Tuesday, October 29, 2024

VIJANA NCHINI KUPEWA ELIMU SERA YA VIJANA

ILI kuwapa ufahamu juu ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka (2007) toleo la mwaka 2024 Kamati ya Vijana Wazalendo itafanya makongamano kwenye mikoa 10 hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa Kamati ya Vijana Wazalendo Omary Punzi amesema kuwa Makongamano hayo yatakutanisha makundi ya vijana ambayo yatapatiwa elimu juu ya sera hiyo.

Punzi amesema kuwa sera hiyo ya vijana ni nzuri lakini vijana wengi hawaifahamu hali ambayo inawafanya vijana wengi kutotambua haki zao za msingi na makongamano hayo yatawafikia vijana zaidi ya milioni nane na tisa.

Mwenyekiti wa Kamati ya vijana Wazalendo Farida Kongoi amesema kuundwa kwa sera ya taifa ya maendeleo ya vijana lengo lilikuwa ni vijana wapate mwongozo wa kuendana na masuala ya siasa na kijamii ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa kiteknolojia.

Mwanasheria wa Kamati ya vijana Wazalendo Godfrey Kizito amesema pia vijana watafafanuliwa kuhusu Sheria zinazohusu haki na masuala ya vijana.

Naye Mkurugenzi wa Great leaders organization na Mratibu na Mwandaaji wa kongamano la Wazazi na Walezi nchini Dubai Dk Debora Nyamlundwa amesema katika kongamano hilo kuna kujifinza fursa mbalimbali zilizopo katika taifa hilo kuja kuendeleza hapa nchini



Sunday, October 27, 2024

NISHIBISHE PROJECT YAKUSANYA UNGA KILO 1,115 WANAFUNZI KUNUFAIKA CHAKULA SHULENU

MPANGO wa Nishibishe umefanikisha kupatikana kwa unga wa mahindi kiasi cha kilogramu 1,115 kwa ajili ya kuwapatia lishe wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kwenye Kata ya Kwala Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Viti Maalum ambaye pia ndiye mwasisi wa mpango huo Josephine Gunda wakati wakukabidhi unga huo kwa viongozi wa Kata ili wasambaze kwenye shule husika.

Gunda alisema unga huo umetolewa na wadau mbalimbali kupitia mradio huo ambapo utasambazwa kwenye Shule ya Sekondari moja na Shule za Msingi tatu.

"Malengo ya kutoa chakula shuleni ni ili kupunguza utoro kwa baadhi ya wanafunzi kwani wanakumbana na changamoto ya chakula na kusababisha kutohudhuria masomo kutokana na hali ya kiuchumi,"alisema Gunda.

Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakila mmlo mmoja ambapo mtoto anaenda shule bila ya kula chochote hadi jioni anaporudi kutoka shule hali ambayo inawafanya washindwe kuhudhuria masomo na kuwa watoro.

"Shuleni kukiwa na chakula hata kama nyumbani kuna changamoto mtoto atakula shuleni na atavutiwa kwenda shule na mafanikio tumeyaona kwani utoro ymepungua na ufaulu umeongezeka kwani mwanafunzi akila na akili inakuwa na uwezo mzuri,"alisema Gunda.

Aliongeza kuwa ifike wakati suala la chakula shuleni iwe ajenda ya kudumu na Halmashauri itenge sehemu ya fedha ya mapato ya ndani kwa ajili ya kununua chakula kwani hilo ni tatizo kubwa kwa watoto mashuleni.

Diwani wa Kata ya Kwala Mansuri Kisebengo alisema kuwa mbali ya changamoto lakini wazazi bado wana nafasi ya kuhakikisha lishe ya watoto wao inapatikana.

Kisebengo alisema kuwa anawapongeza wadau hao ambao wamejitolea unga huo kwani watawapunguzia wazazi gharama za chakula kwa watoto wao ambao ni wanafunzi.

Kwa upande wake mratibu huduma za lishe Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Coletha Chapile alisema kuwa lishe ni kitu muhimu sana kwa wanafunzi kwani endapo mtoto hatapata chakula uwezo wake wa kuelewa utapungua.

Chapile alisema kuwa suala la lishe kwa wanafunzi ni muhimu na ni jambo ambalo wazazi, walezi na wadau kulipa kipaumbe kwa kuhakikisha watoto wanapata chakula wakiwa shuleni ili kuongeza uelewa.



Thursday, October 17, 2024

HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAKUSANYA MAPATO ASILIMIA 33 ROBO YA KWANZA


HALMASHAURI ya Mji Kibaha imefanikiwa kukusanya mapato kwa asilimia 33 ya malengo ya ukusanyaji kwenye robo ya kwanza ya makadirio ya makusanyo ya Halmashauri ya shilingi bilioni 8.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Halmashauri Dk Rogers Shemwelekwa  wakati wa kikao cha baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya Julai-Septemba 2024.

Shemwelekwa alisema kuwa kipindi kama hichi mwaka jana walikuwa wamekusanya kwa asilimia 25 hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 8 ya makadirio ya shilingi bilioni 7.

"Tunawashukuru madiwani na wataalamu wa Halmashauri kwa kufikia makusanyo hayo ambayo ni mwanzo mzuri na tunategemea kufikia asilimia 100 tunaomba ushirikiano huu uendelee ili kufikia malengo tuliyoweka,"alisema Shemwelekwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema huo ni mwanzo mzuri wa makusanyo hayo ni mazuri na ushirikiano huo uendelee ili kufikia malengo yaliyowekwa.

John alisema kuwa kwa upande wa uyoaji mikopo asilimia 10 ya Halmashauri dirisha limeshafunguliwa pia zoezi uchongaji barabara kwenye mitaa unaendelea ambapo Halmashauri imetoa milioni 10 kwa kila kata kwa ajili hiyo.

Tuesday, October 15, 2024

MKUU WA MAJESHI AWAVISHANI NISHANI MAJENERALI, MAAFISA NA ASKARI WA JWTZ




Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda kwa niaba ya Mhe Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt Samia Suluhu Hassan amewavisha nishani mbalimbali Majenerali, Maafisa na Askari wa JWTZ Jijini Mwanza tarehe 15 Oktoba 2024.

Nishani hizo ni Nishani ya Utumishi Uliotukuka, Nishani ya Utumishi Mrefu, Nishani ya Utumishi Mrefu na Tabia Njema, Nishani ya Miaka 60 ya Muungano pamoja na Nishani ya Miaka 60 ya JWTZ.

Aidha,Jenerali Mkunda amewavisha nishani ya Jumuiya ya SADC Maafisa na Askari walioshiriki Ulinzi wa Amani nchini Msumbiji chini ya mwavuli wa Jumuiya hiyo.



Sunday, October 13, 2024

SHULE YA UONGOZI YA MWALIMU NYERERE YAINGIA MAKUBALIANO NA CHUO CHA RENMIN CHA CHINA

SHULE ya Uongozi  ya Mwalimu Nyerere imeingia makubaliano  ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Renmin katika nyanja mbalimbali zikiwemo za mafunzo utafiti na kubadilishana wataalamu.

Wakisaini makubaliano hayo kati ya Mkuu wa Shule ya Mwalimu Nyerere Profesa Marcellina Chijoriga na kiongozi mkuu wa Chama Tawala Cha China Cha (CPC) kwenye Renmin Zhang Donggang katika Shule hiyo iliyopo Kibaha Mkoani Pwani walifurahishwa na ushirikiano huo.

Chijoriga alisema kuwa makubaliano hayo yatakuwa ni kwa ajili ya kubadilishana wataalamu ambapo wao watakuja huku na wa Tanzania watakwenda kwao ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu.

“Chuo hicho ni kikubwa sana na cha muda mrefu na kiko vizuri kwenye masuala ya utafiti wa uandishi wa vitabu na katika masuala ya uandishi wa vitabu ambapo ushirikiano huo utakuwa na manufaa makubwa sana kwa pande zote mbili,”alisema Chijoriga.

Alisema kuwa chuo hicho cha Renmin kinauwezo mkubwa wa kuwajengea uwezo viongozi wa chama na serikali kwani kiko vizuri sana katika ufundishaji masuala hayo na watatumia uzoefu ili kujifunza kupitia kwao kwani kimeanza muda mrefu.

“Faida hiyo ni kwa vyama sita vya ukombozi Kusini mwa Afrika ambapo China ni msaidizi mzuri kwani wamesaidia ujenzi wa shule hiyo ambavyo ni CCM, FRELIMO, SWAPO, ANC na ZANU-PF ambapo CPC .  

Aidha alisema kuwa chuo hicho kilichopo Beijeng China kilianza ushirikiano mwaka jana ambapo uongozi wa Shule walikwenda na katibu mkuu wa CCM wakati ule Chongolo na sasa imeanza safari mpya na kina uzoefu mkubwa nani cha zamani sana.

“Tunashukuru sana kwani wametuonyesha ushirikiano mkubwa na makubaliano ya kutengeneza ushirikiano huu ni sasa safari mpya imeanz na leo waametupa vitabu tunawashukuru kwani maktaba yetu sasa itakuwa na vitabu vingi na wasomaji wataweza kujifunza masuala mbalimbali ya nchi ya China,”alisema Chijoriga.

Naye alisema Dk Evaristo Haule Naibu Mkuu wa Chuo Mipango Fedha na Utawala Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere alisema kuwa China imefanikiwa na tumeona namna gani kutumia njia ili kuona wao wamefanyaje na kufikia hatua kubwa kiasi hicho kwenye maendeleo na CPC inavyotoa dira kuongoza nchi yao wanataka twende pamoja katika miradi yao mikubwa ya kidunia.

 Haule alisema kuwa ili kwenda pamoja hivi karibuni Rais Dk Samia Suluhu Hassan alienda China kwenye mkutano wa ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika wao wana dira  na kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu ya kazi na watu wawe na uzalendo wa nchi watu wanaangalia changamoto badala ya kuangalia fursa zilizopo.

Naye Dk Theresia Dominick kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kujifunza kwa kuwa nadhifu na wanaangalia masuala ya ulaji na wawe watu wa kujishusha na kuachana na matumizi yasiyo ya lazima na wasiwe na tamaa.

Dominick alisema  kuwa badhi ya wafanyabiashara Watanzania wamekuwa wakienda China hivyo wanapaswa kujifunza tabia za Wachina za kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu ya jambo wanalolifanya ni mfano wa kuigwa.

Naye kiongozi huyo Zhang Donggang alisema kuwa ushirikiano uliopo baina ya China na Tanzania nan chi nyingine ni katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ambapo wao wanaangalia sana maslahi ya wananchi.

Donggang alisema kuwa nchi za Afrika na China zinapaswa kushikana mkono katika kuhakikisha zinapiga hatua katika masuala ya kimaendeleoili kudumisha umoja uliopo kwani umoja uliopo umeleta mafanikio makubwa.

Mwisho. 


BASHUNGWA ARDHISHWA UJENZI SEKONDARI MPYA YA MSANGANI


WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa ametaka kukamilishwa kwa ujenziwa Shule mpya ya Sekondari iliyopo mtaa wa Msangani Kata ya Masangani Wilayani Kibaha Mkoani Pwani yenye thamani ya shilingi milioni 528 iliyojengwa kwa fedha zitokanazo na mradi wa Seqip.

Bashungwa ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo ambayo iko kwenye hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na upauaji wa baadhi ya majengo mengine yakiwa kwenye hatua ya linta.

Amesema wajenzi hao wahakikishe ujenzi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa ambapo ni Novemba mwaka huu ili Januari mwakani wanafunzi waanze kusoma ili kuwapunguzia umbali wanaotembea kutoka nyumbani na kwenda shule.

Amebainisha kuwa huo ni mwéndelezo wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan wa kuwekeza kwenye sekta ya elimu ambapo hakuna kijiji wala kata ambayo haijajengwa shule na hilo ni jambo la kupongezwa
na anaonyesha jinsi gani anavyothamini na kulipa  umuhimu suala la elimu kwa watoto.

"Wakala wa Barabaraba Nchini (TANROADS) Mkoa wa Pwani hakikisheni manaandika barua wizarani
mkandarasi alipwe ili arudi kazini kukamilisha ujenziwa kipande cha lami kuja Msangani kilichobaki kinakamilka na barabaraba za Tarura nazo mziangalie kupitia mfuko wa barabara ili kuwaondole a kero wananchi,"a lisema Bashungwa.

Aidha amesema kuwa kuhusu barabara ya njia nane wako kwenye mchakato wa kupata wawekezaji ili kuondoa changamoto ya foleni Kibaha ambapo kwa sasa imekuwa kero kubwa kwa wasafiri lengo ni kurahisisha usafiri maeneo yote.

Katika hatua nyingine amesemna kuwa ataongea na Waziri wa Maji ili kufanikisha kujengwa kisima
kwenye shule hiyo ambayo bado haina miundombinu ya maji ili kukabiliana na changamoto ya jami kwani hata maji ya ujenzi yanatolewa mbali.

Kwa upande vwake mkuu wa mkoa wa Pwani
Abubakari Kunenge amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan jumla ya Shule 10 za Sekondari na Shule 10 za Msingi zimejengwa Wilayani Kibaha.

Kunenge amesema kuwa anamshukuru Rais kwa kuupatia mkoa huo fedha za maendeleo kiasi cha
shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya miradi mbalimbali
ya maendeleo hali ambayo inafanya mkoa huo kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kipindi hichi cha awamu ya sita.

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo Lilian Marandu amesema kuwa mradi huo ulitambulishwa mwezi
mmoja uliopita na unatarajiwa kukamilika Novemba ukiwa na awamu saba za ujenzi ambapo kwa sasa umefikia hatua mbalimbali zikiwemo kupaua, lita na msingi.

Marandu amesema kuwa mradi huo una majengo yakiwemo ya utawala, maabara za masomo ya
5 sayansi, madarasa manne, vyoo matundu 12 kichomea taka na mnara wa tanki la maji na ofisi mbili za walimu ambazo wanategemea kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

WAHITIMU KIDATO CHA NNE WATUMIE RASILIMALI ZILIZOPO NCHINI

WAHITIMU wa kidato cha nne nchini wametakiwa kuacha mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha badala yake watumie rasilimali za nchi kuongeza pato la Taifa.

Hayo yalisemwa Jijini na Mkurugenzi Mtendaji wa (SUMA JKT) Brigedia Jenerali Petro Ngata wakati wa mahafali ya 40 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Jitegemee JKT.

Ngata alisema baadhi ya vijana wamekuwa na mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha mazuri na kuacha rasilimali zilizopo ambazo matafa ya nje wanazifuata.

"Msitamani kwenda majuu kwani wa huko wanatamani kuja huku kutumia rasilimali zetu ambazo Mungu ametubariki kuwa nazo na hazipo kokote kule zaidi ya Tanzania hivyo tumieni maarifa mliyopata ili kuzitumia,"alisema Ngata.

Alisema kuwa moja ya rasilimali ambayo vijana wanaweza kuitumia ni ardhi ambayo ikitumika vizuri inaweza kuwainua vijana kupitia maarifa waliyoyapata shuleni ambapo wamefundishwa ujasiriamali pamoja na kilimo.

"Ardhi ni chanzo kikubwa cha shughuli ya kufanya lakini mbali ya kilimo kuna uvuvi, ufugaji na madini kazi siyo lazima kuajiriwa ofisini unaweza kujiajiri mwenyewe kupitia stadi mlizojifunza,"alisema Ngata.

Aidha alisema vijana wanapaswa kuchangamkia fursa zilizopo na kuacha kushiriki kwenye mambo maovu hasa yale yanayohamasishwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo siasa uchwara na kuwa na nidhamu nakutojiingiza kwenye masuala ya ngono.

Naye Mkuu wa Shule hiyo Kanali Robert Kesi alisema kuwa wamewaandaa vizuri wanafunzi kwa kufanya mitihani mingi ya majaribio yenye hadhi ya kitaifa kwa nadharia na vitendo na wameiva .

Kesi alisema kuwa watawafanyia wahitimu semina kwa ajili ya kujiamini kwani kwenye mtihani hakuna maajabu na wasijihusishe na njia za udanganyifu wamshirikishe Mungu kwa kila jambo na kuwa hawataki daraja la nne kwani mwaka jana hakukuwa na daraja sifuri. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Shule Bregadia Mstaafu Lawrence Magere alisema kuwa wanategemea changamoto zilizopo shuleni hapo zitafanyiwa kazi na wanawapongeza walimu kwa maandalizi mazuri kwa wanafunzi hao.

Awali akisoma risala ya wahitimu Shekha Said alisema kuwa moja ya mafanikio waliyopata ni kujifunza elimu ya ujasirismali ambapo wanaweza kutengeneza sabuni, kilimo cha mbogamboga, kutengeneza balbu zilizoungua na kurudi kufanya kazi kama zamani.

Said alisema kuwa shule inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu pia madarasa hayana dari hali inayofanya sauti kuingiliana kati ya darasa na darasa wakati wa masomo, jumla ya wahitimu 89 waliagwa shuleni hapo.

Mwisho.



Saturday, October 12, 2024

MILIONI 1.2 KUANDIKISHWA PWANI

WATU milioni 1.2 Mkoani Pwani wanatarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Akizungumza baada ya kuzindua zoezi hilo kwenye Mtaa wa Mkoani A uliopo Kata ya Tumbi Wilaya ya Kibaha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa idadi hiyo inatokana na sensa iliyofayika ambapo alisema kuwa vijana wengi watakuwa wamefikisha miaka 18 hivyo kuwa na sifa za kujiandikisha kupiga kura.

Kunenge alisema kuwa mkoa una jumla ya vituo vya kuandikisha wapiga kura 2,374 na kuna Vijiji 417, vitongoji 2,028 na Mitaa 72 ambapo wananchi kwenye maeneo hayo wanapaswa kwenda kujiandikisha ili wapate fursa ya kupiga kura itakapofika wakati wa uchaguzi.

“Tumeweka vituo vingi vya kujiandikisha kupunguza msongamano ili kila mtu apate haki ya kujiandikisha ili aje apate fursa ya kupiga kura ambayo ni haki yako ya kikatiba kwa mujibu wa kanuni taratibu na sheria za nchi yetu hivyo wananchi mjitokeze kwa wingi,”alisema Kunenge.

Alisema kuwa viongozi wa kwanza ni wale wa ngazi za chini hivyo kuchagua viongozi hawa ni wa muhimu sana kwani wao wako na wananchi kuanzia chini kabisa hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kuwachagua lakini waanze kujiandikisha kwanza kwani kama mwananchi hajajiandikisha hatapata fursa ya kupiga kura.

“Viongozi tunaoanza nao ni wa ngazi za chini kwa ajili ya kutuletea maendeleo na ndipo msingi wa utawala bora unapoanzia na hawa watatusaidia kutuletea maendeleo hivyo tuhakikishe tunashiriki kwenye uchaguzi huu ni muhimu sana ili kuchagua viongozi wanaotufaa,”alisema Kunenge.

Aidha alisema kuwa wananchi wajipange kushiriki uchaguzi kwani hiyo ni haki ya kikatiba hivyo wale wote waliofikia umri kuanzia miaka 18 wahakikishe wanajitokeza kujiandikisha ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wanaowapenda.

“Hii ni fursa nzuri ya kuchagua viongozi ambao watatuongoza kwa kipindi cha miaka mitano na tukichagua viongozi bora watatuletea maendeleo ndani ya maeneo yetu kuanzia ngazi ya chini kabisa hivyo hii ni fursa kwetu sote kwa maendeleo yetu,”alisema Kunenge.

Kwa upande wake mmoja ya watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambaye ni moja ya watu waliokwenda kujiandikisha Simon Mwaiteleke alisema kuwa hiyo ni nafasi yake ya kumfanya ili aweze kuja kupiga kura kwa viongozi kwenye mtaa wake.

Mwaiteleke alisema kuwa uchaguzi ni hatua ya kupata viongozi watakaowatumikia wananchi hivyo anawaomba watu kujitokeza kwa wingi ili kutumia fursa hiyo ambayo hujitokeza kila baada ya miaka mitano.

Naye Saumu Almasi alisema kuwa hiyo ni fursa kwao wananchi kuchagua viopngozi wa Mtaa kuanzia mwenyekiti na wajumbe wake hivyo anaona ni fursa ya kumchagua kiongozi ambaye ana sifa ya kuongoza mtaa anaotoka.

Almasi alisema kuwa wananchi watumie fursa hiyo kumpata kiongozi bora na wasibaki kulalamika wakati hawashiriki uchaguzi kwani kiongozi bora anapatikana kwa kupigiwa kura na siyo kukaa pembeni na kulalamika.