Na John
Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Udhibiti
wa usafiri Majini na Nchini Kavu (SUMATRA) imefungua ofisi yake mkoani Pwani na
kuwataka wananchi kutoa taarifa za mabasi yanayokatisha ruti na kutotoa tiketi
kwa abiria.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake ofisa mwandamizi wa SUMATRA wa mkoa Iroga
Nashoni alisema kuwa abiria wanapaswa kukitumia chombo hicho ili kuondoa kero
kwa wasafiri.
Iroga alisema
kuwa ofisi hiyo imefunguliwa mwezi uliopita kwa lengo la kusogeza huduma kwa
wateja wao ambapo inaendelea kujitanua kwenye mikoa, mingine ikiwa ni Singida,
Iringa, Musoma na Rukwa.
Alisema kuwa
changamoto kubwa waliyoiona ni mabasi mengi ya abiria kushindwa kumalizia
safari zao Kukatisha Ruti) na kutotoa tiketi kwa abiria jambo ambalo ni kinyume
cha sheria ambapo watawapiga faini hata ikibidi kuwafungia leseni madereva
watukutu.
“Changamoto
hiyo inakuwa kubwa kutokana na abiria wengi kutokuwa na elimu ya kujua haki zao
za msingi wanapokuwa wanasafiri hivyo kuwapa mwanya madereva kufanya watakavyo,”
alisema Iroga.
Aliongeza kuwa
wataendelea kutoa elimu kwa pande zote ikiwa ni pamoja na abiria, madereva na
wamiliki wa mabasi hayo ili waweze kufuata sheria bila ya kushurutishwa.
“Jana tulifanya
operesheni kukamata magari yenye makosa mbalimbali ambapo magari manne
yamekutwa na makosa na kupigwa faini kutegemea na makosa,” alisema Iroga.
Alibainisha kuwa
wataendelea kufanya operesheni za kushtukiza za mara kwa mara ili kukabiliana
na madereva wengi kukiuka sheria za barabarani na kuwataka wananchi kutoa
taarifa na si kulalamika bali wachukue hatua.
Mwisho.