Na Mwandishi Wetu Dodoma
Monday, February 13, 2023
REDIO ZITANGAZE HABARI ZA VIJIJINI
Friday, February 10, 2023
12 WAFA 63 WAJERUHIWA AJALINI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
WATU 12 wamefariki dunia na wengine 63 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia Alhamisi Februari 9, 2023 Wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 12 (wanaume nane , wanawake wanne) na majeruhi 63 (wanaume 40 wanawake 23).
Senyamule amesema ajali hiyo imetokea usiku Kata ya Pandambili Kijiji cha Silwa wilayani Kongwa, barabara ya Dodoma - Morogoro.
"Majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkoa wa Morogoro na majeruhi wawili wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,"amesema Senyamule.
Amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 6 usiku na imehusisha lori la mizigo lenye namba za usajili T 677 DVX na basi la abiria la Kampuni ya Frester lenye namba za usajili T 415 DPP lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Akizungumza na wakazi wa Pandambili eneo ambapo ajali ilipotokea Senyamule ametoa rai kwa jamii kutii sheria bila shuruti ili kuepuka ajali.
"Serikali ilikuwa na nia njema ya kuruhusu vyombo vya usafiri kutembea usiku, lakini sasa baadhi ya madereva wanaanza kutozingatia Sheria za usalama barabarani, tutaendelea kuwachukulia hatua kali,"amesema Senyamule.a
Pia mewatembelea majeruhi katika Hospitali ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na kutoa pole na kuwatakia uponyaji wa haraka.
Naye Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Kamishna Awadh Haji ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi kutaka kulipita gari la mbele yake bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na lori hilo lililokuwa limebeba saruji.
WATUMISHI HOUSING A YAJENGA NYUMBA KWA WATUMISHI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WATUMISHI Housing Investment (WHI) imeweza kujenga nyumba 983 kwa ajili ya watumishi wa umma katika mikoa mbalimbali nchini.
Aidha kupitia kampuni yake ya ujenzi imeshiriki katika ujenzi wa mji wa serikali Jijini Dodoma pomoja na majengo ya taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa chuo Cha utumishi wa umma katika mkoa wa Singida.
Hayo yamesemwa na Mkurugezi mtendaji wa WHI Dkt Fred Msemwa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa taasisi hiyo ambapo kumekuwa na ongezeko la kushuka kwa bei ya nyumba kutoka asilimia 10 hadi asilimia 30.
Amesema kuwa wanategemea kuwa na miradi mipya ya ujenzi katika mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo ni Kawe, Dodoma, Gezaulole, mradi wa viwanda Arusha pamoja na nyumba za watumishi Halmashauri mpya.
"Yapo baadhi ya mafanikio ambayo taasisi imefanikiwa ikiwa ni pamoja na kupata vifaa vya upimaji wa ardhi vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kutoka serikalini kupitia mkopo wa benki ya dunia unaoratibiwa na benki kuu ya Tanzania,"amesema Msemwa.
Watumishi Housing Investment ni taasisi ya umma iliyo chini ya ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) iliyoanzishwa Mwaka 2014 na ilianzishwa na serikali kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma (PSSSF), mfuko wa hifadhi ya jamii ( NSSF) pamoja na shirika la nyumba la Taifa na mfuko wa bima ya Afya (NHIF)
Wednesday, February 8, 2023
NSSF YAKUSANYA BILIONI 165.7
Na Mwandishi Wetu Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba amesema kuwa katika nusu ya mwaka wa fedha iliyoishia Desemba 2022 umekusanya shilingi bilioni 165.7 kutokana na mapato ya uwekezaji na vitega uchumi vya Mfuko.
Hayo yamebainishwa leo Februari 8,2023 Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mshomba amesema kiasi hicho cha mapato hakijajumuisha ongezeko la thamani ya vitega uchumi vya Mfuko huo na kuongeza kuwa katika kipindi husika thamani ya vitega uchumi vya Mfuko ilikua na kufikia shilingi trilioni 5.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7 ikilinganishwa na thamani ya shilingi trilioni 5.4 iliyofikiwa katika mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022.
"NSSF wana fursa za nyumba za makazi salama kupitia mfuko huo mwananchi anaweza kumiliki nyumba ya ndoto yake kwa kulipa gharama ya nyumba kwa mkupuo mmoja au kulipa kidogo kidogo wakati wakiendelea kuishi katika nyumba husika na nyumba hizo zipo Dungu, Mtoni Kijichi na Toangoma Jijini Dar es Salaam,"amesema Mshomba.
Amesema serikali imetekeleza mikakakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji wakubwa ikiwa ni pamoja na kupitia maonesho ya filamu ya The Royal Tour.
"Miradi hiyo pekee imechangia takribani wanachama wapya 33,066 na kwa ujumla mkakati huo wa Serikali umechangia katika ongezeko la wanachama na michango inayokusanywa na Mfuko,"amesema Msomba.
Ameongeza kuwa kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali kuvutia uwekezaji na kufungua fursa mpya za biashara, wastani wa makusanyo ya michango kwa mwezi yameongezeka na kufikia shilingi bilioni 134 kutoka wastani wa shilingi bilioni 118 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022 ikiwa ni sawa na asilimia 14.
MAMLAKA YA USIMAMIZI BAHARI KUU KUJENGA KIWANDA KUCHAKATA SAMAKI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAMLAKA ya kusimamia uvuvi wa Bahari Kuu inatarajia Kujenga Kiwanda kikubwa cha kuchakata Samaki Mkoani Tanga ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 100 kwa siku ambacho kitagharimu Dola Milioni 10 na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo,Dk Emanuel Sweke wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya usimamizi wa Bahari Kuu.
Sweke amesema kuwa katika kudhibiti uvuvi haramu Mamlaka hiyo imeweza kuweka mifumo madhubuti ambayo inaendana na Teknolojia kwakufanya doria mbalimbali kwa ajili ya kukomesha uvuvi haramu.
"Kutokana na shughuli zake Mamlaka hiyo imeweza kuvunja rekodi ya kukusanya mapato mengi kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi kufikia shilingi bilioni 4.1 na wametoa jumla ya leseni za uvuvi 5336,"alisema Sweke.
Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa Bahari Kuu imeanzishwa rasmi Mwaka 2010 lengo lake likiwa ni kusimamia shughuli zote za uvuvi wa Bahari Kuu na ufuatiliaji.
WACHIMBA VISIMA VYA MAJI WATAKIWA KUWA NA VIBALI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BODI ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu imewataka wadau wa maji nchini kuzingatia na kufuata taratibu za uchimbaji wa visima vya maji ikiwemo kupata vibali halali ili kupata maji yenye ubora na kuondokana na malalamiko mengi ya maji yasiyo na viwango.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji chini ya bodi hiyo.
Mmasi amesema wadau wa maji wanapaswa kufahamu madhara ya kuchimba visima bila vibali na kupelekea changamoto ya ubora wa maji kwenye maeneo mengi jambo linaloweza kuleta madhara kiafya.
"Baadhi ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kutumia maji yasiyo na madhara kuwa ni pamoja na kuhakikisha maji yanayopatikana baada ya kuchimbwa yanapelekwa maabara kuchunguzwa iwapo yanafaa kwa matumizi au la,"amesema Mmasi
Aidha amesema kuwa bodi hiyo imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto ya tatizo la maji katika mikoa ya Dar es salaam,Pwani na Morogoro kwa kuchimba visima vya maji
HUDUMA MTANDAO KUBORESHWA
Na Wellu Mtaki, Dodoma
MAMLAKA ya Serikali Mtandao ( EGA ) kuandaa na kutelekeza mikakati madhubuti ili huduma za Mtandao zote kupatikana ili kudhibiti matishio ya usalama mtandaoni na kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma.
Hayo yamesemwa na Mkurugezi mkuu wa mamlaka ya serikali Mhandisi Benedict Benny Ndomba wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu kikao kazi cha tatu cha serikali Mtandao kinachotarajiwa kufanyika Februari 8 hadi 10 mwaka huu katika ukumbi wa AICC Jijini Arusha ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama ( mb).
Ndomba amesema kuwa takribani wadau 1,000 wa serikali Mtandao kutoka katika mashirika na taasisi za umma wakiwemo maafisa masuuli, wajumbe wa bodi, Wakuu wa vitengo vya tehama, maofisa tehama, rasilimali watu, mipango, mawasiliano, wahasibu pamoja na watumishi wote wa mifumo ya tehama serikali wanatatarajiwa kushiriki kikao hicho.
"Lengo la kikao hicho ni kijadiliana juu ya mafanikio, changamoto pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza serikali Mtandao nchin Ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya tehama katika taasisi za umma,"alisema Ndomba.
Aidha alisema kuwa Mamlaka ya serikali Mtandao( (e-GA) ni taasisi iliyopewa jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza juhudi za serikali Mtandao pamoja na kuhimiza uzingatiwaji wa sera, Sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali Mtandao katika taasisi za umma ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya tehama yanazingatiwa katika taasisi hizo.