Na John Gagarini, Kibaha
KAMATI za Ulinzi na Usalama mkoani Pwani zimetakiwa kujipanga vizuri ili kukabiliana na matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi na kuua askari.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, wakati wa kuwakaribisha wakuu wa wilaya wapya walioteuliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.
Ndikilo alisema kuwa kumetokea matukio mawili ya uvamizi wa vituo vya Polisi vya Kimanzichana wilayani Mkuranga na Ikwiriri wilayani Rufiji ambapo katika matukio hayo askari waliuwawa na wavamizi hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
“Wametupiga mara mbili hatutakubali kupigwa tena hivyo kamati za ulinzi na usalama kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ngazi ya wilaya mnapaswa kuweka mikakati ya kukabilina na uvamizi huo ambao unatishia usalama wa raia,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema msingi mkuu wa nchi yetu ni amani hivyo hatutakubali vitendo hivi viendelee tena kwenye mkoa wa Pwani na wakuu wa wilaya wanapaswa kuhakikisha amani inakuwepo na kuwadhibiti hao wanaofanya hivyo.
“Nisingependa jambo hilo lijirudie tena kwani watu wanaofanya vitendo hivyo wanavuruga amani ya nchi iliyopo na silaha wanazopora zinaweza kutumiwa kwenye uhalifu hivyo kuwanyima amani wananchi,” alisema Ndikilo.
Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani alisema kuwa matukio ya uhalifu iwe ajenda ya kudumu kwenye vikao mbalimbali vya maendeleo ili kufanikisha kutokomeza uhalifu wa aina hiyo ambao umezidi kushika kasi kwenye nchi.
Wakuu wa wilaya waliokaribishwa na wilaya zao ni Majid Mwanga Bagamoyo, Abdala Kihato Mkuranga, Subira Mgalu Kisarawe na Dk Hassan Mohamed Mafia.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wa mkoa wa Pwani wametakiwa kubadili tabia ili kukabiliana na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi ambapo yako juu kwa asilimia 5.6 zaidi ya kiwango cha Taifa cha asilimia 5.2.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Pwani mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa maambukiziu yako juu sana.
Ndikilo alisema kuwa wananchi kwa kushirikiana na wataalamu wa mkoa wanapaswa kuweka mikakati mizuri kwa pamoja kuweka kupunguza maambukizi mapya.
“Hali ni mbaya sana kwani endapo kasi hii endapo itaongezeka itasababisha madhara makubwa sana kwani nguvu kazi kubwa itapotea na familia hazitakuwa na muda wa kuzalisha na kubaki kuuguza wagonjwa hivyo kushindwa kufanya shughuli za maendeleo,” alisema Ndikilo.
Aidha alitoa mfano kwa mwezi Desemba mwaka jana watu waliopima virusi vya ugonjwa wa Ukimwi walikuwa 69,197 waliokutwa na maambukizi walikuwa watu 7,800 sawa na asilimia 7.8.
“Takwimu hizi na wastani wa maambukizi ni mbaya kwani inaleta picha mbaya kuwa watu hawabadili mienenendo yao licha ya kupatiwa elimu mbalimbali ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi,” alisema Ndikililo.
Alikitaka kitengo cha mapambano dhidi ya ugonjwa huo kiendelee kutoa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa huo ambao unaua watu wengi na watu wafuate maagizo ya wataalamu wa afya ili kujiepusha.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAKUU wa wilaya Mkoani Pwani wametakiwa kuachana na urasimu bali waweke mazingira mazuri kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye mkoa huo kwani kwa sasa una fursa nyingi.
Akizungumza na viongozi wa mkoa huo wakiwemo wakuu wa wilaya mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa endapo watakuwa na urasimu watawakimbiza wawekezaji.
Ndikilo alisema kuwa Pwani ina fursa nyingi za kiuewekezaji baada ya Jiji la Dr es Salaam kujaa hivyo wawekezaji kuangalia maeneo ya pembezoni mwa Jiji hilo kw alengo la kuwekeza.
“Wakuu wa wilaya lazima muweke mazingira rahisi kwa wawekezaji na siyo kuwa vikwazo kinachotakiwa ni wawekezaji hao kufuata sheria za uwekezaji zilizowekwa na nchi yetu,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa njia rahisi ni kupima maeneo hayo haraka na kuyatenga kwa ajili ya uwekezaji ili kupunguza malalamiko toka kwa wananchi kuwa maeneo yao yamechukuliwa na wawekezaji pia jengeni miundombinu ya barabara, umeme na maji kwenye maeneo hayo.
“Mkoa unapokuwa na maeneo mengi ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na viwanda vinasaidia kuongeza ajira kukuza uchumi wa mtu mmoja, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla,” alisema Ndikilo.
Alibainisha kuwa mkoa wa Pwani una fursa kubwa kutokana na kuwa na miundombinu mizuri ya usafirishaji ikiwemo kwa njia za meli, ndege, treni na barabara.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAKULIMA wa zao la Korosho mkoani Pwani wametakiwa kuacha kuuza korosho yao ikiwa shambani kwa walanguizi ili kulipandisha thamani zao hilo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Tanzania Jasson Kalile wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU).
Kalile alisema kuwa wakulima wengi wa zao la korosho wamekuwa wakiuza korosho yao ikiwa shambani kwa bei ndogo hivyo kushindw akunufaika na kilimo cha zao hilo.
“Tatizo kubwa lililopo kwa wanachama wengi wa CORECU ni kuuza korosho zikiwa bado ziko shambani ambapo huuza kwa bei ndogo huku walangizi hao wakija kuuza kwa bei kubwa,” alisema Kalile.
Aidha alisema kuwa walanguzi hutumia matatizo ya wakulima hivyo kuwarubuni kwa kuwapa fedha kwa korosho zilizo shambani na zinapofikia hatua ya kuuzwa siyo mali ya mkulima.
“Inapofuikia hauta ya kuuza walanguzi hao huuza kwa bei nzuri wanayoitaka huku mkulima akibaki hana kitu na kubaki na shida zake,” alisema kalile.
Kwa upande wake Mwenyekiti aliyemaliza muda wake alisema kuwa Juma Abeid alisema kuwa kazi kubwa waliyoifanya ni kukiresjesha chama hicho kwenye hadhi yake baada ya kutokea migogoro kwa muda mrefu.
Abeid alisema kwa sasa hali ni nzuri na tayari wameweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya ushirika ili wakulima waweze kukopeshwa kwa riba ndogo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mkuranga
KATIKA kukabiliana na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani inatarajia kukamilisha miradi mitatu mikubwa ya maji yenye thamani ya shilingi milioni 874 mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha baraza la Madiwani wa Halamshauri ya wilaya ya Mkuranga mhandisi wa maji wa wilaya Renard Baseli alisema miradi hiyo iko kwenye hatua za mwisho.
Baseli alisema kuwa miradi mingi inakumbwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha ambazo huichelewa kufika na hazifiki kwa wakati hali inayopelekea miradi mingi kushindwa kukamilika kwa wakati.
“Miradi hii mikubwa mitatu itasaidia kwa kiais kikubwa kukabiliana na ukosefu wa maji kwa wananchi wa wilaya ya Mkuranga na kilio hicho kitapata jibu kwani miradi hiyo ni ya thamani kubwa,” alisema Baseli.
Aliitija miradi hiyo kuwa ni ule wa Mvuleni Kilimahewa Kusini wenye thamani ya shilingi milioni 545, Kilamba wenye thamani ya shilingi milioni 285 na Nyamato wenye thamani ya shilingi milioni 44.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Lukanga Said Kubenea alisema kuwa miradi mingi ya maji imekuwa ikiahidiwa kukamilika lakini inachukua muda mrefu kukamilika huku wananchi wakiendelea kupata taabu.
Kubenea alisema kuwa ucheleweshaji wa miradi ya maji imekuwa kero kubwa kwa wananchivyo kuwataka watendaji wa idara ya maji kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mkuranga
WAKUU wa Idara mbalimbali wilayani Mkuranga mkoani Pwani wametakiwa kuwalipa kwa wakati watumishi wa ngazi za chini ili kuleta ufanisi wa kazi.
Hayo yalisemwa Mkuranga na Mkuu mpya wa wilaya ya Mkuranga Abdala Kihato wakati wa makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Mercy Silla na kusema kuwa hakuna kitu kinamkera kama malimbikizo kwa watumishi.
Kihato alisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakuu wa idara kujilipa posho mbalimbali na kuwaacha watumishi wa ngazi za chini wakidai mishahara ya kila mwezi na kuwaambia fedha iliyoletwa haitoshi.
“Hakuna kitu nisichokipenda kama watumishi kudai kwani serikali huwa inajitahidi kuleta mishahara lakini inapokuja wakubwa wanajipendelea kwa kujilipa malipo mengine na kuwaacha watumishi wa ngazi za chini wakiwa na malalamiko,” alisema Kihato.
Aidha alisema kila mtu ana haki ya kulipwa stahiki yake bila ya kujali ngazi ya kazi kwani wote ni watumishi na hakuna sababu ya kubaguana.
“Ni vema mkagawana kilicholetwa siyo vizuri wengine wapate na wengine wakose wote wana haki sawa kulipwa kwa mujibu wa sheria na si wakubwa kujipendelea kwani kufanya hivyo ni kushusha morali ya kazi,” alisema Kihato.
Kwa upande wake Silla alisema kuwa anawashukuru watumishi wa wilaya hiyo kwa kumpa ushirikiano wa hali ya juu katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Silla alisema kuwa moja ya changamoto zilizopo kwenye wilaya hiyo ni elimu ambapo bado kiwango cha ufaulu kiko chini sana.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mkuranga
BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wameitaka halmashauri hiyo kununua greda kwa ajili ya kujengea barabara ili kukabiliana na changamoto ya miundombinu hiyo kutokamilika kwa wakati.
Madiwani hao walitoa ushauri huo kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Mkuranga na kusema kuwa upatikanaji wa greda kutasaidia kupunguza gharama za ujenzi wa barabara.
Moja ya madiwani hao Karu Kavina Diwani wa kata ya Kiparanganda alisema kuwa barabara nyingi hazikamiliki kwa muda uliopangwa kwa sababu gharama ya kukodisha greda ni kubwa.
“Halmashauri yetu ingekuwa na greda ingekuwa ni rahisi kwani gharama zingekuwa ndogo ambapo wananachi wangechangia fedha kidogo kwa kushirikiana na halmashauri yao,” alisema Kavina.
Kavina alisema kuwa karibu kila diwani ambaye ni mwakilishi wa wananchi analalamika barabara za eneo lake kutokwisha hivyo suluhisho ni kununua greda la Halmashauri.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Vianzi Hamis Kitwana alisema kuwa kumekuwa na mvutano mkubwa wa kila diwani kutaka fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hivyo njia rahisi ni kununua greda.
Kitwana alisema kuwa hata kama Halmashauri haina fedha ikope kwa ajili ya kununulia kama baadhi ya Halmashauri nyingine zinavyofanya vinginevyo hali ya barabara itakuwa ni changamoto kubwa.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ana Mwakalelya alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ya kunua greda ni ukosefu wa fedha lakini akasema hilo ni wazo ambalo watalifanyia kazi.
Mwisho.