Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amepongeza utaratibu wa
viongozi wa dini za kikristo kufunga siku 40 kwa ajili ya kuombea amani ya nchi
ili iweze kuondelea baada ya kutokea matukio yaliyokuwa yakiashiria uvunjifu wa
amani.
Akizungumza juzi na viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali
na uongozi wa jeshi la polisi mkoani humo, alisema kuwa jambo wanalolifanya ni
kubwa na linapaswa kuungwa mkono na wapenda amani.
Mahiza alisema kuwa siku za hivi karibuni kulitokea matukio
makubwa ya uvunjifu wa amani hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutokea milipuko ya
mabomu mkoani Arusha ambapo watu kadhaa walipoteza maisha huku wengine
wakijeruhiwa.
“Tukikumbuka hata kule Kusini mkoani Mtwara zilizuka vurugu
kubwa ambazo nazo matokeo yake hayakuwa mazuri kwani watu kadhaa walipoteza
maisha na mali huku wengine wakijeruhi hivyo kuna haja ya kuwa na mkakati wa
kukabilina na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuiombea nchi amani,” alisema
mahiza.
Aidha alisema kuwa amani kuipoteza ni rahisi lakini gharama
ya kuirudisha ni kubwa sana hivyo lazima kila mtu aangalia ni namna gani
anaweza kunusuru hali hiyo.
“Tunaunga mkono jitihada za viongozi wa dini kuamua kufunga
na kufanya maombi maalumu ili kuinusuru nchi yetu ili isiingie kwenye machafuko
ambayo mara nyingi husababisha vifo na watu kushindwa kufanya shughuli za
maendeleo,” alisema Mahiza.
Alisema kuwa sehemu yoyote yenye machafuko maendeleo hakuna
hivyo kuna kila sababu ya kuiombea nchi ili iepukane na hayo yanayotaka
kujitokeza.
Kwa upande wake katibu wa umoja wa makanisa ya kipentekoste
mkoa wa Pwani Mchungaji Gervase masanja alsiema kuwa endapo amani itatoweka
hata uhuru wa kumwabudu mungu hautakuwepo.
“Baadhi ya watu wameingiza siasa makanisani jambo ambalo
linaweza likawa chanzo cha vurugu hivyo tunawaomba waumini wasiiingize siasa
kwenye sehemu za kuabudia kwani ni hatari na ndiyo sababu ya sisi kuamua
kufunga kuombea amani iliyopo isivunjike,” alisema Mch Masanja.
Kikao hicho pia kiliwajumuisha wakuu wa wilaya, wakuu wa
polisi wa wilaya, vyama vya siasa, vyama vya watu wenye ulemavu na watu maarufu
ndani ya jamii kwenye mkoa huo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA)
mkoa wa Pwani imekunjua makucha yake baada ya kumtaka kondakta wa basi la
kampuni ya Mbazi kuwarudishia nauli waliyoizidisha tofauti na ile iliyopangwa
na serikali.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki kwenye stendi ya maili
Moja wilayani Kibaha baada ya abiria kulalamika kuwa wamezidishiwa nauli wakati
wakikata nauli kwenye kituo cha mabasi cha Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Kondakta wa basi hilo ambalo linafanya safari zake kati ya
Dar es Salaam na Arusha alijikuta matatani baada ya basi lake kuzuiliwa na
kurejesha nauli ambazo zilikuwa zimezidi kwa abiria 19.
Baadhi ya abiria ambao waliongea na waandishi wa habari
kuhusiana na kuzidishiwa nauli kati yao ni Nagi Nurdin aliyekuwa akienda Moshi alisema
kuwa yeye alikatiwa nauli kwa shilingi 29,000 badala ya shilingi 22,700 ambapo
alikata kwenye ofisi za basi hilo.
Naye Forida Faustin alisema kuwa yeye naye alikuwa akienda
Moshi alitozwa 33,000 huku YUda Nduti akitozwa 30,000 ambapo walianza kumtajia
nauli ni shilingi 40,000.
Kwa upande wake ofisa mfawidhi wa SUMATRA Pwani Iroga Nashon
alisema kuwa hatua ya kwanza waliyoichukua ni kumwamuru kondakta wa basio hilo
lenye namba T 600 APN kuwarejeshea nauli zilizozidi abiria hao.
“Baada ya kurejesha nauli zilizozidi ambazo zilikuwa ni zaidi
ya 300,000 pia tuliwapiga faini ya shilingi 250,000 kwa kosa hilo kwa
kuzingatia kifungu cha sheria cha 34 na ndipo tuliporuhusu basi hilo kuendelea
na safari yake,” alisema Nashon.
Kwa upande wake kondakta wa basi hilo hakuwa tayari
kuzungumza na waandishi na kusema kuwa yeye siyo msemaji ambapo alidai abiria
hao walikatiwa tiketi stendi ya Ubungo.
Nashon aliwataka abiria kutoa taarifa kuhusiana na wamiliki
au makondakta na madereva kuwanyanyasa kwa makusudi huku wakijua sheria za
uendeshaji wa mabasi hayo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wanaokiuka.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari la
kunyanyulia vitu vizito (Crane) ikiwemo magari yanayoharibika kwenye barabara
za mkoa huo.
Chanagamoto hiyo ilionekana juzi baada ya magari kukwama kwa
zaidi ya saa tano baada ya magari mawili kuharibika kwenye daraja
linalounganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam eneo la Kiluvya wilayani
Kibaha.
Magari yaliyoharibika ni ya mizigo ambapo la kwanza ni Scania
namba T 503 DTJ na Fuso lenye namba za usajili T 515 DSA magari haya yaliziba
kabisa barabara hivyo kusababisha magari kushindwa kuingia wala kutoka kwa muda
huo.
Akizungumza kwenye eneo la tukio hilo kamanda wa polisi wa kikosi
cha usalama barabarani wa mkoa huo Nasoro Sisiwaya alisema kuwa ilibidi watumie
nguvu ya ziada kuliondoa gari moja ili magari yaweze kupita kwani lori kubwa
liliharibika katikati ya daraja la mto Mpiji.
“Kwa kweli gari la kunyanyua vitu vizito ni changamoto kubwa
kwani magari yanayo anguka au kupata ajali yanashindwa kuondolewa kwa wakati
kutokana na kukosa huduma ya gari hilo,” alisema Sisiwaya.
Sisiwaya alisema kuwa tayari wameshaiomba serikali na wakala
wa barabara TANROADS ili wanunue gari hilo na liwe hapa Kibaha kwani kutegemea
litoke Dar es Salaam ni tatizo kubwa.
“Tumeandika sehemu husika kuomba gari hilo ili kukabiliana
kwani tukio hili limesababisha usumbufu mkubwa sana kwa magari yanayopita barabara
hii ya Morogoro ambayo ndiyo mlango wa kuingilia na kutoka Dar es Salaam.
Aidha alisema wataiomba TANROADS kujenga barabara mbadala
kwani kutegemea barabara moja ni tatizo kubwa na kutokana na tukio hili tumeona
jinsi gani watu walivyohangaika na kusababisha usumbufu mkubwa.
Mwisho.