Thursday, November 10, 2022

PSSSF YAPATA FAIDA KUBWA


PSSSF YAPATA FAIDA YA MABILIONI.

Na Wellu Mtaki, Dodoma

KWA mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022 mfuko wa PSSSF umepata faida ya uwekezaji kiasi cha shilingi bilioni 581.7.

Hayo yameelezwa na CPA Hosea Kashimba Mkurugenzi mkuu Psssf wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu maendeleo ya mfuko huo.

Kashimba amesema kutokana na uwekezaji huu,mfuko hupata faida ya uwekezaji ( return on investment) wastani wa asilimia 8 kwa mwaka,ambayo ni juu ya mfumuko wa bei na hivyo kufanya uwekezaji huu kuwa na tija.

Amesema kuwa mfuko wa Psssf ni mmoja ya waendelezaji milki (real estate developers) wakubwa nchini,mfuko unamiliki majengo ya kupangisha katika miji mbalimbali ambayo hutumika kwa shughuli za kibiashara asilimia 72,ofisi na makazi asilimia 98.

Aidha amesema kuwa wakati wa kuunganisha mifuko psssf ilirithi madeni ya serikali yaliyohakikiwa yenye thamani ya Tsh 731.40 bilioni,mpaka sasa kiasi cha Tsh 500 bilioni kimelipwa na serikali.

“Nirudie kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutambua deni la michango kabla ya 1999 maarufu kama (pre 99 liability) ambalo ni shilingi trilioni 4.6 kwa kutoa hati fungani maalum zenye thamani ya shilingi trilioni 2.1 haya yote yanaleta matumaini ya kuwa na mfuko wenye ustahimilivu na endelevu kwa ustawi wa wanachama,”amesema Kashimba.

Alibainisha kuwa wakati wa kuunganisha mifuko,kiasi kilichokuwa kinalipwa kama pensheni kwa mwezi kwa wastaafu kilikuwa shilingi bilioni 34 lakini mpaka kufikia sasa wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 60 kinalipwa bila kukosa kwa wastaafu zaidi ya 150,000 kila ifikapo tarehe 25 kila mwezi.

"Mfuko umewekeza shilingi trilioni 4.5 katika hatifungani za serikali,pamoja na kuleta faida ya uwekezaji kwa mfuko kupitia riba na uwekezaji huu unauwezesha mfuko kutekeleza majukumu yake ya msingi,"amesema Kashimba.

Amesema vilevile mfuko umewekeza zaidi ya shilingi bilioni 500 katika soko la hisa la DSM kupitia makampuni mbalimbali yaliyoorodheshwa,uwekezaji huu mkubwa wa mfuko unasaidia kukuza soko la mitaji nchini na kuchochea uchumi na maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja.

“Zaidi ya bilioni 400 zimewekezwa katika amana za muda (fixed deposit) katika benki mbalimbali hapa nchini,uwekezaji huu pia kwa mabenki kutoa mikopo mbalimbali kwa Watanzania na hivyo kuharakisha azma ya serikali kukuza uchumi na kuinua,”amesema Kashimba.

Kwa upande wake Msemaji mkuu wa serikali Ndg.Gerson Msigwa amewapongeza Psssf kwa taarifa za kukua kwa mfuko kwa asilimia 8 na kusema ni jambo zuri na inaonyesha jinsi gani mfuko umeweka mazingira mazuri kwa wanachama.

Msigwa amesema kuwa amepata nafasi ya kutembelea ofisi za Psssf na ameridhishwa na namna ambavyo mfuko unafanya kazi zake na kuimarisha huduma kwa wafanyakazi,pia wafanyakazi ni muhimu kufuatilia michango yao inapowasilishwa na kujiridhishwa.


Wednesday, November 9, 2022

RC ASHIRIKI MSIBA WA MTUMISHI MDH ALIYEFARIKI AJALI YA NDEGE


MKUU WA MKOA WA DODOMA MAZISHI MTUMISHI MDH ALIYEFARIKI AJALI YA NDEGE.

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameshiriki ibada ya mazishi ya Marehemu Neema Samwel aliyefariki kutokana na ajali ya ndege ya Precision Air Mkoani Kagera ambapo mazishi hayo yaliofanyika nyumbani kwao Ilazo Jijini Dodoma.

Marehemu Neema alikuwa anafanya kazi shirika  (Management and Development for Health) (MDH) ambapo alikuwa anaelekea kwenye ziara ya kikazi mkoani Kagera na kukutwa na umauti.

Senyamule  ameshiriki ibada ya mazishi na kuwapa pole familia ya Marehemu akiwemo mume wa Marehemu,wazazi na ndugu wa Marehemu Kwa kupatwa na msiba huo.

Aidhaa Senyamule amesema kuwa mkoa wa Dodoma umepatwa na misiba miwili kati ya waliofariki kwenye ajali hiyo ambapo Serikali ya Dodoma iliwajibika kushiriki msiba mwingine uliofanyika Wilayani Kondoa.

"Nafahamu Watanzania wengi tumeumia na msiba huu lakini kama mnavyofahamu kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo tuhakikishe tunashirikiana na tunawapumzisha wenzetu walio tangulia mbele za haki ndio maana nami nipo hapa kuwakilisha Serikali kama tulivyoelekezwa na Rais hivyo nawapa pole wazazi, mume na ndugu kwa msiba mzito uliowapata kubwa ni kuhakikisha tunaendelea kuwaombea katika sala zetu za kila siku,"amesema Senyamule

Pia Sinyamule ametoa pole nyingi kwa shirika la (MDH) kwa kuwapoteza wafanyakazi wengi katika ajali hiyo ya ndege na amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana  na serikali kufanya kazi mbalimbali za afya hapa nchini.

Neema Samwel alizaliwa Oktoba 26 mwaka 1994 ambapo alifariki katika ajali ya Ndege ya shirika la Precision Air iliyotokea Novemba 6 ziwa Victoria Bukoba Mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 19 huku watu 26 wakinusurika kwenye ajali hiyo.

WADAU WATAKIWA KUDHIBITI VITENDO VYA UKATILI

PUNGUZENI VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA MIMBA ZA UTOTONI

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MKURUGENZI wa shirika la Kivulini linalojishughulisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni Yasini Ally amesema kuwa hali ya vitendo vya ukatili na mimba za utotoni katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ipo kwa kiwango cha juu hivyo serikali na wadau wote hawana budi kushirikiana ili kuweza kukabiliana na tatizo.

Ally amesema hayo Jijini Dodoma alipokuwa akifanya mahojiano na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari juu ya utendaji kazi wa shirika lake.

Amesema kuwa Utafiti uliofanywa na shirika hilo umebaini katika kipindi cha mwaka 2015/ 2016 vitendo vya ukatili wa kijinsia ulikuwa wa hali ya uu ambapo mkoa wa Shinyanga ni asilimia 78, mkoa wa Mwanza asilimia 60 , mkoa wa Kigoma asilimia 61 na mkoa wa Mwanza pia una asilimia 25 kwa vitendo vya mimba za utotoni.

Aidha amefafanua kwamba hali hiyo pia inaweza kusababishwa pale jamiii ya kanda ziwa inapokuwa na hali nzuri ya kiuchumi kwa mfano wakati wa mavuno baadhi ya watu hutelekeza familia na kwenda kwenye mambo ya starehe.

Mkurugezi huyo ameongeza kuwa shirika Ilo limefanya kazi kubwa ya kujenga uwezo kwa klabu za wanafunzi Ili kudhibiti mimba za utotoni.


Friday, November 4, 2022

LAINI 58.1 ZASAJILIWA


WATUMIAJI WA SIMU WAONGEZEKA NCHINI 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

SEKTA ya Mawasiliano ya Simu nchini imeendelea kukua hadi kufikia Septemba 2022 kulikuwa na laini za simu za milioni 58.1 idadi hiyo inahusisha laini zinazotumiwa na watu pamoja na zinatotumiwa kwa ajili ya Mashine (M2M).

Aidha takwimu zinaonesha mikoa mitano inayoongoza nchini kuwa na idadi kubwa ya laini za simu zinazotumika (Active SIM-Cards) hadi kufikia Septemba mwaka huu ni Dar es Salaam laini milioni 9.7, Mwanza milioni 3.7, Arusha 3.4, Mbeya 3.08 na Tabora 3.06.

Akizungumza jiijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo ,Dk. Jabir Bakari amesema kuwa wanawatoa huduma sita kwenye soko lao ambao ni Airtel, Vodacom, Halotel, Ttcl, Tigo na Smile.

Dk. Bakari ameeleza kuwa mgawanyo wa asilimia za soko kwa kila mtoa huduma ni kwamba Vodacom asilimia 30, Airtel asilimia 28, Tigo asilimia 26, Halotel asilimia 13, Ttcl asilimia 3 na Smile asilimia 0.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa takwimu zinaonesha matumizi ya Intaneti yameongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka milioni 29 hadi kufikia 31. 12 mwezi Septemba mwaka huu.

Amefafanua kuwa ongezeko la matumizi ya Intaneti limechangiwa na matumizi ya kiswahili na kwamba maudhui hayo kwenye Intaneti yanaongezeka kwa kasi na program tumizi (applications), kwa lugha ya kiswahili nazo zimeongezeka.


KITUO CHA TAALUMA USAFIRI WA ANGA


KITUO CHA TAALUMA USAFIRI WA ANGA KUBORESHWA

Na Wellu Mtaki, Dodoma

TAKRIBANI shilingi bilioni 49 zimekopwa tutoka benki kuu ya Dunia kwa ajili ya kituo cha umahiri cha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga kwa ajili wa utekelezaji wa miundombinu ya chuo hicho.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa chuo cha taifa cha usafirishaji (NIT) Prof.Zacharia Mganilwa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Mganilwa amesema kuwa fedha hizo zimegawanyika katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia wataalam ambapo jumla ya majengo matano yatajengwa Dar- es Salaam kwa gharama ya shilingi bilioni 21 na baadaye kujenga majengo mkoa wa kilimanjaro kwa sababu lazima marubani wafundishwe ndani ya viwanja vya ndege.

Amesema kuwa chuo kimenunua ndege mbili zenye injini moja za mafunzo ambazo ziko njiani zinatazamiwa kuletwa Tanzania kwa gharama ya shilingi dola za Marekani milioni 12 huku akieleza kwamba kumfundisha rubani mmoja nje ya nchi ni shilingi milioni 200 hivyo Serikali inapofanya uwekezaji huu inalifanya shirika la ndege nchini kuleta matumaini ya nchi katika kukuza utalii na uchumi kwa sababu wataalam wa usafiri wa anga watafundishwa hapa hapa nchini.

Aidha amesema kuwa Tanzania ina zaidi ya ndege 400 zilizosajiliwa na mamlaka ya usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya marubani ni wageni,hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 chuo kinanunua tena ndege yenye injini mbili kwa ajili ya mwanafunzi kukamilisha mafunzo yake kwa sababu mafunzo ya urubani yanamtaka mwanafunzi ajifunze ndege yenye injini moja na injini mbili.

NIT watawawezesha vijana wengi kunufaika na miradi mikubwa inayoendelea nchini mathalani ndege tano zinatarajiwa kuja nchini,ambapo kwa mwaka 2023 ndege nne zitaingia nchini.


Thursday, November 3, 2022

WIZARA AFYA KUDUMISHA HUDUMA ZA AFYA


WATUMISHI KUWA WAKUTOSHA KWENYE VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

Dodoma,

Katibu Mkuu,Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuwa na watumishi wa kutosha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Prof. Makubi amesema hayo leo tarehe 3 Novemba, 2020 wakati wa kikao cha Sekretarieti ya maandalizi ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na Menejimenti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ikiwa ni kuelezea hatua iliyofikiwa pamoja na nini kifanyike kama sekta moja endapo Muswada huo utapitishwa na Bunge na kuwa Sheria.

Aidha, Prof. Makubi amesema Wizara ya Afya inaendelea kuboresha upatikanaji wa Dawa, vifaa tiba na vipimo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili huduma zinazotolewa ziwe bora.

"Afya ni kitu muhimu na ndio haki ya kwanza ambayo Mungu amempa Mwanadamu hivyo kila mmoja lazima athamini uhai wake kwa kuwa na Bima ya Afya".

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo alisema dhana ya bima ya afya kwa wote ni kuchangiana pindi mmoja anapougua aweze kupata matibabu bila kuwa na kikwazo cha fedha.

Naye, Naibu Katibu Mkuu-Afya kutoka TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amesisitiza utoaji wa elimu kwa wananchi ngazi zote ili waelewe zaidi dhana nzima ya Bima ya Afya kwa Wote.

HUDUMA ZA NDEGE ZAONGEZEKA NCHINI.

VIWANJA VYA NDEGE VYAONGEZA HUDUMA ZA NDEGE NCHINI.


Na Wellu Mtaki, Dodoma

JUMLA ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 ikilinganishwa na huduma iliyotolewa mwaka 2020/2021 sawa na ongezeko la asilimia 13. 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Huduma za Utabiri - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa Fedha 2022/23 katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO Novemba 2, 2022 Jijini Dodoma.

Dkt Kabelwa amesema kuwa sekta ya usafiri wa anga inaendelea kukua kutokana na kuzingatiwa kwa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma na ongezeko hilo linatokana na jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na serikali, pamoja na kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuihakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa.

Amesema kuwa mamlaka hiyo katika mwaka 2021/22 iliendelea na utengenezaji wa rada mbili zitakazofungwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na cha Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 45.

Ameongeza kuwa Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa Wananchi kujenga utaratibu wa kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)yamegawanyika katika sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya kwanza ni kutoa huduma za hali ya hewa; sehemu ya pili ni kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha (14) na sehemu ya tatu ni kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini Tanzania kulingana na Kifungu cha (5) cha Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019.

Mwisho