Na John Gagarini,
Kibaha
WAFANYABIASHARA
62 wa lililokuwa soko la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani waliofanya mkusanyiko
usio halali na kutaka kumwona Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jaffo wamehukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.
Hukumu hiyo
ilitolewa kwenye mahakama ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Kibaha Aziza
Mbadjo chini ya mwendesha mashtaka mwanasheria wa serikali Auleria Makundi na
mkaguzi wa Polisi Rashid Chamwi.
Mahakama
ilielezwa kuwa wafanyabiashara hao bila ya kibali walifanya mkusanyiko huo huku
wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali na kutaka kumwona Waziri Jaffo.
Na walifanya
mkusanyiko huo wakitaka kutoa malalamiko yao juu zoezi zima la uhamishwaji wao
kutoka soko la Maili Moja ambalo limebomolewa hivi karibuni kwenda soko jipya
la Mnarani au Sagulasagula maarufu kama Loliondo.
Ikaelezwa
kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda kosa hilo Januari 6 mwaka huu majira ya
saa 4 asubuhi eneo la Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi walifanya mkusanyiko
bila ya kibali toka Polisi wilaya.
Pia walikuwa
na mabango hayo jambo ambalo ni kinyume cha sheria jambo ambalo lilionyesha
kuleta usumbufu kutokana na kukosa uhalali wa kufanya hivyo.
Baada ya
kusomewa shitaka hilo ambalo ni kinyume cha sheria namba 74 (1-2) na 75 kifungu
kidogo cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa mapitio mwaka 2002 walikiri kutenda
kosa hilo na walijitetea kwa kusema kuwa walifanya kosa hilo bila ya kujua na
wanamajukumu mengi ya kifamilia hivyo kuiomba mahakama iwapunguzie adhabu.
Kutokana na
utetezi huo hakimu Mbadjo alisema kuwa kutojua sheria siyo sababu ya kuvunja
sheria hivyo mahakama imewakuta na hatia hivyo wanahukumiwa kifungo cha nje
ambapo wataitumikia jamii na hawapaswi kufanya kosa katika muda huo.
Mwisho.