Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya watu nane wamepoteza maisha katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoani Pwani likiwemo la madereva bodaboda wa tano kupoteza maisha kwa kugongana na gari la mizigo aina ya Scania uso kwa uso.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa polisi mkoani Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Pwani Ulrich Matei alisema kuwa matukio hayo yalitokea Novemba 21 mwaka huu majira ya saa 2: usiku.
Kamanda Matei alisema kuwa kwenye tukio la kwanza waendesha pikipiki (bodaboda) walipoteza maisha baada ya kugonga uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T.602 ACT katika kichwa na tela lenye namba T.493 ABP aina ya Scania likiendeshwa na Bw Dastan Migunda (35), mkazi wa Kitunda Dar es Salaam majira ya saa 2.00 usiku huko eneo la Ruvu Darajani kata ya Vigwaza barabara ya Dar es Salaam – Morogoro Wilaya ya Bagamoyo.
“Waliopoteza maisha katika tukio hilo ni, Bw Saidi Dosa (17), Bw Severine Luoga (19), Bw Philemon Job (20), Bw Nassoro Mzalamila (18) na Bw Sadam Mapunda (21) huku majeruhi wa ajali hiyo ni Bw Peter Maswaga (25) wote hawa ni wakazi wa Picha ya Ndege Wilaya ya Kibaha,” alisema Kamanda Matei.
.
Alisema kuwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni mwendo kasi wa waendesha pikipiki watatu pikipiki zao zenye namba T.164 CHF, T.953 CQB na T.426 CJZ zote zikiwa ni aina ya Sanlg ambapo walikuwa wanatokea Picha ya Ndege kwenda Kijiji cha Buyuni kumfuatilia Bw Ramadhani Rajabu (16) dereva wa bodaboda kwa Mathias aliyetuhumiwa kwa wizi wa Pikipiki yenye namba.T.216 CNC aina ya Sanlg.
“Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha ikisubiri kufanyiwa uchunguzi wa Daktari na Majeruhi anaendelea na matibabu Hospitali ya Tumbi Kibaha,” alisema Matei.
Katika tukio la Pili, Kamanda Matei alithibitisha watu watatu kupoteza maisha huko Kitongoji cha Kibong’wa Kijiji cha Kisarawe Kata ya Kisarawe Tarafa ya Sungwi Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani majira ya saa 8.50 mchana.
Alisema kuwa watu hao walifikwa na mauti wakati walikuwa wanachimba kokoto kwenye shimo ambao ni Bi Mwazani Salehe (18), Ally Twaha (2), pamoja na Hasnatha Semin mwenye miezi (5) wote wakazi wa Kibong’wa.
Kamanda Matei aliongeza kuwa watu hao walifariki dunia baada ya kuangukiwa na udongo ulioporomoka na kuwafukia wote kwenye machimbo ya kokoto wakiwa wamejipumzisha chini ya shimo.
Aidha alisema tukio hilo mtu mmoja alinusurika kifo ambaye ni Bi Amina Emil (28), mkulima mkazi wa Kibong’wa ambaye alijeruhiwa na amelazwa Hospitali ya Wilaya Kisarawe akiendelea na matibabu, miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa nduguzao kwa mazishi.
Mwisho.