Sunday, July 27, 2014

JESHI LA POLISI PWANI LAJIPANGA SIKUKUU YA IDDI




Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limewataka madereva kuwa makini waendeshapo magari na kuacha matumizi ya vilevi ili kuepukana na ajalizisizo za lazima ambazo zinaweza zikajitokeza wakati wa kipindi cha sikukuu ya Eid el Fitr inayofanyika leo duniani kote.
Pia limewataka wanafamilia kutotoka wote majumbani bila ya kuacha watu au kutoa taarifa kwa majirani ili kuepuka wizi na uhalifu unaoweza kujitokeza wakati wa sikukuu.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakitumia vilevi wakati wa kiendesha magari jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu.
“Jeshi la polisi liko makini katika kipindi hichi cha sikukuu ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu bila ya matatizo na linawaomba madereva kuachana na tabia ya kutumia vilevi ili kuepuka ajali wakati huu,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kitahakikisha madereva wanafuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zianweza kutokea na kuleta madhara kwa watu.
“Tunasisitiza madereva kuachana na ulevi wakati wa kuendesha kwani uzoefu unaonyesha ajali nyingi zimekuwa zikitokana na matumizi ya ulevi hivyo waache matumizi hayo na endapo watabainika watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Kamanda Matei.
Kwa upande wa wananchi aliwataka kutumia ulinzi jirani kwa kuacha mtu au watu badala ya kuondoka wote na kuacha nyumba peke yake jambo ambalo linaweza likasababisha wizi majumbani.
“Wezi wamekuwa wakitumia mwanya wa kuiba kwenye nyumba ambazo hazina watu hivyo hata kama nyumba nzima imetoka ni vyema wakatoa taarifa kwa majirani ili wawalindie nyumba zao,” alisema Kamanda Matei.
Aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe kutojaza watu kupita kiasi ili kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza endepo watakuwa wamejaza watu wengi kwenye kumbi zao.
“Kuna hatari nyingi zinazotokana na kumbi kujaa kupita kiasi mfano watu kukosa hewa na kusababisha vifo au bahati mbaya shoti ya umeme endapo itatokea hivyo lazima wazingatie masharti ya leseni zao zinavyowataka ili kuepusha athari kama hizo,” alisema Kamanda Matei.
Alibainisha kuwa jeshi lake limejipanga kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafanyika kwa amani na utulivu kwa kuweka ulinzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya doria mitaani.
Mwisho.

MAGUFULI ATOA UFAFANUZI WA FIDIA BARABARA NDUNDU SOMANGA



Na John Gagarini, Rufiji
Serikali kupitia wizara ya Ujenzi imetoa ufafanuzi juu ya suala la fidia kwa wakazi wanaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Ndundu-Somanga iliyopo kati ya Mikoa ya Pwani na Lindi.
Waziri wa ujenzi Pombe Magufuli akizungumzia suala hilo kwa wananchi wakati akikagua barabara hiyo huku akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali,wakala wa Tanroads katika Mikoa ya Lindi na Pwani alisema wale waliojenga nyumba zao ndani ya mita 22.5 hawatolipwa fidia kutokana na kuvunja sheria.
Alieleza kuwa mbali ya kutolipwa fidia pia watu hao watatakiwa kulipia gharama za mafuta ya greda ambalo litafanya kazi ya ubomoaji.
Magufuli Alielezea wale walio nje ya mita 22.5 na ambao makazi yao yamejengwa nyuma ya mwaka 2007 ambapo watawekewa alama ya X kwa rangi ya kijani ikiashiria hao ndio watalipwa fidia .
Aidha Waziri huyo wa Ujenzi alikemea tabia ya kuiba mafuta inayofanywa na baadhi ya watumishi wa mkandarasi huyo sanjali na baadhi ya wananchi kwani kwa kufanya hivyo ni kukwamisha kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.
Alitoa rai hiyo baada ya kufikishiwa malalamiko hayo na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Manzese kilicho mpakani mwa mikoa ya Lindi na Pwani kuwa kuna tabia ya kuibiwa mafuta jambo ambalo linasababisha ujenzi kusuasua.
Magufuli pia alimtaka mkandarasi wa barabara hiyo M.A Kharafi $ Sons Ltd kuwalipa fedha nzuri wafanyakazi wake  ili waweze kuondokana na tamaa za kuiba mafuta na vifaa vingine.
Mwishoni mwa wiki Magufuli alitoa siku 60 kwa Mkandarasi wa barabara ya Ndundu-Somanga iliyopo kati ya Mikoa ya lindi na Pwani M.A Kharafi $Sons Ltd kuhakikisha anamaliza ujenzi wa barabara hiyo .
Agizo hilo ni kuanzia sasa hadi mwezi wa 9 mwaka huu awe ameshamaliza kazi hiyo na kama akizembea serikali itamchukulia hatua zaidi kwani imeshamlipa kwa awamu nyingine Bil 8.91 hivyo hakuna kisingizio kingine.

Waziri Magufuli alisema mkandarasi huyo amekiuka mkataba hivyo serikali imechoshwa na usumbufu na visingizio vyake  .
Alisema Mkataba wake ulikuwa ukionyesha kuanza ujenzi mwaka 2009 na kukamilika 2011 kwa kujenga km 56.318 kwa kiwango cha lami lakini hadi sasa km 10 bado hajazikamilika.
Sambamba na agizo hilo aliwaagiza mameneja wa wakala wa barabara Tanroads ,Mikoa ya Lindi na Pwani kumbana Mkandarasi huyo ili kuhakikisha hazembei kumaliza kazi hiyo kwa muda aliopewa.
Aidha alisema tayari kwasasa wizara imechukua hatua ya kumfukuza kazi Mhandisi Msimamizi ushauri wa awali wa ujezi wa barabara hiyo Engineering System Group –KSCC toka juni 8 mwaka huu .
Ambapo kwasasa barabara hiyo itasimamiwa na Wakala wa barabara –Tanroads-yenyewe kupitia kitengo cha usimamizi wa kazi ndani ya wakala huo kwa mujibu wa sheria namba 16 ya mwaka 1997.

"Wasimamiazi hao wamsimamie mkandarasi hadi atoke makamasi ,na ni lazima kuanzia sasa afanye kazi usiku na mchana,jumatatu hadi jumapili ili amalize ujenzi kwa muda wa miezi hii miwili pekee”alisema Magufuli.

Alieleza kuwa ifikie hatua ya kusema basi kulea wakandarasi wasumbufu ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo vumbi na kukwama kwa magari kutokana na uzembe wa mkandarasi husika.

Nae Mtendaji Mkuu wa wakala wa barabara Tanroads nchini ,Mhandisi Patrick Mfugale alieleza mbali ya changamoto hiyo pia mkandarasi huyo alishindwa kuendesha mradi kwa fedha zake mwenyewe hadi serikali ilipomwezesha.
Sababu nyingine ni kucheleweshwa kwa fedha kutoka kwa wachangiaji wa fedha wengine katika mradi huo ikiwemo OPEC na Quwait fund .
Barabara ya Ndundu-Somanga  ina urefu wa km 56.318 ,zilizokamilika ni km 42 huku km 10 zikiwa bado hazijakamilika,na hadi kukamilika kwa ujenzi itagharimu kiasi cha sh. Bil 58.813 ambapo hadi sasa umegharimu sh.Bil 49.
Katika gharama hizo serikali itachangia asilimia 55,OPEC 14 na Quwait Fund asilimia 31.

Mwisho

MEYA AWATAKA WAISLAMU KUDUMIASHA AMANI NA UPENDO IDDI



Na John Gagarini, Bagamoyo
WAISLAMU kote nchini wametakiwa kusherehekea sikuu ya Eid el Fitr kwa upendo na amani ili funga yao ya mwezi mzima iwe na maana na kuacha kufanya vitendo viovu ambavyo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.
Ushauri huo umetolewa jana mjini Bagamoyo na meya wa Mji wa huo Abdul Sharifu, wakati alipokuwa akifuturisha watu wenye mahitaji maalumu na waumini wa dini hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Sharifu alisema kuwa funga hiyo itakuwa na maana endapo waislamu wataisherehekea kwa kuzingatia imani ya dini ya kiislamu na si kinyume na dini inavyosema.
“Baadhi ya waislamu wamekuwa wakiitumia siku hiyo kwa ajili ya kufanya matendo ambayo hayampendezi mwenyezi Mungu hali ambayo inafanya waonekane mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa hawakufunga kutokana na kwenda kinyume na imani inavyosema,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa pia watumie siku hiyo kwa ajili ya kujitolea kuwasaidia  watu wenye mahitaji maalumu kama vile watu wenye ulemavu, yatima, wajane na wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali ili iwe sadaka ambayo itampendeza Mungu.
Sharifu ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo aliwataka waumini wa dini hiyo na wale wasio wa imani hiyo kuitumia siku hiyo kwa ajili ya kumtafakari mwenyezi Mungu.
 Wakati huo huo wenye uwezo mkoani Pwani wametakiwa kumtukuza Mungu katika kipindi cha siku kuu ya Eid el Fitr kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji ili wapate thawabu mbele ya mwenyezi Mungu.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Mkoani Pwani, Method Mselewa  ambaye alimwakilisha mbunge huyo Silvestry Koka wakati wa kutoa mkono wa Iddi kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutoka misikiti mbalimbali wilayani hapa.
Mselewa alisema kuwa kutoa wakati wa kipindi hichi ni sadaka ambayo ina manufaa makubwa kwa waislamu hivyo wawe na moyo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao wajisikie kama kuna watu wanawajali.
“Mbunge kila mwaka kipindi kama hichi amekuwa akijitolea kwa makundi hayo ambayo ni pamoja na wazee, yatima, wajane na wale wasiojiweza ambapo kila msikiti wanatoka watu 20 ili nao waweze kuandaa futari kwa familia zao,” alisema Mselewa.
Alisema kuwa waumini hao wanatoka kwenye misikiti 64 iliyopo katika Jimbo la Kibaha ambapo kila mmoja anapewa mkono wa Iddi ambao ni mchele kilogramu mbili, sukari kilogramu moja na fedha kwa ajili ya kununulia mboga.
Aidha alisema kuwa mbali ya kuwapatia vitu hivyo pia huwapatia ujumbe wa Iddi wa kudumisha amani, upendo na ushirikiano kwa watu wote katika kipindi hichi na nyakati zingine ambazo si za mfungo.
Alibainisha kuwa mbali ya makundi hayo pia mkono wa Iddi unatolewa kwa viongozi wa chama wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Baraza la Wanawake (UWT), Baraza la Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo jumla ya watu 2,000 watafikiwa.
Mwisho.
     

Saturday, July 26, 2014

PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO YA MBIO ZA MWENGE WA UHURU MKOANI PWANI

MWENGE UKIWASILI WILAYA YA MKURANGA
MKUU WA WILAYA YA RUFIJI NURDIN BABU AKIWA AMEBEBA MWENGE

MKUU WA WILAYA YA RUFIJI NURDIN BABU AKIMKABIDHI MWENGE WA UHURU MKUU WA WILAYA YA MKURANGA MERCY SILA


 KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA RACHEL KASANDA AKIWEKA JIWE LA MSINGI KWENYE MOJA YA MIRADI ALIYOIZINDUA

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA RACHEL KASANDA AKIPANDA MTI KWENYE UZINDUZI WA NYUMBA ZA WALIMU WILAYANI MKURANGA

 KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE TAIFA RACHEL KASANDA AKIMWAGILIA MTI BAADA YA KUUPANDA HUKO MKURANGA

 KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA RACHEL KASANDA AKIANGALIA JIWE LA MSINGI BAADA YA KUZINDUA MNADA WA NGOMBE HUKO MKURANGA

 RACHEL KASANDA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE TAIFA RACHEL KASANDA AKIMWAGIA MAJI KWNYE MTI ALIOUPANDA

 WAMASAI WAKICHEZA KWA FURAHA BAADA YA KUZINDULIWA MNADA WA NGOMBE HUKO MKIU MKURANGA

 MOJA YA WAKIMBIZA MWENGE KITAIFA WITO MNEMWELA AKIWAPA WAZEE MWENGE WAUGUSE HUKO KWENYE KIJIJI CHA MKANOGE WILAYA YA MKURANGA


 BAADHI YA WACHEZA NGOMA WA KIKUNDI KUTOKA WILAYA YA KISARAWE WAKITOA BURUDANI KWENYE MTAA WA KIPANGEGE WILAYA YA KIBAHA

 WATOTO AMBAO NI SKAUTI WA WILAYANI KIBAHA WKIWA WAMESIMAMA KWA UKAKAMAVU KUSUBIRI MWENGE

 KUSHOTO MKUU WA WILAYA YA KISARAWE FATUMA KIMARIO AKIMKABIDHI MWENGE MKUU WA WILAYA YA KIBAHA HALIMA KIHEMBA KULIA KWENYE MTAA WA KIPANGEGE

 MKUU WA WILAYA YA KIBAHA AKIONGEA MBELE YA MBUNGE WA JIMBO LA KIBAHA VIJIJNI ABUU JUMAA, HUKU KUSHOTO KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA RACHEL KASANDA AKISIKILIZA KWA MAKINI KUSHOTO NA KULIA NI MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KIBAHA TATU SAID

 BAADHI YA WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI KIPANGEGE WILAYANI KIBAHA WAKIPEPERUSHA BENDERA KUUPOKEA MWENGE

 ASKARI MAGEREZA KULIA AKIPOKEA MWENGE ULIPOINGIA WILAYANI KIBAHA

 ASKARI MAGEREZA WA MKOA WA PWANI WAKIJIPANGA KUPOKEA MWENGE WA UHURU ULIPOINGIA WILAYA YA KIBAHA

 KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA AKIJIANDAA KUPOKEA TAARIFA KWA MOJA YA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI YA RAFSANJANI ILIYOPO WILAYANI KIBAHA

 KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA RACHEL KASANDA AKIWA NA BAADHI YA VIONGOZI WA WILAYA YA KIBAHA KWENYE SHULE YA SEKONDARI RAFSANJANI

 KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA RACHEL KASANDA AKIHUTUBIA WANANCHI WA WILAYA YA MKURANGA

 KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA RACHEL KASANDA KUSHOTO AKIVISHWA SKAFU NA MOJA YA VIJANA WALIPOKUWA WAKIPOKEWA WILAYANI MKURANGA

WENYE UWEZO WAWASAIDIE WENYE MAHITAJI



Na John Gagarini, Kibaha
WATU wenye uwezo mkoani Pwani wametakiwa kumtukuza Mungu katika kipindi hichi cha mfungo mtukufu wa Ramadhan kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji ili wapate thawabu.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Mkoani Pwani, Method Mselewa  ambaye alimwakilisha mbunge huyo Silvestry Koka wakati wa kutoa mkono wa Iddi kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutoka misikiti mbalimbali wilayani hapa.
Mselewa alisema kuwa kutoa wakati wa kipindi hichi ni sadaka ambayo ina manufaa makubwa kwa waislamu hivyo wawe na moyo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao wajisikie kama kuna watu wanawajali.
“Mbunge kila mwaka kipindi kama hichi amekuwa akijitolea kwa makundi hayo ambayo ni pamoja na wazee, yatima, wajane na wale wasiojiweza ambapo kila msikiti wanatoka watu 20 ili nao waweze kuandaa futari kwa familia zao,” alisema Mselewa.
Alisema kuwa waumini hao wanatoka kwenye misikiti 64 iliyopo katika Jimbo la Kibaha ambapo kila mmoja anapewa mkono wa Iddi ambao ni mchele kilogramu mbili, sukari kilogramu moja na fedha kwa ajili ya kununulia mboga.
“Watu wamekuwa wakifuturisha kwa kuwalisha watu chakula lakini Mbunge kaamua kubadili staili kwa kuwapa vyakula hivyo ambapo wao watenda kuziandalia familia zao tofauti na kuwapa chakula ambapo watakaokula ni wachache tofauti na watakapopeleka nyumbani kuandaa wenyewe kwani yeye hawezi kuja na familia balia atakuja mtu mmoja,” alisema Mselewa.
Aidha alisema kuwa mbali ya kuwapatia vitu hivyo pia huwapatia ujumbe wa Iddi wa kudumisha amani, upendo na ushirikiano kwa watu wote katika kipindi hichi na nyakati zingine ambazo si za mfungo.
Alibainisha kuwa mbali ya makundi hayo pia mkono wa Iddi unatolewa kwa viongozi wa chama wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Baraza la Wanawake (UWT), Baraza la Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo jumla ya watu 2,000 watafikiwa.
Mwisho.