Wednesday, March 5, 2025

WATAALAMU UDSM WAKUTANA NA VIONGOZI TBN

Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamekutana na baadhi ya viongozi na wajumbe wa Tanzania Bloggers Network (TBN) kwa mahojiano maalum yenye lengo chanya la kukusanya maoni yao ili kuimarisha masuala ya blogging, nchini.

Hatua hiyo ya kukusanya maoni imekuja kufuatia wataalamu hao kuagizwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ipo katika utafiti maalum kwa nia ya dhati kuboresha Sera na kanuni zake mbalimbali katika eneo hilo la majukwaa ya mtandaoni.

Kikao hicho kimefanyika kwa mafanikio katika ofisi za TBN zilizopo kwa Aziz Ali, Temeke, watafiti hao wamechukua maoni ya TBN Makao Makuu, wakisema pia watafika katika Ofisi za Kanda za TBN.

Akizungumza Katibu Mkuu wa TBN Khadija Kalili amesema TCRA imefanya uamuzi sahihi kukutana na wadau wake kwa kupitia wataalamu hao kwani maoni yao yatawapa picha halisi juu ya tasnia ya habari na blogging kwa ujumla wake.

Amesema kilio kikubwa cha wana TBN ni gharama za usajili na tozo ya leseni kiasi ni kikubwa ambacho kwa uhalisia wengi bado hawamudu kulipia.

Amesema hali hiyo imefanya idadi kubwa ya wana TBN kushindwa kumudu kuendesha mitandao yao kutoka 300+ waliokuwapo kwanza hadi kufikia 100+ tu wanaoweza kulipia na kwa kusuasua.

Ameshauri pia TCRA kuendeleza utamaduni wa kukutana na wadau wake ikiwamo kwa mafunzo ya kuwaimarisha uwezo wao pamoja na kuangazia athari za gharama za bando za mtandao na vifaa.

Amesema ikiwa sekta ya blogging ndani ya tasnia ya habari ikisimamiwa vizuri kwa ushirikiano wa karibu na TCRA ni wazi kwamba Tanzania itanufaika na maudhui bora na yenye viwango ambayo yatasaidia kulinda maadili ya jamii yetu.

TBN yenye wanachama 300 waliopo wanaendesha mitandao kwa kusuasua kutokana na ada na tozo.

Watalaam hao walionesha kushangazwa na kuwapo kwa Chama Cha Bloggers chenye usajili kamili na wanachama zaidi ya 300, na pia wakaelewa bloggers ni tofauti na jumuiya zingine za waandishi wa mitandao ambao hawana blogs.

Wataalamu hao ni pamoja na Prof. Siasa Mzenzi, Dkt. Patrokil Kanje , Dkt. Said Suluo.

Wengine ni Mjata Daffa , Ally Mshana na Viongozi na wajumbe wa TBN, wakiongozwa na Katibu Mtendaji Khadija Kalili , Beda Msimbe na Rahel Pallangyo.



Mwisho

DOWEI CARE YATOA MSAADA WA FEDHA UJENZI WA DARAJA LULANZI

KIWANDA cha Dowei Care cha Kibaha Mkoani Pwani kimetoa fedha kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa daraja la Mtaa wa Lulanzi-Matunda ili kuboresha barabara ya mtaa huo.

Akikabidhi fedha hizo kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bob Chaing amesema kuwa wameamua kutoa fedha hizo ili kukabili changamoto za jamii.

Amesema kuwa Kiwanda chao kimekuwa kikitoa misaada mbalimbali kwenye jamii ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii kama sehemu ya huduma za jamii ambapo fedha hizo ni zaidi ya asilimia 60 ya fedha za mradi huo.

"Tunashirikiana na jamii kwenye masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja elimu, afya, barabara na masuala yanayohusu jamii,"amesema Chaing.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole amesema kuwa wanakishukuru kiwanda hicho kwa msaada walioutoa utasaidia sana ujenzi wa daraja hilo.

Shilole amesema wananchi wamekuwa wakijitolea fedha kwa ajili ya ujenzi huo hivyo hiyo itakuwa imewaongezea nguvu kwenye kuanza ujenzi wa daraja ili kupunguza changamoto kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo.

Amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kuchangia ujenzi huo ili upunguze changamoto kwa watu wakiwemo wanafunzi wakati wakienda na kurudi shule.


Monday, March 3, 2025

VYAMA SITA RAFIKI KUSINI MWA AFRIKA VISIYUMBISHWE VISIMAMIE SHABAHA YA KUWALETEA WANANCHI MAENDELEO

VYAMA vya Ukombozi Kusini mwa Afrika vimetakiwa vibadili mbinu za kuongoza na visikubali kuyumbishwa na mabadiliko ya dunia na kuacha shabaha ya kuziongoza nchi zao.

Hayo yalisemwa jana kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Mjini Kibaha na Makamu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Steven Wassira wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa vyama hivyo.

Wassira alisema kuwa baadhi ya nchi duniani havipendi kuona vyama hivyo vinaongoza wao wanaona demokrasia ni kuviondoa vyama hivyo madarakani.

"Mabadikiko ni mengi duniani lakini yasivitoe vyama vyetu kwenye shabaha yake ya msingi ambayo ni maisha bora na mazuri kwa wananchi huu ndiyo msingi wa vyama hivi,"alisema Wassira.

Alisema kuwa hiyo ndiyo misingi iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo ambayo yalipigania Uhuru wa nchi zao na kuacha misingi imara ambayo inapaswa kufuatwa.

Kwa upande wake Katibu wa masuala ya siasa uhusiano wa kimataifa na Halmashauri Kuu ya CCM NEC Rabia Hamidu alisema kuwa nchi hizo zinapaswa kuonyesha umoja wao ili kuzisaidia nchi za Afrika.

Naye Naibu Mkurugenzi wa idara ya masuala ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na idara ya kimataifa ya kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na mkuu wa ujumbe wa IDPC Zhang Yanhong alisema kuwa ni jambo zuri kwa ushirikiano wa vyama hivyo sita na CPC.

Naye Mkuu wa Shule ya Mwalimu Julius Nyerere Profesa Marcelina Chijoriga alisema wanatoa mafunzo kwa viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za umma na serikali pamoja na taasisi za watu binafsi.

SERA YA TAIFA YA MAENDELEO YA VIJANA 2007 YAENDELEA KUNADIWA

Leo tarehe 3.3.2025 Ndugu Omary Abdul Punzi Mwanadiplomasia na Mratibu wa Makongamano ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana Mwaka 2007 toleo la Mwaka 2024 katika kamati ya Vijana Wazalendo waliopewa kibali Maalumu na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu 

Kwa ajili ya Kuinadi na kuineza Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 

Amemtembelea Mheshiwimiwa Godfrey Eliakimu Mzanva Mkuu wa Wilaya ya Moshi kwa ajili ya kumpongeza kwa Kuaminiwa na Mheshiwimiwa Dk Samia Suluhu Hasani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya.

Unakumbuka kuwa Mheshiwimiwa Godfrey Eliakimu Mzanva ni miongoni mwa wakimbiza mwenge mwaka 2024 waliofanya vizuri katika kuendesha Makongamano ya vijana.

Aidha mazungumzo hayo yalitoa mwafaka wa Kuandaa Kongamano la Vijana Kuhusu Umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Ambalo litajikita zaidi kuelezea historia ya Tanzania, Itifaki, Maadili na Uzalendo kwa Vijana,Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya, utunzaji wa Mazingira na Fursa zinatopatikana Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro

Friday, February 28, 2025

CCM KATA YA MKUZA YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 9.4

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya  ya Mkuza Wilayani Kibaha kimefanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4 na kurudhishwa na kiwango cha utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza baada ya kukamilisha ziara ya Halmashauri ya Kuu ya Kata kutembelea miradi hiyo Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkuza Matata Ngolo amesema kuwa huo ni utekelezaji wa ilani ya CCM.

Ngolo amesema kuwa kabla ya kikao waliona ni vema wakatembelea miradi hiyo ya maendeleo ili kujionea uhalisia wa utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Mkuza Fokas Bundala amesema  kuwa moja ya mafanikio makubwa ni ujenzi wa shule za sekondari mbili ambapo kiutaratibu kila kata inapaswa kujenga sekondari moja.

Bundala amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni madawati na viti na meza lakini kwenye bajeti inayokuja fedha zimetengwa hivyo itapunguza changamoto hiyo.

Amesema kuwa katika kipindi hicho serikali kupitia mapato yake ya asilimia 10 ilitoa kiasi cha shilingi milioni 660 kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa vikundi.

MWENGE WA UHURU KITAIFA KUWASHWA PWANI APRILI 2,2025

WANANCHI wa Mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia fursa za kiuchumi kwa kuwashwa mwenge wa uhuru mkoani humo Aprili 2 mwaka huu.

Hayo yamesemwa jana Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema kuwa kuwashwa mwenge wa uhuru Mkoani Pwani ni fursa kiuchumi kwa wananchi pia ni chachu ya maendeleo kwani wananchi watafanya biashara za chakula, malazi, usafiri, vinywaji na utalii.

"Wananchi tumieni fursa hiyo ya uzinduzi wa mbio hizo za mwenge wa uhuru kwa kufanyabiashara ambapo kutakuwa na wageni wengi na hata wenyeji ambao watahitaji huduma mbalimbali,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa sherehe hizo za uzinduzi zitapambwa na matukio mengi yakiwemo ya halaiki na burudani nyingine za wasanii.

"Baada ya uzinduzi huo mwenge wa uhuru utakimbizwa katika Halmashauri tisa za mkoa huo ambapo utakagua, kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo,"amesema Kunenge.

Aidha amewahamasisha na kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Pwani na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo.

"Maandalizi yanaendelea vizuri ambapo muda bado unatosha na mwaka huu tumejipanga vyema kuhakikisha tunafanya vizuri,"amesema Kunenge.

mwisho. 


Monday, February 24, 2025

SHULE ZA AWALI NA MSINGI BINAFSI 101 ZANUFAIKA NA MRADI WA OPPORTUNITY INTERNATIONAL-MOSHA

Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam, Eva Mosha, ametoa rai kwa wamiliki na walimu wa shule binafsi za awali na msingi kuimarisha ufanisi wa ufundishaji na kuboresha ubora wa elimu, ili kuinua taaluma katika shule zao.

Amesisitiza ,shule hizo zinapaswa kuongeza ubunifu na kujiendeleza kwa kupata mafunzo mbalimbali ya namna ya kuendesha shule zao, ili kuepuka changamoto za kushindwa kuendeleza shule au kukosa wanafunzi.

Mosha alitoa rai hiyo katika hafla ya kupongeza walimu na wamiliki wa shule binafsi za awali na msingi, ambazo zinatoa ada nafuu, waliopatiwa mafunzo ndani ya miaka mitatu kupitia mradi wa Opportunity International ,kwenye ukumbi wa Victoria uliopo Kimara Temboni, Dar es Salaam. 

Mratibu wa Mradi wa Opportunity International Tanzania (HES Tanzania), Oliver Kapaya, alieleza kuwa mradi huo ulianza mwaka 2018 na umefanikiwa kuhusisha shule 101 katika kipindi cha miaka mitatu.

Alieleza, shule 74 zilipata mafunzo na kufuzu kwa kipindi cha miaka minne na shule 15 zimefanikiwa kupata tuzo za kutambua ufanisi wao huku, shule nane zimetunukiwa tuzo kwa utendaji bora.

Violet Oketch, mratibu wa Mradi wa Opportunity International Afrika (HES Africa), alieleza mradi huu unatekelezwa katika nchi nane za Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Rwanda, Zambia, Ghana, DRC Congo, Uganda, Kenya, na Nigeria.

Violet Oketch alishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ushirikiano wake na wawekezaji na wafadhili mbalimbali katika sekta ya elimu. 

Brayson Ephata Maleko, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu Temeke, alisema mradi huo umehusisha shule za awali na msingi, namna ya kuendesha shule kwa ufanisi, kupanga mipango, na kusimamia rasilimali fedha.