WATU milioni 1.2 Mkoani Pwani wanatarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Akizungumza baada ya kuzindua zoezi hilo kwenye Mtaa wa Mkoani A uliopo Kata ya Tumbi Wilaya ya Kibaha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa idadi hiyo inatokana na sensa iliyofayika ambapo alisema kuwa vijana wengi watakuwa wamefikisha miaka 18 hivyo kuwa na sifa za kujiandikisha kupiga kura.
Kunenge alisema kuwa mkoa una jumla ya vituo vya kuandikisha wapiga kura 2,374 na kuna Vijiji 417, vitongoji 2,028 na Mitaa 72 ambapo wananchi kwenye maeneo hayo wanapaswa kwenda kujiandikisha ili wapate fursa ya kupiga kura itakapofika wakati wa uchaguzi.
“Tumeweka vituo vingi vya kujiandikisha kupunguza msongamano ili kila mtu apate haki ya kujiandikisha ili aje apate fursa ya kupiga kura ambayo ni haki yako ya kikatiba kwa mujibu wa kanuni taratibu na sheria za nchi yetu hivyo wananchi mjitokeze kwa wingi,”alisema Kunenge.
Alisema kuwa viongozi wa kwanza ni wale wa ngazi za chini hivyo kuchagua viongozi hawa ni wa muhimu sana kwani wao wako na wananchi kuanzia chini kabisa hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kuwachagua lakini waanze kujiandikisha kwanza kwani kama mwananchi hajajiandikisha hatapata fursa ya kupiga kura.
“Viongozi tunaoanza nao ni wa ngazi za chini kwa ajili ya kutuletea maendeleo na ndipo msingi wa utawala bora unapoanzia na hawa watatusaidia kutuletea maendeleo hivyo tuhakikishe tunashiriki kwenye uchaguzi huu ni muhimu sana ili kuchagua viongozi wanaotufaa,”alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa wananchi wajipange kushiriki uchaguzi kwani hiyo ni haki ya kikatiba hivyo wale wote waliofikia umri kuanzia miaka 18 wahakikishe wanajitokeza kujiandikisha ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wanaowapenda.
“Hii ni fursa nzuri ya kuchagua viongozi ambao watatuongoza kwa kipindi cha miaka mitano na tukichagua viongozi bora watatuletea maendeleo ndani ya maeneo yetu kuanzia ngazi ya chini kabisa hivyo hii ni fursa kwetu sote kwa maendeleo yetu,”alisema Kunenge.
Kwa upande wake mmoja ya watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambaye ni moja ya watu waliokwenda kujiandikisha Simon Mwaiteleke alisema kuwa hiyo ni nafasi yake ya kumfanya ili aweze kuja kupiga kura kwa viongozi kwenye mtaa wake.
Mwaiteleke alisema kuwa uchaguzi ni hatua ya kupata viongozi watakaowatumikia wananchi hivyo anawaomba watu kujitokeza kwa wingi ili kutumia fursa hiyo ambayo hujitokeza kila baada ya miaka mitano.
Naye Saumu Almasi alisema kuwa hiyo ni fursa kwao wananchi kuchagua viopngozi wa Mtaa kuanzia mwenyekiti na wajumbe wake hivyo anaona ni fursa ya kumchagua kiongozi ambaye ana sifa ya kuongoza mtaa anaotoka.
Almasi alisema kuwa wananchi watumie fursa hiyo kumpata kiongozi bora na wasibaki kulalamika wakati hawashiriki uchaguzi kwani kiongozi bora anapatikana kwa kupigiwa kura na siyo kukaa pembeni na kulalamika.