Friday, February 24, 2017

MWIJAGE AWEKA JIWE LA MSINGI KIWANDA CHA VIGAE PWANI










Na John Gagarini,Chalinze

WIZARA ya Biashara Viwanda na Uwekezaji imesema kuwa imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuzitaka taasisi zinazohusika na uwekezaji kutokuwa na ukiritimba.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Biashara Viwanda na Uwekezaji Charles Mwijage kwenye Kitongoji cha Pingo Chalinze wakati akiweka jiwe la Msingi kwenye kiwanda cha Vigae cha Twyford Ceramics Ltd.
Mwijage alisema kuwa uwekezaji kama huu unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda ambapo itaongeza pato la nchi na itazalisha ajira kwa wingi.
“Baadhi ya idara ambazo zinafanikisha uwekezaji ikiwa ni pamoja na brela, idara ya uhamiaji, idara ya kazi, mamlaka ya mapato TRA, wizara ya ardhi, shirika la viwango TBS, Baraza la Mazingira NEMC na nyinginezo zinapaswa kufanya kazi kwa wepesi ili kufanikisha uwekezaji,” alisema Mwijage.
Alisema kuwa kati ya idara hizo baadhi zimekuwa zikifanya vizuri lakini nyingine zimekuwa zikiwapa usumbufu mkubwa wawekezaji hali ambayo inawakatisha tamaa.
“Kwa upande wa wizara yangu hakuna tatizo lolote lakini kuna baadhi ya idara zimekuwa kero kubwa kwa wawekezaji kwa kuwa na ukiritimba usio na sababu naomba kama kuna idara zinakuwa kikwazo niambieni ili tuwachukulie hatua,” alisema Mwijage.
“Viwanda vikiwa vingi nchi itapata mapato makubwa kupitia kodi ambazo zitalipwa kutokana na uuzwaji wa bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa viwandani,” alisema Mwijage.
Alisema kuwa nchi zilizofanikiwa kukuza uchumi wake kupitia viwanda zimeweza kutoa ajira nyingi hasa kwa vijana kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho Jack Feng alisema kuwa kiwanda hicho asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka hapa nchini ambapo kigae kinatumia maligahafi zaidi ya 10.
Feng alisema kuwa mara kiwanda hicho kitakapokamilika Agosti mwaka huu kitaweza kupunguza asilimia 30 ya uagizaji wa vigae toka nje ya nchi.
“Tunatarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 moja kwa moja na 4,000 kazi za muda na gharama ya mradi huu ni dola milioni 56 sawa na bilioni 120 ambapo tunatarajia kuuza hadi nje ya nchi kama vile Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi,” alisema Feng.
Alisema kuwa wanaunga mkono nchi ya Tanzania kuwa na mpango wa kuwa nchi ya viwanda na wao wanapenda kuwa mfano kwa wawekezaji.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kituo cha uwekezaji Cliford Tandari alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda hicho ni wa mfano kwani utavutia makampuni mengi.
Tandari alisema kuwa hadi sasa kituo chake kimeweza kutoa wigo mkubwa katika kuandikisha miradi mbalimbali toka china na kufikia miradi 667 ambayo itazalisha ajira 83,141 kwa watanzania ambapo miradi 452 ni miradi inayohusiana na sekta ya uzalishaji viwandani.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kwa sasa mkoa huo umeweza kuwa na viwanda 264 huku vikubwa vikiwa ni viwili.
Ndikilo alisema kuwa uwekezaji huo ni mkubwa na unatarajia kukuza ajira kwa vijana wa mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.
Alisema kuwa mkoa wa Pwani bado una maeneo makubwa ya uwekezaji na tayari kuna eneo lenye bukubwa wa hekari 5,000 linahitaji mwekezaji na wameamua mkoa huo kuwa kituo cha uwekezaji.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete aliwapongeza wawekezaji hao kutoka nchi ya China na kusema kuwa Chalinze nayo imejipanga kuwa sehemu ya uwekezaji ambapo kuna ujenzi wa viwanda mbalimbali.
Ridhiwani alisema kuwa changamoto kubwa inayokabiliwa wananchi na wawekezaji ni ukosefu wa maji ambapo wamekuwa wakijitahidi kuikabili lakini bado hawajafanikiwa kuidhibiti aliomba wawekezaji hao kutoa ajira bila ya kuwabagua wenyeji.
Mwisho.









Ramani ya kiwanda cha vigae cha Twyford kilichopo Pingo Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani 


Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage akiongea wakati wa uwekeji jiwe la msingi kiwanda cha vigae cha Twyford kilichopo Pingo Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.




Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wa pili kulia akiwa na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kulia wakifuatilia jambo wakati wa uwekaji jiwe la msingi kwenye kiwanda cha vigae cha Twyford kilichopo Pingo Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.




Katikati Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage akifunua kitambaa kuashiria uwekeji jiwe la msingi kwenye kiwanda cha vigae cha Twyford kilichopo Pingo Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kushoto mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kulia kwa waziri ni Jack Feng mkurugenzi wa kiwanda hicho na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Riziwani Kikwete.


  


Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo kushoto Magid Mwanga akifuatiwa na mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo, mkurugenzi wa kiwanda cha vigae cha Twyford Jack Feng na mbunge wa Jimbo la Chalinze Riziwani Kikwete wakiweka udongo kwenye jiwe la msingi.



Friday, February 3, 2017

VIJANA JKT WALIOJITOLEA UJENZI MABWENI WAPONGEZWA

 Mkuu wa mkoa wa Pwani mwenye shati jeupe Injinia Evarist Ndikilo akionyeshwa ramani ya majengo ya mabweni ya shule ya sekondari ya Nasibugani na moja ya wasimamizi wa ujenzi huo yanayaojengwa na vijana toka Jeshi la Kujenga Taifa JKT Ruvu Mlandizi wilayani Kibaha, kushoto ni katibu tawala wa mkoa Zuber Samataba  
Na John Gagarini, Mkuranga
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo emelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Ruvu Mlandizi wilayani Kibaha kwa kujitolea kujenga mabweni ya shule ya Sekondari ya Nasibugani iliyopo kata ya Msonga Tarafa ya Kisiju wilayani Mkuranga.
Alitoa pongezi hizo alipotembelea shule hiyo ili kujionea maenedeleo ya ujenzi huo wa mabweni matano na nyumba tano za walimu za shule hiyo ambapo wanafunzi wanalala kwenye baadhi ya vyumba vya madarasa.
Ndikilo alisema kuwa kambi hiyo ilitoa vijana zaidi ya 100 ambao wanaenedelea na ujenzi huo ambao umefikia hatua ya linta na kwa sasa wana miezi mitatu.
“Jeshi limeonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kujitolea kujenga bure mabweni hayo lengo ni kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo wanaishi kwenye mazingira mazuri kuliko ilivyo sasa,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa jeshi hilo limeunga mkono serikali kwa kujitolea kujenga mabweni hayo hivyo kuokoa fedha nyingi endapo wamengepewa wakandarasi.
“Hadi sasa wametumia fedha kidogo sana kiasi cha zaidi ya milioni 120 lakini endapo wangewapa wakandarasi fedha ambazo zingetumika zingekuwa ni nyingi zaidi,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa watu wanaojitolea wanaisadia serikali kwa kuiunga mkono kwa mambo mambo ya kimaendeleo inayoyafanya hali ambayo inapunguza gharama na fedha hizo zinazookolewa zinatumika kwenye mipango mingine.
“Kwa kuwa ujenzi unaendelea tunawaomba wadau mbalimbali waendelee kujitokeza kusaidia ujenzi huo ili ukamilike mapema na wanafunzi waweze kuishi kwenye mazingira mazuri na mnachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kufanya upembuzi kujua mahitaji ya vitu vinavyotakiwa ili kukamilisha zoezi hili,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mkuranga Gilbert Sanga alisema kuwa anawashukuru wadau mbalimbali ambao wamejitolea kujenga mabweni hayo na kufikia hatua hiyo.
Sanga alisema kuwa Waziri wa elimu Profesa Joyce Ndalichako alitoa kiasi cha shilingi milioni 250 ambazo zianaendelea kutumika katika ujenzi wa mabweni hayo hadi sasa   
Alisema kuwa kazi ya kupanua ilianza kwa wananchi kuchangia zaidi ya milioni nne na kuwataka wanaochangisha wawasilishe fedha walizochangisha ili zifanye kazi husika
“Halmashauri walisema wametenga fedha kiasi cha shilingi milioni 32 kwa bweni moja wanafunzi 48 tu tuliungana na kamati ya ulinzi na usalama nao walikubali kuongeza mabweni zaidi na mkoa nao ukakubali na kambi ya wazalendo ambao walipiga kambi na walifyetua tofali 45,000 na ni kazi ambayo haina bajeti,” alisema Sanga.
Kwa upande wake msimamizi wa ujenzi toka kikosi cha Ruvu JKT Mohamed Boko alimwomba mkuu wa mkoa wa Pwani kufanya jitihada ili ujenzi huo uweze kukamilika ambapo kazi hiyo ilipangwa kufanyika kwa miezi miwili lakini imekuwa kubwa na muda kuongezeka.
Mwis