Na John Gagarini, Kibaha
WATU sita wamepoteza maisha katika matukio
tofauti yaliyotokea Mkoani Pwani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishna
Msiadizi Juma Yusufu Ally alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kueleza
kuwa katika tukio la kwanza Bw Ramadhani Lubaya (35) mkulima na mkazi wa kijiji
cha Kondo aliuwawa na watu wasiofahamika wakati akichunga mifugo ipatayo 90
porini ikiwa ni mchnganyiko wa ng’ombe na mbuzi mali ya Bw Malick Seif.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 9:00
alasiri Novemba 28 mwaka huu katika Kijiji cha Kondo kata ya Zinga Wilaya
ya Bagamoyo kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kwenye paji la uso.
Bw Ally alisema kuwa katika tukio la pili
huko kijiji cha Gwata Kata ya Mzenga Tarafa ya Mzenga Wilaya ya Kisarawe mfanya
biashara Bw Peter Gumbi (28) mkazi wa Ngerengere Mkoa wa Morogoro aliuwawa kwa
kupigwa risasi na watu wasiofahamika kisha kuporwa Tsh. 1,300,000/= alizokuwa
nazo kwa ajili ya kwenda kununulia ng’ombe majira ya saa 8:00 mchana Novemba tarehe
mwaka huu.
Alisema kuwa marehemu alikutwa na mauti
wakati akitoka kijiji cha Gwata kwenda Dololo kwenye mnada akiwa amepakiwa
kwenye Pikipiki. Dereva wa pikipiki hiyo anshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa
ajili ya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Aidha katika tukio la tatu alisema mkazi
wa Kitongoji cha Madafu Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga Bw Hamadi Juma (46)
fundi ujenzi aliuwawa na wananchi waliojichukulia sheria mikononi baada ya
kumtuhumu kupora pikipiki ambayo mmiliki wake bado kufahamika majira ya saa
3:30 usiku Novemba 28
“Marehemu alifikwa na mauti baada ya
kushambuliwa kwa mawe na vigongo sehemu mbalimbali za mwili, kutokana na tukio
hilo Jeshi la Polisi linaendesha msako mkali ili kuweza kuwabaini wale
waliohusika katika tukio hilo kwa kisingizio cha hasira kali,” alisema Kamanda
Ally.
Alibainisha kuwa katika tukio lingine,
mnamo Novemba 30 mwaka huu majira ya saa 08:30 usiku huko Kijiji cha Msata Kata
ya Msata Wilaya ya Bagamoyo Bw Ally Abdallah Mlenga (56) mkulima na ambaye pia
anajishughulisha na kazi za uganga wa kienyeji alivamiwa nyumbani kwake na watu
nane ambao walimshambulia kwa mapanga na kumuua na kisha kumjeruhi mtoto wake
aitwaye Bw Abdallah Ally (25) kwa kumkata mapanga kichwani na kifuani.
“Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi
walivamia nyumba hiyo na kuvunja mlango kwa kutumia kitu kizito na baada ya
kutenda kosa hilo hawakuchukua kitu chochote,” alisema Kamanda Ally.
Aidha katika tukio linguine Bw Hassan
Hamadi mkazi wa Kijiji cha Mbebetini Kata ya Kibiti Wilaya ya Rufiji (25)
aliuwawa na watu waliojichukulia sheria mkononi katika tukio lilitokea majira
ya Desmba 1 mwaka huu majira ya saa 7:45 usiku baada ya kumtuhumu kuvunja duka
la Bw Selapia Stephen (47).
Kamanda Ally, alithibitisha kupoteza
maisha kwa Omary Milondomo (17) mkazi wa Kinguila baada ya kugongwa na gari
katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Kilwa majira ya saa 2:30 usiku wa Novemba
30 mwaka huu huko katika Kijiji cha
Mbembetini Kata ya Kibiti Wilaya ya Rufiji.
Alibainisha kuwa marehemu alifikwa na
mauti baada ya kugongwa na gari ambayo haikufahamika namba ambayo haikusimama
baada ya kutenda kosa hilo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Rufiji ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa daktari.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment