Na John Gagarini, Bagamoyo
WAISLAMU kote nchini
wametakiwa kusherehekea sikuu ya Eid el Fitr kwa upendo na amani ili funga yao
ya mwezi mzima iwe na maana na kuacha kufanya vitendo viovu ambavyo ni kinyume
na mapenzi ya Mungu.
Ushauri huo umetolewa jana mjini
Bagamoyo na meya wa Mji wa huo Abdul Sharifu, wakati alipokuwa akifuturisha
watu wenye mahitaji maalumu na waumini wa dini hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya
wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Sharifu alisema kuwa funga
hiyo itakuwa na maana endapo waislamu wataisherehekea kwa kuzingatia imani ya
dini ya kiislamu na si kinyume na dini inavyosema.
“Baadhi ya waislamu wamekuwa
wakiitumia siku hiyo kwa ajili ya kufanya matendo ambayo hayampendezi mwenyezi
Mungu hali ambayo inafanya waonekane mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa hawakufunga
kutokana na kwenda kinyume na imani inavyosema,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa pia watumie
siku hiyo kwa ajili ya kujitolea kuwasaidia
watu wenye mahitaji maalumu kama vile watu wenye ulemavu, yatima, wajane
na wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali ili iwe sadaka ambayo itampendeza
Mungu.
Sharifu ambaye pia ni
mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo aliwataka waumini wa dini
hiyo na wale wasio wa imani hiyo kuitumia siku hiyo kwa ajili ya kumtafakari
mwenyezi Mungu.
Wakati huo
huo wenye uwezo mkoani Pwani wametakiwa kumtukuza Mungu katika kipindi cha siku
kuu ya Eid
el Fitr
kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji ili wapate thawabu mbele ya mwenyezi Mungu.
Hayo
yalisemwa jana mjini Kibaha na msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini
Mkoani Pwani, Method Mselewa ambaye
alimwakilisha mbunge huyo Silvestry Koka wakati wa kutoa mkono wa Iddi kwa
waumini wa dini ya Kiislamu kutoka misikiti mbalimbali wilayani hapa.
Mselewa
alisema kuwa kutoa wakati wa kipindi hichi ni sadaka ambayo ina manufaa makubwa
kwa waislamu hivyo wawe na moyo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao
wajisikie kama kuna watu wanawajali.
“Mbunge kila
mwaka kipindi kama hichi amekuwa akijitolea kwa makundi hayo ambayo ni pamoja
na wazee, yatima, wajane na wale wasiojiweza ambapo kila msikiti wanatoka watu
20 ili nao waweze kuandaa futari kwa familia zao,” alisema Mselewa.
Alisema kuwa
waumini hao wanatoka kwenye misikiti 64 iliyopo katika Jimbo la Kibaha ambapo
kila mmoja anapewa mkono wa Iddi ambao ni mchele kilogramu mbili, sukari
kilogramu moja na fedha kwa ajili ya kununulia mboga.
Aidha
alisema kuwa mbali ya kuwapatia vitu hivyo pia huwapatia ujumbe wa Iddi wa kudumisha
amani, upendo na ushirikiano kwa watu wote katika kipindi hichi na nyakati
zingine ambazo si za mfungo.
Alibainisha
kuwa mbali ya makundi hayo pia mkono wa Iddi unatolewa kwa viongozi wa chama
wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Baraza la Wanawake (UWT), Baraza
la Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo jumla ya watu 2,000 watafikiwa.
Mwisho.