Na John Gagarini,
Kibaha
ZOEZI la kuandikisha
wananchi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Pwani linatarajiwa
kuanza Juni 14 mwaka huu kwa watu wenye sifa wakiwemo wale waliokuwa na umri
chini ya miaka 18 wakati zoezi hilo lilipofanyika miaka ya nyuma.
Akizungumza na
waandishi wa habari mjini Kibaha mchambuzi wa mfumo wa kompyuta wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi Mariam Rajab alisema kuwa zoezi hilo litadumu kwa kipindi cha siku
28 kwenye maeneo yote ya mkoa huo.
Rajab alisema kuwa
zoezi hilo ni kwa watu wote wenye sifa wakiwemo wale wenye umri kuanzia miaka
18 na kuendelea ambao ni raia wa kuzaliwa au kuandikishwa kisheria.
“Zoezi hili ni muhimu
kwa wananchi hivyo wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili waweze kujiandikisha kwa
lengo la kupata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,”
alisema Rajab.
Alisema kuwa zoezi
hili litawahusisha hata wale ambao walijiandikisha kwenye daftari hilo kabla ya
uchaguzi mkuu uliopita kwani vitambulisho hivyo havitatumika tena ambapo
uchaguzi huu utatumia vitambulisho vipya.
“Tunawashauri wananchi
wajitokeze kwa wingi kwenye uandikishaji huu kwani endapo hawataandikishwa
watakosa fursa ya kupiga kura ambayo ni haki yao ya msingi,” alisema Rajab.
Aidha alisema Tume
imeshaleta vifaa kwa ajili ya zoezi hilo na hakutakuwa na tatizo la vifaa kwa
ajili ya kujiandikisha kama ilivyotokea kwa baadhi ya mikoa kuwa na upungufu wa
vifaa.
“Changamoto mbalimbali
ambazo tulizipata wakati wa zoezi hili kwenye ile mikoa ya awali tayari
zimefanyiwa kazi hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya vifaa kikubwa ni
kushiriki kwa wingi,” alisema Rajab.
Alisema kuwa tayari
maofisa wa uchaguzi kwenye mkoa huo wameshapatiwa mafunzo kwa ajili ya kutumia
mashine zitakazotumika kuandikishia BVR na kinachosubiriwa ni muda kufika.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kisarawe
SHIRIKA la Kuhifadhi
Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) limeanzisha mitandao kwa ajili ya ulinzi wa
misitu hiyo ili kukabiliana na uharibifu unaofanywa na watu wanaotumia mazao ya
misitu kwa ajili ya kujipatia kipato.
Hayo yalisemwa wilayani
Kisarawe na mratibu wa shirika hilo Yahaya Mtonda wakati wa sherehe za kuwapa
zawadi washindi wa Insha juu ya umuhimu wa misitu zilizoambatana na siku ya
mazingira duniani.
Mtonda alisema kuwa
TFCG imehamasisha kuanzishwa kwa mitandao ipatayo 93 ijulikanayo kwa kifupi (MJUMITA).
“Mbali ya mitandao hii
kulinda misitu hiyo pia tumewawezesha wananchi wanaozunguka misitu hiyo kuanzisha
vyama vya kuweka na kukopa (Vicoba) ili waweze kukopeshana ili kufanya shughuli
nyingine za kujiongezea kipato badala ya kutegemea misitu kama chanzo chao cha
mapato,” alisema Mtonda.
Mtonda alisema kuwa
pia wamewapatia mafunzo walimu wanaofundisha masomo yahusuyo utunzaji wa
mazingira ili kuwa na uelewa juu ya masuala ya kuhifadhi mazingira ili
wawafundishe wanafunzi wa shule za msingi.
“Tunatoa mafunzo kwa
walimu wa shule za msingi ili kuwarithisha wanafunzi tangu wakiwa wadogo waweze
kuona umuhimu wa tangu wakiwa wadogo misitu ili waweze kuitunza na kuhamasisha
jamii kupanda miti,” alisema Mtonda.
Aidha alisema kuwa
lengo la kuwafundisha ni kuwafanya wawe mabalozi wazuri wa kulinda misitu na
kutunza mazingira ambayo yamekuwa yakiharibiwa kwa kasi na waharibifu wa
mazingira.
Juu ya Insha alisema
ilikuwa ni kuataka kujua uelewa wa wanafunzi kutoka shule nane kutoka wilaya za
Ilala, Temeke, Kinondoni, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Kisarawe ambapo
Januari Eric wa Shule Msingi Mtamba alijinyakulia 100,000, Catherine Mbelwa wa
Kongowe 70,000 na Prisca Joseph wa Soga 50,000.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kisarawe
WAKALA wa Misitu Tanzania
(TFS) wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani unatarajia kubadilisha sehemu ya msitu wa
Pugu kuwa sehemu ya Utalii na kuwa hifadhi asilia kutokana na vivutio vilivyopo
kwenye msitu huo ambavyo baadhi havipo sehemu yoyote duniani.
Hayo yalisemwa na
meneja wa (TFS) wilaya ya Kisarawe Andrew Mwenuo alipozungumza na mwandishi wa
habari hizi wilayani humo.
Mwenuo alisema kuwa
kwa sasa tayari wameshaweka baadhi ya maeneo kwa ajili ya watu kupumzika na
njia za kutembea kwa miguu na baiskeli ili watu waweze kuutembelea msitu huo na
kuona mandhari na vivutio vilivyopo.
“Kuna wanyama wadogo
wadogo akiwemo aina ya nyani mwenye aibu kwani amuonapo mtu huficha uso wake
kwa aibu na hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani zaidi ya hapa,” alisema
Mwenuo.
Alisema kuwa mbali ya
nyani huyo pia kuna aina ya tembo mdogo ambao sehemu nyingine hapatikani zaidi
ya kwenye msitu huu pia kuna wanyama wengine, ndege, wadudu kama vipepeo na
wengine ambao ni vivutio.
“Hii itakuwa fursa kwa
Watanzania na raia wan je ambao wanataka kupumzika na kuona mazingira mazuri ya
msitu wakiwemo wasafiri wanaotumia njia ya ndege wanaweza kuja hapa na
kupumzika wakisubiri muda wa kuondoka kwa njia ya anga kwani ni jirani na uwanja
wa ndege,” alisema Mwenuo.
Aidha alisema kuwa
watu wataruhusiwa kuweka mahema na kupumzika na kujipumzisha huku wakila
vyakula pamoja na vinywaji ambapo kiingilio kitakuwa kwa wageni ni dola 10 huku
kwa Watanzania ni 1,500 huku wanafunzi wakitozwa 500.
Mwisho.