Na John Gagarini, Kibaha
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Abdulrahman Kinana amezishauri Halmashauri nchini kulipatia Shirika la
Nyumba Tanzania (NHC) viwanja bure ili liweze kujenga nyumba kwa bei nafauu
ambazo wananchi wa hali ya chini wataweza kuzinunua.
Aliyasema hayo jana mjini Kibaha
kwenye mkutano wa hadhara pamoja na kukabidhiwa mashine rahisi za kufyatulia matofali
kwa vijana wa mkoa wa Pwani kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani hapa.
Kinana alisema kuwa tatizo la ukosefu
wa nyumba za kuishi ni kubwa hasa kwenye miji hivyo endapo NHC ingejenga nyumba
nyingi ingesaidia wananchi kuweze kununua nyumba hizo kwa bei nafuu au
kupangisha kwa gharama ndogo.
“Nawapongeza NHC kwa kufanya mageuzi
makubwa ya ajira kwa kuwasaidia vijana pia kwa kuwapatia mashine hizi ambazo
zitakuwa ni mkombozi kwao kwani mbali ya kujiongezea kipato pia wataweza
kujenga nyumba kwa gharama nafuu na za kisasa,” alisema Kinana.
Alisema haya ni mapinduzi makubwa na
mapya kwenye Taifa ambalo liko kwenye kazi kubwa ya kuhakikisha vijana wanapata
ajira kwani mashine hizo zitawazalishia fedha na kuleta mabadiliko kwenye sekta
ya ujenzi hapa nchini na kufanya gharama za nyumba kushuka.
Akimkabidhi mashine hizo meneja wa
NHC Paulina Mrango alisema kuwa wameamua kutoa mashine hizo kwa lengo la
kuisaidia serikali kukabiliana na uhaba wa ajira pia kufanya ujenzi kwa gharama
nafuu.
Mrango alisema kuwa wametoa mashine
28 kwa vikundi vya vijana kwenye Halmashauri zote za mkoa wa Pwani ambapo
mpango huo utakuwa kwa nchi nzima ili kufanikisha ufyatuaji wa matofali ya kisasa
kwa kutumia gharama ndogo ya malighafi.
“Tumetoa mashine hizo 28 zenye
thamani ya shilingi milioni 12.6 kwa Halmashauri na tutazipatia fedha kiasi cha
shilingi 500,000 kama mtaji wa kuwakopesha wanavikundi hao ambapo vikundi
vitakavyopewa mashine hizi vitapatiwa mafunzo ya wiki mbili na wakufunzi kutoka
VETA ili wajue namna ya kuzitumia,” alisema Mrango.
Aidha alisema kuwa mbali ya tofali
hizo kuwa za gharama nafuu pia itasaidia utunzaji wa mazingira kwani maeneo ya
vijijini wengi wanatumia tofali za kuchoma ambazo zinachomwa kw akutumia kuni
zinazotokana na miti hivyo kuharibu mazingira.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SHIRIKISHO la Watu Wenye Ulemavu
Tanzania (SHIVYAWATA) wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba serikali
kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu na wazee wanapata dawa wanazoandikiwa na
daktari mara waendapo hospitalini.
Akiuliza swali mbele ya katibu mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana kwenye mkutano wa hadhara
wakati wa ziara yake mkoani humo, mwenyekiti wa shirikisho hilo Ally Mkanga
alisema kuwa wamekuwa wakinyimwa dawa na kutakiwa kwenda kununua kwenye maduka
ya dawa.
Mkanga alisema kuwa sera inasema kuwa
wazee, watoto chini ya miaka mitano na wanawake wanaojifungua huduma ni bure
lakini hupaswa kununua pia mbali ya kutakiwa kulipia dawa kwenye mahospitali hazipatikani na kutakiwa
kununua kwenye maduka hayo.
“Tunaiomba serikali ihakikishe sera
zake za matibabu bure kwa makundi yanayopaswa kutolipia dawa hayalipishwi kwani
inakuwa changamoto kubwa kwao hasa wazee na watu wenye ulemavu,” alisema
Mkanga.
Alisema watu wenye ulemavu wanapata
shida wanapokwenda hospitali kwani mazingira kwao si rafiki hivyo wameiomba
serikali kuhakikisha inaweka mazingira rafiki kwa wao kupata huduma za afya.
Akijibu swali hilo mkuu wa wilaya ya
Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa ni kweli kuna changamoto hizo lakini
wameweka madirishwa kwa ajili ya wa wazee kwenye hospitali ya wilaya ya Mkoani
lakini tatizo dawa wanazopewa ni za hadhi ya kituo cha afya.
“Kituo cha afya cha Mkoani
kilipandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya lakini mgao wake wa dawa
inapata kama kituo cha afya na si hospitali ya wilaya jambo ambalo ni
changamoto kubwa hasa ikizingatiwa Hospitali ya Tumbi imepandishwa hadhi na kuwa mkoa ya Rufaa ambapo wagonjwa wote
wanatakiwa waanzie hapa hivyo kumekuwa na mlundikano mkubwa wa wagonjwa,”
alisema Kihemba.
Kihemba alibainisha pia katika
kukabiliana na tatizo la dawa kwenye mahospitali wameunda kamati ya dawa ili
kuhakikisha inafuatilia suala la upatikanaji wa dawa na kutolewa kwa utaratibu
unaotakiwa ili kuondoa malalamiko kwa wagonjwa wanaopata huduma kwenye
halmashauri ya wilaya.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wadogo wilayani
Kibaha mkoani Pwani wameilalamikia Halmashauri ya wilaya ya Kibaha kwa
kuwalipisha kodi na ushuru mkubwa na kuwa mzigo mkubwa kwao hivyo kushindwa
kufanya biashara.
Akiuliza swali mbele ya katibu mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana ambaye alikuwa mgeni rasmi
kwenye mkutano wa hadhara ambao ulifanyika kwenye uwanja wa Bwawani wa Bwawani
Maili Moja wilayani Kibaha, mwenyekiti wa soko la Maili Moja Ally Gonzi alisema
wamekuwa wakilipa kodi nyingi.
Gonzi alisema kuwa halmashauri hiyo
imekuwa ikiwatoza kodi na ushuru mbalimbali na kuwa kero kwa wafanyabiashara
wadogo kwenye soko na maeneo mengine ya mji huo na kuwafanya wawe kwenye wakati
mgumu wa kufanya biashara zao.
“Tunaiomba serikali itupunguzie mzigo
wa kodi kwa ni nyingi na wengine biashara zao ni ndogondogo na za mkopo lakini
tunabanwa tulipie tunajikuta mitaji inakufa kutokana na kodi hizo ambazo ni
kubwa kuanzia 50,000 na hadi zaidi ya 100,000 hivyo tunashindwa kujikwamua
kwenye hali ngumu,” alisema Gonzi.
Aidha alisema kuwa Halmashauri imekuwa ikitumia nguvu kubwa kwa
kutumia askari wenye silaha au mgambo wakati wa kuja kuchukua kodi kwa
wafanyabiashara ambao wanajitafutia riziki za familia zao.
Kwa upande wake Kinana alizitaka Halmashauri nchini kupunguza
kodi ambazo ni kero kwa wananchi pia ziwashirikishe wafanyabiashara kabla ya
kuzipitisha kwani baadhi yao wanatafuta hela za kula tu.
Kinana alisema kuwa miaka michache
iliyopita serikali ilifuta kodi ambazo zilikuwa kero lakini kodi hizo zimerudi
mlango wa nyuma na kuwafanya wafanyabiashara wadogo wazilalamikie kwani
zimekuwa mzigo mkubwa kwao.
“Hawa wanajitafutia fedha kwa ajili
ya familia ili wapate chakula na riziki hivyo lazima halmashauri zifikirie upya
suala la kodi kuwa nyingi kwa wafanyabiashara wadogo kutokana na hali hii
nitaongea na wabunge wa CCM ili kuondoa kodi ambazo ni mzigo kwa
wafanyabiashara wadogo,” alisema Kinana.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji
wa Kibaha Adhu Mkomambo alisema kuwa wao kama Halmashauri watakaa kuangalia
namna ya kurekebisha kodi na ushuru mbalimbali ili kuondoa kero hizo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WALINZI wa Halmashauri ya Mji wa
Kibaha mkoani Pwani wameulalamikia uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kushindwa
kuwaajiri kwa kipindi cha miaka 10 sasa.
Akizungmza kwa niaba ya wenzake mbela
ya katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana kwenye mkutano
wa hadhara kwenye uwanja wa Bwawani wilayani Kibaha mkoani Pwani, Jafar
Mtimbuka alisema kuwa amefanya kazi kwa kipindi cha miaka 10 bila ya kuajiriwa
huku akiwa kama kibarua.
Mtimbuka alisema kuwa wamefanya kazi
kama vibarua kwa kipindi hicho pasipo kuajiriwa na kuambiwa kuwa hawana sifa
jambo ambalo si la kweli kwani baadhi yao wamehitimu mafunzo ya mgambo na
wengine Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Katibu hata kama nitafukuzwa kazi
sawa lakini tunaomba utusaidie kwani tumefanyakazi muda mrefu kama vibarua bila
ya ajira wanasema hatuna sifa wakati mimi nimehitimu mafunzo ya JKT nashangaa
wanasema kuwa hatuna sifa,” alisema Mtimbuka.
Kwa upande wake mkurugenzi wa
halmashauri hiyo Jenifa Omolo alipotakiwa kujibu suala hilo alisema kuwa
analifahamu suala hilo lakini walinzi hao hawana sifa na halmashauri haikuwa na
utaratibu wa kuajiri kada hizo zikiwemo zile za chini.
Omolo alisema kuwa kwa sasa wamepata
kibali kwa ajili ya kuajiri kada za chini wakiwemo walinzi na wengine hivyo
kama watakuwa na sifa wataajiriwa kulingana na uwezo wao.
Naye katibu Mkuu Kinana alisema kuwa
mtu kafanya kazi miaka 10 anaambiwa hana sifa jambo ambalo halipendezi inabidi
waangaliwe na wanastahili kuajiriwa kama wafanyakazi wengine.
“Mwenye sifa aajiriwe na huyu wa
miaka 10 ana haki ya kuajiriwa haiwezekani mseme hana sifa kwa miaka hiyo
aliyofanyakazi kwani sheria ni miezi mitatu na amefanyiwa vibaya si haki,”
alisema Kinana.
Kinana alisema kuwa mlinzi huyo
aajiriwe na fedha zake za utumishi kwa kipindi hicho ziunganishwe kwenye mafao
yake wakati wa kustaafu kwenye pensheni yake.
Mwisho.