Thursday, December 15, 2016
Wednesday, December 14, 2016
MSOGA KUJENGA UWANJA WA KISASA
Na John Gagarini, Msoga
MKOA wa Pwani unatarajiwa kuwa na uwanja wa kisasa ambao utasaidia kukuza soka la vijana na kuinua michezo kwenye mkoa huo ambao umepania kuwa moja ya mikoa itakayolea vipaji.
Uwanja huo unatarajiwa kujengwa kwenye Kijiji cha Msoga kata ya Msoga Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo na serikali ya watu wa China lengo likiwa ni kukuza sekta ya michezo kwa vijana kwenye mkoa na nchi kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kwenda kutembelea eneo ambalo litajengwa uwanja huo Dk Kikwete alisema kwamba uwanja huo wa wa mpira wa miguu utajengwa kwa ufadhili wa serikali ya watu wa china na kuongeza kuwa utakuwa ni mkombozi mkubwa katika kukuza na kuinua vipaji kwa vijana wadogo.
“Tumehamasisha wadau wa michezo kujenga uwanja lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba Tanzania katika siku za usoni inakuwa ni wachezaji wengi wenye vipaji ambao wataweza kuunda timu nzuri ya Taifa ambayo itaweza kufanya vizuri katika mashindano mbali mbali ya Kimataifa,” alisema Dk Kikwete.
“Uwanja huu wa mpira wa miguu pindi utakapokamilika utaweza kuwa ni mkombozi mkubwa wa vijana wadogo hususan wale wa shule, hivyo nimeshazungumza na rafiki zetu wa serikali ya china na wamekubali kutujengea kwa hivyo ni jambo la msingi sana katika kuendeleza sekta ya michezo kwa watoto wetu hawa mbao wataweza kuleta mafanikio makubwa katika siku zijazo,”allisema Kikwete.
Dk Kikwete alisema kuwa anaipongeza serikali ya china kwa kuona umuhimu wa kusaidia kujenga kiwanja hicho, na kuongeza kuwa pindi kitakapokamilika kitakuwa na michezo mingine ambayo itakuwa ikifanyika mbali na mchezo huo wa soka lengo ikiwa ni kuwapa fursa vijana kuweza kuonyesha vipaji walivyonavyo.
Naye Mwakilishi wa balozi wa China nchini Tanzania Yang Tong aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kukuza sekta ya michezo hususani kwa vijana wadogo ikiwa ni sambamba na kujenga viwanja ili watoto wasiweze kucheza katika viwanja vya vumbi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kwamba lengo lake kubwa ni kuhakikisha anakuza michezo wa vijana wadogo katika jimbo lake hivyo kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kutaweza kuwasaidia vijana kukuza vipaji vyao.
Nao baadhi ya wadau wa mchezo wa soka katika kijiji hicho cha Msoga akiwemo Michael James pamoja na Mohamed Halfan wamempongeza Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete kwa ubunifu wa ujenzi huo wa uwanja kwa ajili ya vijana wadogo kwani kutaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko chanya katika michezo ukiwemo wa soka.
Mwisho.
CCM WAANZA MCHAKATO WA KUMPATA MGOMBEA UDIWANI MISUGUSUGU
Na John Gagarini, Kibaha
RAMADHAN Bogas ameshinda kura za maoni za kumpata mgombea udiwani kata ya Misugusugu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupata kura 43 huku aliyeshinda udiwani kabla ya mahakama kutengua matokeo Addhu Mkomambo akiambulia kura mbili.
Uchaguzi huo ambao ulifanyika Misugusugu ulisimamiwa na Yusuph Mbonde, Selina Wilson na Mohamed Mpaki ambao ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya, ulihusisha wagombea saba.
Akizungumza na waandishi wa habari katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa kura zilizopigwa zilikuwa 115 na hakuna kura iliyoharibika.
Mdimu akitaja matokeo alisema kuwa mshindi wa pili alikuwa Eliasi Masenga aliyepata kura 37, Ramadhan Mataula aliyepata kura 15 huku Salumu Mkali akipata kura 14, huku watano akiwa Mkomambo aliyepata kura mbili, Francis Alinamiswe alipata kura mbili na Laurence Likuda naye kura mbili.
Alisema kuwa bado vikao mapendekezo vinaendelea kukaa ambapo jana kilitarajiwa kukaa kikao cha kamati ya siasa ya kata ambapo leo kikao cha kamati ya Usalama na maadili wilaya kinakaa.
“Desemba 16 kamati ya siasa ya wilaya itakaa na baadaye vitaendelea vikao vya mkoa na Desemba 19 Halmashauri Kuu ya mkoa itafanya uteuzi wa mwisho wa mgombea atakayekiwakilisha chama kwenye uchaguzi huo,”alisema Mdimu.
Uchaguzi huo mdogo wa udiwani unarudiwa baada ya mahakama ya mkoa kutengua matokeo kutokana na malalamiko yaliyotolewa na diwani wa Chadema ambapo mgombea wa CCM Addhu Mkomambo alikuwa ameshinda.
Mwisho.
Monday, December 5, 2016
ZAIDI YA 15 WAFAULU DARASA LA SABA PWANI
Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya wanafunzi 15,528 mkoani Pwani wamefaulu
kwenda shule za sekondari kwa mwaka 2017 baada ya kufanya mtihani wa kumaliza
darasa la saba mwaka huu.
Aidha wanafunzi 9,290 wamefeli sawa na asilimia
37.4 na wanafunzi wote waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari
ambapo wamefaulu kwa kupata alama zaidi ya 100 kati yao 288 wamepata daraja la
A.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Kaimu ofisa elimu
mkoa wa Pwani Modest Tarimo wakati wa uchambuzi wa matokeo ya mtihani wa
kuhitimu eilimu ya msingi mwaka 2016 ya mkoa na kusema kuwa wanafunzi
waliofanya mtihani walikuwa ni 24,818.
Tarimo amesema kuwa wanafunzi 2,636 walipata daraja
B, wanafunzi 12,604 wamepata daraja C na wote waliopata daraja A na C wote
wamechaguliwa kujiunga na sekondari
Amesema kuwa wanafunzi waliokuwa wakitarajiwa
kufanya mtihani walikuwani 24,913 ambapo waliofanya walikuwa ni 24,818 wavulana
wakiwa ni 11,334 na wasichana walikuwa ni 13,484 sawa na asilimia 99.9.
Ameeleza kuwa ufaulu kwa mwaka huu umeshuka kwani
ni asilimia 62.5 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo ufaulu ulikuwa ni asilimia
63.1 matokeo haya hayaridhishi kwani ufaulu badala ya kupanda lakini umeshuka
kwa asilimia 0.5 na kwa matokeo hayo mkoa umeshika nafasi ya 21 kitaifa.
Amebainisha kuwa watahiniwa 95 hawakufanya mtihani
sawa na asilimia 0.3 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro,
wanafunzi 75, mimba mwanafunzi mmoja, vifo 11, ugonjwa wawili na sababu nyingine
sita ambapo wadau wanapaswa kupiga vita utoro ambao umepungua 204
ikilinganishwa na mwaka jana.
Kaimu ofisa elimu huyo wa mkoa ambaye ni ofisa
taaluma amesema serikali iliweka wastani wa asilimia 80 ya ufaulu kwa shule za
msingi ikiwa ni mkakati wa kufikia mpango wa matokeo makubwa sasa BRN ambapo
wadau wa elimu wanapaswa kukabiliana na changamoto zinaosababisha ufaulu
kushuka.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Edward
Mwakipesile amesema kuwa wadau wa elimu wanapaswa kushirikiana na idara ya elimu
ya mkoa ili kuhakikisha matokea ya wanafunzi yanakuwa mazuri ambapo kwa mwaka
huu yanaonekana kushuka.
Mwakipesile amesema kuwa mbali ya changamoto ya
matokeo hayo pia changamoto iliyopo ni vyumba vya madarasa ambavyo ni vichache
na kusababisha madawati kukosa sehemu ya kukaa baada ya zoezi la utengenezaji
madawati kufanikiwa.
Mwisho.
HALMASHAURI YA CHALINZE YAANZA KUMWAGA FEDHA KWA WAJASIRIAMALI
Na John Gagarini, Chalinze
HALMASHAURI ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani
Pwani imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 79.8 kwa vikundi vya
wajasiriamali 26 vya akinamama na vijana kwenye kata za Halmasahuri hiyo.
Aidha fedha hizo zinatokana na asilimia 10 ya
mapato ya Halmashauri ya robo mwaka ambazo ni kiasi cha shilingi milioni 809
yaliyokusanywa katika kipindi hicho.
Akikabidhi baadhi ya vikundi hivyo vya vijana na
akaimama kwenye kata ya Msoga ambapo kila kundi linapata asilimia tano kutokana
na mapato hayo Mwenyekiti wa Halmashauri Said Zikatimu alisema kuwa fedha hizo
zitakuwa zikitolewa kwa kila robo ya mwaka.
Zikatimu alisema kuwa lengo la kutolewa fedha hizo
kwanza ni kufuata sheria ambayo inataka asilimia tano ya mapato yote ya
Halmashauri wakopeshwe vijana na asilimia tano kwa ajili ya akinamama kupitia
vikundi vya vya uzalishaji mali.
“Tunaomba vikundi vyote ambavyo vinakopeshwa fedha
hizi wazirejeshe kwa wakati ili ziwe na mzunguko kwa watu wengine na vikundi
vihakikishe vinazitumia kwa malengo waliojiwekea na si kuanzisha miradi ambayo
hamjaombea mnaweza kushindwa kurejesha,” alisema Zikatimu.
Alisema kuwa fedha hizo siyo msaada bali ni fedha
kwa ajili ya kuboreshea shughuli za ujasiriamali na wanapaswa kurejesha kwa
wakati ili vikundi vingi viweze kupata fedha hizo ambazo zinatokana na mapato
ya ndani yanayotokana na vyanzo mbalimbali.
“Hizi fedha ni kwa ajili ya wananchi wote na hasa
wale waliojiunga kwenye vikundi hivyo zitumike kama zilivyoombewa na siyo
kununulia nguo au baadhi huzitumia kwa ajili ya kufanyia starehe mkifanya hivyo
mtaharibu maana ya mkopo huu na mtashindwa kurejesha na kujikuta mkishtakiwa,”
alisema Zikatimu.
Aidha aliyatakama makundi mbalimbali ya vijana na
akimama kujiunga na kuanzisha vikundi vingi kwa ajili ya kukopa kwani fedha si
tatizo bali ni wao kujiunga kwa wingi fedha ziko za kutosha.
Kwa upande wake ofisa maendeleo ya jamii na ofisa
vijana wa Halmashauri ya Chalinze Felista Kizito alisema kuwa vikundi hivyo
vilivyopewa fedha hizo vitapewa mwezi mmoja kabla ya kuanza kurejesha marejesho
yao.
Kizito alisema kuwa vikundi hivyo vimegawaanyika
kwenye shughuli mbalimbali kutegemeana na mazingira yao na vimepewa fedha kati
ya shilingi milioni mbili hadi sita kutegemeana na aina ya mradi ambao
waliuanzisha.
Naye diwani wa kata ya Msoga Hassan Mwinyikondo
alisema kuwa Halmashauri hiyo imefanya jambo kubwa kwa kutoa fedha hizo ambazo
zitasaidia kuboresha maisha ya wananchi.
Mwinyikondo alisema kuwa mikopo hiyo ya Hlamashauri
ni nafuu na haina masharti magumu kama ilivyo kwa taasisi za kifedha ambazo
watu wengi wameshindwa kukopa kutokana na masharti kuwa magumu.
Mwisho.
|
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Said Zikatimu katikati akiwakabidhi hundi kikundi cha ujasirimali cha Wanawake cha Nianjema cha ufugaji wa Mbuzi Kijiji cha Kwa Konje kushoto ni mwenyekiti wa Kijiji hicho Omary Mbwana anayefuatia ni diwani wa kata ya Kibindu Ramadhan Mkufya akifuatiwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii na Ofisa Vijana Halmashauri ya Chalinze Felista Kizito na mwenyekiti wa kikundi hicho Veronica Chusi |
Kushoto Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Said Zikatimu akiwakabidhi hundi ya fedha wana kikundi wa Muungano Mindukene kata ya Talawanda |
Friday, October 21, 2016
WALIBYA WASAIDIA MRADI WA MAJI MKURANGA
Na John
Gagarini, Mkuranga
WANANCHI
wametakiwa kuwa na utamaduni wa kulipa kodi mbalimbali za serikali ili ziweze
kutumika kwa ajili ya maendeleo kama wanavyofanya wananchi wa Libya.
Hayo yalisemwa wilayani
Mkuranga na mkurugenzi wa Taasisi ya World Islamic Call Society iliyopo chini
ya ubalozi wa Libya hapa nchini Ammara Zaiyani wakati akikabidhi mradi wa kisima
cha maji kwenye Kijiji cha Binga–Kisiju.
Zaiyani alisema
kuwa fedha ambazo zimesaidia ujenzi wa kisima hicho cha maji ya kunywa chenye
thamani ya shilingi milioni 18 zimetokana na kodi za wananchi wa Libya kwa ajili
ya kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali za kimaendeleo.
“Wananchi wa
Libya wanajitolea kuwasaidia wenzao hivyo na nyie mnapaswa kuwa na utamaduni wa
kuwasaidia wengine kupitia kwenye malipo mbalimbali ya serikali yenu ambayo ina
sema hapa Kazi Tu,” alisema Zaiyani.
Naye mwakilishi
wa Ubalozi wa Libya hapa nchini Mohamed Atoumi alisema kuwa serikali ya Libya
kupitia taasisi hiyo imekuwa ikipokea maombi mbalimbali na imekuwa ikisaidia
kadiri ya uwezo unapokuwepo.
Atoumi alisema
kuwa wamekuwa wakisaidia kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja kwenye huduma
za afya, maji na shughuli nyingine za maendeleo lengo likiwa ni kudumisha
ushirikiano uliopo na Tanzania.
Kwa upande wake
kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Sheikh Hamis Mtupa alisema kuwa wanashukuru kwa
msaada huo kwani umesaidia kuwaondolea adha wananchi wa Kijiji hicho ambao
walikuwa wakishinda wakitafuta maji ambayo siyo safi wala salama.
Mtupa alisema
kuwa wananchi wanapaswa kulinda miundombinu ya kisima hicho ili isiharibike
kwani maji hayo ni kwa wananchi wote bila ya kujali dini ya mtu na ni huduma
muhimu kwa binadamu.
Naye mkazi wa
kijiji hicho Mwanahawa Maulid alisema kuwa wamekuwa wakihangaika kutafuta maji
ambayo yanapatikana mbali na wamekuwa wakitumia muda mwingi kusubiria maji.
Maulid alisema
kuwa maji waliyokuwa wakiyatumia ni ya kuchimba chini ambayo si salama kiafya
na yamekuwa wakiwasababishia magonjwa mbalimbali kama vile kuhara na UTI.
Mwisho.
Monday, October 3, 2016
MWANAMKE ATUMIKA WIZI CWT WALINZI WAWILI WASHIKILIWA
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la la polisi mkoani Pwani linawashikilia
walinzi wawili wa jengo la ofisi ya Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa baada
ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuvunja na kuiba fedha kiasi ambacho
bado hakijajulikana na computer za ofisi hizo.
Akizungumzia na waandishi wa habari mjini Kibaha kuhusiana
na tukio hilo katibu wa (CWT) Nehemiah Joseph amesema kuwa tukio limetokea
usiku wa octoba mosi kuamkia octoba 2 mwaka huu.
Joseph amewataja walinzi hao kutoka kampuni ya
Noble security Tanzania Ltd ya Kibaha kuwa ni Hamad Kisoki (32) mkazi wa Maili Moja
na Said Mohammed (39) mkazi wa Mwanalugali.
Amesema siku ya tukio walinzi waliotakiwa kuingia
zamu walikuwa ni wawili lakini Said Mohammed pekee ndiye aliyefika kazini na
mwenzake Hamad Kisoki haikuweza kufahamika mara moja ni kwa sababu gani
hakuingia kazini.
Aidha amesema kuwa Said Mohamed alipokuwa kwenye
lindo lake anadaiwa kupatiwa chips na juisi vinavyosemekana kuwa na madawa ya
kulevya kutoka kwa mwanamke asiyefahamika.
Katibu huyo wa CWT mkoa wa Pwani ameeleza kuwa baada
ya kupatiwa chakula hicho mlinzi alipoteza fahamu na hivyo kutoa mwanya kwa
watu hao kuvunja milango ya ofisi hizo na kuingia na kuiba vitu hivyo ambavyo
thamani yake bado haijafahamika.
Ametaja ofisi zilizopo kwenye jengo hilo ambazo
zimeibiwa ni pamoja na CWT mkoa ,CWT wilaya,beem financial services (BFS)
,Chodawu,Tuico na TCCIA ambapo kwasasa wameshafikisha taarifa hizo polisi kwa
hatua zaidi na ofisi ya chama hicho imeshakaa na taasisi zote zilizopanga jengo
hilo kufanya tathmini.
hata hivyo amesikitishwa sana kutokea kwa wizi huo na
kushangazwa na mlinzi huyo kula ama kununua vyakula kwa watu wasiowajua kwani
kwa kufanya hivyo kumesababisha kuwapa wahalifu urahisi kutekeleza tukio hilo
ambalo limesababisha hasara kwa wamiliki wa ofisi hizo.
Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoani Pwani,Bonaventure
Mushongi ,amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema taarifa ya tukio hilo
ilitolewa saa 5 asubuhi kutoka kwa
Elizabeth Thomas ambae ni katibu wa chama CWT wilaya ya Kibaha huko mkoani A
,kata ya Tumbi.
Mushongi amesema kuwa baada ya kufanya wizi huo
watu hao walitokomea kusikojulikana na jeshi hilo bado linawatafuta,huku
akiomba ushirikiano kwa wananchi kuwafichua watu wanaowadhania kuhusika na wizi
huo na kwasasa wanawashikilia walinzi hao kwa ajili ya uchunguzi juu ya tukio
hilo.
Mwisho
Subscribe to:
Posts (Atom)