Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa watu milioni moja na nusu hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani zinazotokea hapa nchini.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini Mohamed Mpinga, wakati wa maadhimisho ya siku ya kukumbuka watu waliokumbwa na majanga ya ajali za barabarani.
Kamanda Mpinga alisema kuwa mbali ya vifo hivyo pia jail hizo zinasababisha majeruhi zaidi ya 20,000 hadi 50,000 huku wengine wakipata ulemavu wa kudumu.
“Ajali ni moja ya vyanzo vya vifo vya watu wengi hapa nchini ambapo zinashika nafasi ya nane kwa kusababisha vifo na ifikapo mwaka 2020 kitakuwa ni chanzo cha tano kwa vifo,” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema kuwa hadi mwezi Oktoba mwaka huu jumla ya ajali zaidi ya 19,000 zimetokea na kusababisha vifo zaidi ya 3,000 ukiachilia jail za hivi karibuni iliyoua watu saba mkoani Morogoro na iliyotokea mkoani Dodoma na kuua watu watatu.
“Watu wanaokufa ni nguvu kazi ya Taifa ambapo wengi wao ni vijana wenye umri kati ya miaka (18) hadi (35) hivyo Taifa kupoteza nguvu kazi kubwa ambayo ndiyo inayozalisha mali na kukuza uchumi wa nchi,” alisema Kamanda Mpinga.
Aidha alisema kuwa jeshi la polisi litaendelea kuchukua hatua kali kwa madereva wazembe ambao wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ajili za barabarani na kuwataka abiria kutoa taarifa kwa madereva wanaoendesha mabasi kwa mwendo wa kasi.
Kwa upande wake mtendaji wa shirika la Global Helmet Vaccine Initiative Bw Alpherio Nchimbi alisema kuwa lengo la maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka ni kuwakumbuka wahanga wote waliopata matatizo kutokana na ajali za barabarani duniani.
Alisema kuwa moja ya wahanga wa ajali ni wanafunzi ambao wamekuwa wakigongwa mara wanapokuwa wakivuka kwenda ama kurudi shuleni.
“Tunawashauri madereva na wale wanaotumia vyombo vya moto kuachana na tabia ya kutumia vilevi ambavyo vimeonekana kuwa ni chanzo kikuu cha ajali za barabarani,” alisema Nchimbi.
Mwisho.