Friday, December 30, 2022

DOREFA YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA



DOREFA YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA 2022

Na Elizaberth Paulo, Dodoma.

VIONGOZI wa michezo na wanamichezo nchini wameaswa kupambania tasnia ya michezo ili iwe na thamani na kupewa kipaumbele kama tasnia zingine ili ichangiae katika ukuaji wa uchumi wa nchini kama nchi zilizowekeza kwenye michezo Duniani. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa michezo Nchini Ally Mayai Tembele wakati akizungumza na wadau wa soka kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Chama Cha Mpira wa Miguu Dodoma(DOREFA).

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuweka wazi mambo yaliyofanywa na kamati tendaji tangu kuingia madarakani pamoja na changamoto zilizowakumba katika utendaji wao.

Mayai amesema kuwa ili tasnia hii ya michezo iendelee kukua ni wajibu wa kila mwanamichezo kuwajibika kwa nafasi yake katika kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na Umuhimu wa michezo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya zetu hata uchumi wetu hii itasaidia kukua kwa tasnia hii bila kusahau kuwa na nidhamu kwa kila mmoja kumuheshimu mwenzake bila kujali cheo.

“Nawapongeza chama cha soka cha Mkoa wa dodoma kwa kuweza kufanya kazi bila kuwa na tofauti katika utendaji na hii itasaidia soka la Dodoma kuweza kukua kwa kasi kwani maendeleo bora huletwa na viongozi bora,"amesema Mayai

Ameongeza kwa kupongeza mkoa wa Dodoma kwa kuwa na programu ya vijana chini ya miaka 17 kwani itawasaidia vijana kukua kisoka na kuweza kuvumbua vipaji wakiwa bado na umri mdogo.

"Milango ya serikali ipo wazi kwa yeyote mwenye nia njema na tasnia hii na tunawakaribisha wadau wote kuweza kujitokeza kusapoti vipaji vya watoto wetu kwani kila mtu anaelewa mpira ni ajira kwa ajili ya kukuza uchumi na kuondokana na umasikini na kila mtu ameshuhudia namna ambavyo familia nyingi zimejikwamua kiuchumi kupitia michezo,"amesema Mayai.

Aidha ametoa rai kwa wadau wa mpira wa miguu kupambania haki za watoto katika kupata maeneo ya wazi ya watoto hao kufanyia mazoezi ya michezo yao ikiwa ni haki ya msingi ya mtoto na serikali imetoa maeneo ya wazi katika kila mtaa kwaajili ya michezo na shughuli zingine za kijamii.

“Ndugu zangu wanamichezo tuingie mitaaani kwenda kusaka vipaji, tukaelimishe jamii kuhusiana na haki za watoto wetu katika suala zima la michezo alafu kuna maeneo ya wazi ambayo hayatumiki kwa kazi zilizopangwa sasa hili nawaachia fuatilieni maeneo ya wazi kwaajili ya hiyo michezo alafu huko mitaani ndiko kwenye chimbuko la mpira wa miguu na hata historia ya watu wengi maarufu waliofanikiwa kwenye soka historia yao inaonyesha wametokea mitaani,"amesema Mayai

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Dodoma (DOREFA) Mohamed Aden amesema kuwa anawashukuru wadau wa soka jijini hapa kwa kuendelea kutoa maoni na ushauri ili kuhakikisha wanaboresha sekta ya michezo haswa mpira wa miguu jijini Dodoma.

Naye mwakilishi wa wanamichezo Jijini Dodoma amesema sekta ya michezo iko vizuri ila wanaiomba serikali chini ya Waziri wa Michezo Mohamed Mchengerwa kuwatatulia changamoto inayojitokeza ya mara kwa mara ya uwanja wa Jamhuri kufungiwa mara kadhaa kutokana na matumizi mengine ambayo ni tofauti na michezo hivyo kufanya wapenzi wa soka Jijini hapa kukosa burudani ya mpira wa miguu na kutumia viwanja vingine vilivyopo nje ya Dodoma.


Friday, December 23, 2022

RAIS DK SAMIA ATOA VYAKULA VITUO VYA WATOTO

RAIS DK SAMIA ATOA ZAWADI VYAKULA KWA NYUMBA MALEZI YA WATOTO MKOA WA PWANI

Na John Gagarini Kibaha

RAIS wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi vyakula vya sikukuu ya Christmas na mwaka mpya makundi maalumu ili nao washerehekee kama walivyo watoto wanaoishi na wazazi.

Akimwakilisha Rais kukabidhi katika kituo cha kulelea watoto wanaoishi kwenye Mazingira magumu cha Makao ya Malezi Madina kilichopo Mtaa wa Vikawe kata ya Pangani Wilaya ya Kibaha Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema kituo hicho kinawakilisha vituo 37 vilivyopo mkoa mzima.

Kunenge alisema kuwa Rais kwa kutambua makundi maalum ametoa zawadi hizo ili watoto hao washeherekee kama watakavyosheherekea wengine ambao wanaishi kwa furaha na familia zao.

"Nimekuja hapa kumwakilisha Rais wetu  amewaletea zawadi pamoja na salamu za sikukuu ya Christmas na mwisho wa mwaka ambapo amewaletea mbuzi wawili, mchele kilo 60, maharage kilo 40, mafuta lita 20, juisi na viungo mbalimbali,"alisema Kunenge.

Alisema kuwa wadau wa maendeleo na wenye uwezo kujenga tabia ya kujitolea kwa vituo vya watoto wenye mahitaji ambapo vitu vilivyotolewa ni pamoja na vitoweo ,mchele , maharage,mafuta ya kupikia ,vinywaji na viungo vingine mbalimbali vya kupikia.

Kwa upande wao watoto wa Makao ya Madina Zainab Athuman na Jumanne Manzi walimshukuru Mungu kwa kumwezesha Rais kupata na kuweza kuwapa zawadi hizo.

Naye Mlezi wa watoto Makao Malezi ya Madina Fatma Abdilai alisema kuwa wananchi waendelee kumuombea Rais Samia kwa mengi anayofanya nchini na kutekeleza ilani kwa kutambua makundi maalum.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka alimshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk Samia kwa kuitendea haki ilani ya Chama na kujali watoto .

Mkoa huo una jumla ya makao ya malezi 37 yenye jumla ya watoto 1,301 na kituo hicho cha Madina kina watoto 30.


Mwisho

Saturday, December 10, 2022

WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUWA WANYENYEKEVU

 


UNYENYEKEVU KWA WAJASIRIAMALI NI MSINGI WA BIASHARA-MAVUNDE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NAIBU Waziri  wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini amewaasa wajasirimali wadogo wadogo kujifunza unyenyekevu pindi wanapokuwa katika shughuli zao. 

Mavunde ameyasema hayo katika ziara aliyoifanya pamoja na wajasirimali (Mama Lishe ) Mkoani Dodoma walipotembelea katika mashamba ya Waziri Mkuu Mstaafu Peter Pinda na kuishukuru  familia hiyo kwa ukarimu wao. 

Ziara hiyo ya kusherehekea maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika na ambapo Naibu Waziri Mavunde aliitumia siku hiyo kwa kusaidia kuwaongezea mama lishe ujuzi katika ujasiriamali wao.

"Lipo jambo la kujifunza kwa sisi viongozi na kwenu nyie mliofika hapa tujifunze unyenyekevu jamani ukiagalia Waziri Mkuu Mstaafu Pinda kwa nafasi alizozishika lakini leo amekubali nimekuja na mama lishe na akakubali kututembeza shamba lote kwahiyo hapa ndipo tunajifunza Unyenyekevu,"alisema Mavunde.

Alisema kuwa ukiwa kiongozi ukiona watu hawaji kwako hata kuomba maji  ujue unashida kwani kiongozi maana yake ni kupokea watu hivyo Pinda na familia yake wana mioyo ya kipekee na ukarimu mkubwa sana. 

Aidha Mavunde ametumia ziara Hiyo kutangaza January kufanyika kongamano kubwa la siku ya MWANAMKE DODOMA JIJI ili kutathimi makubaliano ya mwaka mzima yalipofikia.

" Mimi nimejiitolea  kulilea  hili kundi ili nione mafanikio yao kila mmoja kwa nafasi yake nataka nione wanapiga hatua kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine Serikali ya  CCM chini ya uongozi wa Rais Dk Samia imefanya kazi kubwa ya kuendeleza Dodoma inakuwa makao makuu  fursa zipo nyingi nataka nione akina mama  wa Dodoma wakichangamkia hizi fursa,"alisema Mavunde.

 "Siyafanyi haya ili mnichague kuwa mbunge wenu, Sifanyi siasa nafanya haya kwasababu niliomba dhamana ya kuwa kiongozi nina wajibu wa kuwasaidia watu wangu,"alisema Mavunde. 

Naye Waziri mkuu Mstaafu Mizengo Peter Pinda amewasihi kushirikiana kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani kwani kila mtu mmoja akipanda mti itakua na mwonekano mzuri hiyo hudhihirishwa baada ya mvua kunyesha Dodoma inakuwa na muonekano mzuri.

Pinda alisema kuwa washirikiane katika kupanda miti ili kuifanya Dodoma ipendeze kwani mji ukiwa na kijani kingi ni mji unaovutia sana na kitu kingine yeye huwa anapenda kusema mjasiri wa mali na siyo mjasiriamali kwani ukishakua mjasiri wa mali utakuwa mbali kimaendeleo.

Alimwomba Mavunde amshirikishe kwenye hilo kongamano litakalofanyika Januari ili aweze kuhamasisha washiriki hao kupanda miti.
 
Nao baadhi ya wajasirimali waliozungumza kwa nyakati tofauti wametoa shukrani zao kwa Mavunde kwani hakuna mbunge aliyeifanya tukio kama hilo kwa kuwakutanisha na kuwapeleka katika mashamba ya Pinda kwani wamejifunza vitu vingi na kuahidi kwenda kufanyia kazi.

Mwisho. 

Monday, December 5, 2022

MIPANGO YAANDAA WATAALAMU


WAHITIMU WAANDALIWA KUAJIRIWA NA KUJIAJIRI.

Na Wellu Mtaki, Dodoma

CHUO cha Mipango na Maendeleo Vijijini kimejikita katika utoaji wa Elimu na vitendo katika kuhakikisha wanatoa wahitimu ambao watakaokwenda kujiajiri wenyewe na kuajiriwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi Jenifa Omolo akiwa mgeni rasmi aliyemwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Lameck Nchemba katika mahafali ya 36 ya chuo hiki cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Bi Omolo amesema kuwa kutokana na Mafunzo yanayotokana katika chuo hiko Wahitimu Watatumia ujuzi huo waliopata katika Kujiajiri wenyewe na kwenda Kuisaidia jamii.

Aliwataka wahitimu na wale wanafunzi watakaoendelea na mafunzo kwa ngazi ya juu kuwa na chachu ya kuendelea kujifunza ili kuongeza maarifa,ujuzi na ubunifu unaohitajika katika kuboresha utendaji wao wa kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Mipango Vijijini Prof. Hozen Mayaya ameeleza mafanikio waliyoyapata kwa mwaka 2021/2022 katika miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Mabweni na Kumbi za mihadhara kwa kutumia fedha za vyanzo vya ndani ya chuo na Ruzuku kutoka Serikalini na kueleza matarajio yao ya 2022/2023 ya kujenga Maktaba kubwa na ya kisasa pamoja na bweni la wanafunzi katika eneo la Kisesa Jijini Mwanza.

Akisoma hotuba kwa niaba ya wanafunzi wenzake muhitimu Gift Kyando ameishukuru Serikali na Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni Wizara Mama ya chuo chao na kuomba Chuo kuendelea kuwasaidia ili waweze kusonga mbele zaidi hasa wanapohitaji kupata Barua za uthibitisho kutoka Chuoni .

Mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ya mwaka 2022 yana jumlaya wanafunzi 6,225 waliohitimu wakiwemo wanaume 2,722 na wanawake 3,502 katika fani mbalimbali za Maendeleo vijijini.

Mwisho.