Thursday, July 27, 2017
POLISI PWANI WAKAMATA VIFAA VYA UVUVI HARAMU
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia Makamba Sixbert (32) na Doto Mwinyi (45) wakazi wa Mlingotini wilayani Bagamoyo kwa tuhuma za kukutwa na vifaa vya uvuvi haramu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa watu hao walikamatwa kwenye msako.
Shana alisema kuwa mtuhumiwa Sixbert na Mwinyi walikamatwa Julai 25 majira ya saa 8 usiku maeneo ya Mlingotini kata ya Zinga baada ya msako maalumu wa makosa mbalimbali ukihusisha askari wa Jeshi la polisi wilaya ya Bagamoyo, Polisi Makao makuu, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na maofisa uvuvi na mifugo wa wilaya hiyo.
“Mtuhumiwa huyo wa kwanza alikutwa na Scoopy Net moja, vioo vya kuogelea vitatu, mitarimbo mitatu, bunduki moja ya kuulia samaki, mikuki ya kuulia samaki mitatu na viatu vya kuogelea (Slipers) pea tatu huku mtuhumiwa wa pili akishikwa na Cylinder Gas walivyokuwa wakivitumia kwenye uvuvi haramu,” alisema Shana.
Kwenye tukio lingine madereva wawili wa pikpiki Juma Ally (37) na Mduga Agustino (25) kwa tuhuma za kupatikana na mitambo mitano ya kutengenezea pombe ya Moshi maarufu kama Gongo.
Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo limetokea Julai 25 majira ya saa tano asubuhi maeneo ya Lugoba kata ya Lugoba wilaya ya Kipolisi Chalinze wilayani Bagamoyo.
“Madereva hao wa pikipiki pia walikutwa na pombe ya Moshi lita 40 na lita 60 za Molasesi wakiwa wamezipakiza kwenye pikipiki yenye namba za usajili T 399 BHS aina ya Sanlg,” alisema Shana.
Aidha walifanikiwa kuwakamata Ahmada Hassan (45) mkazi wa Gogoni na wenzake watano kwa tuhuma za wizi wakiwa na Sabufa aina ya Kodec inayodhaniwa kuwa ni ya wizi.
Shana alisema watu hao walikamatwa maeneo ya Dunda kata ya Dunda Tarafa ya Mwambao wakituhumiwa kujihusisha na matukio ya uhalifu ikiwa ni pamoja na uporaji nyakati za usiku kwenye maeneo mbalimbali wilayani
“Misako wanayoifanya ni endelevu na askari shupavu wametawanywa kila kona kuhakikisha hali ya amani inakuwepo kwenye makazi ya wananchi na sehemu za biashara,” alisema Shana.
Aliwataka watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwa kutafuta shughuli nyingine za kufanya za kuwaingizia kipato halali kwani hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Mwisho
WAZIRI WA AFYA ARIDHIA MLANDIZI HOSPITALI WILAYA
Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amekubali maombi ya Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani kuwa Hospitali ya wilaya.
Alitoa tamko
hilo kwenye uwanja wa Mtongani Mlandizi wilayani Kibahya wakati akipokea
Magari mawili ya kubeba wagonjwa na vitanda vitatu vya kuzalishia mama
wajawazito kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa na gari
moja kutoka kwa Rais Dk John Magufuli.
Alisema kuwa
ombi lililotolewa na Mbunge huyo kwa viongozi wa ngazi za juu na kwake
amelikubali hivyo mganga mkuu wa wilaya anapaswa kuandika barua na kuzipeleka
sehemu husika kisha zifikishwe wizarani kwa ajili ya utekelezaji.
“Mbunge wenu
amekuwa akipigania kituo hichi kwa muda mrefu kama alivyosema hivyo naona
hakuna kipingamizi ili mradi tu taratibu zifuatwe ili kufikia hatua hiyo lengo
kubwa ni kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Mwalimu.
Awali mbunge
wa Jimbo hilo Hamoud Jumaa lisema kuwa maombi hayo alishayatoa kwa viongozi
mbalimbali ikiwemo kwa Rais wa Awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete na Rais Dk John
Magufuli.
Jumaa alisema
kuwa kituo hicho kwa sasa kinahudumia watu wengi tofauti na ilivyokuwa zamani
ambapo kwa sasa wanakaribia watu 100,000 hivyo kuna haja kabisa ya kuwa
hospitali ya wilaya.
“Tuliambiwa
tufanye maboresho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga jengo la upasuaji,
chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na kuweka uzio vitu vyote hivyo tayari
tumevifanya hivyo ombi letu hilo tunaomba ulifanyie kazi kwani tunaamini huduma
zitaboreka,” alisema Ummy.
Kwa upande
wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Beda Mmbaga alisema kuwa
watahakikisha wanaboresha mahitaji yote yanayotakiwa ili kutoa huduma za ubora
kwa wananchi wanaokwenda kuhudumiwa hapo.
Mwisho.
Wednesday, June 28, 2017
WAWILI WAUWAWA KWA RISASI KIBITI
Na John Gagarini, Pwani
WATU wasiofahamika wameendelea kufanya mauaji wilayani Kibiti ambapo wamewaua viongozi wawili wa Kijiji cha Mangwi kata ya Mchukwi kwa kuwapiga.
Viongozi waliouwawa ni pamoja na Michael Nicholaus Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi na mtendaji wa Kijiji hicho Shamte Makawa.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 27 majira ya usiku kwenye Kijiji hicho na watu hao baada ya kufanya tukio hilo walichoma nyumba moto kisha kutoweka.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri kutokea na kusema kuwa bado wanaendelea kufuatilia ili kuwabaini wahusika wa matukio hayo.
Mwisho.
Tuesday, June 20, 2017
DK MAGUFULI AWATAKA VIONGOZI WASIOWAJIBIKA WAJIONDOE
Na John Gagarini, Kibaha
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli amewataka
viongozi mbalimbali ambao wanashindwa kwenda na kasi ya awamu ya tano
wajitathmini kwa kujiondoa wenyewe endapo watashindwa kuwajibika.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Bwawani wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Dk Magufuli alisema kuwa kiongozi ambaye ndani ya miezi kadhaa hadi mwaka hajui alichokifanya ni vema akajiondoa mwenyewe na asisubiri kuondolewa.
“Serikali ya awamu huu ni ya uwajibikaji na si kutaka kufaidi ukubwa kufanya kazi lengo kubwa likiwa ni kuwatumikia wananchi hasa wale wanyonge ambao wanahitaji huduma zetu kwa kuwatumikia,” alisema Dk Magufuli.
Alisema kuwa kwa sasa tumeweka utaratibu wa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na si matumboni bali ziguse maslahi ya wananchi wengi.
“Fedha hizo si matumboni, semina wala posho au safari za nje ambapo nimepata mialiko zaidi ya 50 ya nje ya nchi lakini nimekataa kwenda nataka kwanza tunyooshane wenyewe kwanza maana nikitoka watajisahau,” alisema Dk Magufuli.
Aidha alisema kuwa baadhi ya viongozi waliotumia vibaya rasilimali atapambana nao kwani Tanzania haiwezi kuwa nchi maskini kwani ni nchi ya pili duniani baada ya Barazili kwa nchi zenye rasilimali nyingi duniani.
“Tunakila aina ya madini, wanyama, maji, maziwa na mlima mrefu Afrika haiwezekani kuwa wasindikizaji wa matarajiri na sisi ni matajiri haiwezekani watu wale mlo mmoja, wanakosa dawa na huduma nyingine hii haiwezekani tutahakikisha wananchi wanaishi maisha yanayoendana na hali halisi ya mali zetu naombeni mniombee,” alisema Dk Magufuli.
Alisema ataendelea kutumbua ambapo kwa sasa wachache wanalalamika na kulia ni wale waliokuwa wakijinufaisha huku wengi wakiumia huku wengine wakijinufaisha.
Alisema kuwa baadhi ya viongozi walishiriki kuhujumu nchi kwa kuingia mikataba mibovu hasa kwenye upande wa umeme ambapo baadhi ya walidiriki kusaini mikataba mibovu.
“Kwa sasa tuna mipango ya umeme wa uhakika ambapo nilipokwenda Ethiopia nilikutana na waziri mkuu nilimuuliza anafanyaje kupata umeme wa uhakika na kuuza nje tuliongea mengi na sasa wataalamu wake watakaja kwa ajili ya kuweka mazingira ya upatikanaji wa umeme wa uhakika,” alisema Dk Magufuli.
Akizungumzia kuhusiana na mauaji yanayoendelea wilaya za Kibiti na Rufiji alisema kuwa serikali ya awamu hii si ya kuchezea kwani wanaohusika wataona moto kwani watashughulikiwa kikamilifu.
“Tutawanyoosha na tayari tumeanza kuwanyoosha wanafikiri watapita hawatapita kikubwa kinachotakiwa ni wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu hao kwani baadhi ni ndugu jamaa na marafiki na kuendelea kuwaficha ni kujicheleweshea maendeleo ambapo kwa sasa wilaya hizo hazina viwanda kutokana na mauaji hayo,” alaisema Dk Magufuli.
Alibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana kwenye uongozi wake ni pamoja na makusanyo kuongezeka kutoka bilioni 880 na kufikia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi ambapo fedha hizo zimeweza kulipa elimu bure, pensheni ambazo hazikulipwa tangu mwaka 2010.
“Tumeweza kulipa madeni ambayo yalifikia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 sasa yaliyobaki ni bilioni mbili ambapo tutaendelea kulipa madeni hayo kwa watu mbalimbali wanaodai halali na siyo madeni hewa,” alisema Dk Magufuli.
Alibainisha kuwa kutokana na makusanyo hayo serikali imeweza kufuta ada kwenye shule za msingi na sekondari ambapo kwa sasa zinatolewa kiasi cha shilingi bilioni 81.7 kwa ajili ya uendeshaji wa shule.
“Kutokana na elimu bure idadi ya wanafunzi wa darsa la kwanza wanaoandikishwa kwenye shule ya msingi wamefikia milioni mbili toka milioni moja na wanaojiunga na shule za sekondari wamefikia asilimia 27 huku mikopo ya elimu ya juu ikiongezeka toka watu 95,000 hadi 125,000 na bajeti kwa sasa ni bilioni 483,” alisema Dk Magufuli.
Aliupongeza mkoa wa Pwani kuwa na viwanda vingi ambapo na kuwa moja ya mikoa ambayo imetekeleza agizo la kuwa na viwanda ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kuvutia uwekezaji.
Awali akimkaribisha Rais Dk Magufuli mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kwa sasa mkoa una viwanda 371 huku zaidi ya 80 vikiwa ni vikubwa na vya kati na vidogo 260.
Ndikilo alisema hata hivyo pamoja na mafanikio hayo changamoto kubwa ni upungufu wa umeme ambapo mahitaji ni megawati 60 lakini zinazopatikana ni 40, maji yasiyo na uhakika, baadhi ya maeneo kutokuwa na nishati ya gesi na baadhi ya barabara kutokuwa na lami.
Mwisho.
Monday, April 3, 2017
WATUHUMIWA UHALIFU WALIOVALIA HIJABU WAUWAWA NA POLISI
Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu waliokuwa
wamepakizana kwenye pikipiki moja wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu wakiwa
wamevalia hijabu wameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kukaidi amri
ya kutakiwa kusimama.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake mjini Kibaha Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga
alisema kuwa pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa kukimbia.
Lyanga akielezea juu ya tukio
hilo alisema kuwa lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya saa 12:00 mchana eneo
la kizuizi cha Mwembe Muhoro wilaya ya Rufiji mkoani Pwani barabara kuu ya Dar
es Salaam Lindi.
“Siku ya tukio askari walipata
taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini
zikiwa zimebeba watu watatu kila moja huku miongoni mwa pikipiki hizo kati yake
mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.
Alisema kuwa askari wa
barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na kuwasimamisha ili
wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi
cha Ikwiriri lakini walikaidi kusimama.
“Baada ya hapo walifika kizuizi
cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo
walipofika kituo cha Muhoro hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria
wakiwa kwenye gari waliwafuatilia wakijaribu kuwafuatilia na wakavuka daraja la
Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga risasi hewani,” alisema Lyanga.
Aidha alisema kuwa baada ya hapo
watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza kukimbilia msituni na ndipo askari
walipowapiga risasi za miguu na kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.
“Majeruhi hao walijulikana ni
wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki
yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi ambapo watu
hao wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha
Hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.
Lyanga alisema kuwa walipofikishwa
hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia ambapo hata
hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili zilitoroka
na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili wawakamate.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu
pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa
jeshi hilo limeimarisha doria katika kukabiliana na uhalifu.
Mwisho.
Tuesday, March 28, 2017
MBUNGE AZINDUA UJENZI WA UZIO WA KITUO CHA AFYA
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akionyesha shehena na saruji mifuko 500 kwa ajili ya uzio wa Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani |
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akiwa amebeba saruji ambayo itatumika kwenye ujenzi wa uzio wa kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani |
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akizindua ujenzi wa uzio wa Kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani |
Na John Gagarini, Kibaha
KITUO cha Afya cha Mlandizi kimeanza mchakato wa
kuelekea kuwa Hospitali ya wilaya kwa kuanza ujenzi wa uzio ambapo Mbunge wa
Jimbo la Kibaha
Vijijini wilayani Kibaha mkoani Pwani Hamoud Jumaa amewataka
wafadhili mbalimbali kujitokeza kusaidia ujenzi wa uzio huo ambao utagharimu kiasi
cha zaidi ya shilingi milioni 200.
Akizungumza na waandishi wa habari Mlandizi wakati
akizindua ujenzi huo mbunge huyo alisema kuwa wameanza kuboresha huduma
zinazotolewa kituoni hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uzio huo ikiwa ni moja
ya vigezo vinavyotakiwa kufikia hadhi hiyo.
Jumaa alisema kuwa Kituo hicho cha afya ni tegemeo
kubwa kwa wakazi wa Jimbo hilo ambalo kwa sasa lina wakazi 70,000 na wilaya
jirani za Bagamoyo na miji ya Chalinze na Kibaha wanapata huduma hapo.
“Mpango huu nimeuanzisha kwa jitihada zangu binafsi
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo hadi sasa nimepata mifuko 500 ya
saruji, kokoto lori saba mchanga, mchanga na tani moja ya nondo ambavyo
vitasaidia katika ujenzi wa uzio huu tunaomba wadau wengine waendelee
kutusaidia,” alisema Jumaa.
Alisema kuwa kutokana na kituo hicho cha afya kuwa
tegemeo kubwa kwa wameona kuna haja ya kuwa Hospitali ya Wilaya ili waweze
kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi watakaokuwa wanapata huduma hapo.
“Tumekubaliana vitongoji 26 na madiwani sita watoe
240,000 huku mfuko wa jimbo ukitoa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa ajili ya
tofali za uzio ambao utasaidia kuondoa uingiaji holela wa watu bila ya sababu
za msingi ndani ya eneo la Kituo cha afya,” alisema Jumaa.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mlandizi Eufrasia
Kadala alisema kuwa wataungana na Mbunge huyo kuhakikisha wanafanikisha ujenzi
huo ili kuboresha kituo hicho cha afya.
Kadala alisema kuwa kutokana na kutokuwa na uzio
kumekuwa na mwingiliano wa watu kuingia kiholela hasa kutokana na kituo hicho
kuwa jirani na makazi ya watu.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa
Mlandizi Tatu Jalala alisema kuwa waliupokea mkono mpango huo na kuupeleka kwa
jamii kwa lengo la kumuunga mkono mbunge wao.
Jalala alisema kuwa wanaendelea kuihamasisha jamii
ili iweze kuchangia ujenzi huo wa uzio ukamilike kwa wakati lengo likiwa ni
kufanikisha harakati za kuwa Hosptali ya wilaya.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)