CHAMA Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) kimesema kitahakikisha kila Wilaya inakuwa na kituo cha kuandaa vijana ili kuzalisha wachezaji watakaokuja kulitumikia Taifa.
Aidha amesema kwa sasa kuna vituo vinne lakini lengo ni kuwa na vituo saba na baadaye kuwe na vituo kila Halmashauri za mkoa huo ambazo ziko 9.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Mwenyekiti wa Corefa Robert Munis amesema kuwa kwa sasa changamoto za viwanja hazipo kwani viwanja vipo vingi.
Munis amesema kuwa kwa sasa wanahamasisha wazazi kuhakikisha wanawawezesha watoto wao ili washiriki kwenye soka ili vijana wa Mkoa huo waweze kutumia vipaji vyao kujiletea maendeleo
"Tunawapongeza wenzetu Chalinze wameanza ligi ya vijana chini ya miaka 15 haya ndiyo tunayoyataka kwani Pwani lazima Mpira Uchezwe ndiyo kauli mbiu yetu,"amesema Munis.
Amesema kuwa mpira ni ajira lakini ili kufikia lengo hilo lazima ushiriki wa wazazi nao uwepo kwa kuwawekea mazingira ili waweze kucheza na wasiwazuie watoto kucheza.
"Tumeanza mpango wa kusajili shule za soka Academy na kuzitambua ili tushirikiane nao ili malengo yetu yatimie kama viwanja vipo kwa nini vijana wasicheze tuhakikishe vijana wetu wanacheza mpira kwani wataliwakilisha vyema Taifa,"amesema Munis.
Ametaja baadhi ya viwanja vilivyopo ndani ya Mkoa wa Pwani kuwa ni Mwanambaya, Bungu, Mabatini, Tumbi, Mwanakalenge, Kiromo, Msoga, Maili Moja Mwendapole, Kwambonde na vingine vingi ambavyo baadhi vinatumika na vingine viko kwenye ujenzi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya mipango na fedha Mohamed Lacha amesema wanawashukuru wadau mbalimbali ambao wamefanikisha kupata ofisi ya kisasa.
Lacha amesema kuwa jambo kubwa ni kuhakikisha Corefa inasonga mbele kwa kushirikiana na kuepukana na migogoro ambayo huwa inarudisha nyuma masuala ya soka.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Soka la Wanawake Mkoa wa Pwani Asha Mbata amesema kuwa wanafarijika kwani kwa mwaka jana Wilaya zote zikichezesha ligi ya wanawake isipokuwa Mafia pekee ambapo ni mafanikio makubwa sana.
Mbata amesema kuwa wanaandaa ziara ya kutembelea Wilaya ili kuhamasisha wanawake na kucheza soka na Wilaya kuandaa ligi kwa wanawake.