Friday, November 29, 2024

WENYEVITI WAAPISHWA WATAKIWA WASIUZE ARDHI


WENYEVITI wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa hivi karibuni kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa wasijihusishe na uuzaji ardhi ili kuepukana na migogoro ya ardhi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa wakati wa kuapishwa kwa wenyeviti hao pamoja na wajumbe wa Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri hiyo.

Shemwelekwa alisema kuwa wenyeviti hao waachane na masuala ya uuzaji ardhi kwani inayohusika ni Halmashauri kwani baadhi yao walikuwa wakijihusisha na uuzaji ardhi.

"Msijihusishe na masuala ya uuzaji ardhi pia itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi hivyo wao wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo,"alisema Shemwelekwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mussa Ndomba alisema kuwa wenyeviti wasifanye vita na watendaji wa mitaa kama kuna jambo waangalie namna ya kutatua.

Ndomba alisema kuwa wale ni wataalamu wasigombane nao kwani hawatafanya kazi vizuri na wanaweza kuwakwamisha kwani wanambinu nyingi wanaweza kuwakwamisha kwenye majukumu yao hivyo washirikiane nao na kama kuna changamoto wakae nao chini ili kutatua na kurekebishana.

"Masuala ya mihuri nimelisikia wananchi wapate huduma bure bila ya gharama na kuhudumiwa haambiwi toa fedha sijui ya nini anatakiwa apate huduma bora na kwa wakati,"alisema Ndomba.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa jukumu lao kubwa kurudisha deni kwa wananchi ambao wamewakopesha kura walizowapigia na wanatakiwa kuwatumikia na wasinunue bali wapewe huduma bure.

Koka alisema kuwa wanapaswa kuwatumikia na kuwashirikisha kwenye vikao pia waitishe mikutano na kuwapatia mrejesho wa masuala mbalimbali na kutekeleza mipango wanayoiweka.

Mbunge wa Wafanyakazi Mkoa wa Pwani Dk Alice Kaijage alisema kuwa wananchi wamefanya jambo zuri kuwachagua viongozi hao kutoka CCM kwani wana uwezo mzuri wa kusimamia miradi ya maendeleo ambayo mipango huanzia ngazi ya Mitaa na kupitishwa Bungeni.

Kaijage aliwapongeza viongozi hao wa Serikali za Mitaa kwa ushindi walioupata nakuwataka  wakafanye kazi kwa kuwatumikia wananchi na kazi zao wanapozifanya wanapaswa kumtanguliza Mungu.

Moja ya wenyeviti walioapishwa Elizabeth Nyambilila alisema kuwa kipaumbele chake cha kwanza atakachoanza nacho ni kuhamasisha ujenzi wa shule ya msingi.

Nyambilila alisema kuwa tayari walishaanza mikakati kwanza ni kupata eneo hivyo wataenda kutafuta eneo kwa ajili ya kufanya ujenzi hio ili kuwapunguzia changamoto watoto wa mtaa huo kusoma mbali.

DK ALICE AWASHUKURU WANANCHI KWA KUWAPATIA USHINDI CCM UCHAGUZI SERIKALI

MBUNGE wa Wafanyakazi Mkoa wa Pwani Dr Alice Kaijage amewashukuru wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kuwachagua wenyeviti wote na wajumbe wa Serikali za Mitaa wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM)


Dk Kaijage ameyasema hayo wakati wa uapisho wa wenyeviti Serikali za Mitaa wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Amesema kuwa wananchi wamefanya jambo zuri kuwachagua viongozi hao kutoka CCM kwani wana uwezo mzuri wa kusimamia miradi ya maendeleo.

"Nawapongeza viongozi wetu wa Serikali za Mitaa kwa ushindi mlioupata nendeni mkafanye kazi kwa kuwatumikia wananchi na kazi zenu mnapozifanya mnapaswa kumtanguliza Mungu,"amesema Dk Kaijage.

Monday, November 18, 2024

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VINAVYOSIMAMIA ULINZI NA AMANI KUSINI MWA AFRIKA (SADC) ZIANDAE MITAALA KUZINGATIA MATISHIO YANAYOZIKABILI NCHI WANACHAMA

Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu Meja Jenerali Iddi Said Nkambi amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Serikali na Kiraia zinazohusika na Ulinzi wa Amani chini ya Mwavuli wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) kuhakikisha zinandaa mitaala ya kuendeshea mafunzo ya Ulinzi wa Amani kwa kuzingatia matishio yanayozikabili nchi wanachama.

Meja Jenerali Nkambi ameyasema hayo leo tarehe 18 Novemba 2024 wakati wa ufunguzi wa Semina fupi ya siku 5 inayohusu  uwasilishaji wa mitaala mipya ya mafunzo itakayotumika kuandaa  Majeshi ya SADC, semina inayofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani (PTC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es salaam.

Semina hiyo inayoendeshwa na Chuo cha Ulinzi wa Amani cha Kikanda chenye Makao Makuu yake nchini Zimbabwe inahudhuriwa na washiriki kutoka nchi wanachama wa SADC ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo katika kukabiliana na matishio pindi wanapokuwa katika majukumu ya Ulinzi wa Amani ndani ya ukanda wa SADC na sehemu zingine watakapopewa jukumu.

Tuesday, November 5, 2024

TAKUKURU PWANI KUTOA ELIMU KUPAMBANA NA RUSHWA



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani itaendelea kutoa elimu ya kupambana na rushwa kwa makundi mbalimbali wakati huu wa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Aidha makundi hayo ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, wapiga kura, wagombea, wasimamizi, azaki, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Takukuru Mkoani humo Christopher Myava alisema walishatoa elimu juu ya kupambana na vitendo vya rushwa tangu mchakato wa uchaguzi ndani ya vyama vya siasa.

Myava alisema kuwa makundi hayo ni muhimu kipindi hichi cha uchaguzi lengo likiwa ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa hawatokani na rushwa.

"Tunataka wananchi wachague viongozi bora ambao wataendana na dira ya serikali ya maendeleo kwani serikali inatumia gharama kubwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo viongozi watakaochaguliwa wawe na sifa na uwezo wa kuongoza,"alisema Myava.

Alisema kuwa wanatoa elimu kwa makundi hayo ili kama yataona kuna viashiria vya rushwa waweze kutoa taarifa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani viongozi bora hawatokani na kutoa rushwa bali ni kwa uwezo wao wa kuongoza.

"Tutaendelea kutoa elimu hadi itakapofikia hatua ya kutangaza matokeo ili tuhakikishe wanapatikana viongozi wenye sifa, waadilifu ili wasimamie rasilimali na fedha zinazotolewa ili wananchi wapate maendeleo,"alisema Myava.

Aliongeza kuwa kiongozi atakayechaguliwa apambane na rushwa kwani serikali inatumia gharama kubwa hivyo tutatoa elimu kupitia mikutano na semina.

"Wananchi nao ni sehemu ya mapambano ambapo viashiria vya rushwa ni kama vile kupewa simu, ajira, fedha, ahadi mbalimbali au vitu vya thamani katika hatua za mwanzo tulipata taarifa za vitendo vya rushwa lakini hakuna ushahidi ambao unaweza kutumika kwani ili kufungua shauri lazima kusiwe na shaka,"alisema Myava.

Aliwataka viongozi wanaowania nafasi za uongozi wazingatie sheria, masharti, kanuni na utaratibu wa uchaguzi ili wasije kujikuta wanaingia kwenye changamoto kwa kukiuka miongozo iliyowekwa.

Friday, November 1, 2024

WAHITIMU MAFUNZO JESHI LA AKIBA WAOMBA AJIRA HALMASHAURI

WAHITIMU wa mafunzo Jeshi la akiba Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani wameomba kufikiriwa katika kupata ajira kwenye Halmashauri walipo badala ya kufanya kazi katika makampuni binafsi ambayo huwalipa mishahara ambayo haiendani na mali wanazolinda.
Aidha wamesema kuwa wanaiomba serikali kukabili changamoto ambazo zingetatuliwa basi vijana wengi wangeshiriki na kumaliza mafunzo hayo kwani baadhi wanashindwa kununua sare kutokana na hali ya kiuchumi.

Walitoa maombi hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga amnaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla fupi ya kufunga mafunzo ya Jeshi la akiba iliyofanyika kwenye uwanja wa Mwanakalenge.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi mshauri wa mgambo wa wilaya ya Bagamoyo Luteni Kanali Rahimu Tumbi alisema kuna baadhi ya changamoto wanazopata wahitimu wa mafunzo hayo kipindi wanapokuwa kwenye mafunzo hayo.

Mkuu wa wilaya ambae ndio mgeni rasmi Shaibu Ndemanga ametumia fursa hiyo kuwaasa vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la akiba wakaishi kiapo walicho kiapa kwa kuwa waadilifu na wasiyatumie mafunzo vibaya wanapokuwa kwenye jamii.