Tuesday, July 4, 2023

WAKAZI WA DODOMA WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI MAONYESHO YA MIAKA 60 YA JKT


Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa ya jirani wametakiwa  kujitokeza kwa wingi katika maonyesho ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) yanayoendelea katika viwanja vya Jengo la SUMA JKT Medeli Mashariki ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa  kwake.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo  Julai 4, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Jengo la Mkapa Jijini Dodoma. 

Mhe. Senyamule amesema kuwa Maonyesho hayo  yameanza  Julai 1 hadi 9 ndio itakuwa ni kilele chake na yanatarajiwa  kufanyika katika viwanja vya Jamhuri Mkoani Dodoma.

"Niko hapa kutoa rai kwa wakazi wa Dodoma na watanzania wa mikoa ya jirani kutenga muda wao kutembelea maonesho hayo kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yaliyofanywa na Jeshi letu”, amesisitiza Mhe. Senyamule

Vile vile amesema katika maonyesho hayo kuna teknolojia mbalimbali kuhusu masuala ya kilimo, uvuvi, useremala na kadha wa kadha.

Aidha, Mhe. Senyamule ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki maonyesho hayo ili kupata fursa mbalimbali zilizopo katika maonyesho hayo. 

"Ni fursa kubwa sana kwa jamii  hususan vijana kutembelea eneo hilo la maonesho kwa lengo la kujifunza namna ya kujiajiri kwa kutumia fursa zilizopo hapa nchini" amebainisha Mhe. Senyamule 

Hata hivyo,   ameendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa ujumla wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi siku ya kilele ya maadhimisho hayo katika  Viwanja vya Jamhuri na kusisitiza kuwa viwanja vitakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi.

Monday, July 3, 2023

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATAKA UFAFANUZI KWA MAKATIBU WAKUU UNUNUZI WA MARUMARU TOKA NJE


Na. Wellu Mtaki Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa amewaagiza makatibu wakuu kukaa ili kuweze kujua sababu za tiles za ndani hazitumiki mpaka wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa majengo ya wizara wanaziagiza kutoka nje ya nchi.

Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo Julai 3,2023 Jijini Dodoma wakati akikagua mradi wa ujenzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi katika mji wa serikali Mtumba.

Amesema vipo viwanda vingi vya utengenezaji wa vifaa hivyo nchni maeneo ya Mkulanga, Chalinze na Mbagara hivyo ni lazima wajitahidi kutumia bidhaa za ndani ili kuongeza mzunguko wa fedha, dola wanayo ipeleka nje iweze kubakia.

“Tulitarajia viwanda vya ndani ndivyo vinapata haya malipo, watu wa TBS wamekataa bidhaa zetu? Wakatudhibitishia hizo za Uturuki na Ujerumani kwanza tunapoteza muda mwingi kusubulia bidhaa kutoka nje ya nchi tulitegemea viwanda vya ndani ndo viwe vianapata haya malipo, ”amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema kama wanaona bidhaa zinazo zalishwa hazina ubora wawaambie waongeze ubora kuliko kuwaacha wanazalisha lakini hazitumiki na haziuziki ndani ya nchi, maana ya uwekezaji ambao Rais anautaka na unaonekana pamoja na kuwatia matumani wakiwekeza faida itapatikana.

Akitoa tadhmini kuhusu ujenzi wa maradi Waziri Mkuu amesema kazi zinaendelea vizuri, hivyo hawana budi kufuta mbinu sahihi ya kukamilisha ujenzi wa majengo na moja kati ya mbinu rahisi ni kufanya kazi usiku na mchana, pamoja na kuongeza wafanyakazi na kupeana zamu za usimamizi.

“Wakandarasi ndiyo wenye majukumu ya kusimamia kazi kufanyika usiku na mchana, simamieni ujenzi wa majengo ili muhakakikishe unakamilika kwa kiwango bora zaidi kinachohtajika ili magorofa yasije kuporomoka,”amesema.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema mbali na mradi wa ujenzi wa majengo ya wizara pia mradi mwingine unaotekelezwa katika eneo hilo ni ujenzi wa uwanja wa Mashujaa ambao utakuwa na mnara utakaoongoza kwa urefu barani Afrika. Mnara huo utakuwa na urefu wa mita 110.

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi alisema watahakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. “Ifikapo Septemba 30, 2023 mradi huo utakuwa umekamilika.”

WAZIRI DKT. GWAJIMA ASEMA JUMUIYA ZA WANAWAKE ZINA NAFASI KUTOKOMEZA UKATILI.




WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amefungua Warsha ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) ambapo ametoa wito kwa taasisi hiyo kushirikiana na Serikali katika kuwainua wanawake kiuchumi na  kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo, Julai 03, 2023 wakati akifungua warsha ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO) ukumbi wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Dar es Salaam ambapo wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Afrika wameshiriki ufunguzi huo.

"Warsha hii imelenga kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na inawapa nafasi kubwa ya kujifunza na kushirikishana mbinu za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa na sauti ya pamoja.

"Jambo hili ni jema kwani siku zote umoja unaleta matunda chanya na ya haraka zaidi." amesema Dkt. Gwajima.

Dkt. Dorothy Gwajima ameongeza kuwa,  amefarijika kwakuwa WAWATA pia ina lengo la kumfanya mwanamke ajitambue kuwa yeye ni muhimu ndani ya Jamii na maendeleo ya kiroho na kimwili.

Kwa upande wake Rais wa  Umoja wa Wanawake Wakatoliki Afrika, World Union of Catholic Women Organization (WUCWO) na Mwenyekiti wa WAWATA, Eveline Ntenga amesema, kwenye vipaumbele nane vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa bajeti ya mwaka 2023/24 vipo vipaumbele viwili vinavyoendana na Mradi wa World Women Observatory (WWO) ambavyo ni kuratibu hatua za kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kiungozi, kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, Watoto na wazee na kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum.

Aidha Eveline ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kuweka mkazo juu ya suala la kuwataka wazazi waone umuhimu wa watoto wa kike kupata elimu kwanza badala ya kufikiria kuwaozesha mapema.

Aidha Rais huyo ameiomba Wizara iwasaidie kuendelea kuweka utaratibu sahihi na wa haraka kuanzia ngazi ya Msingi  ili kufikisha taarifa za unyanyasaji na ukatili zinazofanywa na jamii kwa makundi yote katika vyombo husika.

“Tunaomba zichukuliwe hatua kali na kwa haraka kwa wale wote wanaohusika na vitendo vya ukatili kwa makundi yote “ amesema Bi. Aveline. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Pd. Dkt. Charles Kitima, amesema katika kufikia maendeleo halisi kama ilivyolengwa kwenye ajenda ya maendeleo ya Dunia (Suistainable Development Goals)  ya mwaka 2030, Kanisa linawaona  wamama kama watendaji wakuu, na wakishikwa mkono na kanisa na Serikali wanaweza wakaifanya Dunia kuwa imara. 

Dkt. Kitima amesema,  jina la Wizara  Wizara ya Maendeleo ya Jamii linasawidi  mambo mengi yanayohusu utu wa mwanadamu ambapo ndipo Mungu Muumba anatukuka, Utukufu wa Mungu uko katika Utu wa mwanadamu, kwani wizara inashughulikia mambo ya Watoto, makundi yaliyotengwa, na akina mama hii ni heshima kubwa kwamba Waziri wa Wizara hii ni mama.

MUNIS ACHAGULIWA MENYEKITI KIBAFA

CHAMA Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA) kimefanya uchaguzi wake Mkuu na kupata viongozi watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne ambapo Robert Munis amechaguliwa kuwa mwenyekiti.

Munis alishinda uchaguzi huo uliofanyika Mjini Kibaha ambapo hakuwa na mpinzani, kwa kupata kura 30 na kura moja ya hapana kati ya wapiga kura 31.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ilichukuliwa na David Mramba aliyepata kura 27 nafasi ya katibu ilikwenda kwa Daud Mhina aliyepata kura 29 na katibu msaidizi ni Omary Pumzi aliyepata kura 28.

Nafasi ya mweka hazina ilikwenda kwa Laurent Shirima aliyepata kura 28, nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu kwenda Corefa ni Japhet Mbogo aliyepata kura 30, Mwakilishi wa vilabu Mohamed Mwenda aliyepata kura 28.

Mwakilishi wanawake ni Jesca Siha aliyepata kura 28 huku kamati ya utendaji ni Method Mselewa, Nasoro Shomvi na Emanuel Mbunda.

Akizungumzia mikakati yake katika kipindi cha miaka minne Munis alisema kuwa moja ya mikakati yake ni kuhakikisha Kibaha inakuwa na timu ya ligi kuu ambapo ataweka mikakati Ruvu Shooting irudi kwenye ligi hiyo baada ya kushuka daraja.

Munis alisema kuwa atahakikisha mpira wa miguu unachezwa na kupata viwanja vizuri ili kukuza vipaji vya vijana kwenye soka ili waje kuwa hazina kwa timu za mkoa na taifa kwa ujumla.

Naye Katibu wa chama cha soka Mkoa wa Pwani COREFA Mohamed Masenga alisema kuwa kwa vyama ambavyo havijafanya chaguzi vifanye hivyo ili kwendana na kalenda ya vyama vikuu vya soka.

Masenga alisema anapongeza uongozi uliochaguliwa na kuwataka kuzingatia mipango na taratibu zilizopo ili soka la mkoa wa Pwani lisonge mbele.

Kwa upande wake ofisa michezo wa Halmashauri ya Mji Kibaha Burhan Tulusubya alisema kuwa uchaguzi huo ulienda vizuri kwa kuzingatia taratibu za chama hicho na sheria kwani ulikuwa wa kisheria.

Tulusubya alisema kuwa viongozi hao wasimamie maneno yao kwa kutafsiri kwa vitendo na wahamasishe vilabu navyo vifanye chaguzi ili wawe kisheria. Uchaguzi huo ulisimamiwa na makamu mwenyekiti wa uchaguzi wa KIBAFA Mabel Nasua.

WAANDISHI WA HABARI WAULA UCHAGUZI WA SOKA WILAYA YA KIBAHA (KIBAFA)



WAANDISHI wa habari waula baada ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi wa Chama Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA) ambapo Hassan Mtengefu amechaguliwa kuwa meneja wa habari wa chama hicho.
Chama hicho kimewateua waandishi hao ikiwa ni sehemu ya uundaji wa kamati mara baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika jana Mjini Kibaha.

Waandishi hao wameteuliwa kwenye kamati mbili ikiwemo ya nidhamu na maadili na kamati ya habari uhamasishaji na zawadi.

Ukiachilia mbali Mtengefu wengine ni Gustaph Haule aliyeteuliwa kwenye kamati ya nidhamu na maadili.

Wengine ni Mariam Songoro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya habari uhamasishaji na zawadi huku wengine wakiwa ni Margareth Malisa, Ben Komba na John Gagarini ambao ni wajumbe.

Saturday, July 1, 2023

MHE.MASANJA ACHANGISHA MILIONI 95 ZA UJENZI WA KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO SDA PASIANSI MWANZA

 





Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja  ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya ibada ya Kanisa la Waadventista Wasabato SDA Pasiansi kwenye Jimbo Kuu la Nyanza Kusini leo mkoani Mwanza na kupata kiasi cha shilingi milioni 95. 2 ambapo  fedha taslimu zilikuwa shilingi milioni 47.3 na ahadi shilingi milioni 47.8.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Masanja amelipongeza kanisa la SDA Pasiansi kwa kuanza ujenzi wa kanisa hilo jipya ambalo ujenzi wake ulianza mwaka 2022 huku waumini wa kanisa hilo wakiwa wameshafanikiwa kuchangia shilingi milioni 56 za ujenzi.

"Serikali inatambua mchango wa kanisa hili katika sekta ya Elimu na Afya. Ujenzi wa kanisa hili ni wito na wajibu wa kila mmoja wetu"  amesema Mhe. Masanja

Amesema lengo kuu la kufanya harambee hiyo ni kutafuta fedha za ujenzi wa kanisa na fedha zinazohitajika ni zaidi ya milioni 200. 

Amewaomba waumini wa kanisa hilo waendelee kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na pia kuendelea kuiombea Tanzania iendelee kuwa na  amani, umoja na upendo.

Naye, Mchungaji wa Kanisa la SDA Pasiansi Harun Kuyenga amesema mradi huo wa ujenzi la kanisa ulianza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2024 na mara baada ya kukamilika kwake kanisa  litakuwa na uwezo wa kubeba waumini 3000 ambapo  kanisa la sasa lina uwezo wa kubeba waumini 800.

Ameongeza kuwa  wameamua kujenga kanisa hilo jipya  kutokana na ongezeko la waumini kutoka maeneo tofauti tofauti huku akisisitiza kuwa kwa sasa kiasi cha fedha shilingi milioni 200 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.

Katika Harambee hiyo, Mhe.Masanja pamoja na familia yake na marafiki zake walifanikiwa kuchangia ujenzi wa kanisa hilo kiasi cha shilingi milioni 51,050,000 ambapo fedha taslimu ilikuwa ni shilingi milioni 30,550,000 na ahadi shilingi milioni 20,500,000.

MHE.MARY MASANJA ATEMBELEA OFISI ZA CCM MKOANI MWANZA

 


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja leo ametembelea Ofisi za Chama cha Mapinduzi jijini Mwanza na kufanya mazungumzo na Katibu wa  CCM, Mkoa wa Mwanza Ndugu Omary Mtuwa.

Pia, alipata nafasi ya kuzungumza na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Ndugu Sixbert Reuben Jichabu.

Mhe. Masanja anatarajia kushiriki katika Harambee ya Kuchangia ujenzi wa Nyumba ya Ibada ya Kanisa la Pasiansi SDA jijini humo tarehe 1 Julai,2023.