Friday, February 28, 2025

MWENGE WA UHURU KITAIFA KUWASHWA PWANI APRILI 2,2025

WANANCHI wa Mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia fursa za kiuchumi kwa kuwashwa mwenge wa uhuru mkoani humo Aprili 2 mwaka huu.

Hayo yamesemwa jana Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema kuwa kuwashwa mwenge wa uhuru Mkoani Pwani ni fursa kiuchumi kwa wananchi pia ni chachu ya maendeleo kwani wananchi watafanya biashara za chakula, malazi, usafiri, vinywaji na utalii.

"Wananchi tumieni fursa hiyo ya uzinduzi wa mbio hizo za mwenge wa uhuru kwa kufanyabiashara ambapo kutakuwa na wageni wengi na hata wenyeji ambao watahitaji huduma mbalimbali,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa sherehe hizo za uzinduzi zitapambwa na matukio mengi yakiwemo ya halaiki na burudani nyingine za wasanii.

"Baada ya uzinduzi huo mwenge wa uhuru utakimbizwa katika Halmashauri tisa za mkoa huo ambapo utakagua, kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo,"amesema Kunenge.

Aidha amewahamasisha na kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Pwani na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo.

"Maandalizi yanaendelea vizuri ambapo muda bado unatosha na mwaka huu tumejipanga vyema kuhakikisha tunafanya vizuri,"amesema Kunenge.

mwisho. 


Monday, February 24, 2025

SHULE ZA AWALI NA MSINGI BINAFSI 101 ZANUFAIKA NA MRADI WA OPPORTUNITY INTERNATIONAL-MOSHA

Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam, Eva Mosha, ametoa rai kwa wamiliki na walimu wa shule binafsi za awali na msingi kuimarisha ufanisi wa ufundishaji na kuboresha ubora wa elimu, ili kuinua taaluma katika shule zao.

Amesisitiza ,shule hizo zinapaswa kuongeza ubunifu na kujiendeleza kwa kupata mafunzo mbalimbali ya namna ya kuendesha shule zao, ili kuepuka changamoto za kushindwa kuendeleza shule au kukosa wanafunzi.

Mosha alitoa rai hiyo katika hafla ya kupongeza walimu na wamiliki wa shule binafsi za awali na msingi, ambazo zinatoa ada nafuu, waliopatiwa mafunzo ndani ya miaka mitatu kupitia mradi wa Opportunity International ,kwenye ukumbi wa Victoria uliopo Kimara Temboni, Dar es Salaam. 

Mratibu wa Mradi wa Opportunity International Tanzania (HES Tanzania), Oliver Kapaya, alieleza kuwa mradi huo ulianza mwaka 2018 na umefanikiwa kuhusisha shule 101 katika kipindi cha miaka mitatu.

Alieleza, shule 74 zilipata mafunzo na kufuzu kwa kipindi cha miaka minne na shule 15 zimefanikiwa kupata tuzo za kutambua ufanisi wao huku, shule nane zimetunukiwa tuzo kwa utendaji bora.

Violet Oketch, mratibu wa Mradi wa Opportunity International Afrika (HES Africa), alieleza mradi huu unatekelezwa katika nchi nane za Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Rwanda, Zambia, Ghana, DRC Congo, Uganda, Kenya, na Nigeria.

Violet Oketch alishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ushirikiano wake na wawekezaji na wafadhili mbalimbali katika sekta ya elimu. 

Brayson Ephata Maleko, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu Temeke, alisema mradi huo umehusisha shule za awali na msingi, namna ya kuendesha shule kwa ufanisi, kupanga mipango, na kusimamia rasilimali fedha.

PWANI YAZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka watumishi ambao ni wanasheria kwenye Mkoa huo kuwahudumia wananchi kwenye kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Kunenge ameyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya siku tisa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Mkoani Pwani.

Amesema kuwa kampeni hiyo ni nzuri na itawasaidia wananchi wanyonge ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za kisheria na kumshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kubuni kampeni hiyo.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini amesema kuwa kampeni hiyo ni kuwezesha wanyonge wanapata haki zao kwa wakati.

Naye Naibu Waziri wa maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum Mwanaid Khamis amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya ukatili wa kijinsia, matunzo ya watoto, ardhi na ubakaji.

Mwakilishi wa bodi ya ushauri wa msaada wa kisheria Nuru Awadh amesema kuwa siku tisa ni chache kwani changamoto ya masuala ya kisheria ni kubwa sana hivyo ili kuwafikia wananchi wengi hivyo huduma ziendelee kutolewa.

Mkurugenzi wa mashirika yanayotoa msaada wa kisheria (TANLAP) Christina Ruhinda amesema kuwa kila kata ina wasaidizi wa kisheria nchi nzima ambao wanasaidia kutoa elimu na msaada wa kisheria.


Saturday, February 15, 2025

WAANDISHI WA HABARI WAJENGEWA UWEZO JUU YA MALEZI MAKUZI MAENDELEO YA WATOTO

WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kuleta mabadiliko chanya kwenye masuala ya malezi na makuzi ya watoto ili kuja kupata viongozi bora wa baadaye.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Osifa Programu kutoka Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Victor Maleko ambaye alikuwa mwezeshaji wa mafunzo kuhusu uandishi wa habari zinazohusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM).

Maleko alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa ukuaji wa watoto ambao wanatakiwa kupata huduma muhimu katika ukuaji wao ili wawe na makuzi mazuri.

WAANDISHI WATAKIWA KUANDIKA HABARI SAHIHI ZA UCHAGUZI

NAIBU Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amevitaka vyombo vya habari kuandika habari sahihi kipindi cha uchaguzi ili kudumisha amani.

Ameyasema hayo Mjini Dodoma alipokuwa akifunga Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini.

Mwinjuma amesema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutoa taarifa sahihi ambazo zitawafanya wananchi kuchagua viongozi bora ambao watailetea nchi maendeleo.

"Kazi yenu kubwa ni kutoa taarifa sahihi kwa wananchi ambao wanaviamini vyombo vya habari kupata taarifa za ukweli na siyo za kupotosha ili kupata viongozi bora,"amesema Mwinjuma.

Kwa upande wake Mhandisi Endrew Kisaka ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) amesema kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuandika habari za vyama vya siasa wakati wa uchaguzi bila ya upendeleo.

Kisaka amesema kuwa waandishi wazingatie kuandika sera na siyo majibizano au udini, ukabila na kutoingilia faragha za watu na kotoegemea upande wowote bali watoe nafasi kwa watu wote.

Naye katibu wa Mtandao wa Bloggers Tanzania (TBN) Khadija Kalili ameishukuru  TCRA na kuiomba kupunguza gharama za usajili ambapo kwa sasa ni shilingi 500,000 ambayo ni kubwa hivyo wengi kushindwa kulipia.

Kalili alisema kuwa TBN ilisajiliwa mwaka 2015 na ilianza na wanachama 100 hadi kufikia 300 ambapo baadhi walijitoa kutokana na kushindwa kusajili.

Mkutano huo wa mwaka ambao uliansaliwa na TCRA ulihusisha washiriki 528 ambao wanajihusisha na masuala ya utangazaji na watoaji maudhui mtandaoni nchini, waandishi wakongwe wa Redio Tanzania.

WAZIRI KABUDI ATAKA WATANGAZAJI KUACHA MBWEMBWE WATUMIE KISWAHILI SANIFU

WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Profesa Kabudi amewataka watangazaji kuacha mbwembwe na kubananga Kiswahili na kutumia Kiswahili Sanifu ili Tanzania iendelee kuwa nchi inayotumia Kiswahili fasaha.

Profesa Kabudi ameyasema hayo Mjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa vyombo vya utangazaji nchini.

Amesema kuwa Tanzania ni nchi kinara wa lugha ya Kiswahili lakini endapo hakutakuwa na juhudi za makusudi za kukisimamia Kiswahili hatutakuwa vinara tena wa lugha hiyo.

"Watangazaji wanapaswa kutumia Kiswahili fasaha na sanifu kwani tuna utajiri wa misamiati hivyo tukitumie vizuri ili kuandaa vipindi vyenye tija kwa wasikilizaji,"amesema Kabudi.

Naye Mkurugenzi wa Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk Jabiri Bakari amesema kuwa wamekuwa wakifanya utafiti juu ya maudhui ya mtandaoni ili kutoa taarifa sahihi na za umahiri.

Bakari amesema kuwa kuna utafiti umefanywa ambapo utakamilika mwezi huu lengo kuu likiwa ni kuboresha utoaji wa maudhui mitandaoni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui Saida Muki amesema kuwa watangazaji wa maudhui mitandaoni wanapaswa kuweka maslahi ya nchi mbele  na kujiepusha na maudhui yanayokiuka maadili.

 

Tuesday, February 11, 2025

WAANDIKISHAJI WASAIDIZI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA HALMASHAURI YA MJI KIBAHA WAASWA





WAANDIKISHAJI wasaidizi wa zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa kuwa waadilifu na waaminifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa waandikishaji wasaidizi kwenye Halmashauri hiyo.

Shemwelekwa amesema kuwa waandikishaji hao wasaidizi wamepewa jukumu kubwa na wameaminiwa kwani zoezi hilo ni la Kitaifa hivyo wahakikishe wanalifanya kwa weledi ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.

Amesema mafunzo hayo yawe chachu ya utendaji kazi wao kwenye zoezi la uboreshaji taarifa za wapiga kura na kuandikisha wapiga kura wapya litakuwa la siku saba kuanzia Februari 13 hadi 19.

Amewataka watumie lugha nzuri wakati wakiwahudumia wananchi ili iwe sehemu ya kuwavutia watu wengi wajitokeze kuboresha taarifa zao na kuandikisha wapiga kura wapya.

Jumla ya waandikishaji 262 wamepatiwa mafunzo hayo na kuna vituo 131 vitatumika kwenye zoezi hilo ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.