasaidia kuboresha ufugaji na kuwa wa kisasa na wenye tija.
“Chuo kinakabiliwa na changamoto lakini tutazikabili kadiri ya uwezo wetu ili tuboreshe elimu inayotolewa chuoni hapo hasa tukizingatia ufugaji ni moja ya chanzo kikubwa cha pato la Taifa na kilimo kwa ajili ya chakula,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa chuo hicho kinajijenga upya baada ya awali kubadilishwa na kuwa shule ya sekondari lakini sasa kimerudishwa mikononi mwao hivyo watahakikisha kinakuwa moja ya vyuo bora hapa nchini kwa kutoa elimu inayokubalika.
“Tunaomba wadau mbalimbali kujitokeza kukisaidia chuo chetu ili kiweze kuboresha wasomi ambao watakubalika kule watakakopangiwa hasa ikizingatiwa wahitimu hao watakuwa ni maofisa ugani wataboresha kilimo na ufugaji,” alisema Sharifu.
Kwa upande wake mjumbe wa baraza la jumuiya hiyo Yahaya Msonde alisema kuwa lengo lao ni kutoa elimu itakayokidhi mahitaji ya wakulima na wafugaji ili waboreshe shughuli zao.
Msonde alisema kuwa kilimo ni uti wa mgongo hivyo lazima kiwekewe mikakati ya kuinuliwa kwa kuzalisha wataalamu wenye uweze na mbinu za kisasa na kwa wafugaji nao waweze kukabiliana na ufugaji usiokuwa na tija.

Mwisho.   

WATAKA TAARIFA RASMI MRADI WA MIWA KUFUTWA

Na John Gagarini, Bagamoyo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani imetakiwa kutoa taarifa rasmi kwenye vijiji vilivyokuwa kwenye mradi wa kilimo cha miwa chini ya kampuni ya Eco Energy uliosimamishwa na serikali ili eneo hilo lisije kuchukuliwa na mtu mwingine ili hali wananchi hao hawajalipwa fidia.
Mradi huo ulisimamishwa kupitia majibu ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa anajibu swali la kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe aliyetaka kujua ni kwanini serikali imeshindwa kuweka jitihada za makusudi ili mradi huo ukamilike ambao ulibainika kuwa ungetumia maji mengi ya Mto Wami na kuathiri usatawi wa wanyama kwenye Mbuga ya Saadani.
Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Bagamoyo katibu wa kamati ya ardhi ya Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Mkombozi Bakari Salum alisema kuwa     kwa kuwa kauli ya Waziri Mkuu ni agizo ni vema Halmashauri ingetoa tangazo rasmi kwa wananchi husika.
“Kwa kuwa wakati anakuja mwekezaji kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya mradi huo kulikuwa na taarifa rasmi na wananchi walitoa maeneo yao kwa ajili ya kilimo hicho cha miwa ambacho baadaye kungejengwa kiwanda kwa ajili ya kuzalisha sukari hivyo baada ya kushindikana wangewajulisha wananchi,” alisema Salum
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo Jackson Mkango alisema kuwa eneo ambalo lilichukuliwa na mwekezaji ni hekari zaidi ya hekta 22,000 wananchi hao hawajalipwa fidia yoyote licha ya kuwa tathmini kufanyika mwaka 2011 hadi leo hawajalipwa.
Mkango alisema kuwa sheria inasema kuwa tathmini ikifanyika walengwa wanapaswa kulipwa ndani ya kipindi cha miezi sita lakini sasa imepita miaka mitano sasa.
“Tunaiomba Halmashauri kutoa tamko juu ya ardhi hiyo ya wananchi ambayo toka imechukuliwa wananchi hawakufanya chochote licha ya kuwa eneo hilo walikuwa wakitegemea kwa ajili ya kilimo na hawajui hatma yao kwani walitegemea wangelipwa fidia,” alisema Mkango.
Vijiji vilivyokuwa kwenye mpango huo ni Razaba, Matipwili, Kitame, Fukayosi, Makaani na Gongo ambapo kuna jumla ya wananchi zaidi ya 700 ambao walikuwa wakiishi kwenye maeneo hayo yaliyoingizwa kwenye mradi huo ambao ulikuwa na lengo la kukabiliana na upungufu wa sukari hapa nchini.

Mwisho.

WAWEKEZAJI WADHIBITI USALAMA WA NCHI

Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wawekezaji kwenye Visiwa vilivyopo Wilayani Mafia kushirikiana na serikali ili kudhibiti usalama wa nchi kukabiliana na wageni wasio waaminifu ambao wanaoweza kuvitumia visiwa hivyo kuhatarisha amani ya nchi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ilipotembelea Kisiwa cha Shungimbili kwenye Hoteli ya Thanda ambayo inamilikiwa na raia wa kigeni na kusema kuwa kuna haja ya kuwa na kituo cha kufuatilia wageni wanaoingia na kutoka.
Ndikilo alisema kuwa kutokana na hali ya sasa kuwa mbaya kiusalama kutokana na matukio ya mauaji ya kutisha ambayo yanatokea hapa nchini ni vema ulinzi ukaimarishwa.
“Kuna haja ya kuwa na ushirikiano na baina ya wawekezaji na serikali ili kukabiliana na wahalifu ambao wanaweza kutumia visiwa kujiingiza hapa nchini na kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa dunia ya sasa imebadilika na baadhi ya watu wamekuwa wakitumia njia ya Bahari kupitisha wahamiaji haramu, dawa za kulevya pamoja na uingizwaji wa silaha.
“Serikali haina nia mbaya ya kutaka kujua mambo yanayofanywa na wawekezaji kwa kujua wageni wanaoingia na kutoka na wameleta nini wanatoka na nini na hapa kutakuwa na kituo cha ukaguzi ambacho kitakuwa na polisi kwa ajili ya kulinda eneo la Kisiwa kwani wageni watakuwa wanafika kwa wingi,” alisema Ndikilo
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Thanda Island Tanzania Ltd Oscar Pucci alisema kuwa hana tatizo na ushirikiano na serikali kwani anashirikiana vizuri na Halmashauri.
Pucci alisema kuwa wamekuwa wakisaidia shughuli za maendeleo kama kuchangia kwenye Hospitali ya wilaya na hata wavuvi wanaovua jirani na hoteli yao.

Mwisho.

Sunday, May 29, 2016

POLISI WATUMIA VIPIMA ULEVI KUDHIBITI AJALI PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
KITUO cha Afya cha Mkoani kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Jenereta ili kukabiliana na tatizo la ukatikaji umeme kwenye chumba cha akinamama wanapojifungulia hivyo kuwaomba wadau mbalimbali.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Happiness Ndosi wakati akipokea msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto waliozaliwa na watakaozaliwa kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la Abubaker Darwesh International Charitable Foundation (ADICF) la Jijini Dar es Salaam.
Dk Ndosi alisema kuwa kukatika kwa umeme kwenye kituo hicho ni changamoto kubwa hasa nyakati za usiku na wakati mama wajawazito wanapokuwa wanajifungua hali ambayo inahatarisha maisha ya akinamama hao.
“Kutokana na hali hiyo tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutusaidia kupata jenereta kwa ajili ya kusaidia mara umeme unapokatika katika chumba cha uzalishaji mama wajawazito ili kunusuru maisha yao,” alisema Dk Ndosi.
Aidha alisema mbali ya changamoto hiyo pia wanakabiliwa na changamoto nyingine ikiwa ni pamoja na ukosefu wa chumba cha upasuaji, Ultra Sound na X-Ray, gari la wagonjwa kwani lililopo ni chakavu, magodoro na vitanda hasa ikizingatiwa kuwa kituo hicho kiko mbioni kuwa Hospitali ya Wilaya.
Kwa upande wake mwanzilishi na meneja mradi wa shirika hilo Bilal Abubekar alisema kuwa shirika lake limeamua kutoa misaada hiyo kwa lengo la kuisaidia jamii hasa kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano ili kuisaidia serikali kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano wanapata huduma bora.
Abubaker alisema kuwa shirika lao limekuwa likisaidia makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajane yatima na watu wenye mahitaji, pia kusaidia elimu watu wenye ulemavu.
Naye moja ya wagonjwa waliopata msaada huo Mariamu Ally alishukuru shirika hilo na kusema kuwa wameonyesha moyo wa upendo na kuwataka waendelee kusaidia hospitali hiyo ili iweze kukabiliana na changamoto zilizopo kwa wagonjwa.
Alisema kuwa moja ya changamoto iliyopo kwenye wodi hiyo ni kuchanganywa kati ya akinamama waliojifungua na wale wanaosubiri kujifungua na kutaka watu hao kutenganishwa ili kila moja wawe na sehemu yao.
Mwisho.   
Na John Gagarini, Kibaha
SAKATA la Mwenyekiti wa Mtaa wa Muheza kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani Maulid Kipilili limechukua sura mpya baada ya wananchi wa mtaa huo kumkataa mwenyekiti huyo kwenye mkutano wa wananchi uliofanyika mtaani hapo.
Wananchi hao walimkataa mwenyekiti wao wakati wa mkutano ulioitishwa na diwani wa kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi ili kujadilia suala la malalamiko ya wananchi wa mtaa huo baada ya kuifunga ofisi ya mtaa hadi pale watakapofikia muafaka juu ya mwenyekiti wao.
Mkutano huo ambao ulifanyika mtaani hapo chini ya diwani huyo wa kata na ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Thadeo Mtae wananchi hao walilalamika kuwa mwenyekiti wao tangu achaguliwe kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2015 hajaitisha mkutano wa wananchi.
Kabla ya kufikia hatua ya kumkataa mwenyekiti wao wananchi hao walitoa malalamiko yao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulalamika kuwa mwenyekiti wao haitishi vikao vya wananchi, hasomi mapato na matumizi, kutofungua ofisi hivyo kuwapa shida wananchi wanapokwenda kupata huduma za kiofisi.
Akizungumza juu ya mwenyekiti wao kushindwa kuwajibika mwananchi wa mtaa huo Kitai Mganga alisema kuwa ni pamoja na tuhuma nyingine ni kushindwa kusimamia mali za mtaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kumega na kuuziana eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Msingi lakini hakuna hatua zozote ambazo amezichukuwa.
“Mtaa wetu una changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji, umeme, Shule ya Msingi, bararabara na zahanati lakini kutokana na mwenyekiti wetu kutowajibika tumeshindwa kufanya lolote hata kuweka mikakati ya maenedeleo hakuna,” alisema Mganga.
Naye Paulo Chacha alisema kuwa mwenyekiti lazima awe na wajumbe wa mtaa lakini cha kushangaza wajumbe hawapo hivyo mwenyekiti anafanya kazi peke yake jambo ambalo haliwezi kuleta mafanikio.
Chacha alisema kuwa kamati ya mtaa ni sawa na baraza la mawaziri sasa haiwezekani Rais kuongoza nchi bila ya kuwa na Mawaziri kwani maendeleo hayawezi kupatikana.
Kwa upande wake Maulid Kipilili alisema kuwa kwa upande wa mikutano alishindwa kufanya kutokana na sababu maalumu ikiwa ni pamoja na shughuli za kitaifa.
Kipilili alisema kuwa aliitisha mikutano mitatu ya dharura na miwili ya kikatiba na kuwashangaa wananchi hao kumsingizia kuwa hajafanya kabisa mikutano na mmoja wa Mei 15 ulishindwa kufanyika kutokana na akidi kushindwa kuenea.
“Kuhusu wajumbe wa serikali ya mtaa hawajafika kwa sababu mbalimbali lakini wapo na sina mgogoro na wajumbe wangu na tunafanya kazi vizuri na baadhi ya kamati zipo na zinafanya kazi kama ya maji na shule zipo na aliyeuziwa eneo la shule kama kuna mtu anaushahidi alete ili tuchukue hatua za kisheria,” alisema Kipilili.
Akielezea juu ya changamoto hiyo ya wananchi kumkataa mwenyekiti wao diwani wa kata hiyo Ramadhan Lutambi alisema kuwa kama hawamtaki wanapaswa kufuata taratibu kwani hatua ya kwanza ni hiyo.
Lutambi alisema kuwa kutokana na hali hiyo itabidi uitishwe mkutano wa dharura wa kata kujadili suala hilo na wao ndiyo watakaoamua hatma ya mweneyekiti wao.
Kufuatia kukataliwa na wananchi ofisa mtendaji wa kata ya Maili Moja Thadeo Mtae alisema kuwa hoja zilizotolewa ni 15 ambapo zimejibiwa na mwenyekiti huyo ambapo baadhi wamekataa majibu yake na nyingine wamekubali majibu.
Mtae alisema kuwa atapeleka sehemu husika kwa ajili ya majibu na hatua zaidi kwani yeye hatoweza kutoa majibu hivyo wasubiri majibu ambapo kutaitishwa mkutano mwingine.  
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wakazi kwneye eneo la Sagulasagula maarufu kama Loliondo Mtaa wa Machinjioni kata ya Tangini wilayani Kibaha mkoani Pwani wanaodaiwa kuvamia eneo lililotengwa kwa ajili ya soko wameiomba Halmashauri ya Mji kuwalipa fidia na maeneo ya kuishi baada ya kupewa siku 14 kuhama kwenye eneo hilo.
Wakizungumza mara baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya kupitia na kuangalia eneo hilo na kutoa maagizo kwa wakazi hao kubomoa nyumba zipatazo 55 zilizojengwa kwenye eneo hilo walisema kuwa kwa kuwa ni mpango wa maendeleo basi nao waangaliwe kwani wamekaa hapo kwa muda mrefu.
Said Tekelo alisema kuwa baadhi ya watu wako hapo tangu mwaka 1970 na mwaka 2003 Rais Benjamin Mkapa wakati ule alifuta hati ya eneo hilo toka eneo la Viwanda na kutaka lirejeshwe kwenye mtaa kwa ajili ya matumizi mengine.
“Baada ya kurejeshwa kwenye mtaa baadhi ya watu walipimiwa maeneo yao baada ya kupigwa picha na kamahaitoshi hata alipokuja waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa miezi mitatu sasa sita Halmashauri ikae na wakazi hao ili kujadili namna nzuri ya kufanya,” alisema Tekelo.
Alisema kuwa licha ya maagizo hayo walikwenda Mahakamani kwenda kulalamika walipotakiwa kuondoka na kesi iliendeshwa na wao kushindwa na Mahakama ili amuru Halmashauri ikae nao lakini hakuna kilichofanyika hadi mwishoni mwa wiki walipotakiwa kuvunja wenyewe na endapo hawatafanya hivyo Halmashauri itabomoa nyumba hizo.
“Tumeambiwa tubomoe wenywe na kuanzia leo Tanesco na Dawasco wameshapewa maagizo ya kuondoa miundombinu yao ilkiwa ni maandalizi ya kubomoa sisi tunaomba Halmashauri itufikirie kwa kutulipa fidia pamoja na maeneo kwa ajili ya kuishi kwani wenzetu jirani ambao tuko kwenye mgogoro mmoja wamelipwa na kupewa viwanja,” alisema Tekelo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Tangini Theodori Joseph alisema kuwa suala hilo ni la muda mrefu ambapo baraza la Madiwani miaka ya nyuma waliwatambua wakazi hao kutaka walipwe fidia na walikuwa wakishirikiana nao katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchukua kodi za majengo.
Joseph alisema kuwa kuna haja ya Halmashauri kuwafikiria wakazi hao kwani wengine wako hapo miaka 40 iliyopita na wameendeleza ardhi kwa kipindi chote hicho lakini jirani zao ambao wametengwa na barabara wao  wamepewa fidia na watapewa viwanja.
Ofisa Habari wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Inocent Byarugaba alisema kuwa eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya soko na liko kwenye Ramani ya Mji na  wakazi hao walilivamia eneo hilo na wanapaswa kuliachia.
Byarugaba alisema kuwa tayari eneo hilo liko kwenye maandalizi ya ujenzi wa soko unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa kwani tayari ramani imeshatoka ambapo soko linalotumika kwa sasa liko kwenye hifadhi ya barabara na litabomolewa muda wowote na Tanroads.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Lucy Kimoi alisema kuwa wakazi hao wanapaswa kuondoka na kwa sasa wanaandaa notisi kwa ajili ya kuwataka waliachie eneo hilo kwani wako hapo kinyume cha Sheria.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani imetenga kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 990 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa kwenye eneo la mnada wa kila wiki  maarufu kama Sagulasagula au Loliondo kwa ajili ya wakazi wa mji huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa habari wa Halmashauri hiyo Inocent Byarugaba alisema kuwa soko hilo litachukua wafanyabiashara wapatao 286 ambao walikuwa kwenye soko la zamani la Maili Moja ambalo linatarajiwa kubomolewa.
Byarugaba alisema kuwa lengo la kujenga soko hilo kubwa na la kisasa ni kutaka kuwarahisishia wananchi kupata huduma bora badala ya kukimbilia kwenye maosko makubwa kama vile la Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
“Tutajenga kwa kushirikiana na wananchi kwa mtindo wa jenga, endesha na rudisha  (BOT) ambapo watajenga kwa mkataba maalumu ambao utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili,” alisema Byarugaba.
Alisema kuwa ujenzi huo wa soko hilo utahusisha maduka ya jumla na rejareja, sehemu ya kuuzia mazao ya nafaka, samaki, mabucha ya nyama 10, mbogamboga, sehemu ya kuchinjia kuku, matunda na sehemu ya kupaki magari.
“Lengo ni kuwa na huduma bora ya soko kwani lililopo lilikuwa ni dogo na halikuwa na huduma nyingi kutokana na ufinyu wake na mabanda yake yalijengwa kwa muda kutokana na kuwa kwenye hifadhi ya barabara ambapo wenywe wanalitaka eneo lao kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo,” alisema Byarugaba.
Aidha alisema kuwa ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kuanza wakati wowote kwani tayari ramani imeshachorwa kinachosubiriwa ni taratibu chache zilizosalia ili kuanza kazi.
Mwisho.   
Na John Gagarini, Kibaha
MADEREVA wa mabasi ya abiria yanayopita mkoani Pwani wametakiwa kuacha tabia ya kutumia vilevi ikiwemo pombe ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikileta madhara na uharibifu wa mali ulemavu na kupoteza maisha ya abiria wanaowasafirisha.
Hayo yamesemwa na mwalimu wa kufundisha matumizi ya vifaa vya kupima ulevi wa Jeshi la Polisi mkoani humo Aisha Sudi na kusema kuwa moja ya vyanzo vikuu vya ajali vinatokana na ulevi hususani ule wa pombe.
Sudi amesema kuwa dereva wa basi hapaswi kabisa kutumia pombe pale anapokuwa akiendesha gari licha ya kuwa ulevi chini asilimia 80 ni wa kawaida ila unapozidi zaidi ya hapo ni hatari kwa uendeshaji wa gari.
Amesema kuwa wanapowapima na kuwabaini wana vilevi hawaruhusiwi kuendesha basi na kutakiwa kubadilisha dereva ili kuendelea na safari na hali hiyo imesababisha kupungua kwa ajali katika mkoa huo.
Aidha amesema kuwa hufikia kuyakagua mabasi hayo baada ya kupata taarifa toka kwa abiria ambao wanaangalia mwenendo wa dereva au wanapomtilia shaka dereva wa basi na anapobainika kutumia kilevi anapelekwa mahakamani kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo Abdi Issango amesema kuwa vifaa hivyo vinatumika kwenye maeneo mbalimbali kwenye barabara za kwenda mikoa jirani ya Tanga, Morogoro na Lindi.
Issango ametaja maeneo ambapo kuna askari wanaotumia hivyo vifaa kuwa ni pamoja na Maili Moja, Mlandizi, Vigwaza, Chalinze, Mdaula, Wami Mbwewe, Mapinga, Kiwangwa, Vikindu, MKuranga, Kimazinchana na Kibiti.
Amesema kuwa kutokana na Jeshi la Polisi kuweka mikakati mbalimbali ya kuzuia ajali katika kipindi cha Januari hadi Aprili hakuna ajali kubwa ya basi iliyosababisha vifo kwani nyingi ni zile ndogondogo ambazo hazina madhara makubwa.
Amebainisha kuwa ajali zinazoleta madhara kwa sasa ni za pikipiki kutokana na madereva wengi wa bodaboda kutozingatia sheria za usalama barabarani ambapo wengi hawana leseni kwani biashara hiyo ilianza bila ya utaratibu ambapo kwa sasa wanaendelea kuwapatia elimu ili waendeshe vyombo hivyo kwa kuzingatia sheria.
Mwisho.       

WAIOMBA HALMASHAURI IWALIPE FIDIA BAADA YA KUPEWA SIKU 14 KUVUNJA NYUMBA ZAO