Thursday, May 12, 2016

KIWANDA CHA TILES KUJENGWA MKURANGA


Na John Gagarini, Mkuranga
WAKAZI wa mkoa wa Pwani wametakiwa kuunga mkono mkakati wa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli ya kuhamasisha ujenzi wa viwanda na uwekezaji.
Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Nyamato na Mkiu wilayani Mkuranga wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Goodwill Tanzania Ceramic mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa wananchi wananafasi kubwa ya kufanikisha nchi kuwa ya viwanda kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanda.
Ndikilo alisema kuwa wananchi wanapaswa kuwapa ushirikiano wawekezaji wa viwanda ili waweze kufanya kazi bila ya kuhujumiwa kwani kuna baadhi ya watu wamekuwa wakihujumu miundombinu ya viwanda.
“Wawekezaji kama hawa wa viwanda mnapaswa kuwaunga mkono kwani manufaa ya uwepo wao ni mengi sana ikiwa ni pamoja na kupata ajira pamoja na nyie kuuza bidhaa zenu kwani biashara zitakuwa nyingi hivyo mtaweza kubadilisha maisha yenu lakini endapo mtawafanyia vitendo vya kuwakatisha tama wataondoka,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kwa sasa mkoa wa Pwani ajenda yake ni kuhakikisha unakuwa mkoa wa viwanda na hilo linawezekana kwa kuwa na viwanda vingi vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.
“Mkoa kwa sasa umeamua kujitangaza kiviwanda kwnai nafasi za uwekezaji bado zipo nyingi na lengo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na uchumi wa kati na utainuka endapo kutakuwa na viwanda vingi mfano tu wilaya ya Mkuranga mmeanza kutekeleza kwa vitendo mkakati wa Rais wa kuwa na viwanda kwnai kwa sasa kuna viwanda 59,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wakurugenzi na wakuu wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuhamasisha wageni na wazawa kujenga viwanda ili kuinua uchumi wa wananchi lakini wahakikishe wawekezaji wan je wanafuata taratibu za nchi kwa wafanyakazi kwa kuzingatia sheria za kazi.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Yang Zhen alisema kuwa kiwanda hicho ni cha pekee kwani kitakuwa cha pili barani Afrika kwa ukubwa na cha kwanza Tanzania kwa uzalishaji wa vigae ambapo kwa siku kitakuwa kikizalisha meta 80,000 kwa siku.
Zhen alisema kuwa maradi huo una thamani ya dola za Kimarekani 100 na umegawanyika kwenye hatua mbili ambapo awamu hii ya kwanza itaisha mwishoni mwa mwaka huu huku ile ya pili ikiisha mwishoni mwa mwakani hivyo bidhaa hizo za vigae zitakuwa zikizalishwa hapahapa na siyo nje ya nchi.
Aidha alisema kuwa wanatarajia kujenga shule, kuwapatia maji, zahanati pamoja na kituo cha polisi ikiwa ni kama mchango wao kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho ambapo mara kitakapokamilika kitaajiri watu 2,000 na kwa sasa kimetoa ajira kwa watu 200.
Mwisho.

Thursday, May 5, 2016

johngagariniblog: ACHINJA MKE NA MTOTO WAKE KISA WIVU WA MAPENZI

johngagariniblog: ACHINJA MKE NA MTOTO WAKE KISA WIVU WA MAPENZI: John Gagarini, Kibaha JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Frowin Peter Mbwale (26) mkazi wa Kawe Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma z...

WATAKA VYUO VYA KATI KUUNGANISHWA NA BODI YA MIKOPO

Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI na Bodi ya Mikopo Nchini (TCU) imeshauriwa kuviingiza kwenye mpango wa mikopo wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Kati kama ilivyo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu wakati mkutano wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Juu wa (CCM).

Sharifu alisema kuwa wanafunzi hao ni sawa na wale wa vyuo vikuu na wengine wanatoka kwenye mazingira magumu na wanahitaji mikopo ili waweze kupata elimu ya juu.

“Hali ya sasa ni ngumu na wazazi ni wale wale wanahitaji kupunguziwa mzigo wa kulipa ada ambazo ni kubwa hivyo tunaona kuwa kuna haja ya serikali kuviingiza na vyuo vya kati kwenye mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi,” alisema Sharifu.

Alisema kuwa kwa kuwa nchi imeamua kuwekeza kwenye elimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora hadi kufikia elimu ya juu ambayo ndiyo inaweza kumsaidia mtoto.

“Kwa sasa elimu ya juu ndiyo inayotakiwa tofauti na elimu ya kawaida ambayo si ya juu ambayo kwa sasa haina nafasi ya muhitimu kupata ajira hivyo kulazimisha watu wapate elimu ya juu,” alisema Sharifu.

Aidha alisema kuwa shirikisho hilo ni mboni ya chama na linafanya kazi kubwa ya kukijenga chama kwani hapo ni tanuru la kuandaa viongozi wa baadaye wa kukiongoza chama pamoja na nchi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kibaha Maulid Bundala  ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa Mkoa Mwinshehe Mlao alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo alisema kuwa Shirikisho la Vyuo Vikuu la CCM linafanya kazi kubwa ya kukitetea chama.

Bundala alisema kuwa CCM imeleta ukombozi ndani ya nchi na ni chama kikongwe hivyo kwa wanavyuo waliojiunga na shirikisho hilo wako sehemu salama kwani mawazo yao yataleta manufaa kwa nchi.

Aidha alisema kuwa nchi kwa sasa ina hitaji kuongozwa na wasomi hivyo wasomi hawa wataleta mabadiliko na chama kiko tayari kubadilika na wao wananafasi ya kumshauri Rais na wao ndiyo watakaoliinua taifa.

Naye naibu katibu mkuu wa shirikisho hilo Siraji Madebe alisema kuwa shirikisho lao linakabilia na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wancahama wake wale wa vyuo vya kati kutotambuliwa na Bodi ya Mikopo hivyo kutopata mikopo.

Madebe alisema kuwa licha ya changamoto mbalimbali lakini watahakikisha wanaendeleza umoja wao ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa shirikisho hilo ambayo ni kuwaunganisha wasomi walio vyuo kuwa na umoja wao ili kukipigania chama.

Mwisho.

TANESCO KUWAUNGANISHIA UMEME WANA VIJIJI MRADI WA BILIONI 30

Na John Gagarini, Kisarawe

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani kupitia mradi wa umeme vijijini (REA) unatarajia kusambaza umeme kwa wananchi 11,000 wenye thamani ya shilingi bilioni 30 kwenye vijiji 109 vya mkoa huo .

Kwa mujibu wa Mhandisi mkuu wa Mradi huo wa REA mkoa wa Pwani Leo Mwakatobe alisema mradi huo wa awamu ya pili utakamilika mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.

Mwakatobe alisema kuwa lengo kubwa kwa sasa ni kutekeleza agizo lililotolewa na serikali la kuhakikisha miradi hiyo ya umemem vijijini inawafiki wananchi wengi na kwa wakati uliopangwa.
“Tumeshaanza katika kutekeleza miradi hiyo katika maeneo ya Chalinze, Kisarawe na tutaendelea katika sehemu mbali mbali za Mkoa wetu wa Pwani na tunatarajia kufikia vijiji vipatavyo 109 vilivyopo katika Mkoa wetu,” alisema Madulu.   
Alisema kuwa kuwa mbali ya kuendelea kukutekeleza miradi hiyo hata hivyo wanakumbana na changamoto nyingi katika utekelezaji wa  wakati wanapotaka kupitisha miundomibu katika makazi ya watu.

“Baadhi ya watu wamekuwa hawataki kuridhia umeme kupita kwenye maeneo yao au kutaka fidia kubwa hali ambayo inasababisha kuwa na changamoto za hapa na pale lakini hata hivyo tunajitahidi kuwaelewe umuhimu wa miradi hiyo na kupata nishati hiyo ya umeme,” alisema Mwakatobe.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani  Martin Madulu alisema kuwa kwa sasa wanatekeleza  agizo lililotolewa na serikali kuhakikisha wanawafikia wateja wao wote hususani wale wa vijijini  kwa lengo kuweza kuwaunganishia umeme kwa bei nafuu.

Madulu alisema kuwa watahakikisha wanafanya jitihada ili kuwafikia wateja wao ili waweze kuwa na nishati ya umeme katika maeneo mbai mbali hususan kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Wakati huo huo wakazi zaidi wa 100 katika  kijiji cha  Nyeburu  Wilayani Kisarawe waliokuwa na tatizo  la upatikanaji wa nishati ya umeme na kuishi  katika giza  kwa kipindi cha muda mrefu kwa sasa wamenufaika baada ya  kuunganishiwa umeme kutokana na  kukamilika kwa mradi wa umeme vijijini (REA) awamu wa pili.

Baadhi ya wakazi hao walisema kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaweza kuleta chachu kubwa ya kimaendeleo katika kijiji hicho kwani mwanzoni   walikuwa wanashindwa tutimiza malengo yao waliyojiwekea kutokana na kutokuwa na nishati hiyo ya umeme.

Mwisho.

ADAMJEE KUIONGOZA TCCIA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
CHEMBA ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoa wa Pwani imemchagua Zainuddin Adamjee kuwa mwenyekiti wake ambaye ataongoza kwa kipindi cha miaka mitatu.
Uchaguzi huo ulifanyika Mjini Kibaha mwishoni mwa wiki ambapo Adamjee ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kawe alichaguliwa bila ya kupingwa kutokana na kutokuwa na mpinzani ambapo uchaguzi huo uliitishwa baada ya uongozi uliopita kumaliza muda wake.
Viongozi wengine waliochaguliwa ni Ana Maridadi ambaye ni makamu mwenyekiti biashara, Karim Mtambo makamu mwenyekiti Kilimo na Mohamed Kiaratu mwakilishi wa mkutano mkuu Taifa.
Wengine waliochaguliwa ni Frank Mzoo mweka Hazina na Attiki Mohamed ambaye ni mjumbe wa kamati ambapo wagombea hao wote hawakuwa na wapinzani.
Akizungumza na wanachama na viongozi waliochaguliwa Rais wa TCCIA Taifa Injinia Peter Kisawilo alisema kuwa viongozi waliochaguliwa wanapaswa kuhakikisha wanawawekea mazingira mazuri wanachama ili waweze kuingia kwenye soko la ushindani la kimataifa.
Kisawilo alisema kuwa nchi ya Tanzania imeingia kwenye mikataba ya masoko makubwa yakiwemo yale ya Comesa, Sadc na la Afrika Mashariki ambapo wafanyabiashara wanapaswa kutengeneza bidhaa zitakazoingia kwenye ushindani na si kuwa watazamaji.
Kwa upande wake Adamjee alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha mkoa wa Pwani unakuwa moja ya mikoa ambayo inainua uchumi wake kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kuwa na viwanda ili nchi iwe na uchumi wa kati.
Adamjee alisema kuwa kwa kuwa mkoa huo una uzalishaji mkubwa wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji viwandani na rasilimali za uvuvi hivyo una nafasi kubwa ya kuinua kipato cha wananchi wa mkoa.
Awali mwakilishi wa mgeni rasmi Anatoly Mhango ambaye alimwakilisha mkuu wa wilaya ya Kibaha alisema kuwa chemba hiyo ina nafasi kubwa ya kuwainua wanachama wake kupitia masoko ya ndani na nje.
Mhango alisema kuwa njia mojawapo wanayopaswa kuitumia ni kujitangaza ili watu waweze kujua fursa zinazopatikana kupitia chemba hiyo pia kupitia Chama Cha Kuweka na Kukopa SACCOS kilichopo ndani yake wanachama wanapaswa kurejesha mikopo kwa wakati ili watu wengi waweze kukopa.
Mwisho.   
      

MADIWANI WATAKA BODI YA TENDA IVUNJWE

Na John Gagarini, Kibaha
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wameridhia kuvunjwa kwa Bodi ya Tenda kwa kushindwa kutekeleza vizuri majukumu yake hivyo kusababisha miradi mingi kukwama.
Wakizungumza kwenye kikao cha Madiwani kilichofanyika mjini Kibaha madiwani hao walisema kuwa kutokana na bodi hiyo kutokuwa makini imesababisha wakandarasi wengi kuidai Halmashauri huku miradi mingi ikiwa imejengwa chini ya kiwango.
Akizungumza kwenye kikao hicho Diwani wa Kata ya Tumbi Hemed Chanyika alisema kuwa wazabuni wengi wameingia kwenye mgogoro na Halmashauri kwani wengi wameshindwa kufikia vigezo vya kazi wanazopewa huku mawakala wakishindwa kupeleka fedha za makusanyo kwa wakati.
Chanyika alisema kuwa bodi hiyo imeshindwa kuchagua wazabuni ambao wana uwezo wa kufanya kazi na inafanya kazi kwa mazoea pia ni ya muda mrefu hivyo inapaswa kubadilishwa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi kwa wazabuni kwa lengo la kuleta maendeleo.
“Baadhi ya miradi mingi imekwama kwani wazabuni wengine wameshindwa kukamilisha kazi zao wengine wamekuwa wakiachia kazi bila ya kukamilika na kuondoka matokeo yake ni kuitia hasara Halmashauri na kudumaza maendeleo ya Mji wetu,” alisema Chanyika.
Kwa upande wake Kambi Legeza alisema kuwa miradi mingi iko chini ya kiwango kutokana na kutokuwa na wakandarasi wasiokuwa na uwezo pia mapato ya Halmashauri yameshuka hivyo kuna haja ya kuibadili ili kupata bodi nyingine itakayokuja na mawazo mapya.
Legeza alisema kuwa bodi hiyo ya tenda ndiyo yenye uwezo wa kuwapitisha wazabuni mbalimbali ambao wanapaswa kuwa na uwezo lengo likiwa ni kuleta maendeleo kwa halmashauri ambayo yanaleta manufaa kwa wananchi ambao ndiyo wanaolengwa.
Akijibu hoja hizo kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Leah Lwanji alisema kuwa ofisi yake imelipokea suala hilo na italifanyia kazi kama mapendekezo ya madiwani yalivyotolewa.
Lwanji alisema kuwa kuna taratibu za kisheria za kuvunja bodi hivyo lazima zifuatwe na endapo itabidi kufanya hivyo itafanyika ili kuhakikisha taratibu zinafuatwa kwa lengo la kuboresha.
Mwisho.

MKUU WA MKOA AWATAKA WAKURUGENZI WATAKIWA KULIPA ZAWADI HEWA

Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametoa muda wa siku tatu hadi Mei 3 kwa wakurugenzi wa Halmashauri tatu za mkoa huo kuwapa zawadi za fedha watumishi  bora kwa mwaka huu baada ya Halmashauri hizo kutoa zawadi hewa kwenye Sherehe za siku kuu ya wafanyakazi May Mosi .
Sambamba na wakurugenzi hao wa Halmashauri pia ofisi ya Katibu Tawala mkoa (RAS) pamoja na mkurugenzi wa Shirika la Elimu nao wametakiwa kuwalipa wafanyakazi ambao walifanya vizuri kwenye vitengo vyao ambapo walipewa vyeti tu bila ya fedha kama taratibu zinavyokuwa za kuwapa fedha taslimu au hundi.
Ndikilo alitoa agizo hilo wilayani Mkuranga kwenye sherehe hizo ambazo kimkoa zilifanyika wilayani humo na kusema kuwa hayo ni masihara na yeye hayuko tayari kufanyiwa mzaha katika suala ambalo liliandaliwa kwa muda mrefu na kuwakopa zawadi hizo za fedha kwani nyingine toka mwaka jana hazijalipwa .
“Katika risala ya Shirikisho la Vyama Huru Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mkoa wa Pwani walilalamika kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri kuwakopa zawadi za fedha watumishi wanaofanya vizuri  kama motisha lakini kwa hali hili siwezi kukubaliana nalo  nawapa siku tatu muwe mmewalipa watumishi hao vinginevyo atakayeshindwa aje ofisini kwangu akutane na adhabu niliyoiandaa,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa hawezi kuvumilia watu wazembe wanaofanya dharau kwenye mambo mazito na kwamba atachukua hatua kali kwa Halmashauri ambazo zitashindwa kutoa zawadi hizo kwani zingene zimetoa kwanini wengine washindwe.
“Mimi siyo mtani wenu wala si saizi yenu haiwezekani mniite nije kutoa zawadi hewa ndo maana hatoa zikichukuliwa za kinidhamu mnasema mnaonewa ikifika Jumatano muwe mmeshawapa zawadi zao wahusika huu ni mzaha umepitiliza kiwango anayedhani tunatania aendelee aone,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa ameshangazwa na kitendo hicho cha wao kumfanya atoe zawadi hewa kwani hiyo ni dharau Ras Pwani, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji na Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha.
“Hatutaniani hapa huu ni mzaha uliopitiliza kiwango ujumbe umefika namna hii mnakatisha tamaa watumishi kwa kudai kuwa mchakato bado ni jambo ambalo halijanifurahisha na nisingependa hali hii isijitokeze tena,” alisema Ndikilo.
Awali akisoma risala ya TUCTA Amini Msambwa alisema kuwa wafanyakazi wana haki ya kutimiziwa haki zao za msingi na siyo lazima zipatikane kwa shinikizo la maandamano, migomo na hata kufungia nje waajiri.
Msambwa alisema kuwa moja ya changamoto ni baadhi ya wawekezaji wa nje na wandani kuwanyima fursa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao sehemu za kazi ambayo ni haki yao ya kisheria na kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ya Dhana ya Mabadiliko ilenge kuinua hali za wafanyakazi.
Aidha wameomba Halmashauri kuruhusu kuwa na mabaraza ya wafanyakazi na ambako yako yakutane kwenye vikao vyao vya kisheria lakini yanafanyika kwa ajili ya kupitisha bajeti za halmashauri.
Mwisho.