TIMU ya soka ya Nyika imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Mkoa wa Pwani kwa kuifunga timu ya Kiduli kwa goli 1-0 kwenye mchezo wa fainali wa ligi daraja la tatu ngazi ya Mkoa.
Mchezo huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Mwendapole Mjini Kibaha ulihudhuriwa na viongozi wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), viongozi wa Chama Cha Soka Wilaya ya Kibaha KIBAFA na vyama vya Wilaya zingine na vyama shiriki na mashabiki wengi wa Kibaha.
Mwenyekiti wa COREFA Robert Munis akizungumza mara baada ya mchezo huo amesema kuwa lengo lao ni kuhakikisha mpira unachezwa ili kukuza vipaji vya soka Pwani.
Munis amesema kuwa fainali hiyo ambayo ilionyesha kiwango kikubwa cha wachezaji wa timu hizo zimeonyesha jinsi gani zilivyojiandaa na vijana kuonyesha uwezo mkubwa.
"Lengo letu ni kuhakikisha tunapambania timu zetu angalau zifike kucheza ligi kuu ya NBC angalau timu moja na hilo linawezekana kama tutaunganisha nguvu na kuziunga mkono timu zetu,"amesema Munis.
Kufuatia ushindi huo timu ya Nyika ilipewa kombe na itawakilisha mkoa wa Pwani kwenye mashindano ya Ligi ya mabingwa wa Mikoa (RCL) mwakani.