Tuesday, November 18, 2014

WALIOUNGULIWA MOTO WASAIDIWA NA MKE WA MBUNGE ASAIDIA MSALABA MWEKUNDU

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wa maduka ambayo yaliungua moto eneo la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wamepewa msaada wa mifuko 30 ya saruji yenye thamani ya shilingi 480,000 kwa ajili ya kujenga maduka yao.
Msaada huo ulitolewa na mdau huyo ambaye pia ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk David Nicas na kusema kuwa ameamua kujitolea ili kuwafariji wahanga hao ambao wamepata hasara kubwa.
Dk Nicas alisema kuwa wafanyabiashara hao walikuwa na mataratijio makubwa ya kuboresha biashara na maisha yao lakini ndoto zao zimekwenda kinyume.
“Janga la moto au lolote halina hodi wa taarifa linatokea wakati wowote bila ya kutegemea na linaleta umaskini kwani hawa waliamka na fedha lakini sasa hawana fedha tena na sisi ndiyo wa kuwasaidia ili kuwapa moyo, alisema Dk Nicas.
Aidha alisema kuwa moto huo umesababisha hasara ambayo haiwezi kulipika zaidi ya kuwasaidia na kuwafariji wafanyabiashara hao ambao bidhaa zao pamoja na fedha viliteketea kwa moto.
“Tunaimba serikali ya mkoa kuhakikisha inakuwa na gari lake la zimamoto badala ya kutegemea kutoka Jijini Dar es Salaam, licha ya kuwa wanalipa fedha kwa ajili ya huduma za zimamoto,” alisema Dk Nicas
Kwa upande wake mwakilishi wa wafanyabiashara hao Ally Gonzi alishukuru msaada huo na kusema kuwa umekuja wakati mwafaka na utawasaidia kukabiliana na gharama za ujenzi mpya wa maduka yao.
“Tunashukuru kwa msaada huu na tunawaomba wadau wengine nao wajitokeze kutusaidia ili angalau tuweze kurejesha biashara zetu kama ilivyokawaida,” alisema Gonzi.
Alisema kuwa gharama za hasara waliyoipata inakadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 700 ambapo katika tukio hilo mfanyabiashara mmoja alijeruhiwa na moto.
Mwisho.   
Na John Gagarini, Kibaha
MKE wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Selina Koka ametoa hundi ya shilingi milioni moja kwa Chama Cha Msalaba Mwekundu tawi la Maili Moja ili wanunulie vifaa vya kutolea msaada wakati wa majanga.
Akizungumza mjini Kibaha wakati wa mkutano wa Chama na kusema kuwa amejitolea fedha hizo kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma kwa chama hicho kwenye jamii.
Koka alisema kuwa chama hicho ni muhimu ndani ya jamii kwani kimekuwa kikisaidia mara yanapotokea maafa mbalimbali katika jamii kama vile moto, ajali, mafuriko, kimbunga na majanga mengine.
“Nimesikia kwenye risala yenu kuwa mnaazima vifaa kwa ajili ya kutolea huduma naomba niwapatie fedha ili mnunue vifaa vyenu ili mfanye kazi zenu kwa uhakika bila ya kubahatisha,” alisema Koka.  
Aidha alisema kuwa chama hicho ni muhimu sana kwa jamii kwani kinajitolea kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali na dhana kuu ya chama ni kujitolea.
“Hawa wanajitolea kwenye shughuli mbalimbali hivyo tunaomba wadau wajitokeze kuwasaidia hawa ili waisaidie jamii yenye matatizo,” alisema Koka.
Naye mwenyekiti wa chama hicho tawi la Maili Moja Lazaro Kwiligwa alisema kuwa wanamshukuru mke wa Mbunge kwani vifaa ilikuwa ni changamoto kubwa kwao.
“Tulikuwa tunaazima vifaa jambo ambalo linatusababisha tushindwe kutoa huduma ipasavyo  lakini sasa tutafanya kazi zetu kwa uhuru,” alisema Kwiligwa.
Lazaro alisema kuwa tawi hilo lilianza mwaka 2013 na lina wanachama 280 huku hai wakiwa 168 ambapo aliwataka wanachama wote walipe ada zao ili wawe hai.
Mwisho.




Picha 3831 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka kushoto akimkabidhi jora la kushonea sare, mwenyekiti wa tawi la Maili Moja la chama cha msalaba mwekundu Lazaro Kwiligwa.
Picha 3830 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka kushoto akimkabidhi kizibao mwenyekiti wa chama cha msalaba mwekundu tawi la Maili Moja Lazaro Kwiligwa.
Picha 3829 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka akionyesha moja ya vizibao ambavyo alivitoa kwa chama cha msalaba mwekundu tawi la maili Moja, kulia mwenyekiti wa tawi hilo Lazaro Kwiligwa na katikati ni msaidizi wa Mbunge Method Mselewa.
Picha 3784 Mdau wa Maendeleo wa maili Moja wilayani Kibaha Dk David Nicas kushoto akimkabidhi mfuko wa sementi moja ya wafanyabiashara ambao maduka yao yaliteketea kwa moto Ally Gonzi kulia
Picha Na John Gagarini



Sunday, November 9, 2014

TALGWU KUTOT

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kimesema kuwa kitadai haki za wanachama wake kwa kukaa mezani na si kwa kufanya migomo au maandamano.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mwenyekiti wa chama hicho Tawi la Kibaha Mji, Adolf Masawa wakati wa kufunga mafunzo ya viongozi wapya wa matawi kwenye halmashauri hiyo
Masawa alisema kuwa baadhi ya vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikidai haki zao kwa kufanya migomo na maandamano jambo ambalo linasababisha utoaji huduma kuwa mbaya.
“Sisi tutafuata taratibu na sheria katika kudai haki na hatutakuwa tayari kuwatetea wanachama ambao hawawajibiki kwani haki inakwenda sambamba na uwajibikaji,” alisema Masawa.
Aidha alisema kuwa wao hawana ushabiki na ndiyo sababu chama chao huwa hakifuati mkumbo katika kudai haki zao kama ilivyo kwa baadhi ya vyama hali ambayo inasababisha usumbufu kwa wateja wanaowahudumia.
Kwa upande wake katibu wa TALGWU wa mkoa wa Pwani Amina Darabu alisema kuwa chama chao kina lengo la kuwaunganisha wafanyakazi ili waweze kuwa na mahusiano mazuri na mwajiri wao ili kuboresha huduma kwa wateja.
“Tuna sisitiza umoja ujshirikiano na upendo baina ya wanachama pamoja na mwajiri na wateja wanaowahudumia kwani kwa pamoja huduma zitakuwa bora mahali pa kazi,” alisema Darabu.
Awali akifungua mafunzo hayo mwenyekiti wa mkoa Mohamed Mahingika alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia viongozi hao wapya kujua wajibu na majukumu yao kwa wanachama.
Mahingika aliwataka viongozi hao kuhamasisha watumishi wa serikali za mitaa kujiunga na chama hicho ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kuboresha utendaji kazi wao.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliwahusisha viongozi kutoka matawi ya Kituo cha  Afya Mkoani sasa Hospitali ya Wilaya ya Kibaha, Kituo cha Afya Mwendapole na kata Kibaha.

Mwisho.

MOTO WATEKETEZA MADUKA 6 MMOJA AJERUHIWA MWINGINE AZIRAI

Na John Gagarini, Kibaha
MFANYABIASHARA  mmoja wa duka la bidhaa mbalimbali Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani Urisha Mwembamba amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na moto ambao uliteketeza duka lake na mengine matano.
Moto huo ambao unadaiwa ulitokana na shoti ya umeme ulianzia kwenye jokufu la kuhifadhia vinywaji baridi ambavyo alikuwa akiuza pamoja na bidhaa nyingine viliteketea kabisa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja wa wahanga wa tukio hilo Ally Gonzi alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi Novemba 10 majira ya saa 2 usiku
Gonzi alisema kuwa moto huo ulianza majira ya saa 2 usiku na ulianzia kwenye duka hilo na kusambaa kwenye maduka mengine baada ya kushindwa kuudhibiti. 
“Moto ulianzia kwenye duka la Mwembamba kwenye jokofu na wakati moto unaanza alikuwepo kwani aliingia kwa mlango wa dharura lakini alishindwa kutoka akiwa hajui nini cha kufanya huku moto ukiendelea ndipo wasamaria wema wakaingia na kumtoa ambapo alijeruhiwa na moto miguuni,” alisema Gonzi
Alisema kuwa moto ulipokuwa ukiendelea watu walifika na kuanza kujaribu kuzima lakini ulikuwa mkali sana kwani kuna pipa kubwa la maji kama lita 15,000 wakawasha mashine lakini moto huo haukuzimika.
“Dada wa Mwembamba aitwaye Nasra alipopata taarifa akaja kutoka Mbezi naye akazimia kutokana na tukio hilo ambapo wote walikimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kwa ajili ya matibabu hata hivyo gari la zimamoto lilifika saa moja na nusu baada ya moto kutokea hata hivyo walifika moto huo ukiwa tayari umedhibitiwa na wananchi,” alisema Gonzi.
Aidha alisema waliwasiliana na kikosi cha zimamoto lakini waliambiwa hakuna gari na askari wakuzuia ghasia FFU walifika na kuzuia wizi lakini hata hivyo watu waliiba vitu walipokuwa wakijidai kuokoa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa jumla ya maduka sita yaliathirika na moto huo na mtu mmoja alijeruhiwa.
“Polisi ilibidi watumie mabomu ya machozi ili kuwatawanya watu ambapo baadhi yao walikuwa ni vibaka waliokuwa wakijaribu kuiba mali kwenye maduka mengine ya jirani,” alisema Kamanda Matei.
Kamanda Matei alisema kuwa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana wala thamani ya mali zilizoteketea bado hakujafahamika na uchunguzi unaendelea aliwataka wananchi kutotumia fursa kuiba yanapotokea majanga kama hayo badala yake watoe msaada.

Mwisho. 

Friday, November 7, 2014

MSAADA WA KISHERIA DC APONGEZA

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Halima Kihemba amekipongeza kituo cha Msaada wa Kisheria  kwa Wanawake (WLAC) kwa kujitolea kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kuwalipa wanasheria.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akifunga mafunzo ya wasaidizi wa Kisheria wilayani humo ya siku 25 yaliyoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).
Kihemba alisema kuwa kituo hicho kimeonyesha umuhimu wa kutoa msaada wa kisheria ni muhimu kwa watu hususani wanawake na watoto ambao wamekuwa wakipoteza haki zao kutokana na baadhi ya watu kutumia unyonge wao wakutokuwa na sauti ndani ya jamii kuwadhulumu haki zao.
“Huduma ya kisehria ni muhimu ndani ya jamii lakini watu wengi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama hizo hivyo kushindwa kupata haki zao hivyo mashirika kama haya ni ya kuigwa,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa makundi hayo mawili ndiyo yamekuwa yakidhulumiwa haki zao kwa kiasi kikubwa hivyo mashirika kama WLAC yanayojitolea lazima yaungwe mkono na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.
Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya mkuu wa idara ya Mafunzo ya WLAC Magdalena Mlolere alisema kuwa lengo la kituo hicho ni kuhakikisha kuwa watu wanapata haki zao ambazo ni za msingi na ziko kikatiba.
Mlolere alisema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo kwa wasaidizi wa kiseheria wa vituo vya KPC na KPP ni ili waweze kusaidia wananchi kutatua migogoro inayojitokeza kabla ya kufika kwenye vyombo vya kisheria ikiwemo mahakama na polisi.
“Mafunzo hayo pia yatasaidia kupunguza kesi zinazopelekwa mahakamani ambazo nyingine zimekuwa zikitumia muda mrefu kuamuliwa na kuwafanya wahusika kutumia muda mwingi kwenda mahakamani huku wakishindwa kufanya shughuli zao za maendeleo,” alisema Mlolere.
Akisoma hotuba mbele ya mgeni rasmi moja ya wahitimu wa mafunzo hayo kwa niaba ya wahitimu John Gagarini alisema kuwa changamoto zinavyovikabli vituo hivyo ni baadhi ya wanajamii kutokuwa wawazi katika kuyapeleka mashauri hayo kwenye vituo hivyo pia ni ukosefu wa usafiri wa kuweza kufika kwenye maeneo hasa yale ya vijijini, jumla ya wahitimu 32 walihitimu mafunzo hayo na kukabidhiwa vyeti na mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba.
Mwisho.
  


UKAWA

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa ndoa ya vya ma vya upinzini
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) si tishio kwani hizo
ni porojo tu na haitaweza kudumu.
Akizungumza kwenye baraza la mkoa la Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Pwani
mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Jackson Josian alisema kuwa muungano huo
hautaweza kudumu.
Josian alisema kuwa hata wakiungana hawataweza kuisumbua CCM kutokana
na viongozi wao kutokuwa na ushirikiano kwani kila mmoja anaangalia
upande wake.
“Ndoa ya UKAWA haiwezi kudumu kutokana na wapinzani kuwa watu wa
vitisho tu na hawawezi kuongoza hata ndani ya vyama vyao,” alisema
Josian.
Alisema kuwa kipimo kizuri kilikuwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba
ambapo walionyesha udhaifu mkubwa kwa kususia ambapo katiba ndiyo
mustakbali wan chi yoyote.
“Wao wanaangalia maslahi ya vyama vyao na si maslahi ya Umma kwani
hata kama walikuwa na hoja za msingi wangepinga wakiwa ndani ya Bunge
na siyo nje hivyo hawa hawafai kupewa madaraka na ndoa yao haitutishi
kwani itavunjika,” alisema Josian.
Kwa upande wake katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa
kipindi hichi ni vita kuelekea uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji
na Vitongoji.
Mdimu alisema kuwa kwa sasa chama kiko kwenye mchakato wa kuwapata
wanachama wenye sifa watakaogombea nafasi za uenyekiti wa nafasi hiyo
ambapo kura za maoni zitafanyika Oktoba 30.
Aliwataka wanachama kutowachafua baadhi ya wagombea kwani mamlaka ya
kujua kuwa mgombea fulani hana sifa ni vikao ambavyo vikao vya
kisheria na si mtu kutoa maamuzi.
Mwisho.

MAHIZA AKIMBIA OFISI KUKAMILISHA UJENZI WA MAABARA NA KUKU MILIONI 20 KUNUSURIKA NA KIFO

> Na John Gagarini, Bagamoyo
>
> SUALA la Maabara kwa shule za Sekondari za Kata limeingia kwenye hatua
> nzito baada ya mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza kuiacha ofisi yake na
> kuhamia Wilaya ya Bagamoyo ili kuhakikisha agizo la Rais Dk Jakaya Kikwete
> la kila wilaya iwe imekamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba 30 mwaka huu.
>
> Sambamba na hilo mkuu huyo amewataka wakuu wa idara wa Wilaya hiyo kila
> mmoja kutokaa ofisini na kuchagua kata ya kwenda ili kusimamia ujenzi huo
> hadi ujenzi wa maabara ukamilike.
>
> Akizungumza juzi kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika mjini
> Bagamoyo Mahiza alisema kuwa ujenzi wa maabara kwenye wilaya hiyo bado
> zoezi hilo haliko vizuri hivyo lazima itumike nguvu ya ziada kufanikisha
> zoezi hilo.
>
> “Kuanzia sasa najua nitaanzia kata gani lakini nahamia Bagamoyo na wakuu wa
> idara kila mmoja tukitoka hapa ataniambia atakuwa kata gani ili tuanze
> usimamizi kwani bila ya kufanya hivi muda utaisha na mambo yatakuwa
> magumu,” alisema Mahiza.
>
> “Kuanzia sasa vikao vya madiwani havitakuwepo kilichobaki wote tuende
> kwenye ujenzi wa maabara na kama mtu anaona hawezi kuwajibika aondoke
> mapema asije akatuharibia mipango yetu ya maendeleo kwani watoto ni wetu,”
> alisema Mahiza.
>
> Mahiza alisema kuanzia sasa hivi hakuna cha mahafali wala sherehe wimbo
> uliopo ni maabara kwa shule zetu za sekondari kwani baadhi ndo wako kwenye
> msingi je ujenzi utakamilika kwa wakati jambo ambalo linatia mashaka.
>
> “Baadhi ya watendaji hawana haraka na kusababisha shughuli kwenda taratibu
> kuanzia sasa hapa ni mwendo wa kufanya kazi kwani tusipokuwa makini muda
> utaisha hatujakamilisha itakuwa haipendezi,” alisema Mahiza.
>
> Aidha alisema kuwa wakuu wa wilaya na mikoa waliitwa Dodoma na Rais na
> kutakiwa wawe wamekamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba 30 mwaka huu na wao
> walimwahidi kuwa watakamilisha ujenzi kipindi hicho.
>
> Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Shukuru Mbato alisema
> kuwa agizo hilo wamelipokea na watahakikisha wanakamilisha ujenzi wa
> maabara hizo kwa muda uliopangwa.
>
> Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

> CHANJO mpya ya ugonjwa wa Mdondo kwa kuku ya ITA NEW itasaidia kupunguza
> vifo vya kuku wa kienyeji zaidi ya milioni 20 wanaokufa kwa mwaka kutokana
> na ugonjwa huo.
>
> Tayari dawa hiyo imeshapitishwa na mamlaka ya vyakula na dawa (TFDA) kwa
> ajili ya matumizi kwa kuku ambapo Tanzania ina jumla ya kuku wapatao
> milioni 60.
>
> Akizungumza mjini Kibaha makamu mwenyekiti wa chama cha waganga waisidizi
> wa mifugo kitaifa (TAVEPA) ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni ya madawa ya
> Laprovet Tanzania Ephrahim Massawe alisema kuwa chanjo hiyo ni ya muda
> mrefu.
>
> “Chanjo hiyo inawakinga kuku kwa kipindi cha mwaka mmoja tofauti na chanjo
> nyingine ambazo huisha nguvu kila baada ya miezi mitatu kabla ya kuchanjwa
> chanjo nyingine,” alisema Massawe.
>
> Alisema kuwa ugonjwa huo ni mbaya kwa kuku ambao unaua kuku kwa muda mfupi
> na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji lakini kutokana na kupatikana
> chanjo hii itasaidia kupunguza vifo vya kuku kutokana na ugonjwa huo
> maarufu kama Kideri
>
> “Ugonjwa huo ambao hutokea kwa misimu ya mvua zinapoanza na zinapoishia
> ulikuwa ni tishio kubwa kwa wafugaji kwani ulifikia hatua ya kuua hata nusu
> ya idadi ya kuku wa kienyeji hapa nchini,” alisema Massawe.
>
> Aidha alisema kuwa kupatikana kwa chanjo hiyo kutasaidia kuongeza pato,
> lishe na kukuza uchumi wa kaya ambazo zifafuga kuku hasa vijijini ambapo
> mikoa inayoongoza kwa ufugaji wa kuku hao ni Singida, Dodoma, Shinyanga na
> Morogoro.
>
> Mwisho.
>

Friday, October 24, 2014

POLISI WAKAMATA LUNDO LA SILAHA, FEDHA NA VITU MBALIMBALI

Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamekamatwa wakiwa na silaha aina ya Short Gun yenye namba 07019302 ikiwa na risasi nane.
Hayo yamesemwa na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mohamed Kalipa (20) dereva wa Bajaji mkazi wa Mbagala Rangi Tatu, Salum Shekivui (20) mkazi wa Buza na Seuli Lucas (18) makazi wa Mbagala Rangi Tatu Jijini Dar es Salaam.
Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 20 mwaka huu majira ya saa 2:30 huko Mlandizi wilaya ya Kibaha.
“Mbali ya silaha pia walikutwa na fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 6,611,800, vocha mbalimbali za simu zenye thamani ya shilingi milioni 2,185,500 na simu za mkononi sita za aina mbalimbali ambazo thamani yake bado hazijafahamika,” alisema Kamanda Matei.
Aaidha alisema kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa walifanya tukio la unyanganyi wa kutumia silaha huko Kijiji cha Mbwewe wilaya ya Bagamoyo kwenye duka la Twaha Mbuta siku ya Oktoba 19 saa 1:30 usiku na kupora kiasi cha shilingi milioni 30,000,000.
“Baada ya kukamatwa walimtaja mtuhumiwa mwenzao ambaye  walikuwa wakishirikiana naye Samwel Joseph mkazi wa Kongowe Kibaha ambapo baada ya upekuzi walimkuta na risasi sita za Short Gun ambazo alikuwa akizimiliki bila ya kibali hata hivyo mtuhumiwa huyo alitoroka,” alisema Kamanda Matei.
Katika tukio lingine watu wawili walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa ngombe 61 wenye thamani ya shilingi milioni 27,450 ,000 mali ya Keke Furaha (37) kwa kutumia silaha aina ya sime.
Alibainisha kuwa tukio hilo limetokea Oktoba Mosi mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi huko Lulenge kata ya Ubena wilayani Bagamoyo ambapo watuhumiwa ni Sadala Lupoto (25) mkazi wa Kimamba Kilosa na Luseky Sogoyo (25) na juhudi za kuwatafuta ngombe wengine 39 zinaendelea.  
Katika tukio lingine watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na silaha aina ya gobore bila ya kibali  huku wengine 11 walikamatwa kwenye matukio ya kukutwa na bangi gunia mbili na kete 250 pamoja na lizla zipatazo 100.
            
Mwisho.









Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei akionyesha moja ya silaha zilizokamatwa kwa watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi. 

Silaha mbalimbali ambazo jeshi la polisi mkoani Pwani limezikamata mara baada ya kufanya misako maeneo mbalimbali ya mkoa huo. 

 Redio na deki vilivyoibiwa na kukamatwa kwa watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi. 

  Bunduki, tv, simu na vifaa vingine ambavyo vilikamatwa na polisi baada ya kuibiwa kwa watu mbalimbali mkoani humo.

Silaha pamoja na kiasi kikubwa cha fedha ambazo ziliibiwa kwa mfanyabiashara Twaha Mbuta wa huko Mbwewe. 

Sehemu ya fedha, vocha na risasi zilizokamatwa na polisi baada ya kufanya masako wa kusaka majambambazi.

 Redio zilizoibiwa kwa watu mbalimbali mkoani Pwani baada ya polisi kufanya misako mkoani humo
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Ulrich Matei akiongea na waandishi wa habari mjini Kibaha hawapo pichani