Na John Gagarini,Rufiji
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi
Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Suleiman
Bulenga kwa kushindwa kudhibiti na kusimamia mapato yatokanayo na shughuli za
misitu hivyo kuikosesha mapato Serikali.
Mbali ya meneja huyo maafisa misitu watatu nao
wamesimamishwa kutokana na kushindwa kudhibiti na kusimamia shughuli za uvunaji
misitu na kusababisha wilaya kukosa mapato .
Maofisa misitu waliosimamishwa ni pamoja na Ofisa
maliasili na mazingira wa wilaya Dk Paul Ligonja,Ofisa misitu Gaudence Tarimo
na Jonas Nambua ambao watsimamishwa hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Majaliwa alichukua hatua hiyo wilayani Rufiji
wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji na wananchi
wa wilaya hiyo na kusema kuwa sekta ya
misitu ni tatizo kwa kila wilaya na Rufiji ni moja ya wilaya hizo .
“Magogo yanasafirishwa bila utaratibu,na ndio
wanakata miti kwenye misitu ya Utete na kupiga nyundo maeneo ya Kilwa,” alisema
Majaliwa.
Alisema kuwa hakuna manufaa na TFS hivyo ameamua
kusimamisha shughuli zote za uvunaji,katika wilaya hiyo na watumishi hao hadi
wizara itakapotoa maelekezo mengine.
“Wilaya ya Rufiji inaongoza katika suala la
utoroshaji wa misitu na kuruhusu uvunaji holela suala ambalo halikubaliki na
nataka uwajibikaji na uadilifu katika maeneo ya kazi na watumishi wanapaswa wabadilike
na waache kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Majaliwa.
Aidha Majaliwa alikemea utozwaji wa ushuru kwa watu
wanaochoma mkaa unaofanywa na halmashauri ya Rufiji kwani kwa kufanya hivyo ni
kuruhusu ukataji ovyo wa miti.
“Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa
halamshauri ya Rufiji mnapaswa kusimamia mapato na matumizi ya fedha ili kuongeza
mapato ya halmashauri iweze kupiga hatua ya kimaendeleo,”alisema Majaliwa.
Naye mbunge wa
Rufiji,Mohammed Mchengelwa alisema kuwa nidhamu kwa watumishi inaonekana
kupungua kwa baadhi ya watumishi kwenye halmashauri hiyo.
Mwisho