WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyang'hwale Mkoani Geita wametaka ujenzi wa ofisi ya chama ufanyike kwani tayari baadhi ya wadau wamechangia fedha za ujenzi huo.
Wamesema moja ya wadau waliochangia fedha kwa ajili ya ujenzi huo ni Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko ambaye alichangia kiasi cha shilingi milioni 50.
Wamesema kuwa fedha hizo zilikabidhiwa kwa Mbunge wa Jimbo la Nyang'hwale Hussein Amar hivyo kutaka fedha hizo zifanye ujenzi huo ili kupata ofisi kwa kazi za chama.
"Tunataka ujenzi ufanyike kwani kama ni fedha zipo hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi huo wa ofisi ya chama ambapo endapo itajengwa itakuwa ya kisasa,"wamesema wanachama hao.
Waliongeza kuwa wanataka fedha hizo zijenge na kukamilisha ofisi ya chama na kwamba wao wanachotaka ni kuona CCM Wilaya ya Nyang'hwale inaendelea kama Wilaya nyingine zilivyoendelea.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyang'hwale Hussein Amar akizungumza kwa njia ya simu ameeleza kusitikishwa na malalamiko ya wananchama hao huku akisema jambo hilo halina usiri wowote.
Amar amesema kuwa yeye ndiye iliyemuomba awasaidie na sio mara moja amekuwa akisaidia na bahati nzuri alipokuja yeye mwenyewe alimkumbushia ombi hilo na akakubali kusaidia lakini hakutamka kiwango.
Aidha amesema kuwa fedha hizo zilivyoingia alimpa taarifa Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Chama, Mwenezi, kamati ya Siasa na kamati ya ujenzi na yeye ndiye aliyetafuta fundi na kuwashauri kuwa kuna fundi kwa hiyo ni vyema akatumika kwakuwa yupo vizuri.
Mbunge huyo ameongeza kuwa yeye binafsi amekuwa na mchango mkubwa sana katika ujenzi wa ofisi hiyo ya Chama maana alishawai kutoa mashine zake na magari yake (Tipa) kufanyakazi katika ujenzi huo.
"Fedha zipo mikono salama na Mei 3 niliongea na Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi kumweleza juu ya fedha kwani zinatakiwa kufanyakazi iliyokusudiwa kwa kuwa mimi sitaki kukaa nazo nipeni akaunti niwahamishie lakini alinijibu kuwa watakaa na kamati yake ya ujenzi na akasema wakati huu aendelee kukaa nazo na wakihitaji kununua vifaa watamjulisha ili atoe hizo fedha",amesema Amar.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyang'hwale Adam Mtore amesema kuwa kama kuna malalamiko ndani ya Chama kuuna utaratibu wake na mara nyingi huanzia ngazi ya chini ya tawi lakini kwakuwa suala hilo linagusa ngazi ya Wilaya ilitakiwa wapeleke malalamiko yao kwa Katibu wa Chama Wilaya.