Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI WA Kitongoji cha Mpiji
wilayani Kibaha mkoani Pwani wameuomba uongozi wa Wakala wa Misitu (TFS) Kanda
ya Mashariki kuwaruhusu kupita kwenye eneo la msituo huo ili waweze kupata
huduma ya maji ya kisima.
Akizungumza kwenye mkutano
ulioandaliwa na Mradi wa Mama Misitu moja ya wananchi wa Kitongoji hicho Bw
Shaban Nyoka alisema kuwa wamekuwa wakichapwa bakora na walinzi wa msitu huo
mara wanedapo kuchota maji.
Bw Nyoka alisema kuwa kutokana na
ukosefu wa maji kwenye Kitongoji hicho huwapasa kwenda kuchota maji kwenye
visima vilivyopo kwenye hifadhi ya msitu huo.
“Tumekuwa tukichapwa bakora mara tunapokwenda kuchota maji
kwenye visima hivyo vya maji lakini cha kushangaza mifugo ya moja ya wawekezaji
kijijini hapo imekuwa haichukuliwi hatua yoyote, tunaomba waturuhusu tuwe
tunachota maji huko,” alisema Bw Nyoka.
Alisema kuwa watu wamekuwa wakienda kuchota maji huko lakini
wanapokutwa huko na walinzi wa msitu wamekuwa wakiadhibiwa kama vile wahalifu
jambo limekuwa likiwafadhaisha.
“Sisi tunaomba hifadhi ituruhusu tuchote maji kwani
hatufanyi uharibifu wowote kwani lengo letu ni kwa ajili ya kupata maji tu na
si kingine hivyo ni vema wanegeturuhusu tupite huko kwa ajili ya kupata maji tu
na si vingenevyo,” alisema Bw Nyoka.
Kwa upande wake mratibu wa mradi huo Bw Yahaya Mtonda
alisema kuwa tatizo kubwa linatokana na uharibifu ambao umekuwa ukifanywa ndani
ya msitu ambapo sheria hairuhusu kufanyika kwa shghuli yoyote.
Bw Mtonda alisema kuwa mipaka iliyowekwa imevikuta visima
hivyo vikiwa ndani ya hifadhi hiyo hivyo kama wanataka kutumia visima hivyo ni
vema wakaandika barua kwa meneja ili waweze kuruhusiwa kuchota maji kwenye
msitu huo.
“Kama mnataka kufanya hivyo ni vema mkaandika barua rasmi
kwenye wakala wa misitu wao ndiyo wenye uwezo wa kuruhusu nyie kupata huduma
hiyo ya maji lakini lengo si kuwasumbua wananchi,” alisema Bw Mtonda.
Aliwataka wananchi kutumi kamati za misitu kudhibiti
waharibifu wa misitu kwani uharibifu umekuwa mkubwa hali ambayo ina hatarisha
misitu hiyo ya hifadhi ambayo ni chanzo kikuu cha utunzaji wa mazingira.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment