Saturday, July 27, 2024

RIZIWANI KIKWETE NDANI YA BARAZA LA MADIWANI UCHAGUZI MAKAMU MWENYEKITI HALMASHAURI YA CHALINZE

Nimeshiriki kikao cha Baraza la Madiwani Cha Chama Cha Mapinduzi kuchagua diwani atakayegombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze kilichofanyika Chalinze ,mapema leo.#KaziInaendelea

TAKUKURU DODOMA YATOA ELIMU KUELEKEA UCHAGUZI WA MITAA MWAKA HUU

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Dodoma imeendelea kutoa elimu kwa Umma kupitia makundi mbalimbali kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini unaotarajia kufanyika mwaka huu.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Dodoma Euginius Hazinamwisho amesema kuwa viongozi wa Kisiasa nchini Tanzania hupatikana kupitia uchaguzi unaofanyika kila baada ya miaka mitano kwa namna mbili uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na uchaguzi wa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Mwaka 2024 utafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2025 utafanyika uchaguzi wa Serikali kuu,"amesema.

Aidha amesema kuwa kuwepo kwa vitendo vya Rushwa wakati wa kuchagua viongozi huwanyima haki wagombea na kuwakosesha maendeleo wananchi 

"Jitihada za Serikali kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki kwa wananchi wameweza kutunga Sheria mbalimbali zinazodhibiti vitendo vya Rushwa,"amesema 

"TAKUKURU kwa kuzingatia kifungu cha 4 kifungu kidogo cha 2 na kifungu cha 7(d) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa vina wajibu wa kuwahakikishia wadau kuweka mikakati dhidi ya Rushwa wakati wa uchaguzi.

Hata hivyo amesema kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake TAKUKURU mwaka 2014 na mwaka 2019 ilifanya uchambuzi wa ufuatiliaji wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2020 ilifanya uchambuzi wa mfumo kwa uendeshaji wa uchaguzii mkuu wa Serikali wa Rais, Wabunge na Madiwani katika majimbo yote ya Uchaguzi Tanzania bara.

"Katika chaguzi zote yalikuwepo malalamiko ya vitendo vya Rushwa,katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2014/2019 vitendo vya Rushwa vilijitokeza kama ifuatavyo kulikuwa na ugawaji wa fedha, ugawaji wa vitu, kama kanga,fulana,vinywaji na vyakula na ahadi za ajira,"amesema

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Mzee Kasuwi amesema kuwa athari za biashara ya Dawa za Kulevya kwenye uchaguzi wa Kisiasa zinaweza kuwa na madhara makubwa na kuathiri mchakato wa Kidemokrasia na utulivu wa jamii.

Aidha biashara na matumizi ya Dawa za Kulevya ni tatizo linaloathiri nchi nyingi dunia.

"Dawa za Kulevya zina athari Kiuchumi,kiafya, kijamii, Kisiasa, kidiplomasia, Kimazingira na usalama,"amesema

PWANI YAPATIWA WAUGUZI 120




MKOA wa Pwani umepatiwa jumla ya Wauguzi 120 ikiwa ni asilimia 50 ya watumishi walioletwa mkoani humo pia umepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 25 kuboresha huduma za afya.

Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Katibu Tawala Mipango na Uratibu wa Mkoa wa Pwani Edina Kataraiya ambaye alimwakilisha Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel wakati wa Maadhimisho siku ya Uuguzi Duniani kwa Mkoa wa Pwani.

Kataraiya amesema kuwa serikali imeendelea kutatua changamoto mbalimbali za huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuongeza wahudumu wa afya ili kuboresha utoaji huduma.

"Kada ya uuguzi ni uti wa mgongo wa huduma za afya ndiyo sababu serikali inaboresha kwani bila ya wauguzi hakuna huduma hizo hivyo toeni huduma kama kiapo chenu kinavyosema upendo, utu na uadilifu,"amesema Kataraiya.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Steven Brown amesema kuwa katika Muundo wa Utumishi wa Kada ya Uuguzi na Ukunga ambacho kinamtaka Ofisa Muuguzi kabla hajafikia Kiwango cha mwisho cha Mshahara wake yaani (TGHSG) awe na Masters ambacho ni kikwazo kwa wauguzi.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Kusirye Ukio amesema kuwa huduma wanayotoa wauguzi ni ibada na Hospitali ni madhabahu hivyo waendelee kudumisha ibada zao.

Thursday, July 25, 2024

MFUMO WA KUSAJILI MIGOGORO CMA UTAEPUSHA MALALAMIKO YA UCHELEWESHWAJI HAKI - MHE. MAGANGA









Na Wellu Mtaki, Dodoma 

Katibu Mkuu, Ofisini ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Mary Maganga amesema mfumo mpya wa kusajili migogoro ya kikazi kwa njia ya mtandao utaepusha malalamiko na ucheleweshwaji wa haki kwa Wananchi ikiwa ni Pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji wa Tume.

Mhe. Maganga ameyasema hayo leo,Julai 24,2024 Jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo maalum ya mfumo wa kusajili migogoro ya kikazi unaofahamika kama ‘Online Case Management’ kwa watumishi wa CMA kutoka Ofisi mbalimbali za  mikoa Tanzania.

Vilevile Mhe. Maganga ameongeza kuwa,matumizi ya mifumo yanaongeza ufanisi wa utendaji kwa namna mbalimbali na pia uwezo wa kutumika katika mazingira mbalimbali bila kuhitaji kwenda katika ofisi husika  kupata huduma.

"Mara nyingi tukiwa tunataka kuongeza ufanisi pa kwenda ni kwenye mifumo kwasababu mifumo unaweza kuitumia popote pale ulipo na bila kuhitaji kwenda kwa uhalisia kwahiyo tuna imani kubwa itaenda kuongeza ufanisi wa Tume yetu", amesema Mhe. Maganga.

Aidha Mhe. maganga amewataka watumishi kuendelea kusimamia haki katika ajira na kazi kwa kuhakikisha wanatatua migogoro kwa njia ya usuluhishi kwani ndio wajimu wao kwa Tume.

Vilevile ameipoingeza Tume kwa kuendelea kusuluhisha migogoro ya kikazi hadi kufikia asilimia 76% ikiwa  ni hatua nzuri kulingana na mpango mpango wa kuhakikisha wanafikia asilimia 81% kwa njia ya Usuluhishina hivyo kuonekana katika hatua inayoridhisha. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Mhe. Usekelege Mpulla amesema mfumo huu unatarajiwa  kutumika kutekeleza lengo la Tume ikiwa ni kuwafikia wadau mbalimbali kwa urahisi  popote walipo.

"Kwa msingi huo tunatarajia kupitia mfumo huu tuweze kuwafikia wadau wetu na kusajili migogoro kwa kutumia, simu janja ili nasi tuweze kuishughulikia kwa haraka maana hili ni takwa na ombi la muda mrefu la wadau wetu hasa wawekezaji kutaka huduma za Tume ziende kwa haraka", ameongeza mkurugenzi. 

Naye Afisa Mfawidhi kutoka Ofisi ya CMA Arusha, Hermenegilda Stanslaus alisema mfumo huo utawasaidia watumishi wa Tume katika kutekeleza majukumu na kurahisisha utendaji kazi bila kuwalazimu wateja na wadau mbalimbali kufika ofisi za Tume.

WANAOZUSHA UZUSHI WATOTO KUTEKWA KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

KUFUATIA watu wanne kukamatwa kwa tuhuma za kuzusha uzushi kuwa kuna gari aina ya Noah linateka watoto mkoa huo umetoa onyo kwa watu wanaoleta taharuki hizo kuwa hawatavumiliwa.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa kuadhimisha Kumbukumbu ya Mashujaa kimkoa alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo.

Kunenge alisema kuwa baadhi ya watu ambao hawana uzalendo wamekuwa wakizua taharuki na kuwafanya watu washindwe kufanya shughuli zao wakihofia watoto wao kutekwa.

"Suala la utekaji watoto baadhi ya watu wanapotosha na kuketa hofu pamoja na kuzua taharuki na tunatoa onyo kwa wale wanaosababisha hali hiyo hatutasita kuwachukulia hatua kali za kisheria,"alisema Kunenge.

Alisema kuwa wananchi wakabiliane na vitendo vya ukatili, mauaji ya watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ualbino, unyanyasaji kwa kutoa taarifa juu ya vitendo hivyo au viashiria.

"Tayari tunawashikilia watu wanne kwa kutoa taarifa za uongo juu ya madai kuwa kuna watoto wametekwa wakati wakijua siyo jambo la kweli hatutasita kuchukua hatua za kisheria kwa watu wa namna hiyo,"alisema Kunenge.

Aidha alisema watu wasishabikie vitendo hivyo kwani wanazua taharuki na mtu kama jambo huna uhakika nalo usisambaze kwani ikiwa ni uongo unaleta uchochezi.

"Jukumu la usalama ni la kila mwananchi tumieni polisi kata, polisi jamii, kamati za usalama za vijiji na jeshi la akiba na sisi tumejipanga yaani ukirekodi uongo tutakukamata kwani hutaweza kujificha,"alisema Kunenge.

Aliongeza kuwa watu wanaoleta mambo hayo siyo wazalendo wa nchi yao kwani matukio ya utekaji baadhi wanayapotosha.

RAIS SAMIA SHUJAA TRENI YA MWENDOKASI (SGR)

RAIS Dk Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuzindua treni ya mwendokasi ya (SGR) kwenda Dodoma kuwa ni tukio la kishujaa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa nchini.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa kuadhimisha Kumbukumbu ya Mashujaa kimkoa alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo.

Kunenge alisema kuwa uzinduzi huo ni jambo kubwa ambalo limeweka historia kubwa ya nchini ambapo baadhi wapinga uchumi walijaribu kuhujumu miradi mikubwa ya kitaifa lakini walishindwa.

"Wakati tukiendelea kuwakumbuka na kuwaombea mashujaa wetu tumwombee Rais kwani uzinduzi wa safari hiyo ni tukio la kishujaa na miradi mingine mikubwa ukiwemo ule wa uzalishaji umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere,"alisema Kunenge.

Alisema kuwaenzi mashujaa ambao baadhi yao wamefariki dunia na wengine wakiwa hai walifanya jambo la kishujaa la kuipigania nchi na sasa tunaishi kwa amani na upendo.

"Tuendelee kuiombea nchi yetu na Rais na viongozi wengine ili tuendelee kuienzi amani na upendo uliopo nchini udumu na tusiwape nafasi wale wanaotaka kuivuruga amani yetu iliyopo,"alisema Kunenge.

Aidha alisema anampongeza Rais kwa kuitendea haki nchi kwani atazindua mnara mkubwa wa Kumbukumbu ya Mashujaa Mnara mrefu huko Dodoma na Afrika utakuwa ni wanne.

Kwa upande wake Mchungaji Julius Shemkai alisema kuwa mashujaa hao lazima wapongezwe kwani walipambania nchi na wale wote wenye nia mbaya wasindwe ili nchi iendelee kuwa na amani.

Shemkai alisema kuwa wao viongozi wa dini wanakemea tabia iliyozuka ya kuiba watoto kwani hiyo roho haina nafasi hapa nchini.

Sheikh Said Chega alisema kuwa wanamwombea Rais ili aweze kuongoza kwa amani na kutekeleza vyema majukumu yake na nchi iendelee kubaki salama.

Chega alisema kuwa wanawaombea wale wote walioipambania nchi hadi hapa ilipofikia ikiwa na amani.

Siku ya mashujaa huadhimishwa kila mwaka Julai 25 ambapo Kitaifa inaadhimishwa Mkoani Dodoma na mgeni rasmi ni Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Mwisho.


Tuesday, July 23, 2024

MKUU WA MKOA PWANI AKABIDHI WAKUU WA WILAYA MAGARI




MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amekabidhi magari mawili kwa wakuu wa Wilaya za Kisarawe na Bagamoyo kwa ajili ya urahisishaji utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Wakuu waliokabidhiwa magari hayo aina ya Toyota yaliyotolewa na Serikali ni Petro Magoti wa Wilaya ya Kisarawe na Halima Okashi wa Wilaya ya Bagamoyo.

Kunenge alikabidhi magari hayo Mjini Kibaha mbele ya wakuu wengine wa Wilaya za Mkoa huo alisema yatawasaidia kufanya kazi zao kwa uharaka katika kuwatumikia wananchi.

Alisema kuwa mkoa una wilaya saba ambapo gari moja litakuja na manne yatakuja kwa bajeti ya mwaka huu ambapo hata wao wamepata magari kuhudumia wananchi.

"Kupata magari haya yatasaidia kuwafikia wananchi kwa urahisi kwani upatikanaji wa magari hayo ni sehemu ya kurahisisha njia ya kuwafikia wananchi,"alisema Kunenge.

Aidha alisema kuwa wanampongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa magari hayo ili kuwarahisishia usafiri kwenda kuwatumikia wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Okashi alisema kuwa magari hayo yatawasaidia kuketa ufanisi watayatunza ili waweze kuwafikia wananchi kwa urahisi na kwa wakati ili watatue changamoto zinazo wakabili.

Alisema kuwa magari hayo watayatunza kwani ni kwa ajili ya kuhudumia wananchi na wanaipongeza serikali kwa kuwapatia magari hayo.

Kwa upande wake Magoti alisema kuwa usafiri huo utawasaidia kuwafikia wananchi waliomoko hata maeoneo yaliyoko mbali watayafikia kwa urahisi na kutoa huduma bora. 

Magoti alisema kuwa sasa hatarudi nyumbani kwani atahakikisha anawafikia wananchi na kuwasikiliza wananchi maeneo mbalimbali.