Na John Gagarini,
Kibaha
CHAMA Cha Wasioona Nchini
kimewataka vijana wenye ulemavu huo kuachana na dhana ya kuwa mara wamalizapo
elimu mbalimbali ni laziwa waajiriwe badala yake wajiandae kwa kufanya shughuli
za kujiajiri wenyewe.
Hayo yalisemwa mjini
Kibaha na makamu mwenyekiti wa chama hicho Taifa Robert Bundala wakati wa
mafunzo ya sera ya ajira kwa watu wenye ulemavu kwa vijana wanachama wa chama
hicho wilayani Kibaha.
Bundala alisema kuwa
soko la ajira kwa sasa ni gumu sana hivyo lazima vijana wajiwekee malengo ya
kujiajiri wao wenyewe kupitia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kuliko kusubiri
kuajiriwa serikalini au sekta binafsi.
“Vijana wasioona
wanapaswa kuachana na dhana hiyo badala yake wajiajiri kwa kupitia shughuli
mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujasiriamali na si kutegemea kuajiriwa kwani
upatikanaji wa ajira kwa sasa ni mgumu,” alisema Bundala.
Alisema kuwa ushindani
wa soko la ajira hapa nchini kwa sasa ni mkubwa sana kwani hata watu wasiona na
ulemavu wamekuwa wakilalamika hivyo lazima vijana hao watumie mafunzo
mbalimbali wanayoyapata ili kujiajiri.
“Kwa sasa ubaguzi umepungua
lakini kikubwa kinachoangaliwa ni uwezo wako wa kielimu kwani kwa wale wenye
elimu nzuri wamepata ajira lakini lazima wabadili mfumo wa kusubiri ajira
badala yake wajiajiri,” alisema Bundala ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi.
Naye Mwezeshaji wa
mafunzo hayo ambaye naye ni mlemavu asiyeona Greyson Mlanga alisema kuwa ni
vema vijana wakaangalia fursa za ajira zilizopo kwenye maeneo wanayoishi na
kuwaondolea fikra kuwa lazima waajiriwe.
Mlanga alisema kuwa
kutokana na ugumu wa ajira vijana wasioona wanapaswa kuangalia suala la
kujiajiri kwani kutegemea ajira za kuajiriwa itakuwa ni vigumu sana kuweza
kufanikiwa kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake moja ya washiriki wa mafunzo
hayo Zuhura Omary alisema kuwa changamoto kwao ni nyingi kutokana na hali
waliyonayo pia ni kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha hivyo kujikuta
wakikosa ajira.
Mafunzo hayo
yaliwahusisha vijana wasioona wapatao 60 kutoka kata nne za Misugusugu, Visiga,
Kibaha na Kongowe na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
WANANCHI wametakiwa
kuhakikisha wanazingatia matumizi ya dawa za minyoo kila baada ya miezi mitatu
ili kuepukana na athari ikiwa ni pamoja na magonjwa ya Kisukari na Presha.
Hayo yalisemwa mjini
Kibaha na Ofisa afya Mstaafu Allice Bakari alipozungumza na waandishi wa habari
na kusema kuwa minyoo ni chanzo cha magonjwa hayo makubwa ambayo yanasababisha
vifo.
Bakari alisema kuwa
kutokana na watu kutotumia kabisa dawa za kuua minyoo kumesababisha watu kupata
athari kubwa za kiafya kutokana na ulaji wa vyakula ambao husababisha watu
kupata minyoo.
“Minyoo ni chanzo cha
magonjwa mengi makubwa yakiwemo moyo kutanuka, kuchanganyikiwa, mba na baadhi
ya viuongo vya ndani kuathirika na kushindwa kufanya kazi na hatimaye ni kifo,”
alisema Bakari.
Alisema kuwa tatizo la
minyoo linazidi kuwa kubwa kutokana na baadhi hata ya wahudumu wa afya kuumwa
kutokana na kutotumia dawa za minyoo kutokana na kutotambua ukubwa wa tatizo
hilo.
“Hata baadhi ya madaktari
wameathiriwa na hali hiyo kutokana na kutoona kuwa minyoo ni tatizo lakini ukweli
ni kwamba hili ni tatizo kubwa sana na inabidi wahudumu wa afya kulifuatilia
kwa umakini ili kuwanusuru watu,” alisema Bakari.
Ofisa afya huyo ambaye
alikuwa akifanya kazi kwenye hospitali ya Tumbi iliyopo wilayani Kibaha alisema
kuwa minyoo inapokuwa imekithiri mwilini hushambulia viungo mbalimbali vya
ndani ya mwili na kuleta athari hizo.
“Ushauri ni kwamba
madaktari wanapaswa kuwa makini kwa kuwashauri wagonjwa kutumia dawa za kuwaua
wadudu hao kwa kujua kuwa endapo walishawahi kutumia dawa kwani watu wanafikiri
minyoo ni kwa watoto pekee,” alisema Bakari.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
MRADI mkubwa wa Maji
wilayani Kibaha mkoani Pwani unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu na kuondoa
tatizo la ukosefu wa maji ambapo baadhi ya vitongoji wananchi wameanza kukimbia
bili za maji.
Akizungumza na
wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa uzinduzi wa matawi
ya chamaa hicho Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa
mara mradi huo utakapokamilika tatizo hilo itakuwa ni historia.
Koka alisema kuwa
mradi huo wa maji ambao chanzo chake ni mto Ruvu utapitia kwenye mitaa yote ya
Jimbo hilo ambapo kwa kipindi kirefu wananchi wamekuwa wakilalamika upatikanaji
wa maji.
“Tunashukuru kuwa
kwenye mradi uliotokea wilaya ya Bagamoyo baadhi ya mitaa ikiwemo ya Vikawe,
Vikawe shule maji yanapatikana kwa wingi ambapo sasa watu wanakimbia bili
kutokanana kushindwa kulipa kwani awali walikuwa na changamoto kubwa ya ukosefu
wa maji,” alisema Koka.
Alisema kwa sasa maji
yamesambazwa kwenye mitaa 14 na mara mradi huo utakapokamilika wakazi wa Kibaha
hawatanyanganyana maji na Jiji la Dar es Salaam ambao wanategemea chanzo kimoja
hivyo maji kuwa ya mgao.
“Nawaomba msiwe na
wasiwasi kwani mradi huo unaendelea vizuri ambapo kwa sasa wanatandaza mabomba
ambayo kwa sasa yamefika eneo la Kongowe kilometa 10 kutoka hapa mjini hivyo
Mungu akipenda wakati huo uliotajwa maji yatapatikana,” alisema Koka.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
WANAWAKE wajawazito
wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuacha kutumia dawa za kienyeji za
kuongeza uchungu ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Hayo yalisemwa na
ofisa muuguzi wa kituo cha afya cha Mkoani, Prisca Nyambo alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho hivi karibuni na kusema kuwa
dawa hizo zianasababisha watoto kufia tumboni.
Nyambo alisema kuwa
dawa hizo za kuongeza uchungu za kienyeji ni mbaya kwa watoto waliotumboni
kwani wengi wamekuwa wakipoteza maisha.
“Tatizo la watoto
kufia tumboni kwa sasa ni kubwa kutokana na wajawazito kutumia dawa hizo ili
waweze kujifungua endapo muda umefika na hakuna dalili za kufanya hivyo,”
alisema Nyambo.
Alisema kuwa
wajawazito wanapaswa kwenda hospitali wanapoona muda wa kujifungua umefika
lakini hawajifungui kuliko kutumia dawa hizo ambazo zinasabisha vifo vya
watoto.
Aidha alisema vifo vya
watoto wachanga ni kati ya saba na tisa kwa kila mwezi kutokana na sababu
mbalimbali mojawapo ikiwa ni matumizi ya dawa hizo za kienyeji za kuongeza
uchungu ambapo wastani wa wanawake wanaojifungua kwa kipindi hicho ni zaidi ya
300.
Alibainisha kuwa
akinamama wajawazito wanaokwenda kujifungua hapo ni wengi kwani baadhi yao
wanatoka maeneo ya Jiji la Dar es Salaam kama vile Mbezi, Kibamba, Kimara na
Ilala kutokana na ukaribu.
Mwisho.