Friday, July 4, 2014

AOMBA MSAADA WA MATIBABU



Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
 MSICHANA Selitian Nata (25) mkazi wa Kijiji cha Kisogo kata ya Vigwaza Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani yuko kwenye hali mbaya ya kiafya baada ya kuvimba mguu na kuwa kwenye maumivu makali.
Ugonjwa huo uvimbe huo ulianza kama kipele kidogo miaka zaidi ya 10  iliyopita lakini kadiri siku zilivyokuwa zikienda ndipo uvimbe huo ulizidi kuongezeka na kufikia usawa wa mbavu.
Akizungumza na waandishiw ahabari ambao walimtembelea nyumbani kwao alisema kuwa uvimbe huo una ambatana na maumivu makali pamoja na homa kali hasa nyakati za usiku.
“Niko kwenye wakati mgumu kama mnavyoniona napata shida naomba nisaidiwe kwani nimekwenda hospitali toka kipindi hicho lakini sikupata matibabu zaidi ya kupewa vidonge tu ambavyo hupunguza maumivu lakini uvimbe uko pale pale,” alisema Nata.
Nata ambaye ana mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka (2) alisema kuwa wakati tatizo hilo linaanza alikwenda hospitali mbalimbali lakini hakuweza kupatiwa matibabu sahihi na kupelekea uvimbe huo kuongezeka hadi hapo ulipofikia na kumkosesha raha.
“Naomba wataalamu mbalimbali pamoja na wafadhili ili niweze kupata matibabu sahihi ambayo yataondoa uvimbe huu ili name niweze kuishi kwa raha kama wengine,” alisema Nata.
Kwa upande wa baba yake Nata Mumbi alisema kuwa alimpeleka mwanae kwenye hospitali mbalimbali kwa ajili ya matibabu lakini hakuna mafanikio yoyote.
“Tatizo matibabu ambayo wanayompa si ya kina jambo ambalo linasababisha mwanangu asipate nafuu, lakini kupitia vyombo vya habari naomba wasamaria wema wamsaidie mwanangu ili aweze kupata matibabu sahihi,” alisema Mumbi.
Aidha alisema kuwa anashangaa kuona kila anapokwenda hospitali mwanae anapewa vidonge tu jambo ambalo linafanya wakate tamaa ya kumpatia matibabu.
Mwisho.

CHANGAMOTO VITAMBULISHO VYA TAIFA



Na John Gagarini, Kibaha
HUKU zoezi  la usajili na utambuzi wa watu Mkoani Pwani ili kupata vitambulisho vya utaifa likiendelea kumejitokeza changamoto kutokana na Ofisi za Serikali za Mitaa kuwatoza wananchi shilingi 1,000 kwa ajili ya kupata barua za uthibitisho wa ukaazi.
Baadhi ya wakazi wa Mitaa ya Kata ya Maili Moja Wilayani Kibaha wamelalamika kutozwa kiasi hicho cha fedha jambo ambalo walisema kuwa huenda ikasababisha watu wengi kushindwa kujiandikisha hali itakayosababisha wakose vitambulisho vya utaifa.
Moja ya wakazi wa mtaa wa Tangini Juma Shamte alisema kuwa taratibu haziruhusu barua hizo kutozwa fedha bali zinatolewa bure hivyo kutoza malipo ni kinyume cha utaratibu.
“Baadhi ya watu hawana vithibitisho vyovyote ambapo taratibu zinawataka endapo hawana uthibitisho wawe na barua ya utambulisho toka kwenye Mtaa anaoishi,” alisema Shamte.
Aidha alisema kuwa wao walitangaziwa kuwa zoezi hilo ni bure na hakuna malipo yoyote lakini wanashangaa kutozwa fedha hizo na kuwapa mzigo michango kupata huduma ambazo hutolewa bure.
“Fedha hizo ni mzigo kwani mbali ya kutoa fedha hizo wanatakiwa kulipa shilingi 3,000 kwa ajili ya kupiga picha za paspoti saizi ambazo wanapiga sehemu mbalimbali si kwenye ofisi hizo za Mitaa kwa ajili ya kuwekwa kwenye barua hizo za utambulisho,” alisema Shamte.
Mkazi huyo alisema kuwa huwabidi kuwa na kiasi cha shilingi 4,000 ambapo 1,000 ya barua ya uthibitisho toka kwenye Mtaa na 3,000 kwa ajili ya picha ili waweze kujiandikisha kupata vitambulisho hivyo vya utaifa ambavyo ni muhimu kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuomba mikopo.
Akizungumzia kuhusiana na changamoto hiyo Diwani wa Kata ya Maili Moja Andrew Lugano alisema kuwa kutozwa fedha hizo ni kinyume na utaratibu hivyo kwa ile mitaa inayofanya hivyo inapaswa kuacha na kuwapatia bure barua hizo.
“Kutoza fedha ili kupata barua hizo ni ukiukwaji wa taratibu na kuwataka viongozi hao wa Mitaa kuacha kufanya hivyo ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kama Serikali ilivyopanga,” alisema Lugano.
Hata hivyo badhi ya wakazi wa mkoa huo wameiomba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA kwa kushirikiana na Halmashauri kutoa matangazo zaidi juu ya zoezi hilo kwani baadhi ya watu hwana taarifa hasa wale waliopembezoni mwa Mitaa na Vijiji vya mkoa huo jambo ambalo litasababisha wengi kutoshiriki zoezi hilo
Mwisho.  

Wednesday, July 2, 2014

PWANI WAANZA UANDIKISHAJI VITAMBULISHO VYA TAIFA




Na John Gagarini, Kibaha
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amewataka wakazi wa mkoa huoa kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa linaloanza leo mkoani humo kwani  zoezi hilo ni muhimu sana linasaidia na ni  mfumo mkuu wa utambuzi na usajili wa watu na mifumo mingine ya serikali.
Mahiza amesema kuwa vitambulisho vitasaidia kupunguza riba ya mikopo ya benki, kuondoa ukiritimba wa kufungua akaunti, kutambua wakwepaji wa kurejesha mikopo ya benki, kupunguza wafanyakazi hewa, kupata malipo ya pensheni, haki za matibabu, kuwatofautisha wageni na wakimbizi na rai wa Tanzania.
Ameyasema hayo mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa zoezi la usajili na utambuzi wa watu mkoa wa Pwani uliowahusisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wanasiasa na viongozi wa dini.
Kutokana na kutotambulika wananchi hao kumesababisha wameshindwa kujiongezea uwezo wa kipato chao pamoja na cha Taifa hali ambayo imefanya uchumi  kushindwa kukua.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa Dickson Maimu amesema kuwa Maimu amesema kuwa kutokana na wananchi hao kutokuwa na utambulisho imesababisha kushindwa kunufaika na rasilimali fedha na fursa zingine kutokana na kutotambuliwa rasmi na mifumo husika.
Amesema Kutokana na hali hiyo serikali imaenza kutoa vitambulisho vya Utaifa ambavyo sasa vitawafanya wananchi wa Tanzania kutambulika na wale wasio raia nao watatmbuliwa hivyo kila kundi litajulikana.
Aidha amesema kuwa wananchi hao endapo watapatiwa vitambulisho wataweza kujijengea uwezo wao wenyewe kupitia taasisi za kifedha na sehemu nyingine hivyo kufanya uchumi wan chi kukua pia kwa wale wanaokopa mkopo utachukua muda mfupi.
Amebainisha kuwa Wananchi wanapaswa kujitokeza kutoa taarifa zao ili waweze kupata vitambulisho hivyo vya utaifa kwani mtu kama utaifa wako hautambuliki basi inakuwa ni tatizo na kushindwa kupata fursa mbalimbali.
Zoezi hilo lilianza mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar na sasa limeanza mkoa wa Pwani tangu Julai Mosi mwaka huu na na baadaye Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Kilimanjaro ambapo wananchi wanatakiwa kutoa taarifa sahihi ili kuweza kupatiwa vitambulisho vya Utaifa.
Mwisho.

NIDA KUJENGA KITUO KIKUBWA CHA KUHIFADHIA KUMBUKUMBU PWANI



Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kujenga kituo kikubwa cha kutunza kumbukumbu za shughuli za mamlaka hiyo ambacho kitakuwa ni cha kipekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kituo hicho kitajengwa eneo la Halmashauri ya mji wa Kibaha wilayani Kibaha mkoani Pwani ambapo kwa sasa tayari wamepata mjenzi na hatua za ujenzi ziko kwenye mchakato.
Akizungumza mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa Usajili wa watu mkoani humo, mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Dickson Maimu alisema kuwa tayari wameshapata eneo kwa ajili ya ujenzi huo.
“Ujenzi wa kituo cha NIDA ambacho kitatunza kumbukumbu za Watanzania wote utaanza wakati wowote ambapo tutapata msaada kutoka serikali ya watu wa Korea,” alisema Maimu.
Maimu alisema kuwa wanaishukuru Halmashauri ya Mji wa Kibaha na mkoa kwa kuwapatia eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na makazi ya watumishi wa mamlaka hiyo ambapo kwa sasa wamepata ofisi za muda kwa ajili ya kuendeshea zoezi hilo lililoanza mkoani Pwani Julai Mosi.
Katika hatua nyingine alisema kuwa zoezi hilo ambalo limeanza litakuwa na lengo la kutambua uraia wa watu wenye umria kuanzia miaka 18 na kuendelea kwa wananchi wanaoishi nchini na kuandikishwa taarifa zao.
Alisema kuwa mamlaka hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2008 na kuanza zoezi hilo kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar litajenga utawala bora wa mamlaka ya kutunza daftari la taifa la utambuzi na usajili wa watu kwa kushirikiana na wadau walioteuliwa.
“Mfumo wa Taifa wa utambuzi umeleta mabadiliko na usajili wa watu umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika serikali nyingi duniani zinazotumia mfumo huu,” alisema Maimu.
Mkurugenzi huyo wa NIDA alisema kuwa mamlaka itatoa vitambulisho vya makundi matatu ya Watanzania, wageni wakaazi na wakimbizi ambapo katika kudhibiti waombaji ambao si raia wanaoomba vitambulisho vimeshirikishwa vyombo vya dola ikiwa ni pamoja na kamati za ulinzi na usalama za mitaa, idara ya uhamiaji, polisi na usalama wa Taifa wanaopitisha maombi ili kuwaengua wasio raia.
Mwisho.

WASOMALI 11 WADAKWA




Na John Gagarini, Kibaha

HUKU zoezi la kuandikisha usajili na utambuzi wa watu mkoa wa Pwani kuanza zoezi hilo Julai 2 mwaka raia 11 wa Ethiopia wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kuingia nchini bila ya kibali.

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoani humo kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa raia hao walikamatwa kwa kushirikiana na rai wema.

Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai Mosi mwaka huu majira ya saa 3 usiku Kijiji cha Ukuni kata ya Dunda Tarafa ya Mwambao wilaya ya Bagamoyo.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Amoree Achem (22), Worko Hule (26), Basiad Tekiara (38), Anamaiyo Ramri (21), Fekri Angole (23), Kassa Dewenj (28) na Antiosogaso Suraj (20).

Wengine ni Abara Charkiso (30), Mmbarak Diljigab (30), Nichacho Abiche (32) na Kafasa Serecho (40).

Aidha alisema kuwa watuhumiwa hao watakabidhiwa idara ya uhamiaji kwa taratibu zingine za kisheria ili wajibu tuhuma zinazowakabili za kuingia nchini bila ya kibali.

Mwisho.