Na John Gagarini, Bagamoyo
KUFUATIA wakazi wa Kijiji cha Ruvu Darajani wilayani
Bagamoyo kuuondoa madarakani uongozi hatimaye tume ya watu sita imeundwa
kuchunguza tuhuma zinazoukabili uongozi huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkuu wa wilaya
hiyo Bw Ahmed Kipozi alisema tume hiyo imepewa muda wa wiki mbili ili kutoa
majibu juu ya uongozi huo.
Bw Kipozi alisema kuwa tume hiyo itachunguza baadhi ya
tuhuma ikiwa ni pamoja na kuuza eneo la umoja wa wauza mboga mboga wa Ruvu,
kuingia mikata na wawekezaji isiyokuwa na masalahi na wananchi ikiwa ni kinyume
cha taratibu, ubadhirifu wa fedha na uongozi kujihusisha na uingizwaji ngombe
kinyume cha taratibu.
“Tume hii itaundwa na maofisa mbalimbali wakiwemo wale
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamaba na Rushwa (TAKUKURU), mkagazi wa wa hesabu wa
ndani, ofisa ardhi, ofisa anayehusika na Vijiji na ofisa usalama,” alisema Bw
Kipozi.
Alisema kuwa tuhuma hizo endapo zitabainika viongozi
hao watachukuliwa hatua za kisheria kutokana na makosa endapo yatakuwepo.
“Wananchi walikuwa na hoja za msingi kwani kwa sasa
wameamka na kujua namna ya kuhoji jinsi gani rasilimali zao zinavyotumika hivyo
lazima viongozi wazingatie taratibu za uongozi,” alisema Bw Kipozi.
Aidha alisema kuwa wananchi wana haki ya kuhoji pale
wanapoona mali zao zinatumika vibaya na milango iko wazi kwenye ofisi yake kwa
wananchi ambao wanaona kuwa kuna mambo ambayo yanakwenda kinyume.
Alisema kutokana na tatizo hilo umeteuliwa uongozi wa
muda ambapo Bw Ramadhan Kondo ataongoza kama mwenyekiti na Jama Ramadhan
atakuwa ofisa mtendaji wa kijiji hadi uchunguzi utakapokamilika.
Mwisho.
Na John Gagarini, Bagamoyo
WILAYA ya Bagamoyo mkoani Pwani inawafuatilia watu 11
ambao wako kwenye mtandao wa wanaowatishia watu kuwa maeneo wanayoishi ni mali
yao kwenye baadhi ya Vijiji.
Mtandao huo ambao hutwaa maeneo makubwa ya Vijiji
hivyo na kuyauza hali ambayo imekuwa ikileta mtafaruku kwa wakazi hao.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya hiyo Ahmed Kipozi alisema
kuwa majina ya watu hao wanayo na kwa sasa wanaendelea kuwafuatilia ili
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Mtandao huu ni wa watu waishio Jijini Dar es Salaam
wenye asili ya Bagamoyo wamekuwa wakifanya vitendo hivyo ambavyo ni vya
kitapeliwa kwa kuyachukua maeneo ya watu wakidai kuwa yaliachwa na mababu zao
jambo ambalo si la kweli,” alisema Bw Kipozi.
Aidha alisema kuwa watu wanaotaka kununua maeneo au
mashamba lazima wafuate taratibu za kisheria ili kukabiliana na matapeli hao
ambao wanamtandao mkubwa unaowahusisha baadhi ya viongozi wa vijiji.
“Mtandao huo umekuwa ukitumia vyombo vya habari
kuhalalisha utapeli wa maeneo na mashamba ya watu kwa kudai kuwa wao ni
wamiliki wa maeneo husika,” alisema bw Kipozi.
Alitaja baadhi ya vijiji ambnavyo vimekumbwa na
mtandao huo wa kutapeli mashamba ya watu kuwa ni pamoja na Talawanda, Masuguru
na Msoga.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI wilayani Kibaha mkoa wa Pwani imetakiwa
kuwadhibiti matapeli wa viwanja ambao wamekuwa wakiwaibia watu kwa kuwauzia
viwanja ambavyo ni mali za watu wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
Mchungaji kiongozi wa Kituo cha Maandiko kilichopo wilayani Kibaha Gervase
Masanja alisema kuwa matapeli hao wamekuwa wakitapeli watu lakini hakuna hatua
zozote zinazochukuliwa dhidi yao.
Mch Masanja alisema kuwa watu hao ambao wanajihusisha
na vitendo hivyo wamekuwa wakitumia fedha kupindisha sheria pale wanapopelekwa
kwenye vyombo vya sheria.
“Tunashangaa watu hawa kuendelea kutapeli watu lakini
hawachukuliwi hatua zozote hata pale wanapopelekwa kwenye vyombo vya sheria
tunaomba serikali iwashughulikie kwani wanafahamika,” alisema Mch Masanja.
Mch Masanja alisema kuwa hata yeye mwenyewe
alitapeliwa kiasi cha shilingi milioni 2.3 kwa kuuziwa kiwanja ambacho ni mali
ya mtu hata alipompeleka kwenye vyombo vya sheria malalamiko yake yaliondolewa
na kupoteza fedha zake.
“Mambo kama haya ndiyo yanayoichafua serikali na
kuonekana kama vile inawakumbatia watu hao ambao wamekuwa wakiwaumiza
wananchi,” alisema Mch Masanja.
Aliitaka serikali kuwachukulia hatua kali baadhi ya
viongozi wa vijji na mitaa kwa kushirikiana na matapeli hao katika kuwadhulumu
wananchi kwani ofisi zao hutumika kufanya makubaliano ya mauzo ya maeneo.
Mwisho.
Na
Mwandishi Wetu, Kibaha
KUFUATIA
aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenezi wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw Suleiman Ndombogani kujiunga na Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kimepata mpiganaji na si mzigo
kama wanavyodai CCM.
Akizungumza
na gazeti hili mjini Kibaha mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA) mkoa wa
Pwani Bw Elison Kinyaha alisema kuwa chama hicho kimelamba dume kumpata
mwanachana huyo.
Bw
Kinyaha alisema kuwa Bw Ndombogani ni mtu makini na atakiletea ushindi chama
hicho kwenye uchaguzi ujao na CCM wataona umuhimu wake.
“CCM
wamesema kuwa huyu ni mzigo lakini kwetu ni sawa na almasi na fisi anapokosa
anasema sizitaki mbichi hizi,” alisema Kinyaha.
Aidha
alisema kuwa Bw Ndombogani ambaye ni mwandishi wa habari atakuwa ni mwenezi wa
habari za chama hivyo watu kukijua ipasavyo.
Alisema
kuwa moja ya changamoto ambayo wanataka ifanyiwe kazi ni kukuza soko la mkulima
kwenye mkoa huo ambao una chanagamoto nyingi za kimaendeleo.
“Tunatarajia
kuwapatia mafunzo vijana juu ya kujua haki zao za msingi ili waweze kujikwamua
na changamoto mbalimbali zinazowakabili,” alisema Bw Kinyaha.
Aliwataka
wanachama katika wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanajipanga kwenye chaguzi zijazo
ili waweze kuongoza kwenye nafasi mbalimbali.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
BENKI ya Familia kupitia Jumuiya ya Wazazi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imetoa kiasi cha shilingi bilioni 10 kila mkoa kwa
ajili ya uanzishwaji wa benki.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha
mkurugenzi wa benki hiyo Bw Dauda Salmin alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa
benki hizo ni kuiwezesha jamii kuondokana na umaskini kwa kukopa kwa masharti
nafuu.
Bw Salmin alisema kuwa uanzishwaji wa benki hizo
utakuwa kwenye mpango wa operesheni jamii kukabiliana na watu wasio kuwa na
ajira ili waweze kupata mikopo kwa ajili ya mitaji ya kuendeleza shughuli zao
za ujasiriamali bila ya kujali itikadi ya chama cha siasa.
“Jumuiya iliamua kuanzisha benki hizo ambazo zitakuwa
zikitoza riba ya asilimia 1.6 kwa kila mkopo ambapo ni ndogo ukilinganisha na
taasisi nyingine za kifedha ambazo ziko kibiashara zaidi na mbali ya
kuweka riba kubwa pia zinaweka masharti magumu mfano kutoa hati ya nyumba au
gari hali inayosababisha watu wengi kushindwa kukopa hasa wale wenye mitaji
midogo,” alisema Bw Salmin.
Aidha alisema kuwa mikopo hiyo itatolewa kwa vikundi
vya watu watano watano ambao kila mmoja atakopeshwa kiasi cha shilingi 500,00
na kila familia ambao ndiyo wakopaji lazima iwe na shughuli ambayo inaingiza
kipato si chini ya shilingi 7,500 kwa siku na marejesho yatakuwa kwa kipindi
cha miezi sita.
“Benki hizo ambazo zitakuwa kila kata tayari
zimeshaanza kufanya kazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam na sasa wanatarajia
kuanza kutoa mikopo kwenye mkoa wa Pwani na wakopaji wataunganishwa na mifuko
ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kukabiliana na majanga mbalimbali,” alisema Bw
Salmin.
Alibainisha kuwa changamoto kubwa wanayoipata ni
wakopaji wengi kuonekana kutaka kukopa kiwango kidogo cha fedha tofauti na ile
iliyopangwa na watakaonufaika na mikopo hii ni wajasiraiamali wadogowadogo kama
vile mama lishe, wenye magenge, waendesha bodaboda na wengineo.
Mwisho.