Thursday, September 12, 2024

*KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ELIMU, UTAMADUNI YAIFAGILIA KIBAHA MJI KWA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO*

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia Wizara ya Elimu na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeridhika na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Shule ya Shimbo iliyopo Kata ya Mkuza,Halmashauri ya Mji Kibaha.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Husna Sekiboko  amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ndoto na maono yake ni kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata Elimu bora  kwenye Mazingira rafiki ili kuandaa Wataalam kulitumikia Taifa lao na kwamba Kibaha Mji wamesimamia Ujenzi wa shule hiyo kwa viwango na thamani ya fedha inaonekana.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Leah Lwanji ameieleza Kamati kuwa Jumla ya Shilingi 528,998,425 kupitia Mradi wa SEQUIP zilipokelewa  ajili ya Ujenzi wa miundombinu  27  na tayari imekamilika  na tayari Wanafunzi 281 kati yake wavulana 149 na Wasichana 132 wameanza kunufaika kwa kuwapunguzia umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 8 kuifuata shule Mama ya Nyumbu.

Mhe.Hamisi Shabani Taletale ameipongeza Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa Mradi na kushauri kujengwa kwa uzio ili kuwawekea utulivu wanafunzi wakati wa Masomo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Husna Sekiboko ametoa maelekezo ya Kamati kama ifuatavyo;

Mosi, Shule zote nchini ziwe na utaratibu wa kukagua maudhui ya vitabu kama vinaendana na maadili ya Watanzania kuelekeza vitabu vihakikiwe na kugongwa mihuri wa kuridhia Matumizi na Kamishina wa Elimu nchini.

Pili,Serikali iangalie upya mgawanyo wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya Miradi kwani yapo maeneo wanakamilisha Ujenzi na maeneo mengine hawakamilishi ama Kujenga chini ya Kiwango na kuathiri matarajio na malengo.Ameitaka Wizara ya Elimu kufanya tathmini ya kimaeneo ili fedha zinazotolewa zitosheleze ili kuongeza tija ya Miradi husika.

Waziri wa Elimu Prof.Adolf Mkenda ameishukuru Kamati kwa kazi nzuri na kupokea maelekezo yote  ya Kamati kwa ajili ya kufanyia kazi.

Aidha,Mwenyekiti wa Kamati Mhe.Sekiboko amempongeza sana Dkt.Rogers Jacob Shemwelekwa Mkurugenzi wa Mji Kibaha kwa usimamizi mzuri wa Miradi ya Maendeleo kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani kuhakikisha Mabilioni ya fedha yanayotolewa na Dkt.Samia Suluhu Hassan yanafanyakazi zinazoonyesha matokeo kwa Watanzania.

Wednesday, September 11, 2024

MAKOCHA WA TIMU ZA SOKA ZA JESHI WAPATA MAFUNZO TOKA KWA WAKUFUNZI TOKA UHOLANZI

Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Jacob Mkunda kupitia uratibu wa Baraza la Michezo la Majeshi ya Ulinzi Dunia (Conseil International du Sports Military) imewaleta wakufunzi na wataalum kutoa mafunzo kwa makocha ikiwa na lengo ni kuwaaendeleza maafisa wa jeshi na aksari wenye taaluma ya  ukocha wa Mpira wa miguu kutokana mahusiano  mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na nchi ya Uholanzi.

Dhamira ya mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania ni  kupata walimu wazuri watakao saidia timu za jeshi zinazoshiriki ligi mbalimbali na Taifa.

Wakizungumza kwa wakati tofauti makocha ambao ni maafisa wa jeshi na aksari wameshukuru mkuu wa majeshi kwa kuliona hilo ambapo mbali na wakufunzi hao TFFwamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali lakini walimu hawa wakigeni wanavifaa  hivyo wanatoa ahadi ya kufanya vizuri katika kuhakikisha timu za majeshi na Taifa zinafanya vizuri.

Mafunzo  haya ni ya wiki mbili na ijumaa jioni yatafungwa rasmi hii inatokana na mahusiano mazuri ya Chama Cha Mpira wa Miguu cha Majeshi .

NYAMA YAPANDA BEI KIBAHA

KUFUATIA bei ya nyama kupanda kutoka shilingi 7,000 hadi 9,000 Kibaha Mkoani Pwani imesababisha wananchi kulalamika na kuiomba serikali kuwasaidia ili bei irudi kama ilivyokuwa awali.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha baadhi ya wananchi walisema kuwa kupanda kwa bei hiyo inasababisha washindwe kununua nyama.

Happy Ngilangwa alisema kuwa kama kuna namna ya kufanya ni vema serikali ikakaa na wafanyabiashara wa nyama ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa wanannchi.

"Tunaomba serikali ikae nao chini ili waangalie kama kuna baadhi ya mambo wayaweke sawa sababu sisi tunashangaa tu kuona bei imepanda ghafla,"alisema Ngilangwa.

Alisema kuwa nyama ni kitoweo muhimu ambacho ndicho chakula kikuu kwa wananchi wengi ukilinganisha na mboga zingine ambapo hata samaki nazo bei iko juu.

"Kwa sasa maisha yamekuwa magumu hivyo kupandisha bei ni kuwaongezea mzigo wananchi kutokana na bei kupanda baadhi ya watu wameshindwa kumudu bei,"alisema Ngilangwa.

Kwa upande wake mama lishe Neema Maneno alisema kupanda kwa bei ya nyama kumewaathiri ambapo kwa sasa imebidi wapunguze ukubwa wa vipande vya nyama.

Maneno alisema wana wateja wengi ambao wanakula chakula pamoja na kunywa supu wanalamika lakini hawana jinsi ya kufanya inabidibwaendane na hali halisi.

Naye moja ya wauzaji nyama Albert Koka alisema kuwa yeye kashindwa kufanya biashara na amefunga bucha kwani yeye hununua mabuchani na kuongeza kidogo ili apate chochote.

Koka alisema kuwa wao nao wanaumia kwani nao wanategemea kununua kwa wenye mabucha makubwa na kuuza kwa wananchi mitaani ili nao wapate riziki.

Naye mwenyekiti wa Chama Cha Wauzaji Nyama Kibaha Aidan Mchiwa alisema kuwa nyama imepanda bei kwa sababu ya nyama nyingi inauzwa nje.

Mchiwa alisema kuwa soko la nyama nje limekuwa kubwa sana ambapo ngombe nyingi zinanunuliwa na makampuni ambayo yanasafirisha kwenda nje ya nchi kwenye soko la Uarabuni.

Saturday, September 7, 2024


VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kutoa nafasi watu wenye mahitaji maalum kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwani nao wana haki ya kushiriki.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu wa Umoja wa Amani Kwanza Mkoani Pwani Halima Yusuph wakati wa mkutano kwa vyama vya siasa na jamii ambapo katiba inaonyesha kuwa binadamu wote ni sawa.

Yusuph alisema kuwa vyama vya siasa kutoa nafasi kwa kundi maalum la watu wenye ulemavu ili wapate nafasi kugombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 2024 mwaka huu bila ya kuwatenga kwani wana haki ya kushiriki uchaguzi.

"Kwa mujibu wa Katiba binadamu wote ni sawa hivyo kuna kila sababu ya watu wenye ulemavu kupata nafasi za kushiriki uchaguzi kwa kuchagua na kuchaguliwa na tunakemea ramli chonganishi ambazo husababisha wenye ulemavu wa ngozi kuuwawa,"alisema Yusuph.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Africa Talent Forum (ATF) MaryRose Bujash aliomba watu wenye ulemavu wasitengwe wala kunyanyapaliwa.

Bujash alisema kuwa elimu inapaswa kutolewa kwa jamii isiwatenge na pia na wao wanahitaji elimu zaidi ya masuala ya uchaguzi na uongozi ili kuweza kushiriki uchaguzi.

Naye Katibu wa siasa na uenezi Mkoani Pwani David Mramba alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajali na kutoa nafasi mbalimbali za ushiriki wa masuala mbalimbali kwa wenye ulemavu mbalimbali.

Mramba alosema kuwa katiba inaeleza kuwa binadamu wote ni sawa kama katiba inavyoelekeza na CCM inasimamia hilo.

Thursday, September 5, 2024

WAHITIMU JKT WAAHIDI KUWA WAZALENDO


WAHITIMU wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamemwahidi Rais Dk Samia Suluhu Hassan kulinda rasilimali na kujenga uchumi imara wa nchi ili ipate maendeleo.

Walitoa ahadi hiyo wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya JKT Operesheni miaka 60 ya Muungano kwenye kambi ya Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akisoma risala ya wahitimu hao Hilda Edward amesema kuwa watayatumia mafunzo hayo kwa kuifanyia nchi yao uzalendo ambao wamefundishwa kwenye mafunzo hayo ya miezi mitatu yaliyoanza Juni mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa Taifa linawategemea vijana kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na wanapaswa kuwa wabunifu.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Brigedia Jenerali Solotina Nshushi amesema kuwa vijana hao wanapaswa kujitunza na kuacha kutumia vilevi ambavyo vitasababisha kupata matatizo ya afya ya akili na miili.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali George Kazaula amesema kuwa vijana hao wanapaswa kutumia nidhamu kama silaha kwa kila jambo wanalolifanya.

Awali Mkuu wa kikosi hicho cha Ruvu Kanali Peter Mnyani amesema kuwa kambi hiyo pia inachukua vijana wenye mahitaji maalumu ambao nao wamehitimu mafunzo hayo.


Wednesday, September 4, 2024

WAHITIMU JKT KULINDA RASILIAMALI ZA NCHI

WAHITIMU wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamemwahidi Rais Dk Samia Suluhu Hassan kulinda rasilimali na kujenga uchumi imara wa nchi ili ipate maendeleo.

Walitoa ahadi hiyo wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria Operesheni miaka 60 ya Muungano kwenye kambi ya Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akisoma risala ya wahitimu hao Hilda Edward alisema kuwa watayatumia mafunzo hayo kwa kuifanyia nchi yao uzalendo ambao wamefundishwa kwenye mafunzo hayo ya miezi mitatu yaliyoanza Juni mwaka huu.

Edward alisema kuwa mbali ya kujifunza mafunzo ya kijeshi pia wamejifunza stadi mbalimbali za maisha ambazo wataziendeleza kule watakakokwenda.

"Tunaishukuru serikali kwa kurejesha mafunzo haya kwa mujibu wa sheria ambayo yatatuwezesha kuitumikia nchi na kulinda rasilimali kwani hapa tuko tayari kulitumikia Taifa tutadumisha nidhamu na uzalendo,"alisema Edward.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa Taifa linawategemea vijana kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na wanapaswa kuwa wabunifu.

Kunenge alisema kuwa wanapaswa kuitumikia jamii na kutatua changamoto kwa kutumia mafunzo hayo pasipo vurugu na anaiona Tanzania yenye Neema na kuilisha dunia na kuwa juu kiuchumi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Brigedia Jenerali Solotina Nshushi alisema kuwa vijana hao wanapaswa kujitunza na kuacha kutumia vilevi ambavyo vitasababisha kupata matatizo ya afya ya akili na miili.

Nshushi alisema kuwa mafunzo hayo yamezingatia kuanzishwa kwa jeshi hilo bila ya kujali dini, kabila wala hali ya mtu kwani wote wamekuwa kitu kimoja.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali George Kazaula alisema kuwa vijana hao wanapaswa kutumia nidhamu kama silaha kwa kila jambo wanalolifanya.

Kazaula alisema kuwa wao ni nguzo ya Taifa wakizingatia kiapo chao cha utii ikiwa ni pamoja na uzalendo mshikamano ukakamavu na kujiamini na kulitetea Taifa.

Awali Mkuu wa kikosi hicho cha Ruvu Kanali Peter Mnyani alisema kuwa kambi hiyo pia inachukua vijana wenye mahitaji maalumu ambao nao wamehitimu mafunzo hayo.

Mnyani alisema kuwa baadhi yao walishindwa kumaliza mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro na utovu wa nidhamu.