Friday, October 6, 2023
MKOA WA PWANI KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI
Thursday, October 5, 2023
JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI MKOA WA PWANI LATOA TAHADHARI MVUA ZA EL NINO
*TAARIFA YA KAMANDA WA ZIMAMOTO PWANI ALIPOKUWA MGENI RASMI MAHAFALI YA 16 SHULE YA SEKONDARI KWALA - KIBAHA*
KAMANDA wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Pwani SSF Jenifa Shirima kuwakumbusha wananchi kuzingatia tahadhari zinazoendelea kutolewa kuhusu uwezekano wa kunyesha mvua kubwa za Elninyo.
Shirima ameyasema hayo alikpokuwa mgeni rasmi Mahafali ya 16 ya Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kwala iliyopo Kata ya Kwala Wilaya Kibaha na kuwataka watu wote wanaoishi maeneo hatarishi kuondoka kabla ya mvua hizo kuanza kunyesha ili kuepuka madhara.
Aidha amewaahidi kwamba atahakikisha changamoto walizoainisha atazifikisha sehemu husika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi ambapo alitoa mchango wake fedha taslimu, vifaa vya kuzima na kung’amua moto kwa uongozi wa shule hiyo.
Pia alitoa zawadi za vifaa vya ki taaluma kwa wanafunzi wahitimu na Wanafunzi Skauti ambapo alipata nafasi ya kugawa vyeti kwa wahitimu pamoja na walimu na wanafunzi waliofanya vizuri zaidi.
NSSF YAPIGA VITA VITENDO VYA RUSHWA
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoani Pwani, imetoa rai kwa Mtumishi ama Mtendaji yeyote anaejihusisha na vitendo vya rushwa kuacha mara moja vitendo hivyo kwani vinachangia kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wateja.
Akifungua maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kimkoa, Meneja wa NSSF Mkoani Pwani, Witness Patrick ,amesema wanashirikiana na Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa (TAKUKURU) kudhibiti mazingira ya vitendo vya rushwa kwenye maeneo ya kazi.
Amewaasa ,kila mmoja kujitathmini na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya rushwa ili kudumisha imani kwa wanachama na wadau.
Witness ameeleza kuwa, mfuko hautamvumilia mtendaji yeyote atakaeshindwa kuendana na viwango na kasi ambayo mfuko unatarajia kuifikia.
Anasema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapinga rushwa kwa vitendo, na Nssf inaunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kukemea masuala yote ya rushwa.
Vilevile Witness amewahimiza ,watumishi na wananchi wema kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotendeka katika maeneo yao ya kazi kwani kutokutoa taarifa ni kushiriki rushwa.
Halikadhalika," anawasihi kutumia mfumo mpya wa NISS katika kuandikisha wanachama wengi zaidi wa mfumo wa kujichangia kwa hiari ili kuongeza wigo wa kinga ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi.
Naye mwanachama wa Nssf Kibaha, Vicent Ndumbili ameipongeza Nssf kwa kujali wateja wake.
Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ilianzishwa rasmi kimataifa mwaka 1984 kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja na juhudi za wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wateja ambapo mwaka huu 2023 yanaanza octoba 2-octoba 6 kilele.
Mwisho
TCCIA INVESTMENT KUONGEZA MTAJI KUFIKIA BILIONI 47
KAMPUNI ya TCCIA Investment inatarajia kuongeza mtaji wake na kufikia bilioni 47 kutoka bilioni 37 ambazo zimewekezwa kwenye masoko mbalimbali ya hisa.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Peter Kifungomali wakati akizungumza na wanahisa wa mkoa wa Pwani juu ya hisa walizowekeza.
Kifungomali amesema kuwa ongezeko hilo ni hadi itakapofika mwaka ujao wa fedha ambapo thamani imeongezeka kwa asilimia 53 kwa mwaka 2022.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa chemba ya wafanyabiashara ya TCCIA Mkoa wa Pwani sehemu ya biashara Fadhili Gonzi amesema kuwa baadhi ya wanahisa walikuwa na maswali mengi juu ya fedha zao.
Naye mmoja wa wanahisa Ayubu Mtawazo amesema kuwa hisa ni moja ya sehemu salama ya kuwekeza fedha ambapo watu wengi wamenufaika.
Clara Ibihya amesema kuwa manufaa ya hisa ni makubwa kwani ukishawekeza fedha zako hupati tena usumbufu kutakiwa marejesho bali unasubiri kupata fedha.
Thursday, September 28, 2023
SHULE BORA YAWAJENGEA UMAHIRI UFUNDISHAJI SOMO LA HISABATI
KATIKA kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi wanapata uelewa wa somo la hisabati Mkoani Pwani Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Elimu Tanzania kupitia program ya Shule Bora imewapatia mafunzo walimu wa somo hilo.
Akizungumza Wilayani Kisarawe baada ya ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa elimu kuhusu uboreshaji ufundishaji na ujifunzaji wa umahiri wenye changamoto katika somo la hisabati Ofisa elimu Mkoani humo Sara Mlaki amesema kuwa mafunzo kwa walimu hao yatawajengea uwezo ili kupata mbinu bora za umahiri za ufundishaji wa somo la hisabati.
Aidha mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania kupitia Program ya Shule Bora ambayo inatekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara kwa Ufadhili wa Serikali ya Uingereza na kwa Usimamizi wa Cambridge Education.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na wawezeshaji kutoka vyuo vya Ualimu vya Tukuyu na Mpwapwa ambapo washiriki wa mafunzo hayo ni viongozi wa Elimu kutoka katika ngazi ya Mkoa wakiwemo Walimu, Walimu wakuu, Maofisa Elimu Kata, Maofisa Elimu Awali na Msingi kutoka katika Halmashauri tisa na shule teule za Wilaya ya Kisarawe.
Wednesday, September 27, 2023
SHULE SALAMA WAJADILI KUMLINDA MTOTO
TIMU YA NYUMBU YAENDELEA NA MICHEZO YA KUJIPIMA NGUVU YATOKA SARE 1-1 NA POLISI TANZANIA
TIMU ya Soka ya Nyumbu ya Mkoani Pwani inayojiandaa na ligi daraja la Pili imetoka sare ya goli 1-1 na timu ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Chuo Cha Polisi Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Nyumbu huo ni mchezo wake wa pili wa kujipima nguvu ambapo jana ilicheza na timu ya Mashujaa ya Mkoani Kigoma ambayo inashiriki ligi Kuu ya NBC Premium League ambapo pia ilitoka sare ya kufungana goli 1-1 kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya michezo hiyo kocha mkuu wa timu hiyo Rajab Gwamku amesema kuwa anafurahishwa na viwango vya wachezaji wake kupitia michezo hiyo ya kujipima nguvu waliocheza.
Gwamku amesema wataendelea kucheza michezo ya kirafiki zaidi ili kuiimarisha timu yake kabla ya kuanza kwa michezo ya ligi daraja la pili kwa kipindi itakapopangwa kuchezwa ligi hiyo.
Amewaomba Wanapwani kuiunga mkono timu yao ili iweze kufanya vyema kwenye ligi daraja la pili na kupanda daraja la kwanza huku malengo yakiwa ni kupanda ligi kuu ili kuuwakilisha vyema mkoa huo.