Monday, March 31, 2025

NMB KUTUMIA ZAIDI YA BILIONI 6 MIRADI YA MAENDELEO

BENKI ya inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 6.4 kwa ajili ya kuchangia shughuli za maendeleo kwa mwaka wa 2025.

Hayo yalisemwa na Meneja wa benki hiyo Kanda ya Dar es Salaam ambaye aliwakilishwa na meneja wa tawi la Mlandizi Wilayani Kibaha William Marwa wakati wa Kongamano la Vijana juu ya umuhimu wa kushiriki mbio za mwenge mkoa wa Pwani 2025.

Alisema vijana wanapaswa kujua historia ya mbio za mwenge wa uhuru na fursa zilizopo kupitia mwenge ambao ni alama ya mshikamano wa kuleta maendeleo ya nchi.

"Tangu mwenge umeanza mbio zake kwa sasa ni miaka 61 na pia tunakumbuka kifo cha mwasisi wa Taifa letu miaka 26 iliyopita lazima tumjue kwani aliifanyia nchi hii mambo makubwa,"alisema Marwa. 

Akizungumzia benki hiyo ambayo ni kubwa kuliko zote nchini imekuwa ikichangia maendeleo na ni chachu kwa kuchangia kwenye sekta ya afya, elimu na kutoa mkono wa pole kwa wananchi wanaopata majanga.

"Benki imekuwa ikirudisha sehemu ya faida kwa kuchangia suala la maendeleo kupitia sekta mbalimbali kwani wao ni sehemu ya wateja kwani ina matawi wilaya zote nchini,"alisema Marwa.

Alisema kuwa benki hiyo ina matawi 241 Atm 720 mawakala 50,000 na wateja milioni 8.7 kote nchini na bado inaendelea kuboresha huduma zake kimtandao.

Sunday, March 30, 2025

WAZIRI MKUU MAJALIWA AUPIGIA DEBE UWANJA WA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KUTUMIWA NA TIMU ZA CHAN NA AFCON

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameupigia debe uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha kutumiwa na Timu za Taifa zitakazokuwa zinajiaandaa na michuano ya  CHAN na AFCON kwa ajili ya mazoezi.

Majaliwa aliyasema hayo alipotembelea kuukagua uwanja huo ambao utatumika kwenye usinduzi wa mbio za mwenge 2025.

Majaliwa alisema kuwa jana alifanya ukaguzi wa viwanja vitatu viyakavyotumika kwa ajili hiyo ambavyo ni vichache.

"Tanzania tumepata uenyeji wa mashindano hayo mawili ambayo ni makubwa hivyo lazima tuwe na viwanja vingi kwa ajili ya mazoezi na hichi kikiboreshwa kinaweza kutumika,"alisema Majaliwa.

Alisema kuwa wataangalia uwezekano wa uwanja huo kutumiwa kwa ajili ya mazoezi na tutaongea na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama watakikubali itabidi kitumike.

"Kiwanja hichi kikiimarishwa vizuri kinaweza kutumika kwa ajili hata ya ligi kuu ni uwanja mzuri unahitaji maboresho kidogo tu kwani hata taa zipo kwa kweli hapa ni pazuri,"alisema Majaliwa.

Aidha alisema hayo ni matunda ya uwekezaji kwenye sekta ya michezo ambapo Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameamua kuwekeza kwenye michezo.

"Kwa vijana wa Halaiki msiishie hapa endeleeni na mazoezi hii iwe ni sehemu ya kuanzia kwa wale watakaocheza mpira wa miguu, pete, riadha na michezo mingine ili muendeleze vipaji vyenu isiwe hapa ndiyo mwisho,"alisema Majaliwa.



WAZIRI MKUU MAJALIWA ARIDHISHWA MAANDALIZI UZINDUZI WA MWENGE WA UHURU PWANI 2025

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kuangalia maandalizi ya uwanja utakaotumika kuzindua mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 mkoani Pwani.

Majaliwa alitembelea uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha kuangalia maandalizi ya uzinduzi huo na kuridhishwa na maandalizi hayo na kutaka wakamilishe sehemu ambazo bado hazijakamilika.

Alisema kuwa ameridhishwa na maandalizi hayo ambapo pia alitumia muda huo kutembelea watoto wa halaiki na kusema amefurahishwa na jinsi walivyokuwa na hamasa ya uzinduzi huo.

"Nawapongeza kwa maandalizi mnayoendelea nayo nimeridhishwa kamilisheni sehemu zilizosalia ili kukamilisha mapema,"alisema Majaliwa.

Alisema kuwa amefurahishwa kuona viongozi wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu wakiwa mstari wa mbele kuhakikisha maandalizi yanakuwa mazuri.

"Alikeni hata mikoa ya jirani Dar es Salaam, Morogoro na Tanga na watu mbalimbali kwani hili ni jambo la kitaifa shirikisheni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili hamasa iwe kubwa,"alisema Majaliwa 

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete maandalizi yako vizuri ila baadhi ya maeneo ikiwemo katikati ya uwanja ndiyo kunahitaji marekebisho kidogo.

Kikwete alisema kuwa mialiko kwa wageni mbalimbali imetolewa ikiwa ni pamoja na wakuu wa mikoa, wakurugenzi na watu wengine ili kushiriki uzinduzi huo.


Friday, March 28, 2025

VIJANA WAFUNDISHWE UMUHIMU WA MBIO ZA MWENGE

TAASISI mbalimbali nchini zimetakiwa kuwajengea uwezo vijana juu ya umuhimu wa mbio za Mwenge wa Uhuru katika kujenga uzalendo na uwajibikaji katika usimamizi wa shughuli za maendeleo na kutambua fursa za kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Skauti Mkuu Nchini na Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta wakati Kongamano la Vijana juu ya umuhimu wa kushiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025.

Mchatta amesema kuwa vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa namna ambavyo mtaelekezwa na viongozi katika maeneo wanayoishi.

"Tukifanya hivyo tutaupata ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa ufasaha ili muweze kushuhudia kwa vitendo yale yote mtakayojifunza katika Kongamano hili,"amesema Mchatta.

Amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kundi la vijana katika kuleta mageuzi ya Kijamii na Kiuchumi kutokana na ari, nguvu na ubunifu walionao. 

"Kwa kutambua hilo serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitoa kipaumbele kwa vijana kupata elimu na makuzi bora kuwapa fursa ya kupata mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri na Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build Better Tomorrow – BBT) 

Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 utazinduliwa mkoa wa Pwani kitendo ambacho kinaonesha nia njema ya Dk Samia Suluhu Hassani Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendeleza na kuenzi kwa vitendo yale yote aliyoturithisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Kwanza wa Tanzania. 

Kwa upande wake mratibu wa Kongamano hilo Omary Punzi amesema kuwa ili vijana waweze kufikia mafanikio ya kimaendeleo lazima wazingatie falsafa za Mwalimu Nyerere alizotumia wakati wa kuwashwa Mwenge wa Uhuru.

Punzi amesema moja ya falsafa za Mwenge wa Uhuru ni kuwafanya watu wawe na uzalendo kwa kujitoa kwa ajili ya nchi yao na kutokomeza maadui watatu ujinga umaskini na maradhi. 

Mbio za Mwenge wa Uhuru zitazinduliwa katika viwanja vya Shirika  la Elimu Kibaha Mkoani Pwani na Mgeni rasmi atakuwa Dk Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

mwisho.


Wednesday, March 26, 2025

MAKAMU WA RAIS DK MPANGO KUZINDUA MBIO ZA MWENGE KITAIFA PWANI

MAKAMU wa Rais Dk Philip Isdor Mpango atazindua mbio za Mwenge kitaifa Mkoani Pwani Aprili 2 mwaka huu kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya juu ya uzinduzi huo amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi yanaenda vizuri.

Kikwete amesema kuwa tayari Makamu wa Rais ameshathibitisha kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa mbio za  Mwenge kwa mwaka 2025.

"Kwa vitu vilivyobakia niwaombe mhakikishe vinafika kwa wakati ili kila kitu kiwe kwenye sehemu yake na bado tutaendelea kuangalia maandalizi ili siku hiyo mambo yawe mazuri,"amesema Kikwete.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maandalizi yako vizuri ambapo hadi Machi 29 mambo mengi yatakuwa yamekamilika.

Kunenge amesema kuwa huduma zote zitapatikana kuanzia suala la afya, vyoo, maji, taa kubwa, umeme ambapo kutakuwa na jenereta endapo umeme utakatika.

Amewataka wananchi wa Mkoa huo na mikoa jirani na Watanzania kwa ujumla kujitokeza siku hiyo ili kuweka historia ya Pwani kuzindua mbio za Mwenge Kitaifa.

Tuesday, March 25, 2025

JK AWASILISHA UJUMBE MAALUMU KWA RAIS WA SENEGAL KUTOKA KWA RAIS SAMIA

Mhe. Rais Mstaafu  Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewasilisha  ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Senegal, Mhe. Bassirou Diomaye Faye jijini Dakar.

Katika mazungumzo  yao ya kirafiki,  Rais Mstaafu alieleza dhamira ya dhati ya Rais Samia na Serikali anayoiongoza ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Senegal.

Pamoja na masuala ya ushirikiano wa kiserikali, Rais Mstaafu pia alisisitiza umuhimu wa kukuza uhusiano baina ya wananchi wa mataifa haya mawili kupitia sekta za elimu, biashara, utalii, na maendeleo ya vijana na wanawake.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Tanzania kuimarisha uhusiano wa kimataifa na mataifa ya Afrika Magharibi, huku ikiweka msisitizo kwa diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa watu kwa watu.

MAANDALIZI UWASHWAJI MWENGE WA UHURU KITAIFA PWANI MBIONI KUKAMILIKA



MAANDALIZI ya Uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa yamefikia asilimia 96 ambapo Mwenge huo utawashwa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani Aprili 2 Mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maandalizi yanaenda vizuri.

Kunenge amesema kuwa kwa sasa zimebaki siku sita ambapo Mwenge utazinduliwa Aprili 2 na utatembelea kwenye Halmashauri tisa za mkoa huo kwa kuanza na Halmashauri ya Mji Kibaha utakapoanzia.

"Uwanja umekamilika yamebaki maeneo machache ambapo hadi leo sehemu kubwa itakuwa imekamilika na kubaki mambo madogo madogo,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa majukwaa yamekamilika na matarajio ni kuwa na watu 16,000 ambapo miundombinu ya maji, sehemu ya magari kukaa tayari, taa, mifumo ya majitaka na ulinzi viko tayari.