TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kurejesha kiasi cha shilingi milioni nne za Kijiji cha Kanga zilifanyiwa ubadhirifu na kaimu mtendaji wa Kata ya Kanga wilayani Mafia.
Tuesday, October 31, 2023
TAKUKURU PWANI YAFANIKISHA MTENDAJI KUREJESHA MILIONI 4 ZA KIJIJI ALIZOZICHUKUA ZA MAUZO YA ARDHI
Wednesday, October 25, 2023
RC KUNENGE ATAKA UJENZI WA MALL YA HALMASHAURI YA MJI UKAMILIKE NDANI YA SIKU 14
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa siku 14 kwa Mkandarasi anayejenga Maduka Makubwa (Mall) inayomilikiwa na Halmashauri ya Mji Kibaha kukamilisha ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni nane.
Ameyasema hayo wakati wa ziara yake kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri hiyo ambapo mradi huo uko kwenye kitovu cha mji karibu na stendi mpya ya Maili Moja Kibaha.
Kunenge amesema kuwa mradi huo ni mkubwa ambao utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni nane hivyo lazima ukamilike ndani ya muda huo ambapo matarajio ni kuingiza kiasi cha shilingi milioni 450 kwa mwaka.
"Nataka mkandarasi Elray asizidishe zaidi ya wiki mbili ahakikishe anakamilisha ndani ya muda huo tunachotaka akamilishe mradi huu ili biashara zianze kufanyika na Halmashauri ianze kupata mapato,"amesema Kunenge.
Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Brighton Kisheo amesema kuwa Halmashauri hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni nane mwaka 2018-2019 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambapo wafanyabiashara 253 watapata fursa za biashara na litahudumia watu zaidi 2,000 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.
Naye mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Pwani Filemon Maliga amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia eneo jirani na Mall hiyo ili wafanye biashara zao na wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kulirasimisha kundi lao ambapo sasa wanatambulika na wanapata fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo.
Miradi mingine aliyoitembelea mkuu huyo wa mkoa ni barabara, ujenzi wa madarasa ya sekondari kata ya Mkuza na maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha utengenezaji wa mitungi ya gesi ya kampuni ya Taifa Gas.
Mwisho.
Wednesday, October 18, 2023
SOKO LA KISASA KUJENGWA MLANDIZI BILIONI 7 KUTUMIKA
KATIKA kuhakikisha Mji wa Mlandizi unavutia Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha inatarajia kujenga soko kubwa na la kisasa kwa ajili ya wakazi wa mji wa Mlandizi ambalo litagharimu kiasi cha shilingi bilioni saba.
Hayo yamesemwa Mlandizi na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo wakati wa kuhitimisha kampeni ya Simika Bendera kwenye Jimbo hilo.
Mwakamo alisema kuwa eneo maarufu kama kwa Mama Salmini tayari limeshapatikana baada ya kununuliwa na mkandarasi wa ujenzi amepatikana na utaratibu unaanza kwa ajili ya ujenzi.
"Soko la sasa ni dogo lakini eneo tulilopata ni kubwa na litachukua wafanyabiashara wengi na litakuwa na huduma nyingi tofauti na la sasa ambalo hata sehemu ya magari kupaki hakuna,"amesema Mwakamo.
Amesema fedha hizo zimetengwa kwenye baheti ya mwaka wa fedha 2023/2024 na tayari bilioni mbili zimetolewa kwa ajili ya kuanza kazi na litaubadilisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini Mkali Kanusu alisema kuwa chama kinataka viongozi waliopo kwenye madarakani wawe na mahusiano mazuri na wananchi.
Kwa upande wake katibu wa CCM Kibaha Vijijini Zainabu Mketo amesema kuwa hamasa ya Simika Bendera imeleta mafanikio kwani wamevuna wanachama wapya 3,500 na kupitia mabalozi wote lengo likiwa ni kuimarisha chama ndani ya chama.
Mwisho.
Sunday, October 15, 2023
MAOFISA TEHAMA WATAKIWA KUENDANA NA TEKNOLOJIA
MAOFISA TEHAMA nchini, wameaswa kwenda na wakati ,kupenda kujifunza kulingana na teknolojia inavyobadilika ili kujiongezea uzoefu na ujuzi.
Aidha wawe wabunifu ,wajitume ili kuacha alama na tija katika kada hiyo kwenye maeneo ya kazi
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala mkoa wa Pwani Rashid Mchatta, wakati alipomwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, kufungua kikao kazi cha mwaka 2023 ,ambacho kimefanyika Kibaha Mkoani Pwani na kukutanisha maofisa hao kutoka mikoa mbalimbali nchini ili kujadili changamoto zinazokikabili kitengo Cha TEHAMA.
"IT ina mambo mengi sana, inabadilika kama mtu wa Tehama hufanyi updating itakupa wakati mgumu, someni masomo ya ziada kuongeza uzoefu,mkoa wa Pwani ndio mwenyeji mwaka huu tumejipanga kuhakikisha tuliyoyajadili yanafanikiwa"anasema Mchatta.
Mchatta alieleza, kada ya TEHAMA imekua kwa kasi kubwa na kupelekea kuwa mhimili mkubwa katika utendaji kazi na Serikali na Taasisi nyingine binafsi kwenye mifumo mbalimbali ikiwemo ukusanyaji mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za mitaa ,mfumo wa kusimamia huduma za hospitali.
"Serikali - TAMISEMI imeipa kada hii umuhimu mkubwa kwa kuanzisha wizara rasmi inayoshughulikia TEHAMA ,hivyo tusimuangushe mh Rais"
Awali Melchiory Baltazary, Mkurugenzi Msaidizi-TEHAMA TAMISEMI alieleza kikao hicho ni kikao kazi ambacho kitafanyika siku mbili.
Mwisho
Saturday, October 14, 2023
LIONS CLUB YATOA MISAADA YA VIFAA VYA SHULE
WATAKA JITIHADA ZIONGEZWE WATU KUKUA KUSOMA KUHESABU NA KUANDIKA
IMEELEZWA kuwa watu wanaojua kusoma kuandika na kuhesabu nchini kwa sasa ni asilimia 77.8 ikilinganishwa na mwaka 1980 ambapo watu hao ilikuwa ni asilimia 9.6.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Profesa Michael Ng'umbi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Nchini wakati wa ufunguzi wa Kongamano la maadhimisho ya kitaifa ya juma la elimu ya watu wazima kitaifa.
Ng'umbi alisema kuwa mwaka 1980 Tanzania iliweza kufikia kiwango cha juu cha kufuta ujinga kwa watu wasiojua kuandika kuhesabu na kusoma na kufikia asilimia hiyo.
Akifungua mafunzo hayo kaimu mkurugenzi elimu msingi wizara ya elimu sayansi na teknolojia Josephat Luoga alisema kuwa mafunzo hayo yatawezesha kuamsha hamasa ya kutafakuri kuwa tunakwenda wapi katika utoaji elimu.
Luoga alisema kuwa mfumo wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi utaweza kubadilisha mtizamo juu ya uendeshaji na usimamizi na tathmini ili kuendana na dira ya maendeleo ya 2025 pamoja na mpango wa maendeleo endelevu 2030.
PROFESA MKENDA AFURAHISHWA TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA INAVYOBORESHA MFUMO HUO
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha elimu ya watu wazima nchini.
Mkenda aliyasema hayo wakati wa kufunga Kongamano la maadhimisho ya kitaifa ya juma la elimu ya watu wazima kitaifa lililofanyika Wilayani Kibaha.
Alisema kuwa serikali itaendelea kujenga uwezo na watendaji kwenye Halmashauri kwenye mikoa zitoe kipaumbele kwa program zote za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Charles Msonde alisema kuwa moja ya mkazo uliowekwa ni kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza wanajua kusoma kuandika na kuhesabu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa Caroline Nombo alisema kuwa jumla ya wanafunzi milioni 5.7 walidahiliwa kwenye elimu changamani kwenye vituo 405.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa baadhi ya program ni pamoja na walimu wa kujitolea kutokuwa na mafunzo ufinyu wa bajeti, upungufu wa vitendea kazi na kushindwa kulipa wa wezeshaji.
Mwisho.