Sunday, December 31, 2023

ALIYEESHINDA TUZO YA MALKIA WA UINGEREZA ATAKA DIASPORA WAPEWE HADHI MAALUM WAWEZE KULETA MAENDELEO NCHINI.





MTANZANIA ambaye alipata Tuzo ya Malkia Elizabeth || wa Uingereza, Prudence Kimiti amesema kuwapa hadhi maalum Diaspora itasaidia waweze kuwekeza nchini.

Kimiti aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipotua nchini akitokea Uingereza anapoishi ambapo  hadhi hiyo ikitolewa itasaidia sana kwa Diaspora kufanya uwekezaji ili kuleta maendeleo.

Prudence ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa baadhi ya Mikoa hapa nchini alisema kuwa yeye anaipenda Tanzania hivyo anatamani kutoa mchango wake wa maendeleo kwa nchi. 

"Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopambana kuwaletea Watanzania maendeleo hivyo watoe hadhi hiyo maalum kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi na ikiwa hivyo itasaidia kuwekeza ndani ya nchi yao,"alisema Kimiti.

Alisema kuwa suala kupewa hadhi maalumu kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni zuri kwani litasaidia kuleta maendeleo kwenye nchi yao.

Akizungumzia kuhusu tuzo aliyoipata ya Malkia wa Uingereza ya (MBE) aliipata kutokana na kutetea haki za watu weusi hasa wafanyakazi ambapo kuna baadhi ya changamoto wanazipata kutokana na rangi zao.

"Tuzo hii inafaida kubwa kwani inanipa moyo kuendelea kupigania haki za watu dunia nzima siyo Uingereza hata sehemu nyingine kwani napenda kila mtu apate haki yake,"alisema Kimiti.

Aidha alisema kuwa anatarajia kuanzisha shirika kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto na wale waishio kwenye mazingira magumu.

"Tunaendeleza falsafa za mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere ambaye Waingereza wanampenda hivyo najivunia kuwa Mtanzania na tutaendeleza mazuri aliyoyaacha Nyerere,"alisema Kimiti.

Kwa upande wake Mzee Paul Kimiti alisema kuwa wanajivunia tuzo aliyoipata mtoto wao kwani imeiheshimisha familia na nchi kwa ujumla.

Kimiti alisema kuwa tangu mwanae akiwa mdogo alikuwa hapendi kuona mtu anaonewa na hilo amekwenda nalo hadi kufikia kupata tuzo hiyo na si bahati bali ni kitu kiko kwenye damu yake.

Alisema kuwa hata babu yake aliwahi kupata tuzo  mwaka 1950 na sasa mwanae naye anapata tuzo hiyo hivyo ni jambo la kujivunia sana kwa nchi kutokana na tuzo hiyo.

Prudencia Kimiti alipata tuzo hiyo ya malkia hiyo wakati wa malkia kutimiza miaka 70 ya uongozi wa Malkia ambapo hutolewa kila mwaka.

Saturday, December 30, 2023

SIKU YA LISHE YA KIJIJI GAIRO DC


GAIRO DC

SIKU YA AFYA NA LISHE YA KIJIJI

NIMEPATA FURSA YA KUZUNGUMZA NA WAKINA MAMA. 

NIMESISITIZA KUHUSU LISHE, NIMEWAKUMBUSHA MALEZI YA WATOTO KWA KUWALINDA DHIDI YA UKATILI. UZOEFU UNAONESHA KUWA MATUKIO MENGI YA UKATILI YANAANZIA KWENYE NYUMBA ZETU KWA KUWAAMINI NDUGU TUNAOWAKARIBISHA HADI KUWALAZA KITANDA KIMOJA NA WATOTO WETU.

GAIRO DC - KAZI INAENDELEA

@ortamisemi 

@wizara_afyatz 

@rs_morogoro 

@jabiri_makame

Thursday, December 28, 2023

WATU WATATU WAMEFARIKI DUNIA BAADA YA GARI WALILOKUWA WAKISAFIRIA KULIGONGA GARI LINGINE KWA NYUMA

WATU watatu wamefariki dunia na wawili kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuligonga gari lingine kwa nyuma ambalo lilikuwa limesimama.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Lutumo amesema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 28 majira ya saa 11:45 alfajiri eneo la Mbwewe Chalinze Wilayani Bagamoyo.

Amesema kuwa watu hao waliofariki walikuwa kwenye gari lenye namba za usajili T 395 DWE aina ya Alphard likiendeshwa na Mohamed Athuman (40) mkazi wa Jijini Dar es Salaam.

"Gari hilo lilikuwa likuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Kabuku mkoani Tanga ambapo liligonga kwa nyuma gari lenye namba za usajili T 300 CLE na tela namba T 399 AUP aina ya FAW lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara,"amesema Lutumo.

Aidha amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Zakia Mohamed (36) ambaye ni mwalimu, Goletha (23) msichana wa kazi na Nadim Nurdin miezi (8) wote wakazi wa Kabuku.

Amewataja majeruhi kuwa ni dereva wa gari hilo Athuman na Alice Sangule (8) ambaye ni mwanafunzi na mkazi wa Kabuku.

"Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari lililosimama Alphonce Bosco (55) Mkazi wa Mabawa Tanga, kuegesha gari pembezoni mwa barabara bila ya kuweka alama za tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara,"alisema Lutumo.

Aliongeza kuwa miili ya marehemu na majeruhi walipelekwa Hospitali ya Mkata Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga kwa hifadhi na matibabu.

"Jeshi la Polisi linatoa rai kwa madereva kuendelea kuchukua tahadhari na kuheshimu sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazosababishwa na uzembe katika kipindi hichi cha sikukuu kwani watu wengi wanasafiri kuelekea mikoa mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea na familia zao,"amesema Lutumo.


Saturday, December 16, 2023

ATFT KUENDELEZA VIPAJI KUPITIA KIPAJI BILA MIPAKA








KITUO cha kuendeleza vipaji Africa Talent Forum-TZ (ATFT) cha Mkoani Pwani imewakutanisha wasanii wa fani mbalimbali ili kujadili namna ya kuendeleza vipaji vya wasanii ili viweze kutoa ajira.

Akizungumza kwenye kikao maalumu kujadili masuala mbalimbali ya namna ya wasanii wanavyoweza kupata fursa za kuinua vipaji vyao Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho Rosemary Bujash amesema kuwa vipaji hivyo bila ya kuendelezwa havitaweza kufika mbali

Bujash amesema kuwa lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusaidia wasanii na watu wenye vipaji au ndoto mbalimbali waweze kuzifikia ili kujiletea maendeleo kupitia vipaji vyao.

"Katika kuhakikisha vipaji vinaendelea na ndoto za watu zinatimia tumekuja na mradi wa Kipaji bila Mpaka ambapo tutahakikisha Tunaibua, Kukuza na Kuvitangaza ili wafikie malengo na kujiajiajiri kwani kipaji ni ajira,"amesema Bujash.

Kwa upande wake ofisa utamaduni wa Halmashauri ya Mji Kibaha Evarista Kisaka amesema kuwa moja ya changamoto kwa wasanii wachanga ni kutojitangaza hivyo kituo hicho wakitumie ili kutangaza kazi zao.

Kisaka amesema kuwa wasanii hao wanapaswa kujisajili na kutumia fursa mbalimbali zilizopo zinazotokana na sanaa na utamaduni na sanaa siyo uhuni bali ajira kama ajira nyingine na wao ni kioo cha jamii.

Naye mwenyekiti wa Wasanii Kibaha Jimanne Kambi amesema kuwa wasanii wako wengi lakini hawapati fursa kuonyesha vipaji vyao hivyo watashirikiana na kituo hicho kuinua wasanii.

Kambi amesema moja ya njia wanazotumia kutangaza kazi za wasanii ni kuwashirikisha kwenye matamasha mbalimbali ili kazi zao zionekane ambapo katika usajili wameandikisha wasanii zaidi ya 700.

Awali Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mkuza Victoria Andrea amesema kuwa wasanii wanapaswa kuwa wabunifu ili kuboresha kazi zao ziweze kuvutia watu.

Andrea amesema sekta ya sanaa ina ajira kubwa endapo itatumika ipasavyo kwani ina fursa nyingi zikiwemo za mikopo kwa ajili ya wasanii hivyo ni wao kujisajili ili watambulike kisheria.

Wednesday, December 6, 2023

TPFNET CHALINZE WATOA MSAADA KITUO CHA WATOTO DOLPHINE.

 

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mkoa wa Pwani, Disemba 05, 2023 wametoa msaada kwa watoto wenye uhitaji katika kituo cha Dolphine kilichopo Kijiji cha Kipera, Kitongoji cha Mwanabele Wilayani humo.

Akizungumza akiwa kituoni hapo,  Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sophia Lyidenge alisema jukumu la ulezi wa watoto wenye uhitaji na kuwatunza ni la jamii nzima hivyo wao wakiwa ni sehemu ya wazazi wameguswa katika siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa Kijinsia kufikia kwa watoto hao wenye uhitaji na kuweza kutoa msaada wa vitu mbalimbali. 

"Jamii inapaswa kutambua malezi ya watoto na kuwatunza na kuwatembelea mara kwa mara kujua changamoto walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi watoto wenye uhitaji kwenye vituo vya malezi ni la watu wote na kufanya hivyo ni kuwapa faraja watoto walio kwenye vituo hivyo kuona jamii ina wajali na kuwathamini".Alisema Lyidenge.

Lyidenge amewapongeza wasimamizi wa kituo hicho kwa malezi ya watoto hao akiweka wazi kuwa jambo wanalolifanya la kuwalea watoto kwenye maadili mema ni kubwa sana mbele ya Mungu na la kupongezwa. 

Amesema kuwa watoto hao endapo wangeachwa bila ulezi kwenye kituo hiki wangeweza kuwa katika makuzi mabaya hivyo kutumbukia kwenye makundi ya kihalifu na hivyo kupeleka Jamii kuwa na kizazi kisichokuwa na maadili.

Aidha, Lyidenge amewaasa watoto hao kuwa wasikivu kwa walezi wao na kutambua kuwa wao ni taifa la kesho akiwasisitiza kusoma kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za changamoto walizonazo kwa walezi wao bila woga ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa jamii  Bi. Linna Jackson Mlay ameahidi kuendeleza ushirikiano na walezi wa kituo hicho katika kutatua changamoto mbalimbali walizonazo.

Nae msimamizi wa kituo hicho Anna Munisi amelishukuru Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze kwa msaada waliowapatia na kuomba wananchi wengine kuendelea kusaidia kituo hiko kwani uhitaji ni mkubwa katika maelezi ya watoto waliopo kituoni hapo.

Msaada uliotolewa na Jeshi la Polisi kituoni hapo ni unga wa sembe, mchele, sabuni,  madaftari, kalamu na taulo za watoto.

Monday, December 4, 2023

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE MKOA WA PWANI YAWATAKA WANAWAKE KUMUENZI BIBI TITI MOHAMED KWA KULETA MAENDELEO

WANAWAKE nchini wametakiwa kupambana kuiletea nchi maendeleo kama alivyofanya Bibi Titi Mohamed ambaye aliasidiana na Mwasisi wa Taifa Julius Kambarage Nyerere kuleta uhuru wa Tanzania.

Aidha amewataka kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuwapatia fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo. 

Hayo yamesemwa Mlandizi Wilayani Kibaha na Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani Omary Punzi wakati wa mafunzo kwa wanawake ya Ijue Kesho yako.

Punzi amesema kuwa katika kupigania nchi kupata uhuru alishirikiana na Bibi Titi Mohamed hadi Uhuru ukapatikana hivyo wanawake nao wawe mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya nchi.

"Nyerere alijenga misingi ya maendeleo na aliona umuhimu wa mwanamke na ndiyo sababu alishirikiana na Bibi Titi katika mapambano ya Uhuru hivyo nanyi msikae nyuma lazima mpambane kuleta maendeleo ya nchi,"amesema Punzi.

TASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA PWANI YAWAPONGEZA WAANDAJI WA MAFUNZO YA IJUE KESHO YAKO KWA WANAWAKE MLANDIZI KIBAHA

 


Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani ndugu Omary Punzi wakati wa mafunzo ya Ijue Kesho yako kwa wanawake wa mkoa wa Pwani yaliyofanyika Mlandizi Wilayani Kibaha.

Punzi alipata nafasi ya kuwashukuru na kuwaambia wanawake kuwa Mwalimu Nyerere alijenga misingi ya Uzalendo, kujituma na kujitoa kwa hali na mali katika nchi na misingi ambapo misingi hiyo ilitokana na nguvu ya Mwanamke katika kuleta maendeleo.

Alisema Mwalimu Nyerere katika Uongozi wake alijitahidi sana kuwainua wanawake mfano mzuri ni Bibi TITI MOHAMMED ambaye alikuwa karibu sana na Mwalimu katika kupigania Uhuru wa Taifa  na hakuna Taifa lolote linaloendelea ikiwa Mwanamke atawekwa nyuma.

"Ushauri wangu serikali inatakiwa kuwekeza nguvu kubwa ya kuhakikisha mwanamke anapatiwa mahitaji yote ya msingi endelevu ya kumwezesha katika kumuinua kiuchumi,"alisema Punzi.

Kwa upande wake mgeni rasmi Mkali Kanusu mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini ambaye alimwakilisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM NEC Hamoud Jumaa, aliwapongeza waandaji na wawezeshaji kwa mada zilizokuwa zinatolewa ni nzuri na mahiri kwa wakati tulionao kwa Serikali ya Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kanusu alishauri matukio kama hayo yafanyike mara mbili kwsa mwaka kwani itasaidia kuwakumbusha watu maadili ya Watanzania na kama chama wamelipokea na kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za maendeleo kwa wanawake wa Kibaha na Tanzania kwa ujumla.

Naye Mwakilishi wa Taasisi ya IJUE KESHO YAKO Ndugu Martha Kyoka alisema lengo kuu la Taasisi hiyo ni kuhakikisha wanamjengea uwezo mwanamke kujitambua na kutekeleza malengo katika maisha na jamii kwa ujumla ambapo takribani wanawake 100 walipatiwa mafunzo hayo.

Masomo waliyofundishwa ni pamoja na Afya ya Akili, malezi ya mume na mtoto nyumbani, nafasi ya kujitambua, Uwekezaji, Maono na Mikopo na Ujasiriamali.