Sunday, October 13, 2024

WAHITIMU KIDATO CHA NNE WATUMIE RASILIMALI ZILIZOPO NCHINI

WAHITIMU wa kidato cha nne nchini wametakiwa kuacha mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha badala yake watumie rasilimali za nchi kuongeza pato la Taifa.

Hayo yalisemwa Jijini na Mkurugenzi Mtendaji wa (SUMA JKT) Brigedia Jenerali Petro Ngata wakati wa mahafali ya 40 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Jitegemee JKT.

Ngata alisema baadhi ya vijana wamekuwa na mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha mazuri na kuacha rasilimali zilizopo ambazo matafa ya nje wanazifuata.

"Msitamani kwenda majuu kwani wa huko wanatamani kuja huku kutumia rasilimali zetu ambazo Mungu ametubariki kuwa nazo na hazipo kokote kule zaidi ya Tanzania hivyo tumieni maarifa mliyopata ili kuzitumia,"alisema Ngata.

Alisema kuwa moja ya rasilimali ambayo vijana wanaweza kuitumia ni ardhi ambayo ikitumika vizuri inaweza kuwainua vijana kupitia maarifa waliyoyapata shuleni ambapo wamefundishwa ujasiriamali pamoja na kilimo.

"Ardhi ni chanzo kikubwa cha shughuli ya kufanya lakini mbali ya kilimo kuna uvuvi, ufugaji na madini kazi siyo lazima kuajiriwa ofisini unaweza kujiajiri mwenyewe kupitia stadi mlizojifunza,"alisema Ngata.

Aidha alisema vijana wanapaswa kuchangamkia fursa zilizopo na kuacha kushiriki kwenye mambo maovu hasa yale yanayohamasishwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo siasa uchwara na kuwa na nidhamu nakutojiingiza kwenye masuala ya ngono.

Naye Mkuu wa Shule hiyo Kanali Robert Kesi alisema kuwa wamewaandaa vizuri wanafunzi kwa kufanya mitihani mingi ya majaribio yenye hadhi ya kitaifa kwa nadharia na vitendo na wameiva .

Kesi alisema kuwa watawafanyia wahitimu semina kwa ajili ya kujiamini kwani kwenye mtihani hakuna maajabu na wasijihusishe na njia za udanganyifu wamshirikishe Mungu kwa kila jambo na kuwa hawataki daraja la nne kwani mwaka jana hakukuwa na daraja sifuri. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Shule Bregadia Mstaafu Lawrence Magere alisema kuwa wanategemea changamoto zilizopo shuleni hapo zitafanyiwa kazi na wanawapongeza walimu kwa maandalizi mazuri kwa wanafunzi hao.

Awali akisoma risala ya wahitimu Shekha Said alisema kuwa moja ya mafanikio waliyopata ni kujifunza elimu ya ujasirismali ambapo wanaweza kutengeneza sabuni, kilimo cha mbogamboga, kutengeneza balbu zilizoungua na kurudi kufanya kazi kama zamani.

Said alisema kuwa shule inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu pia madarasa hayana dari hali inayofanya sauti kuingiliana kati ya darasa na darasa wakati wa masomo, jumla ya wahitimu 89 waliagwa shuleni hapo.

Mwisho.



No comments:

Post a Comment