MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okashi amewataka wananchi kuwafichua watu wanaohujumu miradi ya maji ambayo serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya upatikanaji maji kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Ameyasema hayo Wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akifungua mkutano na wadau wa maji kwenye wilaya hiyo ambayo inaundwa na Halmashauri mbili za Bagamoyo na Chalinze.
Okashi amesema kuwa serikali imetoa fedha hizo kwa lengo la kuhakikisha miradi inatekelezwa ili huduma ya maji safi na salama inapatikana kwa wananchi vijijini kwa umbali usiozidi mita 400.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo James Kionaumela amesema kuwa Wilaya ina vyanzo vikuu viwili vya maji ambavyo ni chini ya ardhi kupitia visima vya kuchimba virefu na vifupi kukiwa na visima 215.
Kionaumela amesema kuwa chanzo cha pili ni maji ya juu inayojumuisha maji ya mito, mabwawa na chemichemi na wilaya hiyo ina vyombo vya watoa huduma 17 ambapo imevipunguza na kufikia vyombo vitano.
Naye mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo Abdul Sharifu amesema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya uboreshaji upatikanaji huduma ya maji.
Diwani wa Kata ya Kibindu na makam mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Ramadhan Mkufya amesema kuwa Vijiji viwili vya Kwa Msanja na Kwa Konje ndiko kuna changamoto ya maji.
Mwentekiti wa vyombo vya watumiaji maji Wilaya ya Bagamoyo Jitihada Mwinyimkuu ameiomba serikali kuvihudumia vyombo hivyo kwani vingine vinashindwa kufanya kazi kutokana na vifaa kufa na kushindwa kuvikarabati.
Mwisho.