Wednesday, March 22, 2023

WACHIMBAJI WADOGO WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

TAASISI YA KUENDELEZA UCHIMBAJI MDOGO IMETAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KAMISHNA wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga ameitaka Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo (FADev) kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ili Serikali na jamii itambue kazi zinazotekelezwa na taasisi hiyo.

Rai hiyo, imetolewa Machi 22, 2023 alipokutana na Uongozi wa taasisi ya FADev ambao umefika kwa lengo la kujitambulisha na kueleza majukumu yanayofanywa na taasisi hiyo Kuendeleza Uchimbaji Mdogo katika kikao kilichofanyika ofisi za Wizara Mtumba Jijini Dodoma.

Dkt. Mwanga ameitaka FADev ishirikiane na Serikali ili kujenga mahusiano mazuri katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali na kusaidia kuepusha kuingiliana na majukumu hayo mara kwa mara.

Aidha ameitaka FADev kuendelea kuilinda taasisi hiyo kwa kuheshimu taratibu na misingi iliyowekwa na nchi ambayo inalinda utu wa watanzania katika majukumu yao.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa FADev Mhandisi Theonestina Mwasha amesema kuwa inaendelea kutekeleza miradi inayokuza na kuimarisha uzalishaji wa dhahabu katika mikoa ya Geita na Shinyanga.

“Tunafanya mafunzo katika maeneo ya uchimbaji tunatoa elimu shirikishi kwa jamii inayozunguka migodi nakuanzisha mchakato wa kutoa elimu ya kuongeza thamani kwa ushirikiano wa wadau,” amesema Mhandisi Mwasha.

Akizungumzia kuwaendeleza wachimbaji wadogo Mhandisi Mwasha amesema taasisi imetoa vifaa vya uchimbaji migodi kwa vikundi mbalimbali walivyofanya navyo kazi sambamba na kuimarisha vikundi vya wanawake 15 katika mikoa ya Geita na Shinyanga.

Mwasha amesema kuwa hadi sasa taasisi ya FADev imefanikiwa kutoa mbinu za ujasiriamali kwenye maeneo ya uchimbaji madini, mafunzo ya utunzaji wa mahesabu, mafunzo ya ukusanyaji na utunzaji wa taarifa na matumizi sahihi ya kemikali zinazotumika kwenye uchenjuaji.

Pia imefanikiwa kutoa mikopo isiyozidi milioni 15 kwa kila kikundi kwa vikundi vitatu kwa kushirikiana na benki ya NBC.

Kikao hicho, kimehudhuriwa na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

KINANA AWATAKA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Komredi Abdulrahman Kinana ameitaka Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) kuhakikisha inahimiza wakinamama wa Chama hicho kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.

Kinana amesema hayo wakati akifungua mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convertion Jijini Dodoma.

Amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitawaunga mkono 2025 wakikishe wanagombea nafasi zote za uongozi na vikao vya Chama kitawaunga mkono wale wote watakaoenda kugombea.

Aidha Kinana ameitaka Jumuiya hiyo kuhakikisha inatetea haki za kinamama kila mahali, katika hatua nyingine ameitaka kujenga Utamaduni wa kuambiana ukweli na si kuogopana na watumie vikao kuamua mambo ndani ya Jumuiya na wasitumie makundi kuamua vikao.




WATUMISHI WA e-GA WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MISINGI MIKUU SITA YA MAMLAKA

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia misingi mikuu sita ya Taasisi.

Ndomba alisema hayo wakati wa kikao cha Watumishi wa Mamlaka kilichofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wa umma

Alisema kuwa e-GA inaongozwa na misingi mikuu sita ambayo inaelekeza kuhusu tabia na mwenendo wa watumishi wake kwa ngazi zote na kufafanua utamaduni wa mahali pa kazi ili kuhakikisha watumishi wote na wateja wa Mamlaka wanaouelewa wa pamoja wa jinsi wanavyotakiwa kuhudumiwa na nini kinachotarajiwa kutoka kwao.

"Nawakumbusha watumishi wote wa Mamlaka kuzingatia misingi hiyo ambayo ni uadilifu, ubunifu, kutathmini wateja, ushirikiano, kufanya kazi kwa pamoja na weledi katika utendaji kazi wao wa kila siku,"alisema Ndomba.

Alisema kuwa Mamlaka imekuwa taasisi ya mfano inayofanya shughuli zake za kila siku kwa kasi na ari inayokubalika, kutokana na uadilifu mkubwa wa Menejimenti na watumishi waliodhamiria kuweka juhudi kubwa katika kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji huduma bora kwa umma.

“Nawakumbusha watumishi wote kuimarisha uadilifu na kila mtumishi na kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kwa weledi kwa kuzingatia misingi hiyo huku Mamlaka ikiendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa watumishi wanafanya kazi katika mazingira bora na salama,”alisema Ndomba.

Aidha alisema kuwa katika kikao hicho mada mbalimbali zilizolenga kujenga uelewa na ufahamu kwa watumishi ziliwasilishwa ikiwemo Afya mahali pa kazi, Rushwa mahala pa kazi, Maadili ya utendaji, Haki na Wajibu, HIV/AIDS na magonjwa sugu yasiyoyakuambukiza, mawasiliano mazuri kwa utendaji bora wa kazi, namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo na maisha kazini.

Kikao hicho kilihitimishwa na Bonanza la Michezo lilifanyika katika viwanja vya Gymkana ambapo michezo mbalimbali ikiwemo kukimbiza kuku, kuvuta kamba, kukimbia kwa kutumia magunia, kukimbia na yai kwenye kijiko na mbio fupi.


Sunday, March 19, 2023

RIDHIWANI AWAAGA KIDATO CHA SITA KIKARO

 


MBUNGE wa Chalinze ameshiriki sherehe za kuwaaga wanafunzi wanaomaliza kidato cha 6 katika shule ya sekondari ya Kikaro Miono. Katika sherehe hizo Mh. Mbunge aliwasisitizia wanafunzi hao kuepuka tamaa za dunia na kujali masomo kwanza. #ELIMU #MionoChalinze

RIDHIWANI KIKWETE AFUNGUA VYOO VILIVYOJENGWA NA IFM CHARITY




MBUNGE wa Chalinze ameshiriki sherehe yaMiaka 10 ya Taasisi ya Ifm Charity kwa kufungua Vyoo vilivyojengwa na Taasisi hiyo na kula chakula nao katika kituo cha kulelea Watoto Yatima cha Hope-Miono, Chalinze. Mh. Mbunge amewashukuru wanachuo hao kwa kujali wenye uhitaji #10IFMSO

Saturday, March 18, 2023

KANUNI UASALAMA MIGODINI

WACHIMBAJI WA MADINI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI ZA USALAMA MIGODINI

SERIKALI imewataka Wachimbaji wa Madini kuzingatia Kanuni za Usalama na kufuata Sheria na Taratibu za Uchimbaji ili kuepusha ajali katika maeneo ya uchimbaji.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa Machi 17, 2023 alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji katika eneo la ajali ya wachimbaji wadogo waliofunikwa na kifusi na kufariki eneo la Igando Kata ya Magenge Tarafa ya Butundwe Mkoani Geita.

Dkt. Kiruswa, ameiagiza Tume ya Madini kutoa elimu ya Sheria ya Madini hususan elimu ya usalama kwa wachimbaji wanaozunguka maeneo ya uchimbaji katika kipindi cha mvua na kuchukua tahadhari.

"Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa pole kwa wananchi waliopoteza ndugu na marafiki katika ajali hii. Tunawataka wachimbaji mzingatie sheria zilizowekwa na Serikali ili mfanye shughuli zenu kwa tija," amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, amewataka wachimbaji katika eneo hilo kushirikiana na Serikali na mkoa kuchukua hatua kwa wachimbaji wote watakaobainika kukaidi maelekezo ya Serikali kwa wote wanaofanya uchimbaji kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewataka wachimbaji katika maeneo yenye uwekezaji kutoa ushirikiano kwa watu wenye leseni ya madini ili wafanye shughuli zao bila usumbufu. Amewataka pia kuzingatia usalama katika kazi zao.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita Mhandisi Martin Shija amemuelezea Dkt. Kiruswa kuwa, hatua mbalimbali zilichukuliwa kabla na baada ya ajali. Amesema mmiliki wa leseni na Serikali ya kijiji waliweka walinzi shirikishi kwenye eneo hilo ili kuzuia uchimbaji haramu na kuepusha madhara.

"Baada ya ajali tumeimarisha ulinzi katika eneo hilo, tumeendelea kufanya kaguzi mara kwa mara ili kubaini kama kazi zinaendelea na kuchukua hatua pale dosari inapojitokeza,"amesema Mhandisi Shija.

Naye, mwekezaji wa eneo hilo lenye leseni ya utafiti Abdul Stanslaus amesema katika eneo hilo ameendelea kuwa na mahusiano mazuri na jamii katika eneo hilo. Ameomba Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini ili wachimbaji wanaozunguka maeneo ya uchimbaji kuwa na uelewa mkubwa.

Naibu Waziri amefanya ziara baada ya wachimbaji wadogo 8 kufariki tarehe 10 Machi, 2023 baada ya kutokea ajali ya wachimbaji kukutwa na maji ndani ya mashimo wakiwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji.

Thursday, March 16, 2023

KAMATI YA NISHATI NA MADINI YAIPONGEZA SERIKALI KUIPATIA GST MASHINE ZA UTAFITI WA MADINI NCHINI

 

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUIPATIA GST MASHINE ZA KISASA ZA UTAFITI WA MADINI NCHINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali Awamu ya Sita kwa kuipatia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) vifaa na mashine za kisasa kwa ajili kuongeza wigo wa  utafiti wa madini nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na makamu  mwenyekiti wa Kamati hiyo Judith Kapinga mbunge wa viti maalum wakati akiongea na vyombo vya habari mapema baada ya kukamilisha ziara hiyo.

Ziara hiyo ya kutembelea maabara za GST kwa ajili ya kujionea utekelezaji wa majukumu ya GST , Mhe.  Mbunge Judith Kapinga aliipongeza serikali kwa kuwekeza mashine za kisasa katika kufanya uchunguzi, utambuzi na unjenjuaji wa madini mbalimbali.

"Kwa kweli niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi inazofanya katika kuiwekeza  taasisi yetu ya GST kwa kuipatia mashine mbalimbali za uchunguzi , utambuzi na uchenjuaji wa madini " alisema Kapinga

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Songwe Philipo Mulugo  ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo alishauri  kuwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2023/2024  GST iongezewe nguvu zaidi ya kibajeti ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Kabla ya ziara hiyo kuanza, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba aliwakaribisha wajumbe wa Kamati na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa wanaotoa katika kusimamia GST katika kutekeleza majukumu yake. 

"Ninashukuru sana Kamati hii kwa usimamizi wake nzuri ambao umeendelea kuifanya GST kuboreka zaidi katika  utoaji wa huduma zake,"Alisema Dkt. Budeba.

Mapema baada ya utambulisho huo Dkt. Budeba alimkaribisha Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa kwa ajili ya kuanza ziara hiyo ambapo Dkt. Kiruswa aliishukuru Kamati kwa namna mnavyoendelea kuishauri na kuisimamia Wizara ya Madini kwa ufanisi mkubwa. 

"Sisi tunafarijika sana kwa namna mnavyotusimamia Wizara  na Taasisi zake na tunawakaribisha GST muweze kujione mlichokisoma kwenye taarifa zetu". Aliongeza Dkt. Kiruswa

Katika ziara hiyo wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali juu ya utekelezaji wa majukumu ya GST hasa juu ya  uchunguzi wa sampuli za madini katika maabara ya GST.