Tuesday, June 10, 2014

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUPIMA AFYA ZAO



Na John Gagarini, Kibaha
IDARA ya Afya ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani imeanza uhakiki wa wafanyabiashara mbalimbali kama wamepima afya zao kwa mujibu wa sheria ili watoe huduma hizo wakiwa na afya njema na endapo watashindwa kufanya hivyo watafungiwa biashara zao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jana  mjini Kibaha ofisa afya wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha David Vuo alisema kuwa wafanyabiashara hao pamoja na wamiliki wa viwanda wanapaswa kuhakikisha watoa huduma wao wanapima afya zao.
“Utaratibu huu ni wa kisheria kwani hata wafanyakazi wa serikali kabla ya kuanza kazi wanapaswa kupima afya zao na hii ni sheria ya afya ya mwaka 2009 namba 169 kifungu namba 17ambapo kwa sasa maofisa afya wa kata wanafanya uhakiki kuona zoezi hilo ili taratibu stahiki zichukuliwe kwa wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo ,” alisema Vuo.
Alisema kuwa jambo hilo si geni kwani liko kisheria na linawagusa wafanyabiashara wote na shughuli mbalimbali za wajasiriamali ambao wanapaswa kufuata taratibu za kiafya.
“Lengo la kupima afya na kuhakikisha kuwa wahudumu hao wanahudumia wateja wakiwa na afya njema na kama kuna atakayegundulika anapaswa kutibiwa kwanza hadi atakapopona ndipo aendelee kutoa huduma na kutakuwa na fomu maalumu itakayokuwa kwenye eneo la shughuli ili kuwatambua waliofanya hivyo na wale watakaoshindwa hawataruhusiwa kuhudumiwa watu,” alisema Vuo.
Aidha alitaja magonjwa ambayo yanapimwa kuwa ni Taifodi, Kuhara, Mkojo, magonjwa ya Kaswende, Gono, Kifua, magonjwa ya ngozi kama vile upele na mengineyo.
“Suala la kupima virusi vya ugonjwa wa UKIMWI ni hiyari ambapo upimaji wa magonjwa haya hayahusiani na kupima ugonjwa huo labda mhusika atake mwenyewe ambapo upimaji huu utafanyika kwenye hospitali ya wilaya ya Mkoani na kituo cha afya Kongowe,” alisema Vuo.
Ofisa afya huyo wa halmashauri ya Mji wa Kibaha alissema kuwa kuhusiana na uchangiaji wa vipimo hivyo kila mhusika anapaswa kutoa kiasi cha shilingi 5,000 kwenye ofisi ya kata kisha atapewa fomu kwa ajili ya kwenda kupima ambapo alisema elimu ilishatolewa.
Alitaja biashara ambazo watumishi wake wanatakiwa kupima afya zao kuwa ni mama na baba lishe, bekari, migahawa, hoteli, baa, nyumba za kulala wageni, mashine za kusaga nafaka, maduka ya vyakula, mabucha, machinjio, saluni, dobi, viwanda, wachoma chipsi, vilabu vya pombe za kienyeji, wafanyakazi wa kampuni na vikundi vya ujasiriamali.

Saturday, June 7, 2014

WATAKIWA KUKABILIANA NA TABIA NCHI



WAKAZI wa wilaya za Bagamoyo mkoani Pwani na Pangani mkoani Tanga wametakiwa kulinda misitu ikiwemo ile ya Mikoko iliyopo kandokando mwa Bahari ya Hindi ili kuinusuru wilaya hiyo na athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Hayo yalisemwa  na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi alipokuwa akifungua mafunzo ya juu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi kwa wajumbe wa kamati za mazingira kutoka wilaya za Bagamoyo na Pangani mkoani Tanga.
Kipozi amesema kuwa watu wengi waliathirika na mvua kubwa zilizonyesha ambazo zilileta mafuriko na kusababisha madhara yakiwemo ya watu kufa, mazao yao kusombwa na maji, miundombinu ikiwemo ya barabara na madaraja zilitokana na mabadiliko hayo ya Tabia Nchi.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mratibu wa mafunzo hayo Dk Beno Mnembuka ambaye ni mtafiti kiongozi kwenye mradi huo unaosimamiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Ardhi, Mamlaka ya hali ya Hewa na mtafiti mmoja toka nchini Norway amesema kuwa mabadiliko ya Tabia Nchi pia yameathiri viumbe hai kama vile samaki.
Dk Mnembuka amesema kuwa viashiria vya mabadiliko ya Tabia Nchi ni pamoja na mabadiliko ya misimu ya mvua, joto, upepo mkali wa Kasi na Kusi, ukame, mafuriko ambapo hutokana na uharibifu wa mazingira ambapo ili kukabiliana na madhara hayo lazima kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti na kutoharibu vyanzo vya maji.
 Naye meneja wakala wa misitu Tanzania (TFS) wilaya ya wilaya Bagamoyo Charles Mwafute amesema kuwa katika kutekeleza kwa vitendo washiriki wa mafunzo hayo walipanda miti ya Mikoko eneo la ukubwa wa hekari mbili na nusu kwenye kijiji cha Kiharaka.  
Mradi huo ambao utaisha mwezi Desemba mwaka huu unatekelezwa kwenye vijiji vya Bumbwini, Kisakasaka Zanzibar, Magomeni, Kiharaka na Kondo wilayani Bagamoyo, Matakani, Kipumbwi na Pangani Mjini wilaya ya Pangani.

Thursday, June 5, 2014

WABUNGE WA KATIBA WATAKIWA KUREJEA BUNGENI




WABUNGE wa Bunge Maalumu la Katiba ambao walisusia vikao vya bunge hilo Mjini Dodoma wametakiwa kurejea kwenye mjadala wa marekebisho ya katiba kwani kuendelea kususia ni sawa na kufanya uasi na usaliti kwa wananchi.
Wanapaswa kuheshimu mamalaka iliyopo kwa kulimaliza tatizo lililopo kwa kutumia busara kwa kukaa chini kwa pamoja na kukubaliana na si kwa kulalamika kwa kupiga kelele nje ya Bunge hilo ili suluhu ipatikane.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha Nabii Jofrey John wa Huduma ya HAKI Ministry ya Kongowe Kibaha mkoani Pwani amesema kuwa endapo wabunge hao wataendelea kususia bunge lijalo kama walivyosusa ni kwamba watakuwa wanaihujumu nchi.
Nabii John amesema kususa na kulalamika nje ya bunge hilo ni sawa na kuasi hali ambayo inaweza kujenga chuki na matokeo yake ni kuleta mafarakano ambayo mwisho wake ni mbaya kwani urithi walionao Watanzania ni amani na si vurugu
Nabii John amesema kuwa kusiwe na kundi ambalo linasusia mchakato wa kuunda katiba hiyo mpya kwani ni moja ya njia ambayo inaweza kusababisha kuvurugika kwa amani na litajenga roho za kuona kuwa wanaonewa.
Amesema kuwa haitapendeza kuona kuwa kuna wabunge wamekwenda kwenye bunge hilo kwa ajili ya kuhujumu mchakato huo kwani watasababisha kuvunja amani iliyopo ambayo imedumu kwa maiaka 50 tangu tulipopata uhuru hivyo haipaswi kuvunjwa na kundi la watu.
Amesema kiongozi yoyote awe wa chama au sehemu yoyote amechaguliwa na Mungu hivyo hapaswi kudharau mamlaka iliyopo madarakani ambayo hata Mungu anaitambua.
Aidha amesema kuwa anaamini kuwa wabunge waliochaguliwa kwenye bunge hilo la katiba ni wasomi hivyo wasijishushie heshima ya usomi wao kwani wako pale kwa niaba ya wananchi na si kwa maslahi yao binafsi bali kwa maslahi ya wananchi.
Amewataka waumini wa dini zote kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya nchi ili Mungu aepushe roho ya umauti katika nchi yetu ambayo inanyemelea  kutokana na sababu ambazo zinaweza kuzuilika za kumaliza tofauti ndogo ndogo zilizopo.
Ameiomba serikali kuwatumia viongozi wa dini kama sehemu ya kudumisha amani ya nchi kwa kuwafanyia maombi viongozi waliopo madarakani ili waweze kuongoza kwa kutumia hekima za Mungu kwani bila ya kuwa na maombi hayo shetani anaweza kuleta roho ya uchonganishi na kusababisha amani kutoweka.
Amebainisha kuwa kwa kipindi chote cha mwezi huu hadi ujao watakuwa na kongamano kubwa la kuiombea amani ya nchi ambapo halitakuwa na itikadi ya dini yoyote bali ni madhehebu yote hivyo kuwataka watu kujitokeza kufanya maombi hayo.
Mwisho.

Saturday, May 31, 2014

BILALI AZINDUA MFUKO WA ELIMU ACHANGIA MILIONI 10



Na John Gagarini, Kibaha
MAKAMU wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mohamed Gharib Bilali ameuchangia mfuko wa elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kiasi cha shilingi milioni 10.
Alichangia fedha hizo jana wakati wa uzinduzi wa mfuko wa elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha uliofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani hapa.
Alisema kuwa katika kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwenye sekta ya elimu lazima kuwe mikakati maalumu ya kuweza kufikia malengo kwa kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.
“Nawapongeza kwa kuanzisha mfuko huu na serikali itawaunga mkono kwa hali na mali na mimi nawachangia milioni 10 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto kwenye sekta ya elimu katika mji wa Kibaha wilaya na mkoa mzima wa Pwani.
“Ningependa suala la choo kuwa historia kwani hii ni aibu na si changamoto ya kudumu na inapaswa kufanyiwa kazi mara moja na kuiondoa kabisa kwani ni jambo lisilo pendeza na changamoto nyingine zilizopo kama vile za upungufu wa madawati kwa shule za msingi, ukosefu wa maabara kwa shule za sekondari, upungufu wa nyumba za walimu, matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa na maktaba kupitia mfuko huo utasaidia kukabiliana na hali hiyo,” alisema Dk Bilali.
Aidha alisema kuwa amefurahi kusikia kuwa fedha hizo zitatumika kujenga maabara tatu katika sekondari za Pangani, Visiga na Miembe Saba na kununua madawati 1,500 kwa ajili ya shule za msingi za Tandau, Lulanzi, Misugusugu, Zogowale, Msangani, Viziwaziwa, Vikawe, Mwanalugali, Mkuza na Kidimu.
Alizitaka halmahauri hapa nchini kuiga mfano wa Halmashauri hiyo ya Mji wa Kibaha kwa kuanzisha mifuko kama hii kwa ajili ya kutatua changamoto za elimu badala ya kuisubiri serikali kwani ni mgao inaoutoa ni mdogo na elimu na mafunzo bora ni mkakati wa kipaumbele katika kufikia malengo ya mipango ya maendeleo ya Taifa ya 2025 na kutumia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza umaskini MKUKUTA na malengo ya milenia.
Awali Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Kasimu Majaliwa alisema kuwa ubunifu wa kupata fedha kwa ajili ya Halmashauri 167 hapa nchini ni mzuri kwnai utasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu.
Majaliwa alisema kuwa uboreshaji wa elimu unapaswa kusimamiwa na watu wote wakiongozwa na madiwani na wananchi wote wanapaswa kujitokeza kuuchangia na wizara yake itachangia kiasi cha shilingi milioni tano.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa amefurahishwa na uzinduzi huo ambapo alisema kuwa moja ya ndoto zake za kukabiliana na changamoto za elimu.
“Ili kuwa na elimu bora ni pamoja na kuwa na miundombinu mizuri na watu wa kuiboresha ni wazazi pamoja na wadau wote ndani ya Halmashauri licha ya kuwa wananchi wanachangamoto kubwa ya kuchangia hata hivyo wameonyesha nia ya kuchangia kwa kujitolea na mimi nawaunga mkono kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 16,” alisema Koka.
Awali mwenyekiti wa mfuko huo Anna Bayi alisema kuwa lengo la kuanzishwa mfuko huo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambapo hadi sasa mfuko huo una kiasi cha shilingi milioni 210 na ahadi ni shilingi milioni 34 huku malengo yakiwa ni kukusanya kiasi cha shilingi milioni 300.
“Tunatarajia kati ya fedha hizo zitajenga maabara tatu katika shule ya sekondari Nyumbu, Miembe Saba na shule ya wasichana Kibaha ambapo tumejiwekea mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiunga na mfuko wa elimu nchini kwa lengo la kupata ruzuku ya miundombinu, samani, vifaa vya kufundishia na kujifunzia,” alisema Bayi.
Mwisho. 

   

Thursday, May 29, 2014

BILALI KUZINDUA MFUKO WA ELIMU KIBAHA MEI 31



Na John Gagarini, Kibaha
MFUKO wa elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani utazinduliwa Mei 31 mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gharib Bilali.
Kwenye uzinduzi huo ambao utafanyika mjini Kibaha mgeni rasmi ataongoza matembezi ya hisani kwa ajili ya kuhamasisha uchangiaji wa mfuko huo ambao una lengo la kupata kiasi cha shilingi milioni 300.
Akielezea juu ya tukio hilo mwenyekiti wa mfuko huo Anna Bayi alisema kuwa  katika uzinduzi huo kutatanguliwa na matembezi ya hisani yatakayoanzia maeneo ya Mkoani hadi viwanja vya Maili Moja ambapo ndipo halfa itafanyika.
Bayi alisema kuwa  hadi sasa tayari wameshapata kiasi cha shilingi milioni 180 zitakazosaidia kuiwezesha halmashauri hiyo kukabiliana na changamoto za sekta ya elimu hususan madawati na maabara.
"Mara zitakapopatikana fedha hizo tutaanzia kununulia madawati 1,500 yenye thamani ya shilingi milioni 90 na kujenga maabara tatu kwa shilingi Milion 210,” alisema Bayi.
Alisema uchangiaji huo utakuwa ni zoezi endelevu ili kuhakikisha wanapunguza ama kumaliza kabisa changamoto za kielimu katika halmashauri ya Mji wa Kibaha.
“Kila mwananchi anatakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 2,000 wakiwemo  ,wafanyabiashara, wamiliki wa makampuni na wadau wa elimu na hadi sasa mwamko unaonekana kwa wananchi hivyo kuwa na imani ya kuwa mfuko utafanikiwa,” alisema Bayi.
Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo, Jeniffer Omolo alisema mfuko huo umeundwa chini ya sheria namba 288 kifungu kidogo namba 80 katika tangazo la serikali namba 218 la tarehe 18 Juni 2010.
“Shule za msingi na sekondari za serikali bado zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinafanya lengo la utoaji elimu bora kushindwa kufikiwa kikamilifu,” alisema Omolo.
Alibainisha kuwa Shule za msingi zilizopo wilayani Kibaha Mji  zinakabiliwa na uhaba wa madawati 3,488 hali inayopelekea baadhi ya shule hizo wanafunzi kutumia kukaa zaidi ya watatu kwenye dawati moja.
Aidha alisema katika upande wa shule za sekondari kuna upungufu wa maabara 24 ambapo kwa sasa kuna maabara 9 pekee, Halmashauri ya mji wa Kibaha ina jumla ya shule za msingi 47 na shule za sekondari za serikali na binafsi 34 .
Mwisho.