Na
Mwandishi Wetu, Kibaha
IMEBAINIKA
kuwa uwepo wa mabanda ya kuonyeshea video mitaani ambayo hayapo kisheria
kumechangia vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto wadogo ambao ni wanafunzi
wa shule za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Kwa
mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha
umebaini kuwa watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo nyakati za usiku
wanapokuwa wamekwenda kuangalia video ambapo waonyeshaji wa video hizo
huonyesha picha chafu za ngono.
Mabanda
hayo ambayo mengi yamejengwa kwa mbao au mifuko ya sandarusi na kuezekwa na
makuti au nyasi na yasiyo na mvuto yamekuwa yakionyesha picha hizo maarufu kama
pilau, kachumbari na ubwabwa na majina mengine ambayo kwa mtu wa kawaida si
rahisi kujua maana yake.
Baadhi
ya wakazi ambao wamelaani uwepo wa mabanda hayo ambayo huanza kuonyesha video
majira ya asubuhi hadi usiku na kusababisha baadhi ya wanafunzi kushinda humo
huku wakiwa wameaga wanakwenda shule na kuishia humo na endapo wazazi
hawatafuatilia kuna hatari ya mwanafunzi huyo kutohudhuria darasani kabisa.
Walimwelezea
mwandishi wa habari hizi kuwa njia wanazotumia wabakaji hao ni kuwalipia
kiingilio cha kuangalia picha ambacho ni shilingi mia tano kwa filamu
ziltakazoonyeshwa kwa siku hiyo ambazo huonyeshwa kwa awamu na huchukua kila
awamu zaidi masaa matatu kisha kubadili picha zingine.
Picha
zinapokuwa zinaendelea mara hubadili na kuweka picha chafu za ngono hivyo
kuhamasisha vitendo hivyo na kwa kuwa vijana hao wanaobaka watoto wanakuwa
wamewalipia kiingilio huwachukua na kuwapakata watoto hao na wanapokuwa
wamepandwa na msisimko huanza kuwaingilia watoto hao hadi wanapomaliza haja
zao.
“Mara
wamalizapo haja zao huwapa fedha kwa ajili ya kuwataka wasiseme kwa wazazi wao
ambapo watoto hao baadaye huzoea na kujikuta kila wakati wakienda kwenye
mabanda hayo na kufanyiwa vitendo hivyo na kuzoea hali ambayo ina waathiri
kisaikolojia na kufanya maendeleo yao shuleni kushuka,” walisema wakazi hao.
Akizungumza
na mwandishi mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lulanzi wilayani Kibaha mkoani
Pwani Anna Bilali alisema kuwa wanafunzi wengi wameathiriwa na hali hiyo ambapo
mbali ya kwenda kwenye mabanda hayo mara wasipokwenda shule huandika kazi
walizofanya wenzao kisha kujisahishia ili kuwadanganya wazazi wao.
“Wanafunzi
wa namna hii wamekuwa wakijisahishia madaftari yao lakini sisi tunagundua kwani
usahishaji wao ni tofauti na wa walimu na tunapowaambia baadhi ya wazazi
wamekuwa wakiwatetea watoto wao hali inayosababisha ugumu wa kuwadhibiti kwani
baadhi ya wanafunzi hukaa kwenye mabanda hayo hadi saa tatu usiku bila hata
kuulizwa walikokuwa,” alisema Bilali.
Alisema
pia baadhi yao humiliki simu ambazo wanakwenda nazo shuleni na kuangalia picha
hizo na kujikuta muda mwingi wakiutumia kwa kuangalia picha hizo kupitia simu
ambazo huwa wanazificha na inakuwa vigumu kuwagundua hadi wenzao watoe taarifa.
Aidha
alisema kuwa kuna watu wamekuwa wakiwaonyesha picha hizo kupitia simu kisha
huwatoza kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kupata huduma hiyo hali amabayo
inaendelea kuongeza kusambaa kwa vitendo viovu.
Kwa
upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema kuwa udhibiti wa
mitandao kama hiyo ya uonyeshaji wa picha za ngono ni viongozi wa mtaa na
vijiji kwa kuwachukulia hatua kwani hayako kisheria hivyo hayana sababu ya
kuwepo ili kuondoa tatizo hilo.
Hivi
karibuni wanafunzi wanne wa shule ya msingi Lulanzi walikamatwa na polisi
wilayani Kibaha kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenzao wa darasa la pili
mwenye umri wa miaka tisa na kumsababishia maumivu makali na kulazwa hospitali
ya Tumbi ambapo aliruhusiwa kutoka wiki iliyopita baada ya kupata matibabu.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu,
Kibaha
MKUU wa mkoa wa
Pwani Mwantumu Mahiza amewashukia maofisa ugani na kusema kuwa hatasita
kuwaondoa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao na kudai maslahi na vitendea kazi
huku uwajibikaji wao ukiwa chini hali inayowafanya washindwe kuwaletea
mabadiliko wakulima.
Mahiza aliaysema
hayo jana mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na madiwani, wenyeviti, watendaji
na wataalamu wa mitaa na kata kwenye mji wa Kibaha, wakati mkutano wa kujadili
changamoto na mafanikio kupitia mpango wa matokeo makubwa kwa sasa.
Alisema kuwa
maofisa ugani wengi mkoani Pwani wamakuwa hawawajibiki na kukaa tu huku
wakifikiri wamekwenda kutalii ndani ya mkoa huo huku wakulima wakiwa hawana
msaada wowote licha ya kulima bila ya kupatiwa stadi za kilimo bora.
“Mimi mwenyewe
nimelima mashamba ya mazao mbalimbali lakini hakuna ofisa ugani hata mmoja
ambaye aliweza kunitembelea kunipa ushauri wa kitaalamu sembuse mkulima wa
kawaida ni jambo la kushangaza sana hakuna anayejishughulisha hali hii
haikubaliki hata kidogo tutawaondoa wale watakaoshindwa kutimiza wajibu wao,”
alisema Mahiza.
“Kama kuna ofisa
ugani ambaye alimtembelea mkulima na kumpa ushauri wa kitaalamu asimame hakuna
hata mmoja aliyefanya hivyo je mnafanya nini kama hamuwezi kazi ni vema
mkaondoka mkafanye kazi sehemu nyingine lakini hapa kwangu sitakubali watu
wasiowajibika,” alisema Mahiza.
Aidha alisema
anashangazwa na maofisa hao kushindwa kuwa na eneo kwa ajili ya hata kulima
bustani ya mchicha ili kuonyesha mfano ambapo kiongozi anapaswa kuwa mfano kwa
wale anaowaongoza si kukaa tu.
“Sasa hivi mnaomba
usafiri wa kwenda wapi wakati uwajibikaji ni mdogo mtapewa pikipiki mtadai
mafuta baadaye mtadai gari kisha dereva lakini utendaji kazi hauonekani itakuwa
haisaidii mnapaswa kuwajibika ndipo mdai haki kwani huwezi kudai haki wakati
hauwajibiki,” alisema Mahiza.
Aliongeza kuwa
maofisa hao hakuna hata mmoja mwenye daftari la kujua idadi ya wakulima au
mpango kazi wa mwaka mzima kujua atafanya nini sasa ataweza vipi kutekeleza
majukumu yake bila ya kujua masuala mazima ya wakulima.
“Kutokuwa makini
kunasababisha kupikwa kwa takwimu sisi tunachotaka hali halisi na si
kutengeneza pia mkumbuke mwaka juzi tuliwaomba mipango kazi ya kata zenu
mlituletea lakini cha kushangaza hamjatekeleza hata jambo moja,” alisema
Mahiza.
Aliwataka
watendaji wa sekta mbalimbali kuwajibika kwa nafasi zao na si kukaa tu pia
watembee wasikae ofisini badala yake wawatembelee wananchi kujua mahitaji yao
na kuachana na tabia ya kutengeneza takwimu mezani bali wajionee hali halisi.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu,
Kibaha
KIJANA aitwaye
Ibrahimu Jumapili (30)mkazi wa Kongowe wilayani Kibaha mkoani Pwani amekufa kwa
kujinyonga kwa kutumia kanga kwenye mti wa mkorosho.
Kwa mujibu wa
mwenyekiti wa mtaa wa Bamba wilayani Kibaha Amry Mavala alisema kuwa marehemu
hakuweza kuacha ujumbe wowote wa sababu ya kuchukua maamuzi hayo ya
kujiua.
Mavala alisema
kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 17 mwaka huu majira ya saa 6:30 mchana
kwenye mtaa wa Bamba kata ya Kongowe wilayani humo.
“Marehemu alikuwa
akijishughulisha na kazi ya ufayatuaji matofali na kabla ya kifo chake alikuwa
akilalamika kuwa kuna watu walikuwa wakitaka kumtoa kafara,” alisema Mavala.
Alisema kuwa
kutokana na hali hiyo marehemu alisema kuwa anamwachia Mungu na itambidi arudi
nyumbani kwao mkoani Singida ili ajinusuru na hali hiyo.
Kwa upande wake
kaimu kamanda wa polisi mkoani Pwani Juma Ali alisema kuwa mwili wa marehemu
ulikutwa ukininginia kwenye mkorosho kwenye shamba la Mzee Rafael.
Ali alisema kuwa
chanzo cha kifo chake hakijaweza kufahamika na mwili wa marehemu uko kwenye
hospitali ya Tumbi kwa ajili ya uchunguzi wa daktari na taratibu za mazishi.
Wakati huo huo
mwili wa mtu asiyefahamika umeokwotwa huko kwenye mtaa wa Kwa Mathiasi wilayani
Kibaha ukiwa umeharibika vibaya ambapo ulikutwa na jeraha shingoni na mtu mmoja
anashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, na mwili huo ulizikwa hapo hapo baada ya
kushindwa kuhamishwa.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu,
Kibaha
WATU sita
wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Pwani wakiwemo wawili wanaodai
kuwa ni askari polisi kwa tuhuma za kukutwa na nguo zinazosadikiwa kuwa ni za
magendo kutokea nchini Kenya.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake jana kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Juma
Ali alisema kuwa watuhumiwa walikamatwa na gari lililokuwa limebeba nguo za
kike na kiume.
Ali alisema kuwa
tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9 alfajiri eneo la Vigwaza wilayani
Bagamoyo kwenye kizuizi wakati askari wakiwa doria kwenye barabara ya Dar es Salaam
Chalinze.
Alisema kuwa
watuhumiwa wawili ambao ndiyo walikuwa kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za
usajili T 303 BAY lenye mzigo huo lilikuwa likiendeshwa na Omary Salehe (66)
mkazi wa Arusha na utingo Fuwad Salimu (46) mkazi wa Moshi.
“Wakati gari hiyo
ikiwa inaendelea na safari yake ilikuwa ikifukuzwa kwa kasi ilipofika Mbwewe na
gari nyingine aina ya NOAH yenye namba za usajili T 641 CCH ikiwa na watu wanne
wakiwemo watu hao wawili ambao bado hawajathibitishwa kama ni polisi kutokea
mkoani Tanga au la huku mwingine akiwa askari mstaafu na mtu mwingine,” alisema
Ali.
Aidha alisema kuwa
wanaendelea na uchunguzi juu ya kujua thamani ya mzigo huo na kuwatambua watu
hao kama ni askari kweli au la ili hatua sahihi ziweze kuchukuliwa ambapo
magari hayo bado yanashikiliwa na watuhumiwa wanahojiwa kupata ukweli.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu,
Kibaha
MTU mmoja mkazi wa
Kongowe Joseph John (17) anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za
kumlawiti mwanafunzi (jina tunalo).wa shule ya Msingi Kongowe mwenye umri wa
miaka 11.
Akizungumza na
waandishi wa habari shangazi wa mtoto huyo Rukia Bora alisema kuwa alimgundua
mtoto huyo kuingiliwa baada ya kulalamika kuwa anasikia maumivu shemu za haja
kubwa.
Bora alisema kuwa
alimgundua mtoto huyo wa mdogo wake wa kiume kuingiliwa Septemba 12 mwaka huu.
Alisema kuwa baada
ya kumhojia alimwelekeza alipokuwa akifanyiwa mchezo huo kwa muda sasa ambapo
ni karibu miezi mitatu iliyopita tangu kuanza kufanyiwa hivyo na mtuhumiwa na
watu wengine ambao walikimbia na bado wanatafutwa.
“Huyu mtoto
anaishi na bibi yake lakini kwa kuwa mimi na bibi yake tuko jirani hapa Kongowe
Kati wakati mwingine anakuja kwangu hivyo tunamlea kwa pamoja ambapo baba yake
yuko Jijini Dar es Salaam na mke we waliasha achana lakini kutokana na tabia za
mtoto za utundu udhibiti wake ulikuwa mgumu,” alisema Bora.
Aidha alisema kuwa
baada ya kumhoji alikataa kusema ikabidi wampeleke polisi na baada ya kubanwa
ilibidi aseme ukweli na kueleza kila kitu.
“Alisema kuwa
chumba (Ghetto) alichokuwa akifanyiwa mchezo huo wanaishi vijana watupu ambao
wanajihusisha na uimbaji kwenye shghuli mbalimbali za sherehe, ambapo walikuwa
wakimwingilia kwa nyakati tofauti muda wa usiku na kumwambia asiseme kwa mtu
yoyote,” alisema Bora.
Alibainisha kuwa
chanzo cha yeye kujua hilo ni baadhi ya majirani kuona kuwa mtoto huyo kuwa
karibu na mtuhumiwa hali ilyowatia shaka majirani.
“Baada ya kugundua
nilimfuata mtuhumiwa na kumkamata na kumpeleka polisi hata hivyo watuhumiwa
wengien wawili walikimbia ambapo jana watoto wawili ambao nao walikuwa
wakimfanyia hivyo walipelekwa polisi kuhojiwa na kinachosubiriwa ni mtoto huyo
kwenda kuwatambua,” alisema Bora.
Alisema kwa sasa
mtoto huyo anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Tumbi.
Kwa upande
wake kaimu kamanda wa polisi mkoani Pwani Juma Ali alisema kuwa mbali ya
mtuhumiwa huyo watuhumiwa wengine walikimbia na wanaendelewa kutafutwa.
Ali alisema
kwa sasa kinachosubiriwa ni gwaride la utambulisho wa watuhumiwa wawili wadogo
ambao ni wanafunzi ili nao waunganishwe na mtuhumiwa wa kwanza.
Mwisho.