Saturday, August 23, 2014

WAETHIOPIA 48 WASHIKILIWA KWA KUINGIA NCHINI KINYEMELA

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia raia 48 wa nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini Kibaha Kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa watuhumiwa hao walitelekezwa vichakani.

Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 21 mwaka huu majira ya saa 7 usiku katika Kijiji cha Visakazi Ubena Zomozi tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Alisema kuwa Wethiopia hao waligunduliwa na askari Magereza wa Gereza la Ubena aitwaye Sospeter ambaye aliwakuta porini alipokuwa akifanya shughuli zake na kutoa taarifa polisi.

"Kati yao 11 wanaumwa na wamepelekwa kituo cha afya cha Chalinze kwa ajili ya matibabu baada ya kuonekana wakitapika baada ya kupewa chakula na walionekana wakiwa na hali mbaya ya kiafya huku wale wengine wakiwa wamehifadhiwa kwenye kituo cha polisi cha kiwilaya," alisema Kamanda Mwambalaswa.

Aidha alisema kuwa raia hao wa Ethiopia wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 40 na wanatarajiwa kukabidhiwa idara ya Uhamiaji kwa ajili ya taratibu zingine ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazowakabili.

Wakati huo huo mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya (25) na (28) amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamaba ya katani.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 22 mwaka huu majira ya saa 2 usiku Kijiji cha Kibiki kata ya Bwiringu Tarafa ya Chalinze.

"Mfanyakazi wa shambani wa mwenyekiti wa Kijiji hicho alimpa taarifa bosi wake aitwaye Ally Hussein (47) kuwa kuna mtu kajinyonga kwenye banda lake ambaye naye alitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo," alisema kamanada Mwambalaswa.

Aliongeza kuwa marehemu aliacha ujumbe amabo uliandikwa kwenye karatasi kuwa anawaachia dunia ili waishi miaka 120, hakuna mtu aliyekamatwa na polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

mwisho.  

Thursday, August 21, 2014

UTINGO AFA AJALINI OFISA WA OFISI YA DCI ANUSURIKA AJALINI

Na John Gagarini, Kibaha
UTINGO wa lori la mizigo Adam Rashid (28) mkazi wa Bwiringu kata ya Pera wilaya ya Bagamoyo amekufa baada ya lori alilokuwa akisafiria kugongana na lori lingine
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa malori hayo yaligongana uso kwa uso.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 19 mwaka huu majira ya saa 10 jioni eneo la Sweet Corner.
“Marehemu alikuwa kwenye gari namba T 650 BED aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa na na Ramadhan Mwarami (40) mkazi wa Bwiringu likiwa limebeba simenti likitokea Jijini Dar es Salaam kwenda Chalinze,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alisema kuwa lori alilokuwa amepanda marehemu liligongana na lori lenye namba za usajili T 853 APA aina ya Fuso ambalo lilikuwa likitokea mkoani Mbeya kwenda Dar es Salaam likiwa limebeba Mahindi likiendeshwa na Shan Iddi (28) mkazi wa Mwanga liligongana na lori hilo na kusababisha kifo hicho.
Aidha alisema kuwa dereva wa lori alilokuwa amepanda marehemu aliumia kidogo ambapo marehemu alifariki dunia wakati akipata matibabu kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani ya Tumbi.
Wakati huo huo Ofisa Mwandamizi wa jeshi hilo anayeshughulikia majalada ya kesi katika ofisi ya mkurugenzi wa makosa ya jinai  (DCI) Ilembo amenusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kugonga mti.
Akifafanua kuhusiana na tukio hilo Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa ofisa huyo alikuwa akitokea mkoani Iringa kikazi.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 20 mwaka huu majira ya saa 9 alfajiri eneo la Vigwaza kata ya Pera wilayani Bagamoyo.
“Chanzo cha ajali hiyo ni gari hilo la polisi kutaka kugongana uso kwa uso na gari lingine baada ya kulipita gari lililokuwa mbele yao na alipotokeza akakutana na hilo gari hali iliyofanya dereva akwepe kisha kuserereka kwenye mtaro na baadaye kugonga mti,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa gari hilo lilipasuka matairi na vioo vilivunjika ambapo gari lililohusika na tukio hilo halikuweza kusimama mara baada ya tukio hilo

Mwisho.

Thursday, August 14, 2014

johngagariniblog: KAMATI ZA MADIWANI SARAKASI TUPU NA DIWANI CHADEMA...

johngagariniblog: KAMATI ZA MADIWANI SARAKASI TUPU NA DIWANI CHADEMA...:  Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo kilichofanyika leo mjini Kibaha  Na...

DEREVA TEXI ALIYEPOTEA SIKU 8 AKUTWA AMEKUFA

Na John Gagarini, Kibaha
BAADA ya dereva wa Texi Richard Ponera (36) mkazi wa Mwendapole wilayani Kibaha mkoani Pwani kupotea kwa siku nane amepatikana akiwa ameuwawa  na kuporwa gari alilokuwa akiliendesha.
Marehemu ambaye alikuwa akifanyia shughuli zake kwenye kituo kikuu cha Mabasi cha Maili Moja wilayani humo alipotea Agosti 6 Mwaka huu majira ya saa 1 usiku alipokodishwa na watu wawili wasio fahamika waliojifanya kuwa ni wateja.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo Mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa mwili wake ulitupwa vichakani.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa huko eneo la Mihande Mashambani Mlandizi wilayani Kibaha ukiwa umeharibika vibaya huku gari  alilokuwa akiendesha lenye namba za usajili T 905 BHT aina ya Corolla nyeupe.
“Chanzo cha mauaji hayo ni katika kuwania mali ambayo ni gari hilo ambalo halijapatikana na hakuna mtu ambaye amekamatwa hadi sasa na bado uchunguzi unaendelea kuwatafuta watu waliohusika na tukio hilo,” alisema Mwambalaswa.
Alisema kuwa jeshi hilo linaendelea kufuatilia juu ya tukio hilo na halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria watu waliohusika na tukio hilo la kusikitisha, marehemu alizikwa juzi na ameacha watoto wawili ambao ni Ruben (14) anayesoma kidato cha kwanza St Anne na Kontrada anayesoma darasa la sita shule ya Msingi Jitegemee Jijini Dar es Salaam.

Mwisho. 

Sunday, August 10, 2014

johngagariniblog: DEREVA TEXI APOTEA MAZINGIRA YA KUTATANISHA ALIKOD...

johngagariniblog: DEREVA TEXI APOTEA MAZINGIRA YA KUTATANISHA ALIKOD...: Na John Gagarini, Kibaha DEREVA wa Texi wa Maili Moja Richard Ponera (36) mkazi wa Mwendapole wilayani Kibaha mkoani Pwani amepotea k...

POLISI YAKANUSHA MTU KUCHUNWA NGOZI PWANI


JESHI la Polisi mkoani Pwani limekanusha uvumi ulioenea na kudai kuwa mkazi wa Kijiji cha Dondo wilaya ya Mkuranga Hamis Mahimbwa (20) kuwa amekufa kwa kuchunwa ngozi mwili mzima ila ni kutokana na kuungua na moto.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini Kibaha kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa amesema kuwa hakuna tukio kama hilo mkoani hapo.
Akifafanua juu ya tukio la mtu huyo kufa amesema kuwa mnamo Agosti 6 mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku huko katika kijiji cha Dondo Tutani kata ya Kisiju wilayani humo Hamis Mahimbwa (27) alikutwa na wananchi akiwa ameungua moto mwili mzima.
Kamanda Mwambalaswa amesema marehemu alipiga kelele kuomba msaada baada ya kuungua na moto na kumchukua na kumpeleka hospitali kwenye kituo cha afya cha Kalole Kisiju na kuanza kupatiwa matibabu lakini kutokana na kuungua sana na moto alifariki dunia Agosti 7 mwaka huu majira ya saa 11:00 alfajiri.
Amesema kuwa baada ya kifo hicho ilipelekwa taarifa kwenye kituo cha polisi cha Mkuranga na jalada la uchunguzi MKU/IR/1202/2014 lilifunguliwa ili kubaini kifo chake.
Amebainisha kuwa baada ya kufunguliwa jalada hilo Ofisa Mpelelezi Mkuu wa Polisi wa makosa ya Jinai wa wilaya akiwa na timu ya askari wa upelelezi waliungana na maofisa wa usalama waliungana na Daktari wa wilaya ya Mkuranga Kibela kwenda kwenye eneo la tukio na kituo cha afya cha Kisiju kwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
Aidha amesema kuwa daktari alichukua sampuli ya ngozi ambapo kwenye eneo la tukio ilikutwa suruali, majivu ya tisheti aliyokuwa amevaa, kandambili, kibiriti, chupa ya plastiki ya soda ambayo ilikuwa na mafuta ya petroli na katika eneo hilo hakukuwa na purukushani ya watu wengi ambapo mashahidi waliokwenda kumsaidia alipopiga kelele walimkuta marehemu akiwa anongea na kudai kuwa ameungua kwa moto bila ya kusema aliye muunguza.
Kaimu kamanda wa polisi huyo wa mkoa wa Pwani amesema baba mlezi wa marehemu Athuman Mahimbwa alipohojiwa alisema kuwa mwanae alikuwa akiugua ugonjwa wa Kifafa kwa miaka 17 na alimwambia kuwa anakufa kwa kuungua na moto na kutokana na uchunguzi uliofanywa na polisi pamoja na daktari umebainisha kuwa kifo chake kimesababishwa na moto na si kuchunwa ngozi.