WAFANYABIASHARA PWANI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA KWENYE JUMUIYA
Na John Gagarini
JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani imewataka wafanyabiashara kujiunga ili wanufaike na fursa mbalimbali zilizopo kwenye Jumuiya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa majukumu ya taasisi hiyo pamoja na fursa zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo katibu wa JWT Mkoa Wellu Mtaki amesema kwenye Jumuiya hiyo kuna fursa nyingi.
Mtaki amesema kuwa Jumuiya hiyo inamuwezesha mfanyabiashara kutatua changamoto zake na mfanyabiashara anauwezo wa kutoa kero maoni na mapendekezo yanayohusu biashara na taasisi ikafikisha sehemu husika kwa ajili ya utatuzi tofauti na mtu kupeleka kero yake mwenyewe.
"Lengo la Jumuiya ni kuwaunganisha kwa pamoja wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwawezesha kutoa mawazo na maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa na kuziwasilisha serikalini,"amesema Mtaki
Amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara nchini Tanzania na moja ya huduma ni kuwaunganisha na bima za aina tofauti ambazo zimeanza kutolewa kwa wanachama.
"Huduma za bima zinazotolewa ni pamoja na bima ya Elimu au Carrier Life Plan kupitia shirika la bima la Jubilee ambalo linamsaidia mtoto wa mwanachama kunufaika kwenye elimu, bima ya Afya ambayo ina kifurushi cha aina tatu ambacho Scare individual and Family health insurance, pamoja Afya, Jubilee Afya na huduma ya bima ya nafaka," Amesema Mtaki.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote mkoani Pwani kuhakikisha wanafuata taratibu na miongozo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kepuka changamoto zitakazojitokeza.
Aidha amesema kuwa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania haijihusishi wala kufungamana na udini, ukabila, siasa, wala ushabiki wa michezo.