Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la ugawaji wa viwanja kwenye eneo la Mitamba limeingia dosari baada ya Madiwani wa Halamshauri ya Mji Kibaha kutaka ufafanuzi juu ya utaratibu wa kugawa viwanja vilivyopo kwenye eneo hilo kabla ya kuvigawa kwa wananchi ambao walilivamia.
Madiwani hao walitaka ufafanuzi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Mjini Kibaha na kusema kuwa kabla ya zoezi hilo wataalamu wanapaswa kuwajulisha utaratibu wa jinsi watakavyovigawa viwanja hivyo.
Eneo hilo lilikuwa chini ya Wizara ya Mifugo Kilimo na Umwagiliaji lakini lilivamiwa na wananchi hali ambayo ilibidi Halmashauri igawane na wananchi nusu kwa nusu ambapo kuna jumla ya viwanja 6,500 kwenye hekari 747.
Diwani wa kata ya Sofu Yusufu Mbonde alisema kuwa mradi huo ambao una thamani ya shilingi bilioni 2.7 ulitakiwa uanze kutekelezwa mwezi huu hauko wazi hasa katika suala zima la jinsi fedha zitakavyotumika katika kuutekeleza kwake.
Mbonde alisema kuwa kwa kuwa serikali imeamua kulipima eneo hilo na kugawana na wavamizi hao wapatao 350 ni vema kukawa na uwazi kwa lengo la kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.
“Tunachokitaka ni kupewa ufahamu juu ya zoezi hili kabla halijaanza kutekelezwa ili tuweze kujua kitakachofanyika pale kwani mradi huo ni mkubwa na utakuwa na faida kubwa kwa wananchi pamoja na Halmashauri hivyo ni vema kukawa na uwazi,” alisema Mbonde.
Kwa upande wake diwani wa Viti Maalumu Tuaje Ponza alisema kuwa moja ya vitu ambavyo vinashangaza ni kukodisha greda kwa ajili ya kazi hiyo huku Halmashauri nayo ikiwa na greda lake kwanini lisitumike hilo.
“Katika kupunguza gharama ni vema tukatumia greda letu kwani hatuwezi kukodisha wakati tuna la kwetu tulinunua kwa ajili ya kufanyia kazi zetu hivyo ni vema tukatumia la kwetu,” alisema Ponza.
Akijibu hoja mbalimbali mkuu wa Idara ya Mipangomiji Lucy Kimoi alisema kuwa viwanja hivyo vitatolewa kwa vipindi vinne tofauti ambapo awamu ya kwanza itakuwa viwanja 500 awamu ya pili viwanja 1,500 ya tatu 2,000 na ya tatu viwanja 2,500.
Kimoi alisema kuwa kutokana na ukosefu wa fedha zoezi hilo la ugawaji wa viwanja hivyo utafanywa na Halmashauri pamoja na wazabuni ambapo vitapimwa kwa shilingi 334,500 huku wazabuni wakivipima kwa shilingi 150,000 kwa kiwanja kimoja.
“Ni kweli tuna greda letu lakini kutoakana na zoezi hilo kuwa la muda mrefu ndiyo sababu tunahitaji mawili kwa ajili ya kufanikisha ugawaji huo kwani moja itabidi lisitoke eneo la kazi huku lingine likifanya kazi za nje kwani kazi zitakuwa ni nyingi sana ikiwa ni pamoja na sehemu ya huduma za jamii, makazi na huduma nyingine muhimu,” alisema Kimoi.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Leah Lwanji alisema kuwa ombi la madiwani kuwapa uelewa juu ya mradi huo limekubaliwa na watakaa nao kabla ya kuanza ugawaji huo.
Mwisho.