Tuesday, January 17, 2023

CHONGOLO ATAKA VIJANA KUSHIRIKI KUJIKWAMUA KIUCHUMI

 

CHONGOLO ATAKA VIJANA WAJENGEWE FIKRA ZA KIUCHUMI

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka viongozi wa vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika kuleta msukumo wa kuwajengea uwezo vijana kifikra na kiuchumi.

Chongolo meyasema hayo kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani wakati akifungua kikao kazi cha makatibu wakuu wa vyama rafiki wanaounda kamati ya usimamizi wa shule hiyo. 

Chongolo amesema kuwa Ukombozi wa nyuma ulikuwa ni wa kujikomboa kutoka kwa wakoloni lakini kujikomboa kwa sasa ni kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kifikra.

"Makatibu Wakuu  kutoka nchi sita marafiki  wanapaswa kudumisha uzalendo ulioasisiwa na viongozi waliotangulia ambao waliweka misingi ya ushirikiano,"alisema Chongolo. 

Aidha amesema kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan anawakaribisha nchini huku akiwawakikishia usalama wao kwa muda wote watakaokuwa hapa nchini hadi watakaporudi makwao.

"Mwaka jana tulipokutana tulijadili mambo mengi kwa kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao sasa leo tumekutana ili tuweze kuchakata  kwa kina yale yote tuliyojadili,"amesema Chongolo.  

Naye Katibu Itikadi na Uenezi CCM Sophia Mjema amesema kuwa kila kitakachokifanyiwa maamuzi  kitajengwa katika sura ya umoja kama ulivyojengwa  katika  historia ya nchi hizo rafiki.

Vyama hivyo vilivyoshiriki ni CCM Tanzania, ZANU PF Zimbabwe, FRELIMO Msumbiji, MPLA Angola, SWAPO Namibia na ANC Afrika Kusini.


Sunday, January 8, 2023

WATANO WAFA AJALINI



WATANO WAFA 10 WAJERUHIWA AJALINI

WATU watano wamefariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster na gari la mizigo aina ya Mitsubishi Canter.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa majeruhi wako hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa matibabu zaidi.

Lutumo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Januari 8 mwaka huu majira ya saa 1:40 asubuhi eneo la Mwavi kata ya Kiwangwa Wilayani Bagamoyo ambapo watu watano wamefariki eneo la ajali huku 10 wakijeruhiwa.

Alisema kuwa basi hilo dogo lenye namba za usajili T 972 DCY lililokuwa likitoka Bagamoyo kwenda Morogoro liligongana na lori dogo lenye namba za usajili T 168 CAZ.

"Katika ajali hiyo waliofariki wanawake wawili na wanaume watatu ambapo majina yao bado hayajafahamika ambapo maiti na majeruhi wako hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo,"alisema Lutumo.

Chanzo cha ajali Coaster lilikuwa linapita gari lingine bila tahadhari na kugongana na gari lingine kusababisha ajali hiyo.

"Madereva wanapaswa kuchukua tahadhari ili kuepuka ajali zisizo za lazima kwa kufuata sheria bila shuruti kwa kuzingatia usalama wao na wengine,"alisema Lutumo.

Mwisho.

Thursday, January 5, 2023

WANAFUNZI WASIYO RIPOTI SHULENI KUTAFUTWA


WANAFUNZI WATORO JIJINI DODOMA KUTAFUTWA WARUDI MASHULENI.

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MKUU wa mkoa wa Dodoma Rosemary Sinyamule amewataka viongozi wa kata, walimu, wazazi na walezi kushirikiana kuwatafuta wanafunzi ambao hawataripoti shuleni baada ya siku 90 mara shule za sekondari zitakapofunguliwa watatafutwa na kurudishwa shuleni.

Ameyasema leo katika kikao kazi kilichojumuisha maofisa elimu wa Wilaya za wa Mkoa pamoja na walimu wa wilaya zote Jijini Dodoma.

Sinyamule amesema kuwa zipo changamoto nyingi ambazo zinapelekea watoto kutokufika shuleni kama watoto kupelekwa kwenda kufanya kazi za ndani pamoja na changamoto za kimaisha zilizopelekea mtoto kutokufika shule.

Amesema kuwa mpaka Sasa wanafunzi 4,000 tayari wamepatikana na hivyo wataaza masomo yao muhulah uu wa mwaka 2023 huku akisisitiza kuwa Halmashauri zote Dodoma kuhakikisha wanafunzi wanasajiliwa kwa asilimia 100.

Amewataka walimu kuwapokea wanafunzi hata wale ambao hawana sare za shule ila watoe taarifa kwa watendaji wa kata au Kijiji kwa lengo la kuwahimiza wazazi au walezi kutimiza majukumu yao huku watoto wakiendelea na masomo.

Kwa upande wake Mkurugezi wa elimu ofisi ya Rais (TAMISEMI) amesema kuwa watahakikisha kupitia mkutano huo wa kupeana maelekezo na utekelezaji wataenda kuimarika katika nafasi zao pamoja na kuhakikisha wanafanya vizuri katika sekta ya Elimu.

DKT BITEKO ASISITIZA UONGEZAJI THAMANI MADINI

Dkt. Biteko asisitiza wadau kuwekeza uongezaji thamani madini

WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Serikali iko mbioni kuanzisha upya Minada ya Madini ya Vito ili kuleta wanunuzi wakubwa, wafanyabiashara na wachimbaji wa madini hapa nchini.

Hayo yamebainishwa Januari 5, 2023 wakati akizindua duka la utalii wa madini la kampuni ya Tanzanite Experience katika eneo la Manyara Kibaoni wilaya ya Karatu Mkoani Arusha 

Amesema kupitia mnada huo kampuni ya Tanzanite Experience kupitia duka la utalii wa madini itapata madini mengi kwa ajili ya kuendeleza kituo hicho na maeneo mengine anayoyafanyia kazi.

Dkt. Biteko amesema kuwa, kupitia kituo hicho kilichopo katika ukanda wenye maeneo ya hifadhi imekuwa ni sehemu kubwa ya kivutio cha utalii kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi. 

"Madini ya Tanzanite yamekuwa yakinunuliwa hapa nchini kwa kiasi kikubwa na watalii wanaokuja kutembelea hifadhi zetu na kupitia wao madini haya yanaendelea kutangazwa duniani," amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, Wizara ya Madini inapongeza uwekezaji huo ambao umefanywa kwa asilimia 100 na watanzania wakiunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan wakati akitangaza vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini kupitia filamu ya "The Royal Tour" ambapo utalii na madini ya Tanzanite ilikuwa miongoni wa vivutio hivyo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema wizara inahamasisha uwekezaji wa namna hiyo ambao unaunga mkono moja kwa moja jitihada zinazofanywa na Serikali za kutangaza madini ya Tanzanite duniani hususan katika eneo la shughuli za uongezaji thamani.

"Duka hili linatarajia kuuza bidhaa mbalimbali za madini ya Tanzanite na Tsavourite ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikitengenezwa na kuuzwa nje ya nchi. Hii ni hatua kubwa ambayo nchi yetu inaendelea kuchukua katika kuhakikisha madini haya yanazalishwa hapa nchini," ameongeza Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko ametoa wito kwa watu wote ambao wana nia ya kuwekeza kwenye uchongaji, ukataji wa madini kuwekeza kwenye uongezaji thamani wa madini ili madini hayo yaweze kutupatia ajira na kodi kubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzanite Experience Hassinne Sajani amesema kuwa, duka hilo limekuwa kivutio kikubwa kwa watanzania na watalii kutoka nje ya nchi ambao wananunua bidhaa za madini zilizopo. Aidha ameongeza kuwa, kampuni imeajiri wafanyakazi 80 na zaidi ya asilimia 80 ni wakazi wa maeneo ya Manyara Kibaoni.

Ameahidi kuongeza juhudi kuendelea kutangaza madini ya Tanzania ambayo ni zawadi kwa Watanzania ili madini hayo yaweze kupanda thamani duniani.

Kwa upande wake, Meneja wa Tanzanite Experience, Junaid Khan amesema kuwa, zaidi ya wageni 6000 wamefika kutembelea Kampuni ya Tanzanite Experience  

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba amesema biashara ya madini imefunguka katika wilaya ya Karatu na kuongeza mapato na kueleza kuwa ameipongeza kampuni hiyo kwa kutoa ajira zaidi ya 80 kwa watanzania katika nafasi mbalimbali.

Tuesday, January 3, 2023

DODOMA WAASWA UPANDAJI MITI



Na Wellu Mtaki, Dodoma

MKUU wa mkoa wa Dodoma Rosemary Sinyamule amewataka wazazi na walezi wahakikishe wanawapeleka watoto wao shuleni mara baada ya shule kufunguliwa.

Sinyamule ameyasema leo katika ziara ya Kampeni ya upandaji wa miti iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Chemba Jijini Dodoma.

Amesema kuwa zipo Sheria ambazo italazimika kuzifuata kuhakikisha kuwa mtoto anapata haki yake ya kwenda shule hivyo inapaswa wazazi na walezi watambue lengo na makusudi ya serikali ya awamu ya sita kwa watoto wa kidato cha kwanza.

Aidha amesema huku kuna umuhimu wa upandaji wa miti ili kurudisha uoto wa asili na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo kuna maelekezo ambayo yametolewa na serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha tunatunza mazingira.

Amebainisha kuwa hilo ni jukumu la kila mwanafunzi kuwa na mti wake shuleni ambao atautuza kwa kipindi chote awapo shuleni na wazazi watambue kama elimu ya vitendo.

Amezitaka shule kuanzisha miradi ambayo itawezesha shule kujikimu na chakula kwani imeonyesha moja ya njia ambazo zitapunguza utoro mashuleni ni pamoja na watoto kupata chakula.

Mwisho.

Friday, December 30, 2022

DOREFA YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA



DOREFA YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA 2022

Na Elizaberth Paulo, Dodoma.

VIONGOZI wa michezo na wanamichezo nchini wameaswa kupambania tasnia ya michezo ili iwe na thamani na kupewa kipaumbele kama tasnia zingine ili ichangiae katika ukuaji wa uchumi wa nchini kama nchi zilizowekeza kwenye michezo Duniani. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa michezo Nchini Ally Mayai Tembele wakati akizungumza na wadau wa soka kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Chama Cha Mpira wa Miguu Dodoma(DOREFA).

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuweka wazi mambo yaliyofanywa na kamati tendaji tangu kuingia madarakani pamoja na changamoto zilizowakumba katika utendaji wao.

Mayai amesema kuwa ili tasnia hii ya michezo iendelee kukua ni wajibu wa kila mwanamichezo kuwajibika kwa nafasi yake katika kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na Umuhimu wa michezo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya zetu hata uchumi wetu hii itasaidia kukua kwa tasnia hii bila kusahau kuwa na nidhamu kwa kila mmoja kumuheshimu mwenzake bila kujali cheo.

“Nawapongeza chama cha soka cha Mkoa wa dodoma kwa kuweza kufanya kazi bila kuwa na tofauti katika utendaji na hii itasaidia soka la Dodoma kuweza kukua kwa kasi kwani maendeleo bora huletwa na viongozi bora,"amesema Mayai

Ameongeza kwa kupongeza mkoa wa Dodoma kwa kuwa na programu ya vijana chini ya miaka 17 kwani itawasaidia vijana kukua kisoka na kuweza kuvumbua vipaji wakiwa bado na umri mdogo.

"Milango ya serikali ipo wazi kwa yeyote mwenye nia njema na tasnia hii na tunawakaribisha wadau wote kuweza kujitokeza kusapoti vipaji vya watoto wetu kwani kila mtu anaelewa mpira ni ajira kwa ajili ya kukuza uchumi na kuondokana na umasikini na kila mtu ameshuhudia namna ambavyo familia nyingi zimejikwamua kiuchumi kupitia michezo,"amesema Mayai.

Aidha ametoa rai kwa wadau wa mpira wa miguu kupambania haki za watoto katika kupata maeneo ya wazi ya watoto hao kufanyia mazoezi ya michezo yao ikiwa ni haki ya msingi ya mtoto na serikali imetoa maeneo ya wazi katika kila mtaa kwaajili ya michezo na shughuli zingine za kijamii.

“Ndugu zangu wanamichezo tuingie mitaaani kwenda kusaka vipaji, tukaelimishe jamii kuhusiana na haki za watoto wetu katika suala zima la michezo alafu kuna maeneo ya wazi ambayo hayatumiki kwa kazi zilizopangwa sasa hili nawaachia fuatilieni maeneo ya wazi kwaajili ya hiyo michezo alafu huko mitaani ndiko kwenye chimbuko la mpira wa miguu na hata historia ya watu wengi maarufu waliofanikiwa kwenye soka historia yao inaonyesha wametokea mitaani,"amesema Mayai

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Dodoma (DOREFA) Mohamed Aden amesema kuwa anawashukuru wadau wa soka jijini hapa kwa kuendelea kutoa maoni na ushauri ili kuhakikisha wanaboresha sekta ya michezo haswa mpira wa miguu jijini Dodoma.

Naye mwakilishi wa wanamichezo Jijini Dodoma amesema sekta ya michezo iko vizuri ila wanaiomba serikali chini ya Waziri wa Michezo Mohamed Mchengerwa kuwatatulia changamoto inayojitokeza ya mara kwa mara ya uwanja wa Jamhuri kufungiwa mara kadhaa kutokana na matumizi mengine ambayo ni tofauti na michezo hivyo kufanya wapenzi wa soka Jijini hapa kukosa burudani ya mpira wa miguu na kutumia viwanja vingine vilivyopo nje ya Dodoma.


Friday, December 23, 2022

RAIS DK SAMIA ATOA VYAKULA VITUO VYA WATOTO

RAIS DK SAMIA ATOA ZAWADI VYAKULA KWA NYUMBA MALEZI YA WATOTO MKOA WA PWANI

Na John Gagarini Kibaha

RAIS wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi vyakula vya sikukuu ya Christmas na mwaka mpya makundi maalumu ili nao washerehekee kama walivyo watoto wanaoishi na wazazi.

Akimwakilisha Rais kukabidhi katika kituo cha kulelea watoto wanaoishi kwenye Mazingira magumu cha Makao ya Malezi Madina kilichopo Mtaa wa Vikawe kata ya Pangani Wilaya ya Kibaha Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema kituo hicho kinawakilisha vituo 37 vilivyopo mkoa mzima.

Kunenge alisema kuwa Rais kwa kutambua makundi maalum ametoa zawadi hizo ili watoto hao washeherekee kama watakavyosheherekea wengine ambao wanaishi kwa furaha na familia zao.

"Nimekuja hapa kumwakilisha Rais wetu  amewaletea zawadi pamoja na salamu za sikukuu ya Christmas na mwisho wa mwaka ambapo amewaletea mbuzi wawili, mchele kilo 60, maharage kilo 40, mafuta lita 20, juisi na viungo mbalimbali,"alisema Kunenge.

Alisema kuwa wadau wa maendeleo na wenye uwezo kujenga tabia ya kujitolea kwa vituo vya watoto wenye mahitaji ambapo vitu vilivyotolewa ni pamoja na vitoweo ,mchele , maharage,mafuta ya kupikia ,vinywaji na viungo vingine mbalimbali vya kupikia.

Kwa upande wao watoto wa Makao ya Madina Zainab Athuman na Jumanne Manzi walimshukuru Mungu kwa kumwezesha Rais kupata na kuweza kuwapa zawadi hizo.

Naye Mlezi wa watoto Makao Malezi ya Madina Fatma Abdilai alisema kuwa wananchi waendelee kumuombea Rais Samia kwa mengi anayofanya nchini na kutekeleza ilani kwa kutambua makundi maalum.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka alimshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk Samia kwa kuitendea haki ilani ya Chama na kujali watoto .

Mkoa huo una jumla ya makao ya malezi 37 yenye jumla ya watoto 1,301 na kituo hicho cha Madina kina watoto 30.


Mwisho