Friday, November 4, 2022

LAINI 58.1 ZASAJILIWA


WATUMIAJI WA SIMU WAONGEZEKA NCHINI 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

SEKTA ya Mawasiliano ya Simu nchini imeendelea kukua hadi kufikia Septemba 2022 kulikuwa na laini za simu za milioni 58.1 idadi hiyo inahusisha laini zinazotumiwa na watu pamoja na zinatotumiwa kwa ajili ya Mashine (M2M).

Aidha takwimu zinaonesha mikoa mitano inayoongoza nchini kuwa na idadi kubwa ya laini za simu zinazotumika (Active SIM-Cards) hadi kufikia Septemba mwaka huu ni Dar es Salaam laini milioni 9.7, Mwanza milioni 3.7, Arusha 3.4, Mbeya 3.08 na Tabora 3.06.

Akizungumza jiijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo ,Dk. Jabir Bakari amesema kuwa wanawatoa huduma sita kwenye soko lao ambao ni Airtel, Vodacom, Halotel, Ttcl, Tigo na Smile.

Dk. Bakari ameeleza kuwa mgawanyo wa asilimia za soko kwa kila mtoa huduma ni kwamba Vodacom asilimia 30, Airtel asilimia 28, Tigo asilimia 26, Halotel asilimia 13, Ttcl asilimia 3 na Smile asilimia 0.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa takwimu zinaonesha matumizi ya Intaneti yameongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka milioni 29 hadi kufikia 31. 12 mwezi Septemba mwaka huu.

Amefafanua kuwa ongezeko la matumizi ya Intaneti limechangiwa na matumizi ya kiswahili na kwamba maudhui hayo kwenye Intaneti yanaongezeka kwa kasi na program tumizi (applications), kwa lugha ya kiswahili nazo zimeongezeka.


KITUO CHA TAALUMA USAFIRI WA ANGA


KITUO CHA TAALUMA USAFIRI WA ANGA KUBORESHWA

Na Wellu Mtaki, Dodoma

TAKRIBANI shilingi bilioni 49 zimekopwa tutoka benki kuu ya Dunia kwa ajili ya kituo cha umahiri cha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga kwa ajili wa utekelezaji wa miundombinu ya chuo hicho.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa chuo cha taifa cha usafirishaji (NIT) Prof.Zacharia Mganilwa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Mganilwa amesema kuwa fedha hizo zimegawanyika katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia wataalam ambapo jumla ya majengo matano yatajengwa Dar- es Salaam kwa gharama ya shilingi bilioni 21 na baadaye kujenga majengo mkoa wa kilimanjaro kwa sababu lazima marubani wafundishwe ndani ya viwanja vya ndege.

Amesema kuwa chuo kimenunua ndege mbili zenye injini moja za mafunzo ambazo ziko njiani zinatazamiwa kuletwa Tanzania kwa gharama ya shilingi dola za Marekani milioni 12 huku akieleza kwamba kumfundisha rubani mmoja nje ya nchi ni shilingi milioni 200 hivyo Serikali inapofanya uwekezaji huu inalifanya shirika la ndege nchini kuleta matumaini ya nchi katika kukuza utalii na uchumi kwa sababu wataalam wa usafiri wa anga watafundishwa hapa hapa nchini.

Aidha amesema kuwa Tanzania ina zaidi ya ndege 400 zilizosajiliwa na mamlaka ya usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya marubani ni wageni,hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 chuo kinanunua tena ndege yenye injini mbili kwa ajili ya mwanafunzi kukamilisha mafunzo yake kwa sababu mafunzo ya urubani yanamtaka mwanafunzi ajifunze ndege yenye injini moja na injini mbili.

NIT watawawezesha vijana wengi kunufaika na miradi mikubwa inayoendelea nchini mathalani ndege tano zinatarajiwa kuja nchini,ambapo kwa mwaka 2023 ndege nne zitaingia nchini.


Thursday, November 3, 2022

WIZARA AFYA KUDUMISHA HUDUMA ZA AFYA


WATUMISHI KUWA WAKUTOSHA KWENYE VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

Dodoma,

Katibu Mkuu,Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuwa na watumishi wa kutosha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Prof. Makubi amesema hayo leo tarehe 3 Novemba, 2020 wakati wa kikao cha Sekretarieti ya maandalizi ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na Menejimenti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ikiwa ni kuelezea hatua iliyofikiwa pamoja na nini kifanyike kama sekta moja endapo Muswada huo utapitishwa na Bunge na kuwa Sheria.

Aidha, Prof. Makubi amesema Wizara ya Afya inaendelea kuboresha upatikanaji wa Dawa, vifaa tiba na vipimo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili huduma zinazotolewa ziwe bora.

"Afya ni kitu muhimu na ndio haki ya kwanza ambayo Mungu amempa Mwanadamu hivyo kila mmoja lazima athamini uhai wake kwa kuwa na Bima ya Afya".

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo alisema dhana ya bima ya afya kwa wote ni kuchangiana pindi mmoja anapougua aweze kupata matibabu bila kuwa na kikwazo cha fedha.

Naye, Naibu Katibu Mkuu-Afya kutoka TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amesisitiza utoaji wa elimu kwa wananchi ngazi zote ili waelewe zaidi dhana nzima ya Bima ya Afya kwa Wote.

HUDUMA ZA NDEGE ZAONGEZEKA NCHINI.

VIWANJA VYA NDEGE VYAONGEZA HUDUMA ZA NDEGE NCHINI.


Na Wellu Mtaki, Dodoma

JUMLA ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 ikilinganishwa na huduma iliyotolewa mwaka 2020/2021 sawa na ongezeko la asilimia 13. 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Huduma za Utabiri - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa Fedha 2022/23 katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO Novemba 2, 2022 Jijini Dodoma.

Dkt Kabelwa amesema kuwa sekta ya usafiri wa anga inaendelea kukua kutokana na kuzingatiwa kwa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma na ongezeko hilo linatokana na jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na serikali, pamoja na kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuihakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa.

Amesema kuwa mamlaka hiyo katika mwaka 2021/22 iliendelea na utengenezaji wa rada mbili zitakazofungwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na cha Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 45.

Ameongeza kuwa Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa Wananchi kujenga utaratibu wa kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)yamegawanyika katika sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya kwanza ni kutoa huduma za hali ya hewa; sehemu ya pili ni kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha (14) na sehemu ya tatu ni kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini Tanzania kulingana na Kifungu cha (5) cha Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019.

Mwisho

Sunday, October 30, 2022

JWT PWANI YAITA WAFANYABIASHARA KUJIUNGA NA JUMUIYA




WAFANYABIASHARA PWANI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA KWENYE JUMUIYA 

Na John Gagarini

JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani imewataka wafanyabiashara kujiunga ili wanufaike na fursa mbalimbali zilizopo kwenye Jumuiya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa majukumu ya taasisi hiyo pamoja na fursa zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo katibu wa JWT Mkoa Wellu Mtaki amesema kwenye Jumuiya hiyo kuna fursa nyingi.

Mtaki amesema kuwa Jumuiya hiyo inamuwezesha mfanyabiashara kutatua changamoto zake na mfanyabiashara anauwezo wa kutoa kero maoni na mapendekezo yanayohusu biashara na taasisi ikafikisha sehemu husika kwa ajili ya utatuzi tofauti na mtu kupeleka kero yake mwenyewe.

"Lengo la Jumuiya ni kuwaunganisha kwa pamoja wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwawezesha kutoa mawazo na maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa na kuziwasilisha serikalini,"amesema Mtaki

Amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara nchini Tanzania na moja ya huduma ni kuwaunganisha na bima za aina tofauti ambazo zimeanza kutolewa kwa wanachama.

"Huduma za bima zinazotolewa ni pamoja na bima ya Elimu au Carrier Life Plan kupitia shirika la bima la Jubilee ambalo linamsaidia mtoto wa mwanachama kunufaika kwenye elimu, bima ya Afya ambayo ina kifurushi cha aina tatu ambacho Scare individual and Family health insurance, pamoja Afya, Jubilee Afya na huduma ya bima ya nafaka," Amesema Mtaki.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote mkoani Pwani kuhakikisha wanafuata taratibu na miongozo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA) ili kepuka changamoto zitakazojitokeza.

Aidha amesema kuwa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania haijihusishi wala kufungamana na udini, ukabila, siasa, wala ushabiki wa michezo.


RAIS SAMIA KUZINDUA MATOKEO YA SENSA


RAIS SAMIA KUTANGAZA MATOKEO YA SENSA KESHO.

Na Wellu Mtaki, Dodoma.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kutangaza matokeo ya Sensa ya watu na Makazi Oktoba 31 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hamza Juma ameyasema hayo Jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwenye kikao maalumu cha wajumbe wa kamati ya maandalizi ya uzinduzi wa tukio hilo.

Juma amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi wa tukio la kutangazwa kwa matokeo ya sensa ya watu na anwani za makazi yamekamilika.

Ameeleza kuwa kazi kubwa ya kuratibu na kusimamia imefanywa na viongozi wa mkoa wa Dodoma na kilichobaki watakuwa wamekamilisha Oktoba 30.

Aidha amesema kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi la mwaka huu limefanyika kisasa zaidi tofauti na miaka ya nyuma na litaisaidia Serikali katika kupanga mipango yake ya kiuchumi,kijamii na maendeleo. Zoezi la sensa ya watu na makazi lilifanyika hivi karibuni.

Saturday, October 29, 2022

MATRILIONI YATENGWA MIRADI YA BARABARA NCHINI


TANROADS YATENGA TRILIONI 3.8 UTEKELEZAJI MIRADI YA BARABARA 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

WAKALA wa Barabara Nchini (TANROADS) imetenga kiasi cha shilling trilioni 3.8 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja makubwa nchi nzima.

Hayo yamesemwa leo na mtendaji mkuu wa Tanrods injinia Rogatus Mativila alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu shughuli mbalimbali zinazoendelea kufanywa na wakala.

Mativila amesema kuwa tayari wakala wa barabara imefanya usanifu wa miradi hiyo ambayo baadhi ni madaraja makubwa sita ikiwa ni pamoja na daraja la bwawa la Mtera Mkoani Dodoma , daraja la Jangwani Mkoani Dar - es- Salam, daraja la mkoa wa Simiyu, daraja la Mzinga, daraja la Mtoroni na makaravati sehemu mbalimbali nchini.

Amesema kuwa mradi mwingine mkubwa utakaotekelezwa ni ule wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ataweka jiwe la msingi Oktoba 30 mwaka huu.

Ametoa wito kwa Watanzania hasa madereva wa magari kuitunza miradi hiyo kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miradi hiyo.